Wednesday, October 31, 2018

Biteko azitaka mamlaka za serikali kufanya kazi kwa pamoja


Na Nuru Mwasampeta,

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amezitaka halmashauri za wilaya kufanya kazi na wizara ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao kabla hazijasababisha madhara makubwa kwa jamii.

Aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki alipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani wilaya ya Mkuranga alipofika ili kukagua shughuli za uchimbaji wa mchanga unavyoendelea pamoja na kukagua namna ya ulipwaji wa mirabaha ya Serikali inavyofanyika.

Akizungumza katika kikao baina yake na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Hassan Sanga, Biteko alisema “Sisi ni wamoja hivyo tufanye kazi kwa pamoja, tunajifunza pamoja ili tuamue kwa pamoja”.
“Tunatamani mambo mengi yaishie huku chini lakini endapo kuna masuala yanahitaji msukumo wa wizara ninyi mtueleze” alisistiza Biteko.

Aidha, Biteko aliwataka viongozi wa wilaya ya Mkuranga kuhakikisha tozo zinazotozwa na halmashauri hiyo ziwe ni zile zinazokubalika kisheria ili kupunguza migogoro midogomidogo baina ya Serikali na wachimbaji lakini pia kuwasaidia wachimbaji ili waweze kukua na kuongeza kipato chao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga alibainisha uwepo wa utoaji wa leseni bila ofisi yake kushirikishwa na hivyo kuwawia ugumu pindi wanapotakiwa kuchukua hatua za kuzuia eneo husika kufanyika shughuli za uchimbaji. “Mchanga unachimbwa kiholela ukiuliza wanasema wanavibali kutoka wizara ya ardhi, madini lakini pia wana vibali kutoka Nemc, tunashindwa kuwachukulia hatua.

Akizungumzia suala hilo Biteko alisema, mmiliki yeyote wa leseni ya madini hatakiwi kuanza kazi pasipo kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ambaye atapaswa kukutambulisha katia ngazi zote mpaka katika uongozi wa kijiji leseni yako.

Aidha aibainisha kuwa maeneo ya jeshi, vyanzo vya maji, maeneo ya hifadhi hayaruhusiwi kutolewa leseni lakini pia aliwataka viongozi hao wa wilaya kusema maeneo wanayodhani hayapaswi kutolewa leseni na kwamba wizara itatii kwa kutokutoa leseni kwa maeneo hayo.

Pia alielezea mamlaka ya wilaya kuwa inauwezo wa kuomba leseni zote zilizoombwa kwa kipindi Fulani ili kujiridhisha kama maeneo hayo yanaweza endeleza shughuli za uchimbaji na kama ni vinginevyo leseni zinafutwa.

Pamoja na hayo, Biteko aliutaka uongozi wa wilaya kuwalea  wachimbaji na kuondokana na urasimu usiokuwa na sababu, “tuwahurumie watu, Urasimu usiokuwa na sababu sisi wizara ya madini tunasema hapana.” Alisema Biteko.

Biteko alitanaibisha kuwa, wawekezaji wanatumia pesa nyingi kuwekeza kwenye uchimbaji na wengine wana mikopo katika mabenki hawalali vizuri hivyo tuwasaidie ili waweze kufanya kazi zao kwa utulivu na kupata kile wanachotarajia.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga mara baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi katika wilaya hiyo kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya hiyo Filberto Hassan Sanga. 
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni alipokuwa akipita katika ofisi ya mwenyekiti wa kijiji cha Mwanandilati wilayani Mkuranga kunakofanyika shughuli za  uchimbaji wa mchanga.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akitembea kuelekea eneo ambako uchimbaji wa mchanga unafanyika.

