Thursday, January 31, 2019

Katibu Mkuu Madini amsimamisha kazi Afisa Dodoma


Na Asteria Muhozya,
                                                                    
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amemsimamisha kazi Fundi Sanifu wa Madini, Asheni Daudi wa Ofisi ya Madini Dodoma baada ya kuagizwa na Waziri wa Madini Doto Biteko.

Hatua hiyo ilifikiwa Januari 30, 2019, baada ya Waziri Biteko akiongozana na Katibu Mkuu na Wataalam wengine wa wizara vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kufanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Dhahabu cha   Umoja kilichopo eneo la Viwanda la Kizota (Industrial Area) na kubaini mapungufu makubwa katika utendaji kazi wa wataalamu hususan uandaaji wa tarifa za uzalishaji wa madini.

Akizungumza katika eneo hilo, Waziri Biteko alisema wizara ilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu mienendo inayoendelea katika eneo hilo ambapo wahusika ambao ni Maafisa Madini wamekuwa hawatoi taarifa halisi za uzito na ubora wa dhahabu zinazozalishwa baada ya kuchenjuliwa, hivyo, serikali kukosa mapato stahiki.

Waziri Biteko aliongeza kuwa, tayari anayo majina yote ya wanaofanya michezo ya ujanja ujanja kwenye viwanda vya kuchenjua dhahabu, huku akieleza kuwa, hatua madhubuti zitachukuliwa kwa wote wanaofanya vitendo hivyo na kuongeza kwamba, zoezi hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwataka maafisa madini kuwa makini.

Aidha, alimwagiza Kamishna wa Madini kufanya kaguzi katika viwanda vyote vya kuchenjua dhahabu kwa lengo la kubaini utendaji wa kazi wa viwanda hivyo, ikiwemo taarifa za uzalishaji zinazotolewa na kusema “Lazima tufike mahali tuheshimu taratibu, madini haya ni mali ya nchi”, alisisitiza Biteko.

Wakati huo huo, Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkoa wa Dodoma kujitathmini kutokana na mambo yanavyokwenda katika eneo lake la kazi na kumtaka kuwasilisha kwa Kamishna wa Madini na kwa Waziri wa Madini taarifa za uzalishaji madini ya dhahabu kwa kipindi cha miezi sita.

Pia, katika ziara yake, Waziri Biteko alibaini mnunuzi wa madini ya dhahabu katika eneo la Kizota aliyefahamika kwa jina la Matondo Michembe ambaye anafanya shughuli hizo bila kuwa na leseni ya biashara ya madini hayo. Hivyo, alimwagiza Michembe kuwasilisha taarifa za utendaji wake kwa Kamishna wa Madini na Waziri wa Madini hususan  soko analouzia madini  hayo ya dhahabu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila alieleza kuwa, kiutaratibu ilikuwa lazima taarifa za uzalishaji na kiasi kilichozalishwa kujazwa katika vitabu maalum ndani ya kiwanda hicho lakini jambo hilo halikufanyika kama inavyotakiwa.

Aliongeza kuwa, Afisa huyo amesimamishwa ili kupisha uchunguzi na endapo itabainika, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa.


Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati alipotembelea kiwanda cha kuchenjua madini ya dhahabu cha Umoja eneo la Viwanda la Kizota wakati wa ziara yake ya kushtukiza. Katikati kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, wengine ni Watumishi wa kiwanda hicho kushoto, Katikati mwenye suruali ya blue ni Afisa aliyesimamishwa kazi, Fundi Sanifu Asheni Daudi, anayefuatia ni Afisa Madini wizara ya madini, Mhandisi Assah Mwakilembe. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akitafakari jambo wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika eneo ambalo shughuli za uuzaji  wa madini zinafanyika bila kuwa na leseni. Mbele ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila. Wengine ni Maafisa wa Wizara.

Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati akimhoji Munuzi wa Madini Matondo Michembe (wa pili kulia) ambaye alikutwa akifanya shughuli hizo bila kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila.

