Tuesday, July 31, 2018

Nyongo aiagiza TRA kuchunguza Kiwanda cha Goodwill katika ulipaji wa mrabaha serikalini


Na Zuena Msuya, Pwani

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na maafisa madini nchini( TRA) kuchunguza na fuatilia kiwanda cha Goodwill  namna ya ulipaji wake  wa  mrabaha na tozo mbalimbali  serikalini kutokana na aina mbalimbali ya madini wanayotumia yakiwemo Kaolin katika uzalishaji wa bidhaa zake.

Madini ya Kaolin hutumika kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwepo Malumalu( Tiles), rangi za nyumba, karatasi, n.k.

Nyongo alitoa agizo hilo alipotembelea kiwanda hicho cha Goodwill  wakati akihitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi katika  ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Julai 26, 2018 ambapo katika ziara hiyo alipata fursa ya kutembelea maeneo ya uchimbaji chumvi na katika kiwanda cha kutengeneza chimvi aina ya NEEL.

Nyongo alieleza kuwa , mara baada ya kutembelea kiwanda hicho, hakuridhishwa na majawabu aliyokuwa akipewa na uongozi wa kiwanda hicho juu ya mahesabu ya manunuzi ya madini kaolin, matumizi ya madini hayo katika uzalishaji wa bidhaa zake, pamoja na uwazi wa ulipaji wa mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini, tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho mwezi April mwaka jana.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa bei elekezi ya serikali katika uuzaji wa madini ya ujenzi,hasa mchanga ni shilingi elfu kumi( 10,000) kwa tani.
Aidha, Nyongo alishangazwa na bei ya madini ya Kaolin yanayotengeneza malumalu( tiles) kuwa ni shilingi elfu  tatu (3,000) kwa tani na mrabaha unaolipwa ni  3% ya bei kitu ambacho si sahihi, na baada ya kupiga hesabu za haraka waligundua kuwa, tani moja ya Kaolin ilipaswa kuuzwa shilingi 35,000, hivyo  serikali ingepata mrabaha wa shilingi 1,500  kutokana na ile 3% , tofauti na ilivyo sasa serikali inapata mrabaha wa shilingi Tisini (90) katika kila tani ya kaolin inayouzwa, kitu alichosema kuwa ni wizi.

Kutokana mkanganyiko huo aliwaagiza  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwenda kufanya mahesabu katika kiwanda cha Goodwill ili kufahamu wanunua au waandika  shilingi ngapi kwa tani ikiwa ni gharama za uzalishaji wa malumalu ( tiles),ili ikifahamika bei halisi ya tani moja, Wizara ya Madini itaanza kutoza mrabaha wa 3% katika kila mahesabu waliokuwa wakiyapeleka TRA.

" unaweza kukuta wamepeleka mahesabu makubwa TRA, lakini katika uchimbaji waandika wamenunua shilingi elfu 3 (3000) hii haiingii akilini kabisa, kila mtanzania anajua Malumalu( tiles) zinauzwa kwa bei juu sana na wakati mwingine watu wanaagiza kutoka nje kupunguza gharama, halafu madini ya kaolin ambayo ni malighafi muhimu katika kuzitengeza malumalu hizo yanauzwa shilingi elfu tatu kwa tani , huo ni wizi mkubwa na haiwezekani", alisisitiza Nyongo.

Alisisitiza kuwa endapo kiwanda hicho kitagundulika kukwepa kodi, kitalazimika kulipa fedha zote ambazo zimepotea katika kipindi chote cha uzalishaji na endapo watashindwa kufanya hivyo,sheria itachukuwa mkondo wake.

Tangu kiwanda hicho kianzishwe mwezi April mwaka jana hadi sasa, kumbukumbu zinaonyesha kuwa wametumia tani elfu sabini( 70,000) za madini ya Kaolin, kwa gharama ya shilingi milioni 6 na laki tatu,      (6,300,000) tu, ila kwa bei haraka iliyopigwa pale na wataalam inaonyesha kuwa zaidi ya shilingi milioni sabini ( 70,000,000,) zimepotea , hivyo wataalamu wa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na TRA  wameagizwa kufuatilia jambo hilo kwa haraka na umakini mkubwa ili kuipatia serikali mapato stahiki.

Katika hatua nyingine, Nyongo alipiga marufuku uchimbaji wa mchanga na vifusi katika jiji la Dar es salaam, na kuwaagiza wachimbaji kwenda katika maeneo yalioanishwa katika Mkoa wa Pwani.

