Friday, August 31, 2018

Tanzanite kuwa na hati ya utambulisho Kimataifa


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Serikali imesema inafanya utaratibu wa kuwa na Hati ya Utambulisho wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite, ambayo yanapatikana katika nchi ya Tanzania pekee katika vilima vya Mirerani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 25 Agosti na Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa Semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo imefanyika Makao Makuu ya Wizara, jijini Dodoma.

Waziri Kairuki amesema kuwa, serikali inataka kuona kuwa dunia inafahamu kuwa, madini hayo yanapatikana Tanzania pekee na kuhakikisha kwamba yanajulikana zaidi.

Semina ya wabunge imefanyika kufuatia maelekezo ya Kamati hiyo ambayo ilitaka kufahamu kuhusu mwenendo mzima wa Madini ya tanzanite, biashara na udhibiti wa madini hayo baada ya kujengwa kwa Ukuta wa Mirerani unaozunguka migodi ya madini ya tanzanite, Muundo wa Wizara ya Madini, Tume ya Madini na majukumu yao.

Waziri Kairuki amesema kuwa, Wizara imepata fursa ya kuwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo mikakati ya serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini hayo na mipango madhubuti ambayo serikali inakusudia kuifanya ili kuhakikisha kwamba rasilimali madini inalinufaisha taifa na hatimaye sekta ya madini iweze kufikia asilimia 10 ya machango wake katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.

Ameongeza ni  kikao ambacho kimekuwa na manufaa kwa upande wa Serikali kwa kuwa imetoa elimu kwa Kamati hiyo kuhusu yale ambayo serikali imefanya na inayokusudia kufanya kuhusuiana na madini  ya tanzanite lakini pia serikali imepata wasaa wa kupokea maoni, mapendekezo na maelekezo kutoka kwa wabunge ambayo yatawezesha kupeleka mbele sekta ya Madini.

Mbali ya tanzanite, Waziri Kairuki amewaeleza wabunge hao kuhusu mkakati wa serikali kuanzisha Mineral Exchange ambapo amesema tayari wizara imeshaandaa timu ya wataalam ili kwenda kujifunza na kufanya utafiti katika nchi nyingine ili suala hilo liweze kufanyika kwa ubora .

Pia, ameeleza kuwa, Wabunge wa Kamati hiyo, wamepata fursa ya kufahamu majukumu ya Wizara baada ya kuundwa kwa Tume ya Madini, majukumu ya tume ya madini na mahusiano ya kiutendaji kati ya Tume na Wizara.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile, amesema kuwa, kamati imebaini kuwa, Serikali imechukua hatua nyingi za kulinda na kudhibiti madini ya tanzanite ikiwemo  kudhibiti utoroshaji wa madini hayo. “Kama kamati tumeona mnyororo mzima wa thamani ya madini ya tanzanite, awali tulikuwa hatunufaiki kama taifa,” amesema Ditopile. 

Awali, akiwasilisha mada kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini ya tanzanite na usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ndani ya ukuta, Afisa Madini Mkazi wa Mirerani Mhandisi David Ntalimwa, amezungumzia sababu za kushuka kwa mapato na kueleza kuwa, kunategemea kiwango cha ubora na sifa za madini husika.

Ameongeza kuwa, kutokana na mazingira hayo, kiwango cha thamani ya madini na tozo ya mrabaha kitakuwa tofauti kutegemea na mwezi na uzalishaji uliopo.

Akizungumzia sababu za utoroshaji wa madini ya tanzanite, Mhandisi Ntalimwa amesema kuwa, zinatokana na uwezo mdogo wa kusanifu na kuongeza thamani na kunga’risha madini ya vito na hivyo watu kutamani kuuza tanzanite ghafi.