Waziri wa Madini Doto Biteko akutana na Mwenyekiti wa TEITI Jijini Dodoma

Na Rhoda James,

Waziri wa Madini Doto Biteko, Januari 29, 2019, alikutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi asilia (TEITI), Ludovick Utouh, ofisini kwake Jijini Dodoma. Lengo likiwa ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu ya TEITI nchini.









Monday, January 28, 2019

Wachimbaji wadogo kutunukiwa Vyeti vya Uhifadhi wa Mazingira


Na Nuru Mwasampeta,

Waziri wa Madini, Doto Biteko amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka Mafwenga, ofisini kwake jijini Dodoma.

Biteko ameshukuru Dkt. Mafwenga kwa kuonesha nia ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata cheti cha mazingira baada ya kubainisha njia bora za kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata uelewa juu ya uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Januari 28, 2019, Dkt. Mafwenga amesema kutokana na mwamko mkubwa iliyonayo Serikali wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kukua na kufanikiwa katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini, Nemc itajikita katika kuhakikisha inashirikiana na wizara katika kuhamasisha na kuelimisha wachimbaji wadogo juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Aidha, amebainisha kuwa, kutokana na vigezo vya awali ambavyo viliwafanya wachimbaji wadogo kutokupewa cheti cha mazingira zitaboreshwa na kuwawezesha kupata cheti hicho.

Amesema, wachimbaji wadogo watapaswa kusajili miradi yao katika Ofisi za Kanda za Baraza la Hifadi la Mazingira  ambao watakagua miradi hiyo na baada ya kujiridhisha watawapatia vyeti hivyo.


Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dr. Samuel Gwamaka Mafwenga (kulia) na Meneja wa kanda ya Kati Arnold Mapinduzi (kushoto) mara baada ya kumaliza mazungumzo mafupi ya namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kuhifadhi mazingira.