Alisisitiza kuwa Mkoa wa Pwani unamaeneo mengi yenye madini ya ujenzi ambayo yakichimbwa yanatosheleza majitaji ya mchanga na kokoto katika jiji la dar es salaam na mikoa mingine, hivyo wachimbaji wazingatie sheria za uchimbaji madini hayo.

Sambamba na hilo aliwaagiza Wakuu wa Wilaya zote wenye maeneo ya uchimbaji wa madini ujenzi pamoja na chumvi, kukamata wafanyabiashara na wachimbaji wa madini hayo wnaofanya kazi hiyo bila kufuata sheria ya madini ikiwemo kutosha madini hayo na kukwepa kulipa mrabaha na tozo mbalimbali serikalini na katika halmashauri.

Vilevile, alisema kuwa kila lori litakalokuwa limepakia madini mchanga lazima liwe na stakabadhi ya vocha inayoonyesha kuwa madini hayo yamelipiwa stahili zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria ya madini.

Pia aliwaagiza maafisa madini kuangalia utaratibu bora utakaofaa kutumika katika kulipa tozo mbalimbali pamoja na mrabaha ikiwezekana zilipwe kwa mfumo wa kieletroniki ili kukwepa wafanyabiashara wasio waaminifu.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, akiwa katika kiwanda cha goodwill. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akikagua chumvi iliyovunwa tayari kupelekwa kiwandani. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo,(katikati) akipata maelezo alipotembelea kiwanda cha kuzalisha chumvi katika wilaya ya Mkuranga.  

Thursday, July 26, 2018

Shughuli za uchimbaji madini ya Kaolin zasimamishwa mgodi RAK Kaolin


Na Zuena Msuya, Pwani

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amesimamisha shughuli za uchimbaji madini ya Kaolin katika mgodi unaomilikiwa na kampuni ya RAK Kaolin hadi pale wahusika watakapoeleza thamani halisi ya bei ya madini hayo yanayouzwa na kutumika viwandani, leseni ya mgodi, uchimbaji pamoja na umiliki ardhi.

Pia, alimtaka mmiliki wa leseni ya mgodi huo kuwasilisha wizara ya madini nakala ya mkataba walioingia kati yake na wachimbaji wa madini hayo katika mgodi huo, na namna ambavyo aliweza kumiliki eneo husika.

Nyongo alisimamisha shughuli za uchimbaji katika mgodi huo ulipo katika Kijiji cha Kimani wilayani Kisarawe mkoani Pwani, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini ya ujenzi Julai 25,2018.

Akizungumzia uamuzi wa kufunga mgodi huo ambao baadhi ya viwanda hutumia madini hayo kutengeneza bidhaa mbalimbali, Nyongo alisema kuwa, haridhishwi na shughuli za uchimbaji zinazofanya katika mgodi huo ikiwepo suala la umiliki wa ardhi, leseni ya mgodi, uchimbaji pamoja na biashara ya madini hayo viwandani.

Alifafanua zaidi kuwa, shughuli za uchimbaji na biashara ya madini katika mgodi huo hazionyeshi wazi taratibu wa ulipaji serikalini, mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho 2017.

“Shughuli za uchimbaji wa madini hapa nchini ni lazima ziwanufaishe watanzania na taifa kwa ujumla kwa kuwawekea mazingira mazuri wamiliki wa ardhi, wamiliki wa leseni pamoja na wachimbaji na siyo kuwanyonya, pia kulipa mrabaha na tozo mbalimbali kwa lengo la kuongeza mapato serikalini, sasa mgodi huu taarifa zake zinakinzana licha yakuwawepo kwa muwekezaji kufanya shughuli za uchimbaji na kuendelea na biashara ya madini,” alisisita Nyongo.

Aidha, aliiagiza ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kushirikiana na maafisa madini kufuatilia maeneo yote yenye madini ya Kaolin na kuhakiki leseni zilizopo pamoja na uhalali wake ili kufahamu idadi ya zilizokuwa hai na zilizomaliza muda wake.

Pamoja na mmbo mengine, aliendelea kusisitiza kuwa serikali itayafutia leseni zote sizoendelezwa na kuwa maeno hao wale wenye nia ya kuendeleza maeneo hayo kwa shughuli za uchimbaji madini.

Sambamba na hilo kuwataka wachimbaji na wamiliki wa migodi na wafanyabiashara ya madini kulipa mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 na kufanyiwa marekebisho 2017 pamoja na kushiriki shughuli za kimaendeleo na kijamii katika maeneo yanayowazunguka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happyness Seneda alimuhakikishia Naibu Waziri Nyongo kuwa, kwa kushirikiana na Wizara ya Madini,anaimani mapato yote yaliyokuwa yakipotea sasa yataingia serikalini.