Pia, amesema utoroshaji wa madini unatokana na kukwepa kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa na serikali ili kujipatia faida kubwa, kuwepo kwa raia wa kigeni nchini wanaofanya biashara ya madini kinyume na sheria kwa kushirikiana na wazawa na kukosekana kwa masoko ya uhakika ya kuuzia madini yanayozalishwa.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini baada ya kujengwa ukuta amesema kuwa, serikali imeimarisha ulinzi na ukaguzi getini kwa kutumia vikosi vya ulinzi na usalama, kuzuia magari kuingia na kutoka ndani ya ukuta, watu kuingia ndani ya ukuta kwa vitambulisho maalum.

“Sasa watu wanaingia kwa utaratibu maalum tofauti na walivyozoea awali. Ukuta umeleta utaratibu mzuri na si kero, kama baadhi ya watu wanavyodhani,” amesisitiza Ntalimwa.

Amezitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuzuia Mabroker kwenda migodini na badala yake kutakiwa kusubiria madini getini, uthaminishaji madini kufanyika ndani ya ukuta na serikali kujenga jengo lenye ofisi ya ukaguzi, uthaminishaji na ukumbi wa mabroker ndani ya ukuta.

Aidha, pamoja na kushiriki semina hiyo, pia wabunge hao wamepata fursa ya kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Jiolojia na Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, (GST).


Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini wakifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali zilizotolewa kwa kamati ya Bunge.

Afisa Madini Mkazi wa Mirerani, Mhandisi David Ntalimwa, akieleza jambo wakati akiwasilisha mada kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ushauri na Uchambuzi wa Kazi   kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Nolasco Kipanda, akiwasilisha mada kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Sehemu ya Maafisa Waandamizi wa Wizara na Tume ya Madini wakifuatilia mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, akieleza jambo wakati akiwasilisha mada kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Wizara ya Madini yakutana na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini


Na Asteria Muhozya,

Kuanzia tarehe 21, 23 na 24 Agosti, Wizara ya Madini ilikutana na  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambapo taarifa  mbalimbali za Utekelezaji wa Majukumu na Miradi zimewasilishwa.

Baadhi ya taarifa zilizowasilishwa katika vikao hivyo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Madini kuanzia mwezi Aprili hadi Julai,2018, Taarifa kuhusu Uendelezaji na Uwekezaji katika Madini Mkakati na Taarifa kuhusu Uendelezaji ya Migodi ya Makaa ya Mawe.

Aidha, katika vikao hivyo,  Kamati ilitoa maagizo mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi na Wizara ili kuboresha Sekta ya Madini nchini.

* ALICHOKISEMA WAZIRI WA MADINI ANGELLAH KAIRUKI

# Graphite ni madini ambayo tunayapa kipaumbele. Ninawaomba wananchi na ninyi Waheshimiwa Wabunge mtusaidie kuwaambia wananchi wasikwamishe miradi ya uwekezaji.
# Tutakapokuwa katika hatua za uchimbaji wa madini ya Urani, tutakuwa karibu sana na kila hatua itakayofanyika kuhakikisha kwamba hakuna athari zozote za kijamii. Serikali haitaweka maslahi ya kiuchumi mbele kuliko ya kijamii.
# Tutafanya Jukwaa kubwa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini mwaka 2019. Lengo ni kuvutia Wawekezaji na kuwakutanisha wachimbaji na Wabia lakini pia Taasisi za Kifedha.

*ALICHOKISEMA NAIBU WAZIRI WA MADINI,  DOTO BITEKO

# Wachimbaji wetu wanahitaji huduma za umeme, maji na barabara katika maeneo yao. Yapo baadhi ya maeneo ambayo  tayari  Mhe. Waziri  amewasiliana na Mamlaka husika kwa ajili ya masuala hayo.

* ALICHOKISEMA NAIBU WAZIRI WA MADINI STANSLAUS NYONGO

#  Tuna madini mengi ya Kimkakati. Tunaangalia madini ambayo yatasaidia kusukuma mbele Sekta ya Viwanda.

* ALICHOKISEMA KATIBU MKUU WIZARA YA MADINI, PROF. SIMON MSANJILA

# Kama Wizara tunayo nia ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini. Tunaangalia mfumo mzuri wa namna ya kuwasaidia. Tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge kuhusu namna ya kufanya jambo hilo kwa ubora zaidi.