Mmoja wa wamiliki wa leseni ya uchimbaji wa mchanga katika kijiji cha Mwanandilati akieleza jambo kwa Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (Hayupo pichani)

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wafanyakazi wa eneo la Mwanajilatu wanaojishughulisha na uchimbaji wa mchanga alipotembelea ili kukagua shuhguli za uchimbaji na mfumo wa ulipwaji wa mirabaha ya serikali kwa wachimbaji

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wafanyakazi wa eneo la Mwanadilatu wanaojishughulisha na uchimbaji wa mchanga alipotembelea ili kukagua shuhguli za uchimbaji na mfumo wa ulipwaji wa mirabaha ya serikali kwa wachimbaji

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wafanyakazi wa eneo la Mwanadilatu wanaojishughulisha na uchimbaji wa mchanga alipotembelea ili kukagua shuhguli za uchimbaji na mfumo wa ulipwaji wa mirabaha ya serikali kwa wachimbaji

Monday, October 29, 2018

Ujenzi wa Mgodi wa mfano Lwamgasa wafikia asilimia 80


Na Asteria Muhozya,

Wizara ya Madini imeanza kukutana na Kamati Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuanzia leo tarehe 29 Oktoba hadi Novemba 1, 2018.

Katika kikao cha leo Wizara imewasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

Akiwasilisha Taarifa kuhusu Ujenzi wa Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa,  Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini, Augustine Ollal amesema hadi kufikia mwezi Septemba,2018, kazi ya ujenzi wa mgodi na usimikaji wa mitambo ya uchenjuaji imekamilika kwa asilimia 80.

Kuhusu mradi wa One Stop Center, eneo la Mirerani, amesema uko kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi  na kuongeza kuwa,   jengo hilo litakapokamilika litakuwa na miundombinu  mbalimbali ikiwemo huduma za Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini, Uhifadhi wa madini kwa usalama  , Kodi na tozo mbalimbali ikiwemo ofisi za TRA, Huduma za kifedha, ikiwemo Benki na Ofisi za Benki kuu, Hud za tathmini na uthamini madini, Ofisi za Madini na Chumba maalum cha kufanyia minada ya madini.




Hotuba ya Waziri wa Madini Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb.), akizindua Kamati ya uhamasishaji uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia nchini


Mheshimiwa Stanslaus Nyongo (Mb.), Naibu Waziri, Wizara ya Madini;

Prof. Simon Msanjila, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini;

Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati;

Ndugu Ludovick Utouh, Mwenyekiti Kamati ya TEITI;

Wajumbe wa Kamati ya TEITI;

Sekretarieti ya TEITI;

Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote ninapenda kuanza kwa kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema kwa kutujaalia kukutana siku ya leo katika uzinduzi wa Kamati ya TEITI. Kamati ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi asilia nchini Tanzania kwa kipindi cha Oktoba 2016 – Oktoba 2019. Ninakushuru ndugu Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI kwa kunialika kujumuika nanyi katika tukio hili muhimu ambalo ni kielelezo na nyenzo ya kufanikisha kuboresha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji hapa nchini. Kama mnavyofahamu, mwaka 2009 Nchi yetu ilijiunga katika mpango wa kimataifa wa kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya Uchimbaji wa Rasilimali (Extractive Industries Transparency Initiative) lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha kwamba mapato yanayotakiwa kulipwa Serikalini kutoka Sekta ya uziduaji yanapatikana na kuwekwa wazi kwa wananchi. Msingi wa falsafa hii ya uwazi na uwajibikaji kwenye Sekta ya uziduaji umejikita kwenye Ibara ya 8 (1) (c) na Ibara 27 (1) & (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Ibara hizi zinazungumzia Serikali kuwajibika kwa wananchi wake na kwamba rasilimali zote za nchi zitatunzwa na wananchi wote kwa manufaa ya wote. Aidha, Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania ya mwaka 2015 nayo imeweka msingi imara wa kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji kwenye Sekta ya uziduaji Nchini. Hivyo, Kamati hii ninayoizindua leo hii ina umuhimu mkubwa kwa mustakabali ya maendeleo ya Taifa letu iwapo mtatekeleza majukumu yenu kwa weledi, uzalendo na kwa kuipenda nchi yenu. Ni matarajio yangu na matarajio ya kila mwenye kuitakia mema Nchi yetu, mnakwenda kutekeleza wajibu wenu ipasavyo kwa maslahi mapana ya Nchi yenu kwani Taifa limewaamini hivyo msiliangushe.