Seneda aliwaonya wawekezaji uchwara, wamiliki wa leseni na wachimbaji wasiowaaminifu kuwa kuanzia sasa kuacha    kufanya udanganyifu au ujanja ujanja katika sekta ya madini baada ya sheria ya madini ya 2010 kufanyiwa marekebisho 2017, kwa lengo la kuifanya sekta hiyo kuwanufaisha watanzania na taifa kwa ujumla.

Mkoa wa Pwani hasa katika Wilaya ya Kisarawe unasifika zaidi kwa upatikanaji wa madini ya Kaolin yanayotumika viwandani kutengeza bidhaa mbalimbali zikiwepo,Malumalu (Tiles) zinazotumika katika shughuli za ujenzi, karatasi, rangi ya nyumba n.k.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akiongozana na mmoja wa wazee (katikati) katika kijiji cha Kimani wilayani Kisarawe baada ya kusimamisha shughuli za uchimbaji madini ya Kaolin katika mgodi unaomilikiwa na kampuni RAK Kaolin. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happyness Seneda.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia), akionyeshwa jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Happynes Seneda( wa pili kulia) wakati wakikagua migodi ya uchimbaji madini ya Kaolin wilayani humo.

Naibu Moja ya maeneo yaliyokuwa yakichimbwa madini ya Kaolin katika Wilaya ya Kisarawe ambayo uchimbaji wake umesimamishwa kutokana na kutofuata sheria ya uchimbaji wa madini

Wednesday, July 25, 2018

Serikali yasema wasioendeleza maeneo ya uchimbaji madini ujenzi kufutiwa leseni


Na Zuena Msuya, Pwani

Serikali imesema itazifutia leseni za umiliki kampuni zote na wamiliki wa ardhi walioomba leseni za uchimbaji madini ya ujenzi ikiwemo mchanga, kokoto pamoja na mawe kwa kushindwa kuendeleza maeneo hayo kwa lengo lililokusudiwa.

Kauli hiyo ilitolewa  na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus  Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua migodi ya uchimbaji wa madini ya ujenzi  yaliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani pamoja na kuzungumza na wakazi wa vijiji hivyo, Julai 24, 2018.

Nyongo alisema, kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi na kampuni mbalimbali zilizoomba  leseni za uchimbaji madini ya ujenzi katika maeneo tofauti nchini,miaka mingi iliyopita pasipo kuyaendeleza na hivyo kusababisha maeneo hayo kuwa vichaka na kuwazuia wengine  kuomba leseni  za uchimbaji na kuendeleza maeneo hayo.

Aidha, alitoa onyo na kuwataka  baadhi ya watu wasiowaaminifu kuacha mara moja tabia ya kuwahadaa wawekezaji wanaotaka kuomba leseni katika maneo ya uchimbaji kwa kuwaeleza kuwa wanamiliki leseni za maeneo hayo na kuwataka waingie nao ubia, jambo ambalo si kweli na kwamba tabia  hiyo inachafua dhana halisi ya uwekezaji nchini.

“Kuna mapori na maeneo mengi nchini yanayofaa katika uchimbaji wa madini ya ujenzi, lakini mtu akijitokeza kutaka kufanya kazi katika moja ya maeneo hayo anaalezwa kuwa eneo hilo linamilikiwa na mtu na linaleseni ya uchimbaji, lakini eneo hilo limeendelea kuwa pori au kichaka kwa miaka mingi, hili haikubaliki. Leseni za aina hiyo lazima zifutwe na tutazifuta hivi karibuni”, alisema Nyongo.

Sambamba na hilo, aliwaagiza maafisa madini wote kushirikiana na Serikali za Vijiji husika kukagua maeneo na leseni zote za uchimbaji madini hayo, kubaini zilizohalali na zisizohalali ili ziweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria ya madini.

Vilevile, aliwata baadhi ya wamiliki wa migodi ya uchimbaji madini ya mchanga, wenye tabia ya kutorosha madini hayo na kukwepa kulipa mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 na kufanyiwa Marekebisho 2017, kuacha mara moja tabia hiyo na kwamba sheria itachukuwa mkondo wake kwa yeyote atakayebainika.