Biteko awataka Maafisa madini kuepuka tuhuma za rushwa, urasimu


Na Nuru Mwasampeta,
Waziri wa Madini Doto Biteko, amewataka Maafisa Madini wa mikoa kuepuka tuhuma za rushwa na urasimu na kubainisha kuwa, hatamfumbia macho Mtumishi yeyote atakayebainika kutekeleza majukumu yake kinyume na Sheria.
Aidha, amewataka maafisa hao kuwabaini na kuwatambua wachimbaji wadogo waliopo katika maeneo yao ya kazi.
Biteko aliwaeleza maafisa hao kuwa wizara haita mfumbia macho mtumishi yeyote asiyetekeleza majukumu yake na kukiri kuwa ni vema kufanya kazi na watu wachache kuliko kufanya kazi na mamia ya watu wasiokidhi mahitaji na kasi ya wizara katika kutekeleza majukumu yao.
Biteko alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki alipofanya mkutano baina yake, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na maafisa Madini wa Mikoa. Mkutano huo uliolenga  kutoa msisitizo katika kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji na wafanyabiashara wa madini katika maeneo yao ya kazi.
“Tunao wachimbaji wadogo wengi, wengi sana. Walio rasmi na wasio rasmi. Mwenye wajibu wa kuwatambua wachimbaji hao ni ninyi. Lazima sasa hivi mkatengeneze data base kwenye mikoa yenu ili kujua  akina nani wanajihusisha na shughuli za uchimbaji mdogo ili tutakapotaka  kuwasaidia wachimbaji wadogo misaada hiyo itolewe kwa wahusika kuliko kubahatisha,” alisisitiza Biteko.
“Tunataka kuanzisha soko la madini, na Serikali itatoa nafuu (incentive) kwa wachimbaji wadogo,  nafuu kwenye kodi, nafuu kwenye ushuru,  sasa hawa wachimbaji wadogo watakaonufaika na punguzo hilo lazima tuwajue ni akina nani, lazima tuwe pro- active katika utendaji wetu wa kila siku” alikazia.
Aidha, Waziri Biteko aliwataka Maafisa hao kwenda kutekeleza na kusimamia  Sheria  na kukataa kila aina ya maelekezo yanayotolewa kwao  ambayo yanayokiuka sheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
Biteko aliongeza kwa kuwataka Maafisa madini wa mikoa kuhakikisha wanafanya kazi na kulifanya jina la Wizara ya Madini linakuwa zuri kuliko kuonekana kama watu wasiokuwa na mwelekeo wa kiutendaji.
Biteko alibainisha kuwa mpaka sasa wizara imehamisha watumishi 57 makao makuu ya wizara ambao wizara imejiridhisha kuwa utendaji kazi wao hauridhishi na kwamba zoezi hilo litaendelea kwa lengo la kuimarisha utendaji wizarani.
Zaidi ya hayo, Biteko aliwataka Maafisa Madini hao kuhakikisha kuwa wanashirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuwataka kuwajibika kwao kwani ni wawakilishi wa Rais na wanasimamia shughuli za Serikali.
Aliongeza kuwa, wakuu wa wilaya ni wasimamizi wa Serikali katika maeneo hayo, ni wawakilishi wa Rais katika wilaya na mikoa hiyo ni wasimamizi wa kazi zote za serikali ikiwepo ya madini hivyo hawana budi kushirikiana nao.
Biteko aliwataka maafisa Madini hao kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo ziwe ni za kibajeti au vifaa  ili waweze kusaidiwa na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao na kuwaagiza kumtumia Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Simon. Msanjila katika kutatua changamoto hizo.
Akizungumzia suala la uanzishwaji wa vituo vya madini katika mikoa. Biteko alisema, Kanuni za kusimamia vituo hivyo zimekwisha andaliwa na zitasainiwa wakati wowote na kuwataka maafisa hao kutambua kuwa wao ni watu muhimu katika kusimamia vituo hivyo.
Biteko alisema anatamani ndani ya miezi sita sekta ya madini ibadilike, mtu akija aone kuna maendeleo, aliwasihi kuhama kwenye majina ya kuitwa wala rushwa, tuhame kuitwa warasimu tuhame kwenye sifa za watu wanaosimamia masuala ya madini pamoja na kujihusisha na shughuli za uchimbaji jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Akihitimisha kikao hicho, Biteko aliwataka maafisa hao kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa katika mkutano wa kisekta kila mtu katika mkoa wake akayafanyie kazi. Pia  aliwaagiza kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi wa wizara kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na yale yaliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Madini,  Angellah Kairuki pamoja na  Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani  Manya alieleza kufurahishwa na kukiri kwenda kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kiongozi wa wizara hiyo.

Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao baina ya uongozi wa wizara na Maafisa Madini wa Mikoa kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam

Waziri Biteko aanza kutatua mgogoro kati ya Mzee Mchata, Kampuni ya Mantra


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Januari 28, amekutana na Mzee Eric Mchata na Kampuni ya madini ya Uranium ya Mantra Tanzania kwa lengo la kutatua mgogoro uliopo baina ya pande hizo mbili.

Kikao hicho, kinafuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli Januari 22 na Mzee Mchata wakati wa mkutano wa Kisekta ulioshirikisha wachimbaji wadogo na wadau wa madini uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakati akisikiliza kero za wachimbaji na wadau wa madini walioshiriki kikao hicho, Rais Magufuli alipokea kero ya Mzee Mchata aliyemweleza kwamba amekuwa na mgogoro na kampuni hiyo kwa kipindi cha takribani miaka 12 na bado hajapata suluhu.

Akijibu kero iliyowasilishwa na Mzee Mchata, Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Madini kuhakikisha mgogoro huo unafikia mwisho.


Sehemu ya Wataalam wa wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini wakifuatilia kikao cha kusuluhisha mgogoro kati ya kampuni ya Mantra na Mzee Eric Mchata. Kutoka kulia ni Kamishna wa Tume ya Madini, Prof. Abdulkarim Mruma, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Afisa Sheria wa Wizara ya Madini, Joseph Nyamsenda. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akimweleza jambo Mzee Eric Mchata wakati wa kikao cha kusuluhisha mgogoro baina yake na kampuni ya Mantra Tanzania. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Mzee Eric Mchata (kushoto) wakati wa kikao cha kusuluhisho mgogoro baina yake na Kampuni ya Madini ya Uranium ya Mantra Tanzania.