Saturday, August 18, 2018

Serikali kutoa eneo la Buhemba kwa wachimbaji ikiwa itanufaika


Na Asteria Muhozya, Mara

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema Wizara italigawa kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini eneo lote la mgodi wa Buhemba linalomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ikiwa Serikali itanufaika ipasavyo  na makusanyo kutokana na shughuli za wachimbaji hao.

Kauli ya Waziri Kairuki imekuja kufuatia maombi yaliyotolewa na Chama Cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara (MAREMA) kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Stephano Mseti ambaye alimuomba Waziri Kairuki kulitoa eneo lote la STAMICO kwa wachimbaji hao kwa kuwa wana uhakika wa kuchangia zaidi kodi za serikali ikiwa watamilikishwa eneo husika.

Aidha,  Mseti alimweleza Waziri Kairuki kuwa  wachimbaji katika eneo hilo wamejiandaa kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wanalipa kodi stahiki kwa kuwa, ndani ya mwezi mmoja waliopewa kufanya kazi katika eneo husika, wamekusanya kiasi cha shilingi milioni 107 kama mrahaba.

Katika hatua nyingine, wakati akisikiliza kero za wachimbaji hao, Waziri Kairuki aliiagiza Tume ya Madini na Wataalam kutoka Wizara hiyo kuchunguza kwa kina suala la migogoro ya migodi  yote iliyopo katika eneo la Buhemba iliyotolewa awali na STAMICO kwa wachimbaji hao  na kukamilisha kazi husika ndani ya kipindi cha wiki 3 ikiwemo  kutoa mapendekezo  aweze kujua hatua za kuchukua.

Akizungumzia mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Waziri Kairuki alieleza kuwa, tayari serikali imeanza kujenga kituo cha umahiri katika mkoa huo ili kuwezesha wachimbaji wadogo  kujifunza uchimbaji bora na kuwataka wachimbaji mkoani humo kukitumia kikamilifu kituo hicho mara baada ya kukamilika kwake.

Akizungumzia muda wa uhai wa leseni, alisema kuwa suala hilo limebainishwa kisheria kuwa ni ndani ya kipindi cha miaka saba na kufafanua kuwa, ipo haki ya kuhuisha  muda wa leseni na hivyo kuwataka wamiliki wote wa leseni kuzingatia muda husika uliowekwa kisheria.

Pia, aliwataka wachimbaji hao kutoa taarifa za kuwepo Maafisa Madini wanaomiliki leseni za uchimbaji madini au wanaomiliki leseni hizo kupitia  kwa kutumia majina tofauti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Akizungumzia kuhusu suala la migogoro, alisema kuwa Serikali haifurahishwi na migogoro inayotokea katika maeneo ya migodi na hususani ile inayohatarisha maisha na kuongeza kuwa, serikali haipendi kufunga migodi hiyo kutokana na umuhimu wa migodi hiyo kwa pande zote.

Pia, Waziri Kairuki alisisitiza kuhusu suala la uchimbaji salama  migodini na Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii na kuongeza kuwa, suala hilo ni lazima litekelezwe na wamiliki wote wa leseni wakiwemo wachimbaji wadogo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, alisema Mkoa huo umejipanga kuwa na Gold Exchange ili kuwezesha mkoa huo pia kunufaika na rasilimali hiyo.

Aidha, alisisitiza suala la uchimbaji salama wa madini ikiwemo utunzaji wa mazingira na kuwataka wachimbaji hao kubadilika kwa kuhakikisha wanafanya shughuli zao kisasa.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa, Serikali inawaona wachimbaji wadogo kwa jicho la kipekee na inajua kuwa, ikiwawezesha itapata fedha nyingi kutokana na rasilimali hiyo.

