Friday, March 29, 2019

Waziri Biteko azindua Bodi ya GST


v AITAKA KUIWEZESHA GST KURAHISISHA MAISHA YA WACHIMBAJI

Asteria Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma

Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imetakiwa kuiwezesha taasisi hiyo kurahisisha maisha ya Wachimbaji Wadogo, wa Kati na Wakubwa kwa kuhakikisha wanapata taarifa za tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizundua Bodi ya GST na kueleza kuwa, shughuli za utafiti ni moja ya maeneo muhimu katika sekta ya madini kutokana na kutoa uhakika kwa wachimbaji na hivyo kukidhi matarajio ya wadau.

Pia, ameitaka bodi kuiwezesha taasisi hiyo kutoa ubunifu mpya utakaowezesha taasisi hiyo kuongeza mapato kwa serikali kutokana na shughuli na huduma zinazotolewa na GST.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ameitaka bodi hiyo kuhakikisha GST inapata Ithibati ya maabara yake ikiwemo kutangaza huduma zinazotolewa na maabara hiyo ili kuwawezesha wadau kuifahamu na kuitumia.

Aidha, ameitaka bodi husika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sera, sheria na taratibu zilizowekwa na kueleza kwamba, taasisi hiyo inao watendaji wazuri wa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kiamilifu na kutumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST Yokberth Myumbilwa, kwa kusimamia vema utendaji wa GST.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema taasisi hiyo ni kitovu cha sekta ya madini nchini na kwamba ndiyo imeshikilia mstakabali wa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.

Ameongeza kuwa, bado yapo majukumu ya taasisi hiyo ambayo hayajafanikiwa na hivyo kuitaka bodi hiyo chini ya Prof. Ikungula kuhakikisha yanafanikiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Justinian Ikingura amesema bodi hiyo inatambua umuhimu wa rasilimali madini katika kuchangia pato na kukuza uchumi wa taifa ikiwemo kutambua nia na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

Amesema ili kufikia lengo hilo, ni muhimu GST ikawezeshwa ipasavyo kupitia wizara ili iongeze kasi na tija zaidi katika kutekeleza majukumu yake, hususan katika maeneo ya kufanya utafiti na kukusanya taarifa muhimu za kijiosayansi za kubaini maeneo yenye miamba yenye vishiria vyakuwepo madini ya kimkakati yanayohitajika zaidi katika matumizi ya teknolojia ya viwanda vya kielekitroniki, zana za utafiti wa mawasala ya anga na matumizi maalum katika viwanda vingine, ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchini katika maeneo hayo.

Kwa mfano madini lithium, cobalt na palladium yanazidi kupata umuhimu wa pekee katika matumizi ya viwanda vya kimkakati. Hivi majuzi takriba wiki moja iliyopita bei ya Palladium ilifikia kiasi cha dola za kimarekani 1,600 kwa wakia na kuzidi hata dhahabu ambayo ikiwa karibu dola 1,300 kwa wakia moja. Lakini si wengi wanatambua madini ya Palladium ambayo yako katika kundi la metali za Platinum, yaani Platinum Group Metals (PGM),” amesisitiza Prof. Ikingura.

Ameongeza kuwa, eneo jingine ni uboreshaji wa huduma za maabara za uchunguzi na upimaji wa miamba na madini yake ili zikidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini kutumia zaidi maabara za ndani ya nchini badala ya kupeleka sampuli katika maabara za nje ya nchi, na hivyo kupoteza fedha za kigeni.

Vilevile, amesema ipo haja ya kuboresha na kuongeza thamani taarifa za jiofikizia na jiokemia zilizo katika hifadhi au kanzidata ya GST ili ziweze kuwa na thamani kubwa zaidi  kwa taifa na kwa wawekezaji katika sekta ya madini, suala ambalo  litaiweesha GST kuongeza maduhuli ya serikali kupitia wizara.

Mbali ya Mwenyekiti, wajumbe wa bodi hiyo ni Abdulkarim Hamisi Mruma, Emanuel Mpawe Tutuba, Bibi Bertha Ricky Sambo, Shukrani Manya, David R. Mulabwa na Bibi Monica Otaru.

Bodi hiyo imezinduliwa Machi 27, 2019 Makao Makuu ya GST, jijini Dodoma.