Waziri Mkuu Majaliwa ataka kanuni za uanzishwaji masoko ya madini kukamilishwa haraka


Ø Aitaka Wizara ya Madini kutoa Mwongozo wa Usafirishaji Madini Nje.

Ø Waziri Biteko asema, Rasimu ya Kwanza imekamilika.

Ø Asisitiza Masoko yaanze mwezi Februari.

Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Madini kuharakisha ukamilishaji wa Kanuni za Uanzishwaji Masoko ya Madini nchini, ikiwemo kuhakikisha masoko hayo yaanza haraka.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo Januari 26, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha Mawaziri kutoka wizara mbalimbali, Wakuu wa Mikoa yote nchini, Wizara ya madini, Makatibu Tawala wa Mikoa, Taasisi mbalimbali zikiwemo Tume ya Madini, Benki Kuu ya Tanzania na Kituo cha Uwekezaji Nchini, (TIC).

Amesema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli aliyayotoa Januari 22 wakati akifungua Mkutano wa Kisekta uliowashirikisha wachimbaji na wadau wa madini nchini ambapo Rais Magufuli alisisitiza juu ya kuanzishwa kwa masoko ya madini.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kikao hicho na kusema kwamba, kimelenga katika kujenga uelewa wa pamoja kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Madini wa Mikoa kuhusu kanuni na namna ya kuendesha Masoko hayo.

Akisisitiza kuhusu usimamizi wa masoko ya madini, Waziri Mkuu amesema kuwa, Wakuu wa Mikoa kwa kushirikiana na Maafisa Madini ndiyo watakuwa wasimamizi wakuu wa masoko hayo  na kuongeza kuwa, katika ngazi ya Wilaya, masoko hayo yatasimamiwa na wakuu wa wilaya na kueleza “kwenye wilaya msimamizi ni mkuu wa wilaya, wakuu wa wilaya mkaripoti kwa wakuu wa mikoa wawasaidie,”.

Pia, ametaka pindi kanuni hizo zitakapokamilika kuzifikisha kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri za Wilaya na  katika maeneo yote yenye machimbo wakiwemo wachimbaji na Wafanyabiashara ikilenga kuwezesha wadau hao kufikiwa na kanuni hizo na kuwa na uelewa wa kutosha na hatimaye ziweze kusimamiwa kikamilifu kwa kushirikiana  na Tume ya Madini.

Katika kuhakikisha kwamba masoko hayo yanaendeshwa  kwa usalama, ameitaka mikoa kuhakikisha kunakuwa na na hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo hayo ili  kuwahakikishia wafanyabiashara, wachimbaji na wananchi kwa ujumla usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini hayo katika masoko yatakayoanzishwa.

Akizungumzia mwongozo wa usafirishaji madini nje ya nchi, ameitaka  wizara  ya madini kutoa mwongozo huo mapema na kueleza kuwa, baada ya serikali kutafakati kwa kina, imetoa mwongozo wa kusafirisha baadhi ya madini nje ya nchi na hivyo kuitaka wizara kutoa mwongozo huo kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa, tayari rasimu ya kwanza ya Kanuni hizo imekamilika na kueleza kuwa, kikao kazi kinalenga jambo ambalo halikuwahi kufanyika tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru na hivyo kuwataka wakuu wa mikoa kulifanya kuwa jambo linalowahusu wote.

Amesema kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalum wanayoweza kufanyia biashara  ya madini hali ambayo inachangia kuwepo utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Ameongeza, ili  kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati iliyojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki  Kuu na Tume ya Madini.  

Amesema kuwa, Kamati hiyo iliundwa ili kuandaa rasimu ya Kanuni za kuanzisha na kusimamia Masoko ya Madini Nchini na kuongeza kuwa katika kuandaa kanuni hizo, jina la Kanuni linalondekezwa The Mining (Mineral and Gem House) Regulations, 2019," amesema Waziri Biteko.