"Nawaonya wale wote wenye tabia ya kuchimba madini ujenzi, kwa maana ya kokoto, mchanga, mawe kisha kuyatorosha na kukwepa kulipa mrabaha na tozo, pindi utakapokamatwa serikali haitavumilia uhalifu huo kwani unaipoteza mapato,tutakufutia leseni na kutaifisha vifaa vyako vyote", alisisitiza Nyongo.

Hata hivyo, aliwaagiza maafisa madini kuangalia uwezekano wa kubadilisha vocha za ulipaji mrabaha kuwa wa kieletroniki ili kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.

Akizungumzia suala la ulipuaji wa miamba, lililolalamikiwa na wananchi, Nyongo aliwashauri wamiliki wa migodi katika maeneo hayo, kuzungumza na wananchi wa maeneo husika ikiwezekana kuwalipa fidia ili wananchi hao waweze kuondoka katika maeneo hayo kuepuka  madhara yanayoweza kutokea.

Pia aliwashauri wananchi hao kuwa, endapo watakubalina na wawekezaji hao, kuridhia kile watakachokubaliana ili kuondoa migogoro na migongano ambayo hutokea mara kwa mara kati ya muwekezaji na wananchi mara baada ya kulipwa fidia ama vinginenyo.
Mwaka 2017, serikali kupitia Wizara ya Madini ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 8, ikiwa ni mrabaha pamoja na tozo mbalimbali zilizotokana na sekta ya madini pekee.

akiwa wilayani bagamoyo, nyongo alitembelea baadhi ya migodi ya uchimbaji madini ya mchanga ukiwepo wa Suma JKT uliyoingia ubia na kampuni ya uwekezaji kutoka nchini Uturuki, mgodi wa kampuni ya Ashraf, Mgodi wa kampuni ya uwekezaji ya Yaate ulioshinda tenda ya kuzalisha kokoto za aina zote zinazotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa( Standard Gauge)kutoka Dar es salaam hadi Dodoma, mgodi wa kampuni ya Tan-Turk, mgodi wa kampuni ya uwekezaji Even pamoja na mgodi wa kampuni ya Kerai.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus  Nyongo,( pili kulia) akiwa katika chumba cha mizani katika mgodi wa Suma JKT ulioingia ubia na kampuni ya uwekezaji ya Uturuki,kukagua zoezi la upimaji wa uzito kwa magari yanayobeba madini ujenzi kabla ya kutoka mgodini.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus  Nyongo( katikati) akitembelea Mgodi wa SumaJKT ulioingia ubia na kampuni ya uturuki. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus  Nyongo (wa pili kushoto)akipata maelezo juu ya uchimbaji na uzalishaji wa madini ya ujenzi kutoka kwa Meneja Mtendaji wa Kampuni ya uwekezaji ya Yaate,Mhandisi Eugen Mikongoti( katikati). 

Mmoja wa mtambo wa mgodi wa madini ujenzi wa kampuni ya ..... aliyoitembelea Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus  Nyongo wakati wa ziara yake wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus  Nyongo, akizungumza na wanakazi wa kijiji cha kinzagu kata ya msata wilayani bagamoyo mkoani Pwani alipofanya ziara katika migodi ya madini ujenzi iliyopo katika eneo hilo.

Waziri Kairuki aweka malengo ya uanzishwaji Soko Huria la Madini ifikapo Desemba, 2018

Na Asteria Muhozya

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema anatamani kuona ifikapo mwezi Disemba mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaanzisha Soko Huria la Madini nchini (Tanzania Mineral Exchange).

Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 24 Julai, 2018, wakati wa kikao cha Menejementi ya Wizara ya Madini na Taasisi zake ambapo Wataalam kutoka Kampuni ya Tanzania Mecantile Exchange PLC  (TMC) waliwasilisha mada juu ya Elimu ya Soko la Bidhaa Tanzania.

Aidha, Waziri Kairuki aliishukuru kampuni hiyo kwa kutoa wasilisho hilo ikiwemo utaalam wao katika masuala ya soko huria la madini na kuongeza kuwa, anatamani kuona suala hilo linafanikiwa na kufanyika mapema kwa kuwa, litawezesha Watanzania kumiliki uchumi wa madini hata wale wenye kipato cha chini.

“Natamani kuona ndani ya kipindi cha miezi sita vinavyowezekana kufanyika vinaanza kufanyika. Lakini tutazingatia sheria, taratibu na utalaam kuhakikisha kwamba suala hili linafanikiwa,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Akiwasilisha mada, Mtaalam mwelekezi kutoka kampuni hiyo, Girish Raipurie, alieleza faida za soko huria la madini kwa Tanzania, huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa kutolewa mafunzo kwa wadau na elimu ya kutosha kuhusiana na   suala hilo.