Waziri wa Madini Doto Biteko,  akimkabidhi  kitendea kazi mmoja wa wajumbe wa Bodi ya GST , Kamishna wa Madini, David Mulabwa wakati wa uzinduzi wa bodi. Anayeshuhudia kulia ni Mwenyekiti wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan  Kitandula.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wajumbe wa  Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti  wa  Madini Tanzania (GST), Watendaji wa wizara  pamoja na watumishi  mbalimbali kutoka  GST wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Bodi ya GST uliofanyika jijini Dodoma tarehe 27/3/2019.

Waliokaa kutoka kushoto ni  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya  Bunge ya Nishati na Madini  Dustan  Kitandula, Waziri wa Madini Doto Biteko , Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula, na Naibu waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. Wengine katika picha waliosimama ni Wajumbe wa Bodi ya GST na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya GST. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akimkabidhi moja a kitendea kazi mjumbe wa Bodi ya GST Prof. Shukran Manya wakati wa Uzinduzi wa Bodi ya GST uliofanyika tarehe 27/3/2019 katika ukumbi wa mikutano wa wizara , pembeni anayeshuhudia makabidhiano hayo ni mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Justinian Ikingula.

Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto) akizungumza na jambo wakati wa uzinduzi wa bodi ya GST . Kulia anayefuatilia hayo ni Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula.

Thursday, March 28, 2019

Waziri Mkuu atembelea Mji wa Serikali


Na Greyson Mwase,

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewapongeza wakandarasi kwa kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma.

Ametoa pongezi hizo leo tarehe 27 Machi, 2019 mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo na kuonesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.

“Nimefurahishwa sana na wakandarasi waliochukua zabuni za kujenga majengo ya ofisi hizi, hivyo ninawaomba Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA) watoe vyeti kwenye majengo ambayo yamekamilika kwa asilimia mia ili waanze kutumia majengo hayo kama ilivyokusudiwa,” alisema Majaliwa.

Katika  hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa  hakuridhishwa  na ubora  wa milango iliyopachikwa kwenye jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Jengo la Wizara ya Fedha na kuagiza milango hiyo kubadilishwa.

Pia, Majaliwa ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme mkubwa katika eneo hilo kwa wakati ili majengo yakamilike kwa asilimia mia na kufikia azma ya Serikali ya kuhamia katika mji wa Serikali baada ya ofisi hizo kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Mgufuli.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Philip Mpango, amesema mradi wa ujenzi wa nyumba hizo umezalisha ajira kubwa kwa vijana kutokana na kuajiri takribani watu 1141 walioshiriki katika ujenzi huo.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Jengo la Wizara ya Madini,   Naibu Waziri wa  Madini, Stanslaus Nyongo, amesema jengo la Wizara limekamilika kwa asilimia 99, na kubainisha kuwa, mkandarasi yupo katika hatua za mwisho ili aweze kukabidhi jengo hilo.


Sehemu ya Jengo la Wizara ya Madini lililopo katika eneo la mji wa Serikali Ihumwa jijini Dodoma ambalo mpaka sasa limekamilika kwa asilimia 99.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati mbele) wakipata maelezo ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Madini kwenye mji wa Serikali, Ihumwa jijini Dodoma kutoka kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi huo (kulia).


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kutoka kushoto) akiwa pamoja na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali wakati wakimsubiri  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye jengo la Wizara ya Madini  kabla ya kuanza kwa ukaguzi kwenye jengo hilo.

Wednesday, March 27, 2019

Waziri Biteko afanya mazungumzo na Kampuni ya PRNG Minerals


Na Issa Mtuwa,

Waziri wa Madini  Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya PRNG Minerals Ltd, ya  Marekani, Rocky Smith na Mkurugenzi wa Maendeleo wa Kampuni hiyo Lucas Stanfield ofisini kwake Jijini Dodoma. 

Watendaji hao wapo nchini kwa ziara ya kawaida ya kikazi ya siku tano  ambapo waliomba kukutana na Waziri wa Madini.

Pamoja na mambo mengine, kampuni hiyo inakusudia kuwasilisha taarifa juu ya hali na Maendeleo ya soko la dunia kwa Madini ya Rare Earth Elements na kuzungumzia hatua iliyofikiwa kwa ombi la leseni ya  uchimbaji  Mkubwa wa madini hayo.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko  amesema wizara iko tayari kuipokea kampuni husika nchini baada ya kukamilika kwa taratibu kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu Rocky Smith, amesema kuwa, amefurahishwa na  ushirikiano unaooneshwa na wizara na kuahidi kuanza shughuli za uchimbaji mara baada ya kukamilika kwa taratibu.


Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya PRNG Minerals Ltd kutoka Marekani Rocky Smith kushoto kwa Waziri. Smith alimtembelea Waziri ofisini kwake jijini Dodoma kwa mazungumzo akiwa ameambatana na Mkurungenzi wa Maendeleo wa Kampuni hiyo Lucas Stanfield wa kwanza kulia, na wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa huduma za sheria Wizara ya Madini Edwin Igenge.
Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya PRNG Minerals Ltd kutoka Marekani Rocky Smith kushoto kwa Waziri. Smith alimtembelea Waziri ofisini kwake jijini Dodoma kwa mazungumzo, wa kwanza kushoto ni Ali Ali, Kamishna Msaidizi Uendelezaji Migodi na Madini Wizara ya Madini, anaefuatia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini Edwin Igenge.

Kituo cha Madini na Jiosayansi Kunduchi, kinavyowanufaisha Watanzania


Na Nuru Mwasampeta,
TAARIFA za kijiolojia zinaonesha kuwa, Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali madini huku sehemu kubwa ya madini hayo yakiwa bado hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.

Aidha, rasilimali za madini zilizopo barani Afrika hususani Tanzania, taarifa za kijiolojia zinadokeza kuwa yanaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa na kijamii ikiwa kila mmoja aliyepewa jukumu la kuwajibika katika sekta ya madini atatumia utaalamu wake, weledi na ufanisi ili kupata matokeo chanya.

Ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli kwa kutambua utajiri mkubwa wa madini tuliyonayo hapa nchini yakiwemo ya tanzanite, almasi,dhahabu, chuma au vito ameendelea kutoa hamasa kwa viongozi wenye mamlaka ya kuyasimamia madini kuongeza ubunifu na usimamizi wenye tija.

Kwa kutambua umuhimu wa madini katika kuharakisha maendeleo ya nchi, Wizara ya Madini kupitia viongozi wake kila kukicha wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali ili kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kuleta tija kubwa kwenye sekta ya uchimbaji wa madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta kwa matokeo makubwa.

WAZIRI NYONGO

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameshiriki katika kikao cha 39 cha kutathmini utendaji wa Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC)) katika kutekeleza maazimio ya nchi wanachama kilichofanyika nchini Sudani Februari 18, mwaka huu.

Neno jiosayansi linamaanisha sayansi inayohusu Dunia ikihusisha masuala yote yanayohusisha elimu ya miamba kama vile utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji pamoja na biashara ya madini.

Hivyo, AMGC ni kituo kinachoratibu masuala hayo kwa nchi mwanachama wa umoja huo katika Bara la Afrika.

Kituo hicho kilichoanzishwa na Kamisheni inayohusu masuala ya Kiuchumi katika Umoja wa Afrika (UNECA) kwa lengo la kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazohusu sekta ya madini chini ya Mwamvuli wa Dira ya Afrika kuhusu Madini (AMV) ili kupelekea maendeleo endelevu kwa nchi wanachama pasipo kuathiri mazingira. 

Umoja huo ulianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977 ukijulikana kama Southern and Eastern African Mineral Centre (SEAMIC) ambapo shughuli zake zilikuwa zikifanyika katika jengo la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) jijini Dodoma, kabla ya kuhamia katika ofisi zilizopo Kunduchi jijini Dar es Salaam. 

Gharama za ujenzi wa ofisi za kituo hicho zilitokana na michango ya nchi wanachama.

Aidha, kituo hicho kinafanya shughuli mbalimbali za madini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya namna ya kukata na kuchenjua madini, kukata madini na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na madini, uchambuzi na huduma za ushauri katika maeneo tofautitofauti ya kimadini, pamoja na tafiti juu ya madhara yatokanayo na kemikali za kuchenjulia madini kwa mazingira. 