Ameongeza kuwa, Marekebisho ya sheria yaliyofanyika mwaka 2017 katika sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yalilenga kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha sekta ya madini inachangia ipasavyo katika kukuza na kuimarisha mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuongeza kwamba, si kweli kwamba marekebisho hayo yamefukuza wawekezaji bali yameongeza idadi ya wanaotaka kuwekeza katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha masoko ya madini yanaanza mara moja wakati kanuni hizo zinaendelea kuboreshwa na kusisitiza wakuu hao wahakikishe yaanza ifikapo mwezi Februari mwaka huu.

“Lazima Wakuu wa Mikoa tuanze. Wakuu wa Mikoa tutaanza na Kanuni hizi, hizi. Tutaendelea kuziboresha lakini lazima tuanze. Na kanuni hizi zikipita, lazima kila anayehusika atafanya biashara kupitia kanuni hizi,” amesisitiza Waziri Biteko.

Halikadhalika, amewataka washiriki wa kikao hicho kuhakikisha wanazipitia kanuni hizo kwa lengo la kufanya maboresho na kutoa mapendekezo yatakayowezesha kuwa na kanuni zitakazowezesha taifa kunufaika na rasilimali hiyo na kuongeza, “ hizi kanuni zikiwa mbovu itakuwa yetu wote,”.

Pia, amewaomba Wakuu wa Mikoa, Maafisa Tawala wa Mikoa, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na Wadau kwa ujumla kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kutimiza ndoto za muda mrefu za Wachimbaji wadogo Wafanyabiashara wa Madini, Wadau na Watanzania wote kwa ujumla za kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika taifa na inalinufaisha.

Naye, Waziri , Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo amesema kuwa, Waziri Biteko ameanza vizuri na  kueleza kuwa,  kikao hicho kitasaidia kupata mambo mbalimbali yatakayosaidia katika uanzishwaji wa masoko hayo na kueleza kuwa, timu yake ya mikoa iko tayari.

“Mhe. Waziri nimefurahi sana namna wakuu wa mikoa walivyozungumza wakati wa majadiliano ya kuboresha Kanuni hizi. Tunakwenda kuona namna ya kuanzisha masoko haya,”.

Aidha, amewataka wakuu wa mikoa kulichukulia jambo hilo kama matarajio ya Rais Magufuli anavyotaka kuona kwamba madini yanalinufaisha taifa.






Waziri Biteko amaliza mgogoro kati ya Kampuni ya BEAL na MTL


Na Rhoda James,

Waziri wa Madini, Doto Biteko amemaliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Barrick Exploration Africa Limited (BEAL) na Megagems Tanzania Limited (MTL) uliodumu kwa muda mrefu.

MTL ambaye ni mlalamikiji alikuwa anadai kulipwa kiasi cha Dola za Marekani 10,000 na Kampuni ya BEAL.

Akisuluhisha mgogoro huo Waziri Biteko ameitaka Kampuni ya BEAL kumlipa mlalamikaji kwa kuwa vibali vyote vinaonesha kuwa anastahili kulipwa.

Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 25 Januari, 2019 jijini Dodoma katika Ofisi ya Waziri wa Madini, Doto Biteko.

Waziri wa Madini, Doto Biteko akishuhudia Mwakilishe wa Kampuni ya Barrick Exploration African Limited (BEAL), Janet Lekashingo akipeana mkono na mmiliki wa kampuni ya Megagems Tanzania Limited (MTL) baada ya kufikia mwafaka wa mgogoro wao wa MTL kulipwa haki yake.

Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa (wa kwanza kushoto) akifatilia  kikao cha kusuluhisha mgogoro kati ya Kampuni ya Barrick Exploration Africa Limited (BEAL) na Megagems Tanzania Limited (MTL). Wengine katika picha ni Mwanasheria wa Wizara, Godfrey Nyamsenda (wa pili kushoto), Mwanasheria wa Novelty Advocate Joseph Asenga na Mmiliki wa Kampuni ya MTL, Suleiman Nasib.