Pia, alieleza kuhusu namna ambavyo Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo zinafanya vizuri katika suala hilo huku akielezea mazingira wezeshi ambayo yanawezesha Tanzania kufanikiwa katika uanzishaji wa soko hilo, huku akijaribu kufananisha na mazingira ya nchini India ambayo mfumo wa soko hilo unafanya vizuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMC, Godfrey Marekano, alitoa mada kuhusu Mpango wa uwekezaji katika Soko huria na pia amegusia kuhusu masuala ya kisheria na namna ambavyo Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa Mwaka 2017 inavyoweza kusimamia uanzishaji wa suala husika.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, alimpongeza Waziri Kairuki kwa kuanzisha wazo hilo ambalo litawezesha kuleta mageuzi katika Sekta ya Madini na kuwataka wataalam katika Wizara ya Madini na Tume ya Madini kulichukulia suala hilo kwa uzito ili utekelezaji wake uweze kufanyika kama ilivyopangwa.

“Kuna maelekezo mengi kwenye Sheria ambayo tunahitaji kuvipitia na kuyafanyia kazi. Maarifa tuliyoyapata ni makubwa. Rai yangu ni kwa wataalam kuhakikisha wanalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa lisibaki mikononi mwa Waziri tu, alisisitiza Biteko”.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akifuatilia uwasilishaji wa mada juu ya Elimu ya Soko la Bidhaa Tanzania katika kikao kilichowashirikisha wizara na taasisi.

Mtaalam Mwelekezi kutoka kampuni ya, Girish Raipurie, Tanzania Mecantile Exchange PLC  (TMC) akiwasilisha mada wakati wa kikao cha Waziri na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake. 

Mkurugenzi Mkuu wa TMC, Godfrey Marekano akizungumza jambo wakati akiwasilisha mada kwa menejimenti ya Wizara na Taasisi. 
Baadhi ya Wataalam kutoka Wizara na Taasisi wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kutoka kwa Wataalam wa kampuni ya Tanzania Mecantile Exchange PLC  (TMC).

Tuesday, July 24, 2018

Serikali kuimarisha soko la chumvi la ndani kwa kuzuia chumvi kutoka nje


Na Zuena Msuya, Pwani

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaangalia namna bora ya kuimarisha soko la chumvi inayozalishwa nchini yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya ndani na ziada, kwa kuzuia ile inayoingizwa kutoka nchi za nje.

Nyongo alisema hayo, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Julai 23, 2018, baada ya kutembelea Mgodi wa kuzalisha chumvi wa kampuni ya Stanley and Sons ulioanzishwa mwaka 1948/49 uliopo katika Kijiji cha Kitame wilayani humo.

Akizungumzia uzalishaji chumvi, Nyongo alitolea mfano mgodi pekee wa Stanley kuwa, huzalisha chumvi kati ya tani 4000 hadi 6000 kwa mwaka kulingana na hali ya hewa, licha ya kuwepo migodi mingi ya uzalishaji chumvi katika baadhi ya Mikoa nchini ambapo mara nyingi wazalishaji wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa soko la chumvi wanayozalisha.

Alitaja baadhi ya Mikoa iliyokuwa na migodi ya kuchimba na kuzalisha chumvi kuwa ni pamoja Pwani yenye zaidi ya mgozi mmoja, Kigoma katika eneo la Uvinza, Lindi pamoja na Mtwara.

" Tanzania ina migodi mingi ya kuchimba na kuzalisha chumvi bora, ya kutosha na yenye kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza nje, hivyo ni wakati sasa, serikali kuangalia namna bora ya kulinda soko la ndani la chumvi kwa kuzuia ile inayoingizwa kutoka nje, ili wazalishaji waweze kupata soko la uhakika", alisisitiza Nyongo.

Aidha aliwaagiza wachimbaji na wazalishaji wa chumvi nchi, kusindika chumvi hiyo katika ubora unaotakiwa na kukidhi viwango vya soko la Kimataifa kwa kuzingatia kuwa, Tanzania inazalisha chumvi iliyobora.

Sambamba na hilo, alieleza kuwa kwakuwa chumvi ni bidhaa mtambuka inayotumika kama chakula, dawa, pamoja na kuwa ni madini hivyo, aliwataka wachimbaji na wazalishaji wa chumvi, kusindika chumvi hiyo katika ujazo tofauti na kwa bei nafuu ili kila mmoja aweze kumudu gharama za kununua chumvi hiyo kwa matumizi husika ikiwemo majumbani, viwandani na hata katika mifugo.