Alisema kuwa, mkoa huo una migogoro mingi ikilinganishwa na mingine na kumshauri Waziri Kairuki kupokea  vizuri malalamiko yote ya wanaolalamika kwani si wote wanalalamika kihalali.

Pia, aliwashauri Maafisa Madini nchini kuhakikisha kuwa, wanapotatua migogoro zawanavishirikisha Vyama vya Wachimbaji katika kutatua migogoro hiyo ikiwemo katika suala la ukusanyaji kodi za serikali.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Chama Cha Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, aliiomba  Serikali kuiwezesha Tume ya Madini ili iweze kuwafikia wachimbaji katika ngazi za chini.

Pia, aliwataka wachimbaji kuwa wakweli na kuacha ubifasi, na kueleza kuwa, kuna watu ndani ya umoja huo wananufaika pindi panapokuwa na migogoro na kuongeza kuwa, migogoro katika jamii ya wachimbaji ni mdudu anayekua kila siku.

Awali, akiwasilisha taarifa ya chama hicho, Katibu Mkuu wa MAREMA, Milele Mundeba, alisema Chama hicho kinakusudia uanzishaji wa biashara ya vifaa vya uchimbaji madini.

Mbali na wachimbaji mkutano huo uliofanyika tarehe 16 Agosti, ulihudhuriwa na benki ya CRDB, SIDO, Benki ya Posta Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya NMB, FINCA, Shirika la Bima la Taifa ( NHIF),  Mamlaka ya Maji, Musoma (MUWASA), Migodi ya Wachimbaji wa Kati ya CATA Mining, ACACIA na  Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akipokewa na viongozi mbalimbali MAREMA na FEMATA.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya pamoja  na Baadhi ya Viongozi na Wanachama wa MAREMA na Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini, ( FEMATA).



Waziri wa Madini Angellah Kairuki akizungumza jambo wakati wa mkutano na Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara (MAREMA).

Serikali kuleta timu jumuishi ya wataalamu utafiti wa madini Muheza


Na Zuena Msuya, Mheza Tanga

Serikali imesema itawaleta wataalam kutoka kituo cha Utafiti wa Miamba(GST), Wizara ya Maliasili  na  Mazingira kwenye eneo walilokuwa wakitumia wachimbaji wadogo kwa shughuli za madini, ambalo pia linadaiwa kuwa liko katika chanzo cha maji, kufanya utafiti na kujiridhisha kama eneo hilo liruhusiwe kuendeleza na shughuli za uchimbaji madini  ama laa. 

Hayo yalisemwa na Naibu waziri wa Madini Dotto Biteko alipotembelea katika kijiji cha Sakale katika Kata ya Mbomole Tarafa ya Amani wilayani Mheza mkoani Tanga, wakati akizungumza na wananchi waliomuelezea kero yao ya kuzuiwa na serikali kutokuchimba madini eneo hilo licha ya kuwatokuwepo na viashiria vya uharibifu wa mazingira na misitu kama serikali inavyosema.

Naibu Waziri Biteko, alisema kuwa kiu ya serikali ni kuwapatia maeneo ya uchimbaji wachimbaji wadogowadogo ili waweze kubadilisha maisha yao kupitia uchumi wa madini, hii ni kutokana Rais kubadilisha sheria za nchi kwa upande wa madini kutoka kuwanufaisha wageni na sasa kuwanufaisha watanzania.

“Serikali yenu ni sikivu,Mheshimiwa Rais amebadilisha sheria ya madini ili kuwanufaisha watanzania badala ya wageni ,hapa leo tumekuja kuangalia kwa macho ili tufanye uamuzi sahihi …siwezi kumiambia mchimbe sasa hivi ila tutaleta wataalamu wetu wa GST,maliasili na mazingira kwa pamoja ili waje kuona uwezekano wa kupewa eneo la kuchimba ikiwa hapa au kwengine”alisema.