Mwakilishi wa Kampuni ya Barrick Exploration African Limited (BEAL), Janet Lekashingo akimkabidhi Waziri wa Madini, Doto Biteko nyaraka kwa ajili ya kupitia kabla ya kumaliza Mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya Barrick Exploration Africa Limited (BEAL) na Megagems Tanzania Limited (MTL).

Waziri wa Madini, Doto Biteko akipitia nyaraka iliyokabidhiwa kwake na Mwakilishe wa Kampuni ya Barrick Exploration African Limited (BEAL), Janet Lekashingo (hayupo pichani) kabla ya kumaliza mgogoro kati ya Kampuni ya Barrick Exploration Africa Limited (BEAL) na Megagems Tanzania Limited (MTL).

Mliliki wa Kampuni ya Megagems Tanzania Limited (MTL), Suleiman Nasib (wa kwanza kulia) akimsikiliza Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) wakati alipokuwa akisikiliza kesi iliyokuwepo kati yake na Kampuni ya Barrick Exploration Africa Limited (BEAL). Wengine katika picha ni Wanasheria kutoka Novelty Advocate Joseph Asenga na Godfrey Nyamsenda kutoka Wizara ya Madini.

Monday, January 21, 2019

Kamati ya Bunge yaipongeza Wizara ukusanyaji maduhuli


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kwa ukusanyaji maduhuli ambapo katika kipindi cha nusu Mwaka wa Fedha 2018/19, cha kuanzia mwezi Julai hadi 31 Disemba, 2018, ilikusanya shilingi 167,742,947,332 kati ya shilingi 310,598,007,000 iliyopangiwa.

Akiwasilisha taarifa kwa Kamati hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, amesema kuwa, shilingi 310,320,0004,000 zilipangwa kukusanywa kupitia Tume ya Madini, na shilingi 278,003, 000 katika Makao Makuu ya Wizara na Chuo cha Madini Dodoma.

“ Mhe. Mwenyekiti, hivyo lengo la makusanyo kwa kipindi cha nusu mwaka Julai hadi Disemba 2018 ni shilingi 155,299,003,500. Hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2018, wizara ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 167,742,947,332 sawa na asilimia 108.01 ya lengo,” amesema Kamishna Mulabwa.

Akizungumzia juhudi za wizara katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, amesema wizara iliandaa kongamano la kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya madini nchini lililojulikana kama China Tanzania mining Forum lililenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini nchini, ikiwemo kutafuta soko la madini hayo nchini China na kuangalia fursa za ushirikiano kati ya Wizara ya madini Tanzania na Wizara ya maliasili ya China.

“ Mhe. Mwenyekiti kongamano hilo pia lilitumika kuwakutanisha wachimbaji wa Tanzania na watengenezaji wa mitambo mbalimbali ambayo hutumika kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini,”amesema Kamishna Mulabwa.

Kamishna Mulabwa ameongeza kuwa, katika kongamano hilo jumla ya wachimbaji wadogo 40 na wakubwa 4 kutoka Tanzania walishiriki kongamano hilo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akijibu hoja za Kamati kuhusu suala la ukusanyaji wa maduhuli amesema bado Wizara haijaridhika na kiwango kilichokusanywa na kuongeza kuwa, kama wizara katika mipango yake yenyewe ya ndani, imepanga kukusanya zaidi ya kiwango cha bilioni 310 iliyopangiwa.

“ Mhe. Mwenyekiti sisi wenyewe ndani tumejiwekea malengo yetu ya kukusanya zaidi ya kiasi tulichopangiwa. Tunajiongeza tuongeze kiwango hicho sisi wenyewe.  Tunafanya hivyo ili mwakani hata kama tutaongezewa kiwango basi tuwe tayari tumekwisha jipanga,” amesisitiza Naibu Waziri Nyongo.

Akizungumzia udhibiti wa madini, amesema kuwa, Wizara inaendelea za jitihada na kudhibiti utoroshaji madini ambapo kwa upande wa madini ya tanzanite udhibiti unaendelea na kusema kuwa, kwa sasa madini hayo yanapita katika mfumo unaoeleweka.

