Nuru Mwasampeta na Tito Mselem
Naibu Waziri wa Madini, Stansilaus
Nyongo jana tarehe 28 April, 2019 amepokea ujumbe ulioongozwa na Naibu Waziri
wa Maliasili wa Jamhuri ya Watu wa China waliofika kwa ajili ya kujadili maeneo
ya kushirikiana katika sekta ya madini baina ya nchi hizo mbili yaani Tanzania
na China.
Akizungumza wakati akifungua kikao cha
majadiliano baina ya nchi hizo mbili, Nyongo aliwahakikishia wageni hao kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mazingira mazuri ya kuwekeza nchini kupitia
sekta ya Madini na kuwataka kutosita kutembelea maeneo mbalimbali ili kujionea
fursa zilizopo na kuwekeza nchini Tanzania.
Nyongo amewadhihirishia wageni hao
uwepo wa sera na sheria zisizokandamiza
upande wowote baina ya wawekezaji, wananchi na Serikali na hivo kuzifanya pande
zote kunufaika na rasilimali na uwekezaji unaofanyika katika sekta ya madini.
Aidha, Nyongo amebainisha kuwa
ushirikiano baina ya Tanzania na China ni wa muda mrefu ikiwa ni takribani
miaka 50 na kufika kwa ujumbe huo kunabainisha wazi kuwa urafiki na ukaribu baina ya nchi hizo hauna
mashaka.
Akizungumza na waandishi wa Habari
mara baada ya mkutano huo, Nyongo alisema wataalamu kutoka China wamekuja
kuunganisha nguvu ya pamoja na watanzania ili kuweza kusaidiana katika kufanya
tafiti za kina katika kujua kiasi cha madini yaliyopo, namna nzuri ya kuvuna
madini hayo pamoja na namna ya kuyaongezea thamani madini yaliyopo nchini kabla
ya kuyasafirisha nje ya nchi.
Pia, Nyongo amebainisha kuwa China ipo
tayari kuleta wataalamu katika masuala ya madini watakaojikita katika kufanya
shughuli za uchimbaji wa madini.
Naibu Waziri Nyongo amebainisha kuwa ujio
wa ujumbe kutoka China utasaidia kuweka makubaliano ya pamoja baina ya Taasisi
ya Utafiti na Jiolojia Tanzania na Taasisi ya Jiolojia na utafiti ya nchini
China katika kusimamia masuala ya utafiti wa madini katika maeneo ambayo
hayajafikiwa.
Zaidi ya hayo Nyongo amewadhihirishia
wageni hao uwepo wa mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji yanayotokana na
uwepo wa sera na sheria zisizokandamiza upande wowote baina ya wawekezaji na
Serikali na kuwataka kutosita kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Taasisi ya Utafiti na Jiolojia nchini Bi Yourghbert Myumbilwa amesema
ushirikiano huo utaleta manufaa makubwa kwani uzoefu wa China katika masuala ya
utafiti ni mkubwa hivyo itawawezesha watumishi wa taasisi hiyo kupata uelewa
mkubwa katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumzia ujio wa ujumbe wake
nchini, Naibu Waziri wa Maliasili wa China Dkt. Zhong Ziran amesema ni kuweza
kujadili na kukubaliana juu ya maeneo ya kushirikiana baina ya Tanzania na
China kupitia maliasili madini inayopatikana nchini.
Ushirikiano huu baina ya Taasisi ya
Utafiti na Jiolojia nchini na Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia nchini China ni
matokeo ya kikao kilichofanyika mwezi Desemba, 2018 baina ya aliyekuwa Waziri
wa Madini, Angellah Kairuki na Waziri wa Maliasili wa China kilichofanyika katika
ofisi za Wizara ya Maliasili nchini China ambapo Mhe. Kairuki alishiriki
kongamano la uwekezaji lililofanyika
nchini humo na kuibua fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus
Nyongo (Mbele Kushoto) akiwa na Naibu Waziri wa Maliasili wa China Dkt, Zhong
Ziran (Kulia) pamoja na wajumbe walioambatana nao katika kikao kilichofanyika
katika ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. JK Nyerere Jana.