Ndugu Mwenyekiti na ndugu Wajumbe wa Kamati, Itakumbukwa kuwa, tangu TEITI ianzishwe Mwaka 2009 hii ni Kamati ya tatu. Kamati mbili za awali ziliongozwa na Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mark Bomani. Ninayo faraja kubwa ya kuishuhudia siku hii na kushiriki tukio la leo nikiwa Waziri wa Madini. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua mimi kwenye wadhifa huu na kwa kukuteua wewe Bw. Ludovick Utouh Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Mstaafu) kuiongoza Kamati ya tatu ya TEITI. Maamuzi ya Mheshimiwa Rais kumteua Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI ni maamuzi ya kimapinduzi katika kuboresha usimamizi wa rasilimali nchini ilizo nazo katika Sekta ya uziduaji na kuhakikisha kuwa manufaa yanayopatikana kutokana na rasilimali hizi yananufaisha Watanzania wote na kuleta maendeleo kwa nchi. Uteuzi wa Mwenyekiti umezingatia uwezo wake wa uongozi na kubeba dhamana hii kwa kushirikiana na wajumbe kumi na tano kutoka Serikalini, Kampuni za madini, mafuta na gesi asilia na Taasisi za Kiraia. Ni matumaini yangu utaendeleza kazi nzuri ulizokwishafanya huko nyuma katika kuiongoza Kamati hii. Aidha, kwa upande wenu wajumbe wa Kamati hii mlioteuliwa, tunaamini mnao uwezo na weledi wa kuifanya kazi hii. Vile vile tunaamini mna nafasi kubwa ya kuisaidia Serikali katika agenda yake ya kuboresha Sekta hii muhimu kwa kuainisha njia za kuboresha usimamizi wa Sekta ya uzuduaji, kuvutia wawekezaji, kuongeza pato la Taifa na kujenga imani kwa wadau wa sekta hii. Katekelezeni majukumu yenu kwa maslahi ya Nchi yenu.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, Nataka mtambue kuwa ninyi ndiyo wasimamizi wa kuhakikisha kuwa Serikali inaboresha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa Sekta ya uziduaji hususan kwenye utoaji wa leseni na mikataba; usimamizi na uendeshaji wa kampuni; ukusanyaji wa mapato; na mgawanyo wa mapato na matumizi. Vile vile, mtambue kuwa mmepewa mamlaka makubwa na mmeaminiwa kulinda maslahi ya Nchi yenu kwa kusimamia Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania ya mwaka 2015 na vigezo vya Kimataifa vya Uwazi (Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) Requirements).

Ndugu Mwenyekiti na ndugu Wajumbe wa Kamati, Sote ni mashahidi wa jinsi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilivyo na dhamira ya dhati kuona kwamba Sekta ya uziduaji inawanufaisha watanzania wote kwa kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato yake stahiki na wananchi wanashiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za Nchi yao. Napenda kuwakumbusha kuwa Serikali na wananchi wake wana matarajio makubwa kwenu kuwa mtahakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi ili kuzuia na kupunguza udanganyifu na ukwepaji wa ulipaji wa kodi kulingana na sheria za nchi yetu ili hatimaye vizazi vijavyo vinufaike na utajiri huu wa rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia za madini, mafuta na gesi asilia. Ni imani yangu na pia ni imani ya Mheshimiwa Rais kuwa kupitia uongozi wa Bw. Ludovick Utouh katika Kamati hii mtaibadilisha TEITI ile ya toka 2009 ambayo haijulikani kwa wananchi walio wengi na kuwa TEITI ambayo inajulikana na kila Mtanzania. Taasisi hii ina umuhimu wa kipekee katika kuliwezesha Taifa kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati kwa kupitia viwanda ifikapo Mwaka 2025. Ili Serikali iweze kufikia lengo hili, ni lazima jitihada ziongezwe katika kukusanya mapato ya Serikali na kuyatumia mapato hayo kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kulingana na bajeti zilizoidhinishwa.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, Kamati hii ipo kisheria kulingana na Kifungu cha 10 cha Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilimia ya Mwaka 2015. Kamati itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mapato ya Sekta ya uziduaji yanayopaswa kuwasilishwa Serikalini, yanahakikiwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote.
Majukumu mengine ya Kamati yatakuwa ni pamoja na:-
(i)        kuandaa mfumo wa uwekaji uwazi na uwepo wa uwajibikaji wa malipo yaliyofanywa na kampuni za uziduaji Serikalini;

(ii)      kuzitaka kampuni zote za uziduaji na taasisi za Serikali zinazoshughulika na uziduaji kutoa taarifa sahihi juu ya malipo na mapato yaliyokusanywa na taasisi hizo katika mwaka husika wa fedha;

(iii)    kuzitaka kampuni za uziduaji kuwasilisha kwenye Kamati gharama za uwekezaji, takwimu za uzalishaji na mauzo ya nje katika mwaka husika wa fedha;
(iv)     kuhamasisha ufahamu juu ya mchango wa Sekta ya uziduaji na maendeleo yake kiuchumi na kijamii pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika katika Sekta ya uziduaji; na

(v)       kusababisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya uchunguzi wa tofauti ya hesabu za malipo na mapato yanayotokana na Sekta ya uziduaji kulingana na vifungu vya sheria hii.