Pia, alisema wazalishaji wakubwa wawasaidie na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wa chumvi ili na wao waweze kuuza na kusambaza chumvi hiyo ili iwafikie watumiaji wa aina mbalimbali kwa urahisi zaidi na kukidhi mahitaji ya walaji kwa wakati.

" Watumiaji wengi wa chumvi majumbani wananunua na kutumia iliyosindikwa katika ile mifuko midogo ya robo au nusu kilo, sasa ninyi wachimbaji na wazalishaji wa chumvi muangalie namna ya kuwafikia watumiaji wote wa chumvi hapa nchini, hii italeta tija kwa watanzania kutangaza na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini", alisema Nyongo.

Nyongo aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za wachimbaji na wazalishaji wa chumvi nchini kwa kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha kufanya kazi hiyo katika kiwango kikubwa na ubora unaotakiwa.

Pamoja na mambo mengine, alisema kuwa, tayari serikali imewafutia wachimbaji na wazalishaji chumvi, kodi kumi na moja ambazo zilikuwa kero kubwa kwao, na kwamba serikali inaendelea kushughulikia vikwazo vingine vinavyokwamisha shughuli zao.

Aidha alitaja baadhi ya nchi zinazonunua chumvi ya Tanzania kuwa ni pamoja na Jamuhuri ya Watu Congo, Malawi, Msumbiji,pamoja na Uganda na kusema kuwa lengo ni kufikia nchi nyingi zaidi duniani.

Aliwaagiza wachimbaji na wazalishaji wote wa chumvi nchini kulipa mirabaha na tozo mbalimbali na kushiki katika shughuli za kijamii zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini, kwa lengo la kuongeza pato la taifa kwa manufaa ya watanzania.

Mmoja wa Wakurugenzi katika Mgodi wa Chumvi wa Kampuni ya Stanley and Sons, Richard Stanley aliiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara itakayorahisisha usafirishaji ya chumvi hiyo, kwa kuwa katika kipindi cha wa mvua hakuna vyombo vya usafiri vinavyoweza kufika katika eneo hilo.

Vilevile, Richard aliiomba serikali kuwapelekea huduma ya umeme katika kijiji hicho ili kupunguza gharama za uzalishaji ambapo kwa sasa hutumia mafuta mazito kuendeshea mashine za uzalishaji.

Hata hivyo, Naibu Waziri Nyongo aliwahakikisha wawekezaji hao kuwa changamoto zote zitashughulikiwa katika kipindi kifupi kijacho kwa kuwa nia ya serikali ni kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje waweze kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na rafiki ili kuunga mkono azma ya serikali ya kuwa tanzania ya viwanda kutokana na rasilimali zilizopo nchini.


Naibu Waziri  Stanslaus Nyongo, (katikati) wakijadiliana hatua za uzalishaji chumvi, katika mgodi wa chumvi wa kampuni ya Stanley and Sons, wa pili kushoro ni mmoja wa Wakurugenzi wa mgodi huo, Richard Stanley.


Baadhi ya vitalu vya kuzalisha chumvi katika mgodi wa kampuni ya Stanley and Son, uliopo katika Kijiji cha Kitame wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. 

Moja ya mashine za kuvuna chumvi katika mgodi wa kampuni ya Stanley and Sons.

Kairuki aitaka NBS kuishauri Wizara kubaini maeneo yanayoweza kuongeza mchango wa Sekta ya Madini


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuisaidia wizara iweze kubaini maeneo maalum ya kuzingatia yatakayowezesha kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa.

Aliongeza  kuwa, ushauri utakaotolewa na NBS utaisaidia wizara kujipanga zaidi kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo katika sekta husika na sekta nyingine ili kuhakikisha kuwa pato la Sekta linaongezeka.

Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 23 Julai, Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma, wakati wa kikao kati ya Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake ambapo Kaimu Mkurugenzi Takwimu za Uchumi kutoka NBS, Damian Masolwa, aliwasilisha mada kuhusu Mchango wa Shughuli za Madini katila Pato la Taifa.

Kikao hicho kinafuatia maelekezo ya Waziri Kairuki aliyoyatoa kuhusu wizara kukutana na NBS ili isaidie kuona ni namna gani wizara itaongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka asilimia 4.8 ya sasa kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Pia, Waziri Kairuki aliwataka Watendaji wa wizara na taasisi husuan Tume ya Madini kupitia kila vifungu vya Sheria ya Madini na kuhakikisha kuwa vinatekelezwa kikamilifu.

