Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kwa
ukusanyaji maduhuli ambapo katika kipindi cha nusu Mwaka wa Fedha 2018/19, cha
kuanzia mwezi Julai hadi 31 Disemba, 2018, ilikusanya shilingi 167,742,947,332 kati ya shilingi 310,598,007,000
iliyopangiwa.
Akiwasilisha
taarifa kwa Kamati hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Kamishna wa Madini Mhandisi
David Mulabwa, amesema kuwa, shilingi 310,320,0004,000
zilipangwa kukusanywa kupitia Tume ya Madini, na shilingi 278,003, 000 katika
Makao Makuu ya Wizara na Chuo cha Madini Dodoma.
“ Mhe.
Mwenyekiti, hivyo lengo la makusanyo kwa kipindi cha nusu mwaka Julai hadi
Disemba 2018 ni shilingi
155,299,003,500. Hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2018, wizara ilifanikiwa
kukusanya kiasi cha shilingi 167,742,947,332
sawa na asilimia 108.01 ya lengo,”
amesema Kamishna Mulabwa.
Akizungumzia
juhudi za wizara katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, amesema
wizara iliandaa kongamano la kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya
madini nchini lililojulikana kama China
Tanzania mining Forum lililenga kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo
katika sekta ya madini nchini, ikiwemo kutafuta soko la madini hayo nchini
China na kuangalia fursa za ushirikiano kati ya Wizara ya madini Tanzania na
Wizara ya maliasili ya China.
“ Mhe.
Mwenyekiti kongamano hilo pia lilitumika kuwakutanisha wachimbaji wa Tanzania
na watengenezaji wa mitambo mbalimbali ambayo hutumika kwenye shughuli za
uchimbaji na uchenjuaji wa madini,”amesema Kamishna Mulabwa.
Kamishna
Mulabwa ameongeza kuwa, katika kongamano hilo jumla ya wachimbaji wadogo 40 na
wakubwa 4 kutoka Tanzania walishiriki kongamano hilo.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akijibu hoja za Kamati kuhusu
suala la ukusanyaji wa maduhuli amesema bado Wizara haijaridhika na kiwango
kilichokusanywa na kuongeza kuwa, kama wizara katika mipango yake yenyewe ya
ndani, imepanga kukusanya zaidi ya kiwango cha bilioni 310 iliyopangiwa.
“ Mhe.
Mwenyekiti sisi wenyewe ndani tumejiwekea malengo yetu ya kukusanya zaidi ya
kiasi tulichopangiwa. Tunajiongeza tuongeze kiwango hicho sisi wenyewe. Tunafanya hivyo ili mwakani hata kama
tutaongezewa kiwango basi tuwe tayari tumekwisha jipanga,” amesisitiza Naibu
Waziri Nyongo.
Akizungumzia
udhibiti wa madini, amesema kuwa, Wizara inaendelea za jitihada na kudhibiti
utoroshaji madini ambapo kwa upande wa madini ya tanzanite udhibiti unaendelea
na kusema kuwa, kwa sasa madini hayo yanapita katika mfumo unaoeleweka.
“Kesho Januari
22, tutakuwa na mkutano wa Kisekta, watakuja wachimbaji na wafanyabiashara
naamini watamweleza Mhe. Rais kero zao na tutasikia. “Lakini pia tumewaalika
wakuu wa Mikoa ambayo shughuli za madini zinafanyika, tunataka kuweka mazingira
mazuri kwa sekta.
Kuhusu
changamoto za masoko ya madini, amesema wizara inataka kuhakikisha kwamba
biashara ya madini inakuwa wazi na halali huku ikijipanga kukusanya zaidi kodi
za serikali na kuongeza kuwa, wizara inajipanga kuweka mfumo mzuri wa soko la
madini jambo ambalo litazinufaisha pande zote.
“ Mhe. Rais
anataka tununue tuweke reserve.
Lakini pia Serikali ikinunua kwa bei ya soko, hata wachimbaji watafurahi,”
amesema Nyongo.
Akizungumzia
suala la uhifadhi wa mazingira amesema kuwa wizara imeweka utaratibu wa pindi
wawekezaji wanapoanzisha mgodi ni lazima waweke mpango wa namna watakavyofunga
migodi huku suala la uhifadhi wa mazingira likipewa umuhimu wake.
Ameongeza
kuwa, wizara inaweka mkazo kwa migodi kueleza mpango wa ufungaji migodi ambao utaacha
mazingira yakiwa salama.
Wakizungumza
katika kikao hicho kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Kamati hiyo, licha ya
kuipongeza wizara kwa ukusanyaji wa maduhuli, wameitaka wizara kuweka mikakati madhubuti
katika suala uongezaji thamani madini kutokana na zuio la usafirishaji madini
ghafi nje ya nchi.
Aidha, wajumbe
hao wameitaka Wizara kuendelea kukiimarisha Kituo chake cha Jimolojia Tanzania (TGC)
ili kuweza kutoa wataalam wa kutosha katika tasnia hiyo ya uongezaji tthamani
madini.
No comments:
Post a Comment