Ndugu wajumbe, Baada ya uteuzi wa Bw. Utouh nilishakuwa na mazungumzo naye kuhusu changamato na matatizo yanayoikumba Sekretarieti ya TEITI. Nilifurahishwa sana Mwenyekiti aliponipa taarifa ya mabadiliko ya msimamo wa EITI Makao Makuu yaliyo Oslo nchini Norway, kuwa mahusiano ya kikazi yamerejeshwa kati ya Ofisi hiyo na Ofisi yetu. Sisi Wizarani tunawaahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano mtakaouhitaji. Tutafanya hivyo maana sote tunajenga nyumba moja. Milango yangu iko wazi wakati wote. Karibuni sana.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Kwa hakika mna kazi kubwa mbele yenu. Ninafahamu kwamba ili muweze kutekeleza majukumu yenu kama yalivyoelezwa kwenye kifungu cha 10(1)(2) cha Sheria ya TEITI ya Mwaka 2015, mnahitaji rasilimali watu na vitendea kazi. Ninafahamu kuwa kazi za kila siku za Kamati yako zinatekelezwa na Sekretarieti ya TEITI. Naomba kuwafahamisha kuwa tumeanza kushughulika changamoto mbalimbali zinazofanya msitekeleze majukumu yenu ipasavyo. Kwa mfano mchakato wa uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti umefikia hatua nzuri. Hivyo, ninaomba muwe na subira wakati tukishughulikia changamoto hizo. Kwa sasa, endeleeni kuwatumia watumishi wa tuliowaweka kwenye Sekretarieti kutekeleza majukumu yenu. Mambo yatakuwa sawa siku siyo nyingi. Katibu Mkuu wa Madini yupo hapa, ninamuelekeza afuatilie Muundo wa TEITI ukamilike haraka iwezekanavyo kuwezesha uwepo wa kuajiri watumishi wa Sektretarieti kuendana na mahitaji. Pia, ili Kamati iweze kutekeleza vyema majukumu yake, ninamkabidhi Mwenyekiti kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati vitendea kazi kwa ajili ya rejea ambavyo ni Taarifa ya nane ya TEITI, Taarifa ya uwekaji wazi wa majina ya watu wanaomiliki hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia hapa nchini, Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Sheria ya Madini, Sheria ya Mafuta, Sheria ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi na EITI Standards 2016. Katika kupitia taarifa ya nane ya TEITI, mtaona mapungufu mengi yaliyoibuliwa na Mtaalam Elekezi aliyetayarisha ripoti hiyo ambapo ni jukumu lenu kutafuta majibu na suluhisho ya matatizo hayo.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Kulingana na matakwa ya Kifungu cha 10 (1) na (2) cha Sheria ya TEITI ya Mwaka 2015, majukumu yenu ni mengi na mazito. Hata hivyo, bado Kifungu 10 (3) cha Sheria hiyo, kinaitaka Kamati iandae na kuwasilisha kwangu, ripoti ya utekelezaji wa shughuli zote zilizotajwa katika kifungu kidogo cha (2) kwa ajili ya hatua stahiki katika kuboresha usimamizi wa Sekta ya uziduaji hapa nchini. Hivyo Mwenyekiti, nitakuwa nategemea kuipata mapema ripoti tajwa kwa ajili ya kuifanyia kazi.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Mwisho, Wizara inawatakia utekelezaji mwema wa majukumu yenu na kwa mara nyingine tena mimi na wenzangu Wizarani tunawaahidi kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yenu.

Baada ya kusema hayo, napenda sasa kutamka kuwa Kamati ya tatu ya TEITI nimeizindua Rasmi leo tarehe 25 Oktoba, 2018.