Kabla ya mkutano uliowahusisha mawaziri wenye dhamana na sekta ya madini, kulitanguliwa na mikutano mingine miwili iliyohusisha Bodi ya Wakurugenzi wa kituo hiki ni kikao kidogo zaidi wakiwa ni wasimamizi wa karibu wa kituo kikao cha pili kinawahusisha watendaji wakuu katika wizara zenye dhamana ya madini, ambacho baada ya kikao waliwasilisha taarifa za kikao katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la nchi wanachama kwa ajili ya kutolea maamuzi.

Kuhudhuria katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini Nyongo amesema, amejifunza namna sekta ya madini nchini Sudan ulivyojipanga katika kuikwamua Sudan kiuchumi kutokana na rasilimani madini. 

Ameendelea kueleza kuwa, nchi ya Sudan inazalisha madini ya dhahabu kwa wingi kwa kiasi cha tani 107 ukilinganisha na Tanzania inayofikisha kiasi cha takriban tani 50 kwa mwaka.

Nyongo anaeleza kuwa, kiasi cha tani 107 cha dhahabu kilichozalishwa nchini Sudan mwaka uliopita kiliuzwa nje ya nchi ambapo asilimia 90 ya madini hayo yalichimbwa na kuuzwa kutoka kwa wachimbaji wadogo. 

Waziri Nyongo amekiri kuwa, sekta ya uchimbaji mdogo inao uwezo mkubwa wa kuchangia katika pato la Taifa tofauti na fikra za wengi zilivyo.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia uwajibikaji wa migodi katika kutoa huduma na unufaikaji wa wazawa, Torence Ngole amesema uwepo wa kituo hicho kwa Watanzania una manufaa makubwa kwa Watanzania hususani wachimbaji wadogo katika kujipatia ujuzi.

Lakini pia kituo hicho kina maabara kubwa inayotumika katika kuchunguza madini na kuyabainisha ambapo wachimbaji wanaweza kupeleka madini yao na kuwa na uhakika zaidi wa mali waliyonayo. 

Katika kupunguza migogoro katika kanda ya maziwa makuu kama vile Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi zenye migogoro na vita, Ngole amebainisha uwepo wa mashine maalumu inayoyafanya uchunguzi wa madini na kubaini madini hayo yanachimbwa nchi gani. 

Amesema, ikibainika kuwa madini husika yanapatikana katika nchi zenye vita basi hayapewi kibali cha kuweza kuyauza na hivyo kuyanyima sifa ya kuuzika. 

Hiyo ni moja kati ya mbinu ya kuleta amani na kupunguza kasi ya mauaji miongoni mwa nchi katika Bara la Afrika.

Pamoja na kuiwakilisha nchi katika kikao hicho cha mwaka, Ngole amesema alipata fursa ya kutembelea maonesho ya madini yanayoandaliwa na wizara yenye dhamana na madini nchini Sudan na kujifunza mambo muhimu ambayo nchi yetu ikiyafanya itasaidia katika kukuza sekta ya madini.

Amesema, kuwepo kwa maonesho ya madini kunafungua ukurasa kwa wachimbaji na wauzaji wa madini kukutana na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusiana na sekta ya madini. 

Swali unaweza kujiuliza je? Umoja wa kusimamia sekta ya madini Afrika una umuhimu gani?. 

Akifafanua swali hilo, Ngole anasema, wakati wa uumbaji wa nchi/dunia mipaka ya kikanda na kijiografia havikuwepo, kutokana na hilo mipaka hiyo haizuii miamba ya madini iliyopo Tanzania inapofika baina ya mpaka wa nchi na nchi kukoma na kutokuendelea, kutokana na ukweli huo ushirikiano huo utazifanya nchi mwanachama kufanya shughuli za uchimbaji kwa namna zinazofanana na kutumia uzoefu wa nchi jirani kutambua uwepo wa madini katika nchi nyingine. 

Ameongeza kuwa, katika kufanya tafiti za madini kuna ramani za madini zinatengenezwa, endapo kutakuwa na ushirikiano ramani hizo zitaandaliwa kwa vigezo vinavyofanana hivyo utangazaji wa sekta ya madini kufanana kwa nchi zote mwanachama.

Ameendelea kueleza kuwa, tafiti za pamoja zinasaidia sana katika kugundua aina mbalimbali za madini yaliyopo kwenye nchi wanachama kutokana na kufanya tafiti kwa pamoja na kubainisha kuwa mipaka ya kijiolojia iko tofauti na mipaka ya kijografia.