Aidha, Waziri Kairuki alimshukuru mtaalam huyo na kuikaribisha ofisi ya NBS kuendelea kuishauri wizara kuhusu masuala ya takwimu kwa lengo la kuipeleka mbele sekta ya madini.

Wakati akiwasilisha mada, Musolwa aliishauri wizara kusimamia vizuri mianya ya mapato yatokanayo na madini pamoja na kuongeza  juhudi katika kuhakikisha inapata taarifa za kutosha hususan katika madini ya ujenzi.

Pia, aliishauri wizara kuhusu kufanya tafiti za madini katika maeneo mbalimbali ya nchi jambo ambalo litaiwezesha kupata taarifa zitakazosaidia katika ukusanyaji wa mapato stahiki kutokana na shughuli  za madini zinazofanyika katika sekta ikiwemo zile zinazokwenda sambamba na sekta ya madini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko alimshukuru mtoa mada kutokana na elimu ya takwimu aliyoitoa na kuahidi kuufanyia kazi ushauri alioutoa.

Pia, ameitaka NBS kuendelea kutoa ushauri wa mara kwa mara wizara lengo likiwa ni kuhakikisha sekta ya madini inachangia zaidi katika pato la taifa.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki, akifuatilia jambo wakati Kaimu Mkurugenzi Takwimu za Uchumi kutoka NBS, Damian Masolwa akiwasilisha mada Mchango wa Shughuli za Madini katila Pato la Taifa.Kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko.

Kaimu Mkurugenzi Takwimu za Uchumi kutoka NBS, Damian Masolwa akiwasilisha mada ya Mchango wa Shughuli za Madini katila Pato la Taifa kwaWaziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) na Menejimenti ya Wizara pamoja na  watumishi kutoka Taasisi zake wanaofuatilia.

Kaimu Mkurugenzi Takwimu za Uchumi kutoka NBS, Damian Masolwa akiwasilisha mada ya Mchango wa Shughuli za Madini katila Pato la Taifa kwaWaziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) na Menejimenti ya Wizara pamoja na  watumishi kutoka Taasisi zake wanaofuatilia.

Wachimbaji wadogo wajanja watafute kazi nyingine-Biteko


Na Greyson Mwase

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini kwa njia ya ujanja ikiwa ni pamoja na kukwepa kulipa kodi serikalini, kutafuta kazi nyingine kwani Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Madini imejipanga kudhiti biashara haramu ya madini.

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo leo tarehe 21 Julai, 2018 kwenye mkutano wake na wazalishaji wa chumvi, wachimbaji madini ya jasi pamoja na wawakilishi kutoka kampuni ya saruji ya Dangote uliofanyika mjini Mtwara wenye lengo la kufuatilia maelekezo aliyoyatoa katika kikao kilichofanyika mapema tarehe 19 Januari, 2018, kubaini changamoto kwenye shughuli za madini pamoja na kuzitatua.

Alisema kuwa Wizara ya Madini imejipanga katika kudhibiti mianya yote ya ukwepaji kodi, utoroshaji wa madini na rushwa ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akielezea mikakati ya Serikali katika kuboresha shughuli za wachimbaji wa madini ya chumvi Biteko alisema kuwa, Serikali imeondoa kodi zote zisizo za lazima ili wachimbaji wadogo wapate faida zaidi na kulipa kodi stahiki  serikalini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliagiza wachimbaji madini hao kuhakikisha wanalipa kodi stahiki ya madini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa madini hayo na si mgodini,” alieleza Biteko

Aliendela kusema kuwa wakati wa kufanya biashara ya madini kwa ufanisi ni sasa kwani hakuna urasimu na ujanja serikalini, hivyo kupelekea leseni za madini kutolewa kwa wakati na kusisitiza kuwa kinachohitajika kwa wachimbaji wadogo ni kufuata sheria na kanuni za uchimbaji madini.

Wakati huo huo wachimbaji wadogo wa madini katika mikoa ya Lindi na Mtwara walimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 kwa muda mfupi tu wa miezi sita tu.

“Mheshimiwa Naibu Waziri tunashukuru mno kwani tangu ulipokutana na sisi mapema Januari 19, mwaka huu mjini Mtwara na kutoa maelekezo kwa watendaji na kufuatilia maelekezo yako, changamoto zote zimeisha ndani ya miezi sita, tuaendelea kuunga mkono juhudi zako za kuboresha sekta ya madini kupitia wachimbaji wadogo,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Lindi (LIREMA), Peter Ludovick kupitia taarifa yake kwa Naibu Waziri Biteko.