Asanteni kwa kunisikiliza.


Hotuba ya Waziri wa Madini Mheshimiwa Angellah J. Kairuki (Mb.) akifungua jukwaa la sekta ya uziduaji Tanzania, lililoandaliwa na hakirasilimali


HOTUBA YA WAZIRI WA MADINI MHESHIMIWA ANGELLAH J. KAIRUKI (MB.) AKIFUNGUA JUKWAA LA SEKTA YA UZIDUAJI TANZANIA, LILILOANDALIWA NA HAKIRASILIMALI - MTANDAO WA ASASI ZA KIRAIA UNAOFANYA KAZI ZA UCHECHEMUZI KATIKA SEKTA YA UZIDUAJI HAPA TANZANIA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HOTELI YA AFRICAN DREAMS, DODOMA
TAREHE 24 OKTOBA 2018

Waandaaji wa Jukwaa la Sekta ya Uziduaji Tanzania 2018;

Watoa mada kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania;

Wawakilishi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha;

Madhehebu ya Dini (BAKWATA, CCT and TEC);

Wawakilishi wa Mashirika ya Vyama na Asasi za Kijamii;

Washirika wa Kimaendeleo;

Waandishi wa Habari;

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Habarini za asubuhi na Karibuni katika Jiji la Dodoma.

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana siku ya leo katika ufunguzi wa Jukwaa la Sekta ya Uziduaji Tanzania ambalo limewaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka nyanja zote ndani na nje ya Tanzania, kwa kusudi la kujadili, kujifunza na kushirikishana uzoefu katika utetezi na ushawishi wa michakato ya maamuzi yatokanayo na sekta ya uziduaji ili kuleta maendeleo endelevu yanayotarajiwa na sekta hii kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla. Jukwaa hili limeandaliwa wakati muafaka kwani katika kipindi hiki, tumefanya mageuzi makubwa nchini na tunaendelea na mageuzi mbalimbali lengo ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na hivyo kulazimika kuweka mkazo katika kuihuisha sekta ya uziduaji na ajenda ya viwanda kwa ifikapo mwaka 2025.

Ndugu Washiriki, Usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ni chachu ya maendeleo ya Tanzania. Mabadiliko ya Sera, Sheria, Taratibu na Kanuni yamefanyika kuinua uzalendo, kurudisha uhuru wa umiliki na usimamizi wa rasilimali za nchi.

Ndugu Washiriki, Nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuonesha uzalendo katika kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya watanzania. Hii imejidhihirisha kupitia Serikali kuendesha majadiliano na kampuni za uchimbaji madini ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kupitia rasilimali zake lakini pia kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.

Sekta ya uziduaji nchini inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu, hususan kutokana na ongezeko kubwa la uwekezaji. Hivyo, upo umuhimu wa kuendelea kupanua wigo wa majadiliano na kusimamia rasilimali kwani kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasisitiza mara kwa mara kuwa uzoefu katika nchi nyingine unaonesha rasilimali hizi zinaweza kugeuka na kuwa laana itakayoharibu na kudunisha matokeo ya maendeleo na kuleta umasikini mkubwa.

Ndugu Washiriki, Ni muhimu kwa Tanzania kuweka zana thabiti ili kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na usimamizi endelevu wa sekta za madini, mafuta na gesi asilia. Hii inajumuisha kuwepo kwa ufanisi wa ushirikishwaji wa wadau kutoka nyanja mbalimbali zikiwemo ASASI ZA KIRAIA.

Sisi kama Serikali, kupitia Wizara zote mbili ya Madini na ya Nishati, jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kusimamia utendaji kazi kwenye sekta ya uziduaji kwa kuzingatia kikamilifu utekelezaji wa Sera, Sheria na mahitaji ya udhibiti wa kitaifa na kimataifa. Lakini pia, kuendelea kushirikiana na wadau ili kuweza kuishauri Serikali njia sahihi zitakazoiwezesha Nchi kunufaika na rasilimali hizi. Mbali na hayo, kuwa na jitihada za kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia na makundi maalum yanapata fursa kushiriki kikamilifu katika Sekta ya uziduaji.