“Kesho Januari 22, tutakuwa na mkutano wa Kisekta, watakuja wachimbaji na wafanyabiashara naamini watamweleza Mhe. Rais kero zao na tutasikia. “Lakini pia tumewaalika wakuu wa Mikoa ambayo shughuli za madini zinafanyika, tunataka kuweka mazingira mazuri kwa sekta.

Kuhusu changamoto za masoko ya madini, amesema wizara inataka kuhakikisha kwamba biashara ya madini inakuwa wazi na halali huku ikijipanga kukusanya zaidi kodi za serikali na kuongeza kuwa, wizara inajipanga kuweka mfumo mzuri wa soko la madini jambo ambalo litazinufaisha pande zote.

“ Mhe. Rais anataka tununue tuweke reserve. Lakini pia Serikali ikinunua kwa bei ya soko, hata wachimbaji watafurahi,” amesema Nyongo.

Akizungumzia suala la uhifadhi wa mazingira amesema kuwa wizara imeweka utaratibu wa pindi wawekezaji wanapoanzisha mgodi ni lazima waweke mpango wa namna watakavyofunga migodi huku suala la uhifadhi wa mazingira likipewa umuhimu wake.

Ameongeza kuwa, wizara inaweka mkazo kwa migodi kueleza mpango wa ufungaji migodi ambao utaacha mazingira yakiwa salama.

Wakizungumza katika kikao hicho kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Kamati hiyo, licha ya kuipongeza wizara kwa ukusanyaji wa maduhuli, wameitaka wizara kuweka mikakati madhubuti katika suala uongezaji thamani madini kutokana na zuio la usafirishaji madini ghafi nje ya nchi.

Aidha, wajumbe hao wameitaka Wizara kuendelea kukiimarisha Kituo chake cha Jimolojia Tanzania (TGC) ili kuweza kutoa wataalam wa kutosha katika tasnia hiyo ya uongezaji tthamani madini.

Maafisa madini watakiwa kutobagua Migodi


Na Asteria Muhozya, Mbinga

Maafisa Madini nchini wametakiwa kutobagua migodi midogo kwa kuelekeza nguvu kwenye migodi mikubwa  tu  huku wakisisitizwa kutatua migogoro kwenye maeneo yao ya kazi na kuelezwa kuwa,  watakaobainika wakibagua migodi hiyo na kutotatua migogoro wataondolewa  kwenye nafasi zao.

Hayo yalibainishwa Januari 17 na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati  akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini aina ya Sapphire wakati wa  ziara yake katika kijiji cha Masuguru, Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

 Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara hiyo ikilenga kukagua shughuli za uchimbaji madini wilayani humo pamoja na kusikiliza kero za wachimbaji katika migodi hiyo,  ambapo wachimbaji waliwasilisha kero za kutaka kutengewa maeneo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji, bei elekezi za madini  ikiwemo kuunganishwa na  huduma ya umeme kwenye migodi yao.

Akizungumza kijijini hapo, alimtaka Afisa Madini mkoa wa Ruvuma hukakikisha anaishughulikia kero hiyo na kuitatua  mara moja na kuongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano anataka wachimbaji nchini wachimbe madini, hivyo,  maafisa madini   kote nchini wahakikishe wanashughulikia kero katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kusuluhisha migogoro.

“Sisi ni matajiri, tumebarikiwa madini ya vito. Wachimbaji chimbeni lakini mchimbe katika maeneo yaliyoruhusiwa kuchimbwa”.alisisitiza.

Alisema kuwa, kama mgogoro ni mkubwa wapo viongozi wa vyama vya wachimbaji wahakikishe kuwa  wanafikisha migororo hiyo na kusema “tuleteeni na sisi lakini  usipoishughulikia migogoro hiyo tutakuondoa.
Aliongeza kwamba, serikali inalenga katika kuwatoa wachimbaji wadogo kutoka katika uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji wa  kati na hatimaye mkubwa na ndiyo sababu inaendelea na ujenzi wa vituo vya umahiri  katika maeneo mbalimbali nchini ikilenga katika kutoa elimu ya uchimbaji bora, uchenjuaji bora, biashara ya madini na ujasiliamali ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanakua.