Aidha aliongeza kuwa wananchi lazima wafundishwe kufuata sheria za madini haswa katika kuhama  matumizi ya zebaki katika kuchenjua madini ambayo yana athari kubwa kwenye mazingira na miili ya binadamu kutumia madini ya Sayayi ambayo hayana madhara. 

Kwa upande wa wananchi wa eneo hilo, walimueleza naibu waziri huyo kuwa madini katika eneo hilo yaligunduliwa mwaka 2013 na yanapatikana kwenye miamba na siyo kwenye chanzo cha mto kama serikali inavyosema lakini walizuiwa kwa tahadhari ya uharibifu wa mazingira na misitu ya asili.

Walisema kuwa kutoka uliopo mwamba unaosadikiwa kuwa na madini na chanzo cha maji ni zaidi ya mita sitini na ilipo hifadhi ya msitu wa asili wa Amani ni zaidi ya mita 3,000 lakini wamekuwa wavumilivu kusubiri hatima ya serikali.

“Mheshimiwa Naibu Waziri uchumi tunao lakini tunakufa maskini…hapa madini yapo lakini serikali imetuzuia kwa hatari ya uharibifu wa mazingira ..sisi tunakuhakikishia hakuna uharibifu wowote wa mazingira  utakaotokea,” alisema Shetwai.

Naye diwani wa kata hiyo Anord Mlowe alisema kuwa wataalamu walikuja kupima mwamba  na baadae ukaanza kutoa madini lakini baadae kukaanza mabishano kati ya watu wa maliasili,maji na mazingira kuhusu usafishaji wa madini kwa kutumia zebaki lakini mkuu wa wilaya  ya Muheza  aliyepita Subira Mgalu alijiridhisha kuwa hakuna madhara lakini serikali ikaweka zuio.

Alimuomba waziri kuwaruhusu ili waweze kuchimba kutoka maeneo yalipo mmwamaba wa madini ni mashamba ya wananchi na sio eneo la hifadhi kutokana wameyarithi kutoka kwa mababu zao.                    

Akizungumzia eneo hilo,  mbunge wa jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu alimuomba Naibu Waziri , Biteko kuleta wataalamu wa madini kuja kupima ili kuona kama madini hayo yanatoka milimani au yapo kwenye mto ili kuona namna ya kuwasaidia kupewa eneo la uchimbaji.

“Mheshimiwa naibu waziri pale mwamba uko pembeni kutoka chanzo cha maji na wananchi wa Sakale kata ya Mbomole wametunza msitu wa asili wa Amani….hivyo wakipewa eneo la uchimbaji wataweza kutunza msitu bila ya kuathiri  chanzo cha maji” alisema.

Aliongeza “kwa niaba yao tuma wataalamu wako waje ili wakuletee taarifa ili wananchi hawa waweze kuchimba”.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo akisoma taarifa ya zuio la uchimbaji wa madini eneo hilo, alisema lengo ni kulinda mazingira na chanzo cha maji licha ya sheria katika maeneo hayo matatu ya madini, mazingira na maliasili kukinzana jambo ambalo linaleta ugumu kwa watendaji kuwadhibiti wachimbaji hao.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, (mwenye Tshit nyekundu) na Mbunge wa Mheza Balozi Rajab Adad (mbele) wakielekea eneo lililokuwa likitumiwa na wachimbaji wadogo kuchimba madini pia likidaiwa kuwa chanzo cha maji katika hifadhi ya misitu wa asili wa amani, mheza Tanga. 

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko,( katikati) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sakale, Mheza mkoani Tanga, waliokuwa wakiomba kuruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji madini katika eneo linalodaiwa kuwa ni chanzo cha maji yanayotumika Mkoa wa Tanga.