Pia ushirikiano unasaidia kupunguza changamoto ya utoroshwaji wa madini na kubainisha kuwa kutokuwepo na ushirikiano na mbinu za kuwafanya watoroshaji wa madini kukaguliwa katika mipaka ya nchi, nchi mwanachama hazitanufaika na madini yanayochimbwa kwani hayatalipiwa tozo zinazotakiwa na Serikali.

Katika hatua nyingine, inabainishwa kuwa, ushirikino ukiwepo baina ya nchi wanachama nchi hizo zitakuwa na sera zinazofanana kusimamia sekta ya madini. 

Hii itatokana na mijadala wanayoifanya ya kubaini na kuchangia uzoefu katika kuendesha sekta, wawekezaji watashindwa kukimbia kimbilia, kwani sera zinafanana za nchi hizo zinafanana na kuamua kuwekeza mahali walipoanzia.

 UMOJA UNAVYOJIENDESHA

Uendeshwaji wa kituo hicho unategemea michango ya nchi wanachama kwa asilimnia 60 ambapo kila nchi mwanachama anatakiwa kuchangia kiasi cha sh.milioni 150 (zaidi ya dola za Kimarekani 62,000) kwa mwaka na asilimia 40 zinatokana na kipato kitokanacho na ada za huduma zinazotolewa na kituo hicho.

KILICHOJADILIWA

Aidha, katika kikao hicho, kilijadili tathmini ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na kikao cha maamuzi cha mwaka uliotangulia ili kujiridhisha na mwenendo wa kituo hicho na kubaini changamoto zinazopelekea maagizo hayo kutokutekelezwa.

UMUHIMU WA KITUO

Kwanza kabisa kituo cha umoja huo kipo nchini Tanzania katika Jiji la Dar es Salaam. Uwepo wa kituo hicho ni heshima kubwa taifa limepewa na kuaminiwa na nchi wanachama.

Umuhimu wa kwanza unaotokana na kituo ni elimu inayotolewa katika kituo hicho kwa wachimbaji wadogo wa madini, hivyo Watanzania wengi kunufaika. 

Wachimbaji wanafundishwa namna ya kukata madini, kuyaongezea thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na madini pamoja na njia bora za uchenjuaji wa madini.

Pili kituo kinatoa huduma za kimaabara, hivyo mtu yeyote mwenye madini na anataka kutambua madini yake anaweza kupata huduma hiyo katika kituo hicho.

Vikao vya utendaji wa kituo vinakaliwa kila mwaka sawasawa na utaratibu uliowekwa na nchi wanachama.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kutoka kulia)  akifuatilia mada wakati wa kikao kilichowahusisha Mawaziri wenye Dhamana na madini kwa nchi wanachama wa Kituo cha Madini na Jiosayansi Afrika kilichofanyika mwezi Februari nchini Sudan, kushoto kwake ni Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia uwajibikaji wa migodi katika kutoa huduma na unufaikaji wa wazawa, Torence Ngole. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa kwanza kulia) akiwa pamoja na wawakilishi wengine kutoka mataifa wanachama wa Kituo cha Madini na Jiosayansi Afrika kilichofanyika mwezi Februari nchini Sudan, wakifuatilia mada.

Tuesday, March 26, 2019

Wizara ya Madini yaieleza Kamati ya Bunge utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19


Ø YATAJA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA

Ø TUME YA MADINI YAPONGEZWA

Wizara ya Madini na Taasisi zake leo Machi 25, imewasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, kwa  kipindi  cha kuanzia  mwezi Julai 2018 hadi Februari, 2019.

Akiwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa ya utekelezaji wa Wizara, Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila pamoja na mambo mengine, ameelezea Mafanikio ya utekelezaji  wa bajeti kuwa ni pamoja na wizara kuvuka lengo la makusanyo ya maduhuli kwa asilimia 5.6 kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Februari 2019. Lengo la makusanyo kwa kipindi kinachorejewa lilikuwa shilingi 207,065,336,001 ambapo makusanyo halisi yamekuwa shilingi 218,650,392,234.

Pia, amesema Serikali imeondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la thamani (VAT 18), na kodi ya zuio
(Withholding tax  asilimia 5).