Aliongeza kuwa,  elimu  ya ujasiliamali ni muhimu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa itawaandaa kuwa na uchimbaji endelevu na wenye tija.

Akijibu ombi la ruzuku,  aliwataka wachimbaji wadogo kujiunga katika vikundi vidogo vidogo  ili iwe rahisi kwa wachimbaji hao kufikiwa  ikiwemo kupatiwa huduma za leseni, elimu, vifaa, kuwamilikisha, kuwapatia mikopo na  kuwafuatilia  jambo ambalo litapelekea wafanye kazi kwa urahisi na kwa kulipa kodi za serikali na  wao kubaki na kipato  kitakachowezesha maisha bora.

Alisema uwepo wa mazingira mazuri migodini utasaidia vijana kufanya kazi na hivyo kuwa na taifa lenye watu wanaofanya kazi.  Aliwataka maafisa madini wote kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya wachimbaji wadogo na kueleza kwamba, endapo serikali itakuta migogogoro ya wachimbaji wadogo  katika maeneo yao wataondolewa.

Aliongeza kwamba, wizara imejipanga na tayari kuna baadhi ya maeneo yametengwa kwa ajili ya wachimbaji  na kuwasisisitiza kuhakikisha wanauza madini  wanayoyachimba katika maeneo rasmi.

Akizungumzia suala la broker, aliwataka kuhakikisha wanakuwa na leseni ya kufanya shughuli hizo ikiwemo vifaa vya kupimia madini na kuwataka kulipa kodi. Pia, aliwatahadharisha wachimbaji wanaoshirikiana na broker wasiokuwa  na leseni   kuacha kwani kwa kufanya hivyo ni kwamba  kwamba wote wanaliibia taifa.” Maafisa madini hakikisheni mnawajua ma broker wote  na wawe na leseni na walipe kodi, “ alisisitiza Nyongo.

 Akijibu ombi la  ruzuku lililowasilishwa  kwake,  alisema fedha za ruzuku zilizokuwa zikitolewa awali  hazikuwafikia walengwa wote  na kueleza kuwa, wapo waliopata ruzuku hizo lakini hawakuwa wachimbaji na kuongeza kwamba, hivi sasa wizara inaangalia namna bora ya kuwasaidia wachimbaji.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkoa wa Ruvuma  Abraham  Nkya alisema kuwa, mkoa huo tayari umetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kwamba watashirikiana na wachimbaji hao ili  suala hilo liweze kuwasilishwa Tume ya Madini kwa  ajili ya hatua zaidi.

Awali , kiongozi wa wachimbaji   aliwasilisha ombi kwa Naibu Waziri   la wachimbaji kupatiwa  ruzuku. Alisema mkoa huo umebarikiwa madini ya ujenzi, nishati, viwanda    huku eneo la Masuguru likibariwa madini ya Sapphire. Alisema eneo hilo liliombwa kwa ajjili ya uchimbaji mdogo lakini mpaka  sasa bado halijatengwa.

Pia, alisema ipo changamoto ya kukosekana elimu kwa watendaji vijijini ambao wamesababisha mgizo mkubwa wa kodi kwa wachimbaji.

Sehemu ya Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Saphire wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe Maalum kwa Naibu Waziri Stanslaus Nyongo baada ya kuwasili katika kijiji cha Masuguru  Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo mwenye sweta (nyekundu) katika picha ya pamoja na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Sapphire katika kijiji cha Masuguru Wiaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Ishenyi akizungumza jambo wakati wa  mkutano wa hadhara katika kijiji cha Masuguru. Katikati ni Naibu Waziri wa  Madini Stanslaus Nyongo.

Mmoja wa wachimbaji wananwake katika kijiji cha Masuguru akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo  na Mkuu wa  Wilaya ya Mbinga Cosmas Ishenyi ( hawapo  pichani) wakati  wa ziara ya viongozi hao kijijini hapo.