Serikali yawataka Watanzania kuacha migogoro katika ubia wa uwekezaji


Na Zuena Msuya, Kilimanjaro

Serikali imewataka Watanzania  kuepuka migogoro katika maeno ya migodi hasa inayomilikiwa Kwa ubia na wawekezaji wazawa ili kuondoa taswira mbaya kwa wawekezaji kutoka Matifa mengine yanayokuja nchini kwa lengo la kuwekeza badala yake waungane  kuweka mazingira mazuri na rafiki ya kuvutia wawekezaji hao kuwekeza nchini.

Hayo yameelezwa na Naibu  Waziri wa Madini, Dotto Biteko wakati wa ziara yake mkoani Kilimanjaro  alipotembelea mgodi wa Madini wa Mega unaochimba madini ya shaba .( Mega Copper Company) uliopo katika Kijiji cha Chang`ombe wilayani Mwanga  Mkoani Kilimanjaro, Kwan lengo la kumaliza mgogoro uliopo katika mgodi huo unachimba na kuchenjua madini ya Shaba.

Mgodi huo wa madini ya Shaba unaomilikiwa na Watanzania umekuwa katika migogoro ya kutoelewana wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka 10 sasa, Licha kumepiga hatau katika uchenjuaji  wa shaba na kwamba hausafirishi madini ghafi nje ya nchi  kama serikali ilivyoagiza.

Kwa mantiki hiyo, Biteko alisisitiza kuwa migogoro haipaswi kupewa nafasi na inarudisha nyuma maendeleo ya watanzania na kuleta taswira mbaya ya Uwekezaji Tanzania katika Mataifa mengine Duniani Kwani kusengskuwa na mgogoro katika mgodi huo wangekuwa wamepiga hatua zaidi kwa manufaa yao na Taifa kwa jumla.

Biteko  alisema “migogoro miongoni ya wabia hasa wazawa haipaswi kufumbiwa macho na mtu yeyote Yule, ambapo alishauri kuwa kama watu, au kikundi wameingia makubaliano ya pamoja katika kuendeleza mgodi au jambo fulani  basi, makubaliano hayo yapelekwe Wizara ya madini  au katika mamlaka husika yasajiliwe kuepusha migogoro.

Aidha aliweka wazi kuwa kutokana na mgogoro, Serikali imetoa Miezi 3 kwa mgodi huo kumaliza tofauti zao na kuendelea na shughuli za uzalishaji, na endapo watashindwa kufanya hivyo, itawaandikia hati ya makosa na kisha kuwanyang'a mgodi huo na kuwapa watu wengine.

“Ninyi wote ni Watanzania tena ni ndugu kwa nini mnagombana? , Mnakuja kuwa Sheria ya madini inaruhusu kuwafungulia hati ya mashitaka na kuwafutia leseni endapo mgogoro huo  hautakwisha na utakuwa na  viashiria vya uvunjivu wa amani na Mkishindwa kuumaliza ndani ya muda uliotolewa Serikali unaingia Kati na kufanya maamuzi,  nawakumbusha  watanzania wote  hasa wanaoishi katika maeneo karibu na migodi kuepuka migogoro ili sekta ya mdini iendeleee kuimarika” alisisitiza Naibu waziri Biteko.

Vilevile alitoa  wito kwa wanatanzania wenye uwezo wa kuongeza thamani  ya madini wafanye hivyo ili kuongeza pato la taifa na mwananchi mmoja mmoja  kuliko kusafirisha  madini ghafi  nje ya nchi kwa kuwa faida kubwa zinapata nchi zinazo nunua madini ghafi hayo na kuyaongeza thamani.

Kwa mujibu wa Naibu waziri Biteko  mgogoro ulipo katika mgodi huo kati ya  wabia Watanzania wawili ambao kila mmoja alikuwa na mbao wake kutoka nje, ambao waliingia  makubaliano  ya kuanzisha mradi huo ndani ya miezi sita,  baadae Kuliitokea kutoelewana na kUsababisha   mmoja kati yao kuanza uzalishaji  kabla ya kumshirikisha mwenzie.