Pia, amesema kuzinduliwa kwa Soko la Madini katika mkoa wa  Geita ni juhudi za kuhakikisha uwepo wa masoko ya madini na bei inayoridhisha kwa wachimbaji wa madini hususan wachimbaji wadogo ili kudhibiti uuzaji holela na utoroshaji madini hayo.

"Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi soko hilo tarehe 17 Machi, 2019," amesema Prof. Msanjila.

Vilevile, ameeleza kwamba, kufuatia Kongamano lililofanyika nchini China lililojulikana kama China Tanzania Mining Forum, kampuni tatu zimewasilisha maombi ya miradi ya ubia (JV) kati ya watanzania na wageni Ofisi ya TIC Kanda ya Kati kwa ajili ya kupatiwa Cheti cha Vivutio vya Uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda vya kuchataka madini ya Graphite. Miradi hiyo inatarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 30 na kuzalisha ajira mpya 600 itakapokamilika.

Naye, Waziri wa Madini Waziri wa Madini Doto Biteko, akizungumza katika kikao hicho, ameishukuru Kamati hiyo kwa kuendelea kuisimamia na kuishauri vizuri na kueleza kwamba, Dira Kuu ya wizara ni kuongeza mchango kwenye uchumi wa nchi unaotokana na rasilimali madini.

Pia, Waziri Biteko ameiomba Kamati hiyo kuendelea kuishauri wizara ikiwemo kuikosoa kwa lengo la kuwezesha kuongeza tija zaidi kwenye sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula, amepongeza  jitihada zilizofanywa na wizara hususan kwa kuwezesha mkutano wa Kisekta baina ya serikali na wadau wa madini uliofanyika Januari 22 mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri wa Muungano  wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kueleza kwamba, mkutano huo ulifungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau na hivyo kuutaka ushirikiano huo kuendelezwa ili uwezeshe kuendeleza sekta ya madini nchini.

Amesema matarajio ya Rais Magufuli kwenye sekta ya madini ni makubwa na hivyo kutaka jitihada zaidi kufanyika ili kukidhi maratajio hayo.

Aidha, wakichangia hoja kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Tume ya Madini kwa ukusanyaji maduhuli na kwa utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo ukaguzi migodini.

Monday, March 25, 2019

Biteko azitaka Taasisi za Madini kufikiri kibiashara


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini Doto Biteko amezitaka taasisi zilicho chini ya Wizara kufikiri kibiashara ikiwemo kutafuta njia zitakazowezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 23, jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) iliyoandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Aidha, amezitaka taasisi hizo kuhama katika mtindo wa kutegemea ruzuku ya serikali badala yake zijiendeshe kibiashara na kuwataka watendaji wa wizara na taasisi kuhakikisha wanafanya mageuzi yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia zaidi sambamba na kasi yake ya ukuaji kiuchumi.

“Serikali kwa upande wake imeshafanya mageuzi makubwa. Tunataka Idara, kitengo na taasisi zifanye mageuzi. Tuwe na taasisi ambayo mfanyakazi anaweza kueleza amefanya nini kipya,” amesisitiza Waziri Biteko.

Pia, ameongeza kuwa, ukataji madini ni suala ambalo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee kutokana na umuhimu wake katika biashara ya madini na hususan kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini ikiwemo kuhamasisha ujenzi wa viwanda hivyo.

Vilevile, amewataka washiriki wa kikao hicho kuwasilisha mawazo chanya yatakayosaidia kuboresha mkakati huo utakopelekea uboreshaji wa kituo cha TGC.

Aidha, amewataka watendaji wa Kituo cha TGC kuhakikisha wanakitangaza kituo hicho ikiwemo kuwafanya wachimbaji wadogo wa madini kuwa marafiki wa kituo hicho.

Kwa upande wake, Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, amesema serikali iliona umuhimu wa Kituo cha TGC hali ambayo imepelekea kuandaliwa kwa mikakati hiyo na kueleza kuwa uwepo wake unapaswa kutoa mabadiliko katika kituo hicho na hususan katika eneo la uongezaji thamani madini.

 Ameongeza kuwa, uongezaji thamani madini ni jambo ambalo serikali inaliangalia kwa umuhimu wake na kueleza kuwa ni miongoni mwa mambo  yaliyopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na 2017 ili taifa liweze kunufaika zaidi.