Ndugu Washiriki, Kwa upande wa Wizara ya Madini, katika suala hili la usimamizi wa rasilimali za nchi na hususan katika Sekta ya Madini ninayoisimamia, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Spika wa Bunge la Tanzania kwa kuunda Kamati ambazo zilishughulikia changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini. Mapendekezo ya Kamati zote yamefanyiwa kazi na baadhi ya mapendekezo mengine yanaendelea kutekelezwa.

Hata hivyo, Wizara yangu imeweka vipaumbele vifuatavyo ili kuhakikisha sekta hii ya madini inaimarika na inanufaisha Watanzania wote:

(i)  Kuwa na uwazi na uwajibikaji zaidi katika Sekta ya Madini na uziduaji kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini. Tuna uhakika wa kufanikisha lengo hili kwa kuwa tuna mikakati madhubuti ya  kuimarisha ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na ya uchimbaji mdogo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji, uzalishaji, mauzo na kodi mbalimbali; kudhibiti utoroshwaji wa madini katika maeneo ya uzalishaji na ya kutokea nchini (Exit Points); kuimarisha ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwandani; kufuatilia taarifa za ununuzi na uuzaji (returns) kwa wafanyabiashara wa madini (Dealers & Brokers); kufuatilia wadaiwa wa tozo mbalimbali za madini kwa mujibu wa Sheria kwa wakati; kudhibiti uchimbaji na uchenjuaji haramu wa madini; na kuboresha na kuimarisha mfumo wa utoaji wa leseni za madini na kutunza taarifa zake.

(ii)  Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo na wa Kati wa Madini. Katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanaendelea kutoka hatua waliopo sasa na kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wachimbaji wakubwa, Wizara imetenga jumla ya maeneo 4 nchini kwa ajili ya wachimbaji wadogo na tutaendelea kutenga maeneo hayo kabla ya kugaiwa kwa wachimbaji wadogo yatabainishwa uwepo wa mashapo ya madini na Taasisi yetu ya GST ya utafiti wa madini ili kuepusha kufanya uchambuzi kwa kubahatisha. Vilevile, Wizara ya Madini kupitia STAMICO, itawaelimisha wachimbaji wadogo namna ya kutumia teknolojia ya kisasa na rahisi katika kuongeza uzalishaji na tija wakati wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Aidha, Wizara ipo katika hatua nzuri ya kukamilisha ujenzi wa Vituo 7 vya Mfano (Centres of Excellency) kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini, uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo na Serikali. Vile vile, katika vituo hivi tutatoa Huduma za uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu. Lwamgasa ambao ni mgodi wa mfano, mwisho wa mwaka huu utakamilika.

(iii)  Kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini. Katika eneo hili, Wizara imejiwekea mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali. Hadi sasa, Wizara kupitia Tume ya Madini imeshatoa leseni kadhaa za uchenjuaji, na katika hili nawasihi wananchi wenye vigezo kulingana na Sheria waombe leseni hizo. Aidha, Wizara inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa inapata wawekezaji mahiri na wenye sifa stahiki katika Vinu vya uchenjuaji na usafishaji wa madini. Ili kufanikisha suala hili la uongezaji thamani madini, Wizara yangu imekwishaanza taratibu za kuandaa Muswada wa Sheria ya Uongezaji Thamani Madini kwa lengo la kukuza na kusimamia vyema shughuli za uongezaji thamani madini nchini.

(iv)   Kuimarisha Ukaguzi wa Usalama, Afya, Mazingira na Uzalishaji wa Madini Migodini. Kama inavyoeleweka, shughuli za uchimbaji wa madini huweza kuambatana na athari za kiafya, usalama na uharibifu mkubwa wa mazingira. Ili kuondokana na athari hizo, Wizara imeimarisha kaguzi migodini na maeneo ya uchenjuaji wa madini, kuongeza huduma za ugani hususan kwa wachimbaji wadogo, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na usimamizi wa masuala ya Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Minamata wa kupunguza na hatimaye kuzuia matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji. Kwa kuwa usalama migodini ni muhimu sana; natoa rai kwa wachimbaji wa madini na wale wanaofanya shughuli za uchenjuaji hususan madini ya dhahabu kuhakikisha wanaimarisha miundombinu ya mabwawa ya kuhifadhi mabaki yenye kemikali (Tailings Storage Facility – TSF) kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2017.