Akielezea pongezi hizo, Biteko alisema yeye hastahili pongezi hizo bali ni  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa yeye ndiye aliyeelekeza Wizara ya Madini kuwaondolea wachimbaji kero.

Aliendelea kusema kuwa  anayestahili kupongezwa ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ambaye  ndiye msimamizi mkuu wa Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Fedha kwa kukubali kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha na kusisitiza kuwa hao ndio  wanaostahili pongezi na sio yeye.

Wakati huohuo, Biteko alikutana na watumishi wa Ofisi ya Madini Mtwara na kuwataka kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa  huku akiahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa (kulia) kabla ya kuanza ziara ya kikazi katika mkoa Mtwara tarehe 21 Julai, 2018.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Madini Mtwara.

Monday, July 23, 2018

Migodi nchini yatakiwa kuweka mitambo ya kuchejulia madini


Na Greyson Mwase, Tunduru

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewataka wamiliki wa migodi nchini kuhakikisha wanaweka mitambo ya kuchenjulia madini ili kuyaongezea thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Naibu Waziri Biteko ametoa wito huo kwenye mkutano wake na wachimbaji wadogo alioufanya katika kijiji cha Mbesa kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma mara baada ya kutembelea Mgodi wa Shaba wa Mbesa kama moja ya ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za madini katika mikoa ya Kusini ili kubaini changamoto pamoja na kuzitatua.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Madini, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Tunduru.

Alisema kuwa, wamiliki wa migodi wanatakiwa kuhakikisha wanaweka mitambo ya kuchenjulia madini ili mbali na kuongeza mapato nchini watoe ajira kwa wananchi wanaozunguka migodi.

Katika hatua nyingine, Biteko aliwataka wamiliki wa migodi kununua bidhaa za ndani badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi pamoja na kutoa ajira kwa wazawa ili wananchi wanufaike na rasilimali za madini hayo.

Pia aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanasajili mikataba yao kwenye Ofisi za Wizara ya Madini kama Sheria ya Madini inavyotaka.

Awali wakiwasilisha changamoto mbalimbali kwa Naibu Waziri Biteko, wachimbaji hao walitaja kuwa ni pamoja na mitaji midogo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini, vifaa duni vya uchimbaji pamoja na leseni za madini kulipiwa kwa fedha za kigeni.

Walitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa maabara za kupima madini migodini na baadhi ya wachimbaji kufutiwa leseni zao.

Wakati huo huo akielezea shughuli za uchimbaji madini ya shaba katika eneo la Mbesa lililopo Tunduru mkoani Ruvuma, Afisa Madini wa Tunduru Mjiolojia Abraham Nkya  alisema Serikali ilitenga eneo la Mbesa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 156.053 ambalo liko umbali wa takribani kilometa 66 kutoka Tunduru Mjini.

Alisema leseni nyingi zimekuwa hazifanyiwi kazi hali iliyopelekea leseni zaidi ya 1000 kufutwa.

Aliendelea kufafanua kuwa kwa sasa Mbesa ina jumla ya leseni 441 za wachimbaji madini wadogo ambazo kati ya hizo 158 ni hai na 283 zina makosa mbalimbali ikiwemo kutokulipa ada ya pango, kutowasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa kila robo mwaka n.k.

Akielezea faida za uchimbaji madini ya shaba katika kijiji cha Mbesa Mjiolojia Nkya alieleza kuwa ni pamoja na ulipaji wa kodi mbalimbali ikiwemo mrabaha, ajira kwa vijana wa kijiji cha Mbesa pamoja na vijiji vya jirani.

Aliendelea kutaja faida nyingine kuwa ni pamoja na uchangiaji wa shughuli za kijamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa soko, uchimbaji wa kisima katika shule ya sekondari ya Mbesa, hospitali na ajira kwa wakinamama wanaohudumia eneo la uchimbaji.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (wa pili kulia) pamoja  na msafara wake wakiendelea na ziara katika Mgodi wa Shaba wa Mbesa uliopo katika  wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma tarehe 20 Julai, 2918.
Mkurugenzi wa Mgodi wa Shaba wa Mbesa, Ziadi Igangula (kulia) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) jiwe lenye madini ya shaba mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mbesa kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kulia) pamoja na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera (kushoto) wakisikiliza kero ,mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko  (kushoto) akiagana na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera (kulia) mara baada ya kukamilika kwa ziara kwenye wilaya hiyo.