Ameeleza masuala mengine yaliyopelekea serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya madini ni pamoja na kutaka kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na madini, serikali kushiriki katika uchumi wa madini na kumiliki hisa, kushirikisha jamii katika miradi ya madini na kampuni za madini kushirikiana  na jamii.

Aidha, amewashukuru wataalam washauri Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutokana na ushauri wao walioutoa kwa wizara wakati wa kupitia Mikakati hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara yaMadini, Prof. Simon Msanjila amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha kila mmoja anaangalia eneo linalomhusu katika kituo hicho na kulifanyia kazi kikamilifu ili kufikia lengo linalotarajiwa.

Wizara ya Madini iliona umuhimu wa kukiimarisha Kituo cha TGC ili kijiendeshe kibiashara kutokana na fursa zilizopo katika sekta ya madini hususan kwenye ukataji wa madini. Pia, kutokana na fursa zilizopo katika ukataji wa madini ya vito na jimolojia kwa ujumla, wizara iliona TGC inaweza kujiendesha kibiashara na hivyo kuongeza mapato kwa serikali.

Kazi ya kuandaa Mikakati hiyo imetekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na  kuandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na kupitiwa kikamilifu na Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizarani na taasisi zake.


Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Wengine ni watendaji wa Wizara na Taasisi. 

Waziri wa Madini Doto Biteko katikati kipitia jambo wakati wa kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na kushoto ni Katibu Mkuu, Prof. Simon Msanjila. 

Viongozi Waandamizi wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa wizara na taasisi, Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu Cha Mzumbe na Wataalam Washauri kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. 

Mtaalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe  Dkt. George Mofulu akieleza jambo wakati akiwapitisha wajumbe wa kikao hicho katika mikakati  hiyo.

Viongozi Waandamizi Madini watembelea jengo la Wizara, Ihumwa


v Waziri Biteko asema wizara iko tayari kuwahudumia watanzania kutokea Ihumwa

v Mkandarasi aahidi kukamilisha ujenzi ndani ya siku Tano

Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini, wakiongozwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Machi 23, wametembelea Jengo la Wizara ya Madini lililopo mji wa Serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo, Waziri wa Madini Doto Biteko amewahakikishia watanzania wote pamoja na wadau wa madini kuwa, wizara iko tayari kuwahudumia kutokea eneo hilo la Ihumwa pindi itakapohamia na kuwataka watumishi kujiandaa kuhamia eneo hilo mara baada ya mkandarasi kukabidhi jengo kwa wizara.

Vilevile, Waziri Biteko amezitaka taasisi nyingine zenye uhitaji wa kutumia madini ya mawe yanayopatikana nchini ikiwa ni pamoja na mable, kuwa wizara iko tayari kuwasaidia kwa kuwaunganisha na wajeta wake.

Pia, amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutokana na msukumo alioutoa kuhakikisha ujenzi wa majengo ya serikali unakamilika kwa wakati.

Aidha,  amempongeza Mkandarasi kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd kutokana na kuongeza kasi ya ujenzi ikiwemo kuzingatia ubora nakuongeza kwamba, wizara imeridhika na ujenzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ameeleza kuwa, wizara imepanga kulifanya eneo la ofisi hiyo kuwa kijani kwa kuhakikisha inapanda miti ya aina mbalimbali na kuhakikisha kwamba eneo hilo linawekewa mazingira mazuri ya kuvutia.

Naye, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila Amesema Mkandarasi Kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd imeahidi kuikabidhi Wizara jengo hilo ndani ya kipindi cha siku Tano zijazo “awali ujenzi ulianza kwa kusuasua lakini sasa uko katika hatua nzuri na mkandarasi amezingatia ubora,” amesema Prof. Msanjila.

Akizungumzia mahitaji ya ofisi na idadi ya watumishi, amemsema kwa idadi ya watumishi wa wizara Makao Makuu ofisi zilizopo katika jego hilo zinatosheleza mahitaji na kuongeza kuwa, kwa kuanza Idara zote na Vitengo vya Wizara vinatarajia kuhamia katika eneo hilo isipokuwa Idara ya fedha kutokana na masuala ya mfumo wa kifedha.

Pia, ameeleza kuwa, wizara imetumia malighafi inayopatikana nchini yakiwemo madini ya mable ambayo yamepatikana kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa kampuni hiyo   Hamisi Msangi ameihakikishia wizara kuwa , ndani ya siku tano zijazo, jengo hilo litakabidhiwa rasmi kwa wizara hiyo.