(v)   Kuelimisha Umma na kuboresha Mawasiliano baina ya Wizara na Wadau wa Sekta ya Madini. Wizara yangu imeweka mikakati ya kuhakikisha inafanya mikutano ya ana kwa ana na wawekezaji na kutoa elimu kwa Umma kuhusu rasilimali madini. Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya kina kuhusu masuala ya rasilimali madini. Kuhusu hili, ninyi wote ni shahidi wa kazi kubwa inayofanywa na mimi mwenyewe, Manaibu wangu na Tume ya Madini ya kukutana na kutembelea wananchi wanaofanya shughuli za madini na kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria za Nchi. Aidha, Wizara yangu inaahidi kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu rasilimali madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia vipindi mbalimbali vya redio na televisheni na njia nyingi za uelimishaji Umma.

Ndugu Washiriki, Natoa wito kwa wadau wote watumie majukwaa mbalimbali kama hili kama njia mojawapo ya kuboresha mazungumzo na mijadala ya namna gani tunaweza kunufaika na utajiri wa rasilimali iliyopo katika sekta ya uziduaji ili kuinua uchumi, kupunguza umaskini na kukabiliana na laana inayoweza kujitokeza kwenye rasilimali hizi.

Ndugu Washiriki, Kwenye Kongamano hili, nimefurahishwa na uwepo wa watu kutoka nyanja mbalimbali na mashirika yaliyowakilishwa hapa yakiwemo makampuni, mitandao ya asasi za kijamii, makundi ya madhehebu ya Imani, watafiti, wasomi, jamii, washirika wa maendeleo na viongozi wa mashirika na taasisi za kiserikali. Tunathamini michango yenu katika sekta hii na kujitoa kwenu katika mijadala ndani ya kongamano hili kutatusaidia sana kuimarisha sekta hii. Jadilianeni na badilishaneni mawazo mliyo nayo na hatimaye ibukeni na mawazo mapya ya kuboresha na kuimarisha sekta ya uziduaji nchini. Nitapenda pia kupata maazimio na mapendekezo mtakayoyafikia.

Ndugu Washiriki, Napenda nitumie fursa hii kuzihakikishia Asasi zote za Kiraia kwamba Serikali inathamini mchango wenu katika Sekta ya Madini na Sekta ya Uziduaji kwa ujumla na kuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa Sheria na Kanuni mpya za Madini. Nitumie fursa hii pia kukaribisha wananchi wote ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini katika sekta ya madini. Nimefarijika sana kuona Asasi za Kiraia zinatoa ushirikiano kwa Serikali katika usimamizi wa rasilimali zetu kwa kuhakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha wananchi bila ubaguzi wowote. Hii inathibitisha kwamba ushirikiano baina ya wadau mbalimbali, Serikali, Wawekezaji na CSOs katika Sekta ya Uziduaji ni jambo la msingi na lenye manufaa kwa Serikali na Wananchi wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo nchini. Nipende tu kuzihakikishia Asasi za Kiraia kuwa milango yetu Wizarani iko wazi kwa kupokea ushauri na maoni yenye lengo la kuboresha na kuimarisha Sekta hii muhimu. 

Ndugu Washiriki, Kwa mara nyingine tena nawashukuru kwa kunialika katika ufunguzi wa mkutano huu muhimu na nawakaribisha katika Jiji la Dodoma hususan Wizara ya Madini kwa ajili kuwekeza katika Sekta hii. Baada ya kusema maneno haya machache natangaza kwamba Jukwaa la Sekta ya Uziduaji Tanzania limefunguliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza

FEMATA kuimarisha sekta ya madini kupitia kodi


Na Greyson Mwase, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa  Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa  Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Haroun Kinega amesema kuwa, shirikisho hilo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Madini limeweka mikakati katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Kinega ameyasema hayo leo tarehe 29 Oktoba, 2018 katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa FEMATA Nchini uliofanyika jijini Dodoma wenye lengo la kuchagua viongozi wapya pamoja na kujadili changemoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini.

Akielezea mikakati ya ongezeko la mapato kutokana na kodi zinazolipwa na wachimbaji wadogo wa madini, Kinega alisema kuwa FEMATA kwa kushirikiana na Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha maeneo zaidi yanatengwa na kutolewa leseni kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kuwataka wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi, kusajili ili kuomba leseni na uchimbaji wao kuwa rasmi.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa asilimia kubwa ya wachimbaji wadogo wa madini nchini wanakuwa rasmi kwa kupatiwa leseni za madini ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali, ninaamini tunaweza kufikia lengo kupitia mikakati tuliyojiwekea.