Mmoja wa wabia hao ni Ally Nyanza kutoka ambaye  alisema kuwa mgodi huo una ukubwa wa heka 25, ambapo  kwa sasa  wapo kwenye majaribio ya kuchimba na kuchenjua shaba Ambapo wanauwezo wa kuzalisha tani 8-10 za shaba kwa siku.  

Alisema Bado wanaendelea na tafiti huku wakiendelea na uzalishaji, soko kubwa la shaba hiyo  liko nchini  China na kutokana na tafiti hizo wamegundua eneo hilo lina  chokaa ambayo hutumika kwenye uzalishaji wa saruji.

Nyanza alismea changamoto kubwa ilikuwa na mgogoro kati yao na uliosabababisha kusimamisha uzalishaji kwa muda mrefu, kwa sasa wanafuata maelekezo ya Naibu waziri kupata muafaka wa kufanya kazi pamoja.

Naye Nassib  Mfinanga  alisema   wamemeridhika na maamuzi ya Naibu Waziri wa Madini na kwamba watakaa kama familia ili tusonge  mbele kwani mgogoro huo umekuwa ukituchelewesha na kutupa hofu kuwekeza bila kuwa na usalama, jambo hili lilikuwa ngumu kwetu.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Aaron Mbogho alisema uwepo wa mgodi huo ni chachu ya maendeleo katika wilaya hiyo tunasuburi wameanza uzalishaji pamoja wazingatie sheriana kanuni za wizara  serikali bado inatamani kuona watoka kwenye uongezajiwathani ya shaba 90% hadi kufikia 100%.


Naibu Waziri  wa madini, Dotto Biteko, akizungumza na akina mama wanaofanya kazi katika mgodi wa shaba wa Mega. 

Naibu waziri wa madini, Dotto Biteko (kulia) akipita katikati ya Mbale za shaba zilizoandaliwa tayari kwa kuchenjuliwa. 

Sehemu ya mtambo unaotumika Kuchenjua shaba. 

Ujumbe wa CRDB wafanya ziara Tume ya Madini


Na Greyson Mwase, Dodoma

Jana tarehe 14 Agosti, 2018  ujumbe kutoka CRDB ukiongozwa na Mkurugenzi wake Dk. Charles Kimei ulifanya ziara katika Ofisi za Tume ya Madini zilizopo jijini Dodoma lengo likiwa  ni kufahamu majukumu na shughuli za Tume.


Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei  (kulia) akifafanua jambo kwenye kikao kilichoshirikisha ujumbe wake na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei  (kulia) akibadilishana mawazo na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto) kwenye Ofisi za Tume ya Madini zilizopo jijini Dodoma.

Afrika Kusini yaonesha utayari kuwa na ushirikiano sekta ya madini


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki jana tarehe13 Agosti alikutana na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mheshimiwa Thami Mseleku. Katika mkutano huo, Balozi huyo alimueleza Waziri Kairuki kuhusu utayari wa Nchi hiyo ya Afrika Kusini kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya madini nchini.

Ujio wa Balozi Thami Mseleku, Makao Makuu ya Wizara ya Madini, unafuatia ziara ya Kamati ya Jamii na Masuala ya usalama ya Bunge ya Jimbo la Gauteng Pretoria- Afrika Kusini ambao walifika nchini mwezi Juni mwaka huu kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa namna sekta ya madini nchini inavyoendeshwa.

Aidha, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya Bunge hilo nchini, ilikubalika kuwa na haja ya kuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali ya namna ya kusimamia sekta ya madini ikiwa ni pamoja na shughuli za uchimbaji madini, kubadilishana uzoefu katika udhibiti wa uchimbaji holela wa madini, usimamizi wa migodi na wachimbaji wadogo wa madini.

Maeneo mengine ni pamoja na namna ya kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini kutoka katika uchimbaji mdogo kwenda katika uchimbaji wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.