Muonekano wa Jengo la Wizara ya Madini linalojengwa katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko, (mwenye koti) Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto) na Prof. Simon Msanjila (mwenye tisheti nyekundu) wakikagua maeneo maeneo mbalimbali ya jengo la Wizara


Waziri wa Madini Doto Biteko (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto ) na Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila, wakijadiliana jambo wakati wakikagua maeneo mbalimbali ya jengo la Wizara, eneo la Ihumwa.

Waziri wa Madini Doto Biteko  katikati na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakiangalia kitu wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara, Ihumwa. 

Monday, March 18, 2019

Majaliwa atoa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa kukamilisha masoko ya madini


Nuru Mwasampeta na Greyson Mwase, Geita

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa hususan mikoa yenye utajiri mwingi wa madini ya metali na vito nchini kuhakikisha wanakamilisha na kufungua masoko ya madini ili kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuwa na soko la uhakika la madini hayo.

Majaliwa alitoa  agizo hilo kwenye uzinduzi wa Soko la Madini la Geita tarehe 17 Machi, 2019 uliofanyika katika viwanja vya Soko Kuu mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa kiserikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya.

Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, watendaji kutoka Tume ya Madini, Wakuu wa Mikoa, wabunge, madiwani, viongozi wa dini, waandishi wa habari pamoja na wananchi kutoka katika mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya  jirani.

Alisema kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini ni  sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa tarehe 22 Januari, 2019 kwenye mkutano wake na wachimbaji wa madini nchini uliofanyika jijini Dar Es Salaam. 

“Ninawataka wakuu wa mikoa kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kabla ya mwaka wa fedha kumalizika Juni 30, 2019,” alisema Majaliwa.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwanufaisha watanzania wote, Serikali kupitia Wizara ya Madini ilianza kwa kuboresha Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Aliongeza kuwa, serikali imeamua kuondoa tozo mbalimbali zilizokuwa mzigo kwa wachimbaji wa madini uli uchimbaji wao uwe na faida kubwa na kuwawezesha kulipa kodi mbalimbali za Serikali.

Alisema kuwa, kufutwa kwa kodi na tozo mbalimbali kutapunguza kwa kiwango kikubwa utoroshwaji wa madini nje ya nchi na Serikali kujipatia pato kubwa linalotokana na shughuli za madini nchini.

Akielezea umuhimu wa masoko ya madini, Majaliwa alieleza kuwa mbali na kupunguza utoroshwaji wa madini, hakutakuwepo na dhuluma kwa wachimbaji wadogo wa madini kwani watakuwa na sehemu yenye uhakika ya kuuzia madini hayo kulingana na bei elekezi iliyotolewa na Serikali.

Aliendelea kueleza kuwa, soko la madini  litarahisisha huduma za uuzaji na ununuzi wa madini ambapo huduma zote zitatolewa ndani ya jengo moja hivyo kuokoa muda wa wauzaji na wanunuzi wa madini.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alitoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa, atakayekamatwa anatorosha madini atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.

Pia aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali  kuhusu sekta ya madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje ya nchi.

Aidha, aliitaka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara na Taasisi nyingine za Serikali  zinazohusika na maendeleo ya sekta ya madini kuheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

“Wizara ya Madini, ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hilo ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini,” alisisitiza Majaliwa.

Aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na maendeleo ya  sekta ya madini ambapo utekelezaji  wa dhamira hiyo unakwenda sambamba na kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha kuimarika kwa sekta ya madini nchini.


Jiwe la Msingi kwenye viwanja vya Soko la Madini Geita mara baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto) akielezea namna Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita ilivyojipanga kwenye usimamizi wa  Soko la Madini Geita kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kabla ya kuanza kwa shughuli za uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kabla ya kuzindua Soko la Madini  Geita tarehe 17 Machi, 2019. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) akizugumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Soko la Madini la Geita kufanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Soko la Madini Geita kabla ya uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa hotuba ya uzinduzi wa Soko la Madini Geita kwa wananchi na watendaji waandamizi wa Serikali (hawapo pichani) tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo kwenye uzinduzi huo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Simon Msanjila akitoa taarifa ya uzalishaji wa madini nchini kwenye uzinduzi huo.