Wakati huo huo akielezea mikakati ya Serikali katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini,  Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma,  Jonas Mwano alisema kuwa mbali na Serikali kupitia Wizara ya Madini kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini, elimu imekuwa ikitolewa kwa wachimbaji wadogo kuhusu sheria na kanuni za uchimbaji wa madini pamoja na usalama migodini.

Alisema kuwa elimu ambayo imekuwa ikitolewa kwa  wachimbaji wadogo wa madini imepunguza kwa kiasi kikubwa migogoro iliyokuwa ikijitokeza kwenye maeneo yao ya uchimbaji wa madini.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa  Madini Nchini (FEMATA), John Bina mbali na kupongeza juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Madini  aliiomba Serikali kuhamasisha wawekezaji kutoka nje kwa ajili ya kujenga mitambo ya kuchenjulia madini nchini na kukuza pato la taifa.

Katika uchaguzi huo wa viongozi wa FEMATA nafasi zinazogombewa ni pamoja na Rais, Makamu wa Rais,  Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Mweka Hazina Msaidizi, Mwakilishi  wa Wanawake na Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Dhahabu.

Nafasi nyingine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Nishati, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Viwanda, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Chumvi, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Tanzanite, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Almas, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini Mengine ya Vito na  Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Usuluhishi na Kanuni.

Aidha, Nafasi nyingine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mjumbe wa Afya, Mazingira na Usalama Migodini, Mwakilishi wa Wafanyabiashara, Mwakilishi wa Wachimbaji Wasio Rasmi, Mjumbe wa Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Gesi na Mafuta (TEITI) na Bodi ya Wadhamini nafasi tano.


Mtendaji Mkuu wa  Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa  Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Haroun Kinega (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA) uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2017 

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA), John Bina akielezea mafanikio ya shirikisho hilo mbele ya wawakilishi wa vyama vya wachimbaji wadogo wa madini mikoani (hawapo pichani) 

Sehemu ya wawakilishi wa vyama vya wachimbaji wadogo wa madini mikoani wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA), John Bina (hayupo pichani) 

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia) akielezea mikakati ya Serikali kwenye uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini kwa waandishi wa habari. 

Sehemu ya wajumbe wa meza kuu wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Mtendaji Mkuu wa  Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa  Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Haroun Kinega (hayupo pichani)

Monday, October 22, 2018

Naibu Waziri Nyongo afanya ziara katika Migodi ya makaa ya mawe ya Kabulo na Kiwira


Na Greyson Mwase,

Tarehe 19 Oktoba, 2018 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alifanya ziara katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo (Kabulo Coal Mine) uliopo katika eneo la Kabulo lililopo katika wilaya Songwe mkoani Songwe na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira (Kiwira Coal Mine) iliopo katika Wilaya ya Ileje mkoani Mbeya. Mara baada ya kufanya ziara katika migodi husika, alizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Akizungumza katika mkutano wa wafanyakazi alisema kuwa, kwa sasa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya kutoka Kabulo hadi Kiwira itakayotumika kwa ajili ya usafirishaji wa makaa ya mawe pamoja na kuhakikisha inalipa stahili za wafanyakazi mara baada ya taratibu kukamilika. Katika hatua nyingine, Nyongo aliwataka watumishi kufanya kazi kwa ubunifu na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri.

Wafanyakazi wa Mgodi wa Kiwira walimpongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kazi kubwa ya kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini nchini pamoja na Taasisi zilizopo chini ya Wizara.


Meneja Migodi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Alphonce  Bikulamchi (katikati) akielezea shughuli za uchimbaji  wa makaa ya mawe zinavyofanyika katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo uliopo katika mkoa wa Songwe kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) 

Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira uliopo katika wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya,  Samwel Kibaranga (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto) reli inayotumika kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe (haionekani pichani) 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto mbele) akitoa maelekezo katika eneo la Mgodi wa Mkaa ya Mawe wa Kiwira 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tano kushoto mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira mara baada ya kumalizika kwa mkutano