Pia, masuala ya utafiti wa miamba ya uchimbaji madini, mafunzo kwa ajili ya wataalam, kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa sekta ya madini, masuala ya umiliki wa migodi na namna ya kuwawezesha wazawa kumiliki uchumi kupitia sekta ya madini.

Kwa upande wake, Waziri Kairuki alimhakikishia Balozi Thami kuhusu nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kumarisha na kukuza zaidi mahusiano baina ya nchi hizo mbili pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika sekta mbalimbali hususan katika sekta ya madini ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.

Vilevile, Waziri Kairuki alimueleza Balozi huyo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ambapo ameendelea kuwakaribisha zaidi wawekezaji kutoka Afrika Kusini kuwekeza katika sekta ya madini nchini.

Vilevile, Waziri Kairuki alimpa pole Balozi huyo kufuatia kifo cha Mama Winnie Mandela aliyefariki dunia mwezi Aprili mwaka huu.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimweleza jambo Balozi ya Afrika Kusini nchini Tanzania Thami Mseleku (kushoto) wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri kairuki ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Thami Mseleku, wakijadiliana jambo ofisini kwa Waziri Kairuki, jijini Dodoma.

Friday, August 17, 2018

Biteko atoa wiki moja kwa muwekezaji kulipa kodi ya madini serikalini


Na Zuena Msuya, Tanga

Serikali imempa muda wa wiki moja nwekezaji  mmiliki wa kampuni ya Amazon Trading (T)Company Limited Abdi Hozza kuhakikisha anailipa serikali kodi ya pango ya uwekezaji kiasi cha dola za Marekani  70,020 sawa na zaidi ya shilingi milioni 140 za kitanzania  anazodaiwa tangu mwaka 2011 katika machimbo ya Kalalani eneo la Umba wilayani Korogwe kutokana na leseni nane za uchimbaji wa madini kuanzialeseni  namba (102-109/2001) anazomiliki.

Sambamba na hilo imeiagiza serikali ya wilaya ya Korogwe  kuhakikisha inatenga maeneo ya wachimbaji wadogowadogo wa madini ili kuepusha migogoro iliyodumu kwa muda mrefu hali ambayo imeleta hali ya chuki baina ya mwekezaji na wananchi.

Waziri Biteko alitoa agizo hilo alipotembelea katika machimbo hayo juzi Jumamosi katika vijiji vya Kigwasi na Kalalani kata ya Kalalani wilayani humo.
Biteko alimtaka ndani ya wiki moja mwekezaji huyo kulipa kodi hiyo ya pango anayodaiwa na serikali na amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuwabaini wageni na watu wanaonunua madini  kwa njia za panya.

“Haiwezekani tangu madini yaanze kuchimbwa katika machimbo haya serikali haijapata kodi kutokana na mgodi huu tunakuta sifuri nimewaambia wailipe haraka nataka nikifika Dodoma kuna commitment statement mnalipa lini” alisema.

Aliongeza  “Na yule anayedhani atakuja Kalalani kununua  madini kwa njia ya panya muda huo umekwisha,na tumekwenda kwenye mto tumekuta mnachimba madini,sheria inakataza kuchimba madini kwenye vyanzo vya maji naomba kuanzia sasa mkaondoe vifaa vyenu kule mtoni”.

Aidha Waziri Biteko, aliongeza kuwa eneo hilo la Kalalani lina leseni za wachimbaji wadogo wa madini ya vito zipatazo 400 lakini leseni zilizohai na zinaendelea kufanya kazi ya uchimbaji ni 70 tu kati ya hizo. 

Awali diwani wa kata hiyo Amati Ngerera alimueleza naibu waziri kuwa mwekezaji huyo(Amazon)hana mahusiano mazuri na wa wanakijiji pamoja na wachimbaji wadogowadogo wa hapo kutokana baada ya kupewa leseni na serikali kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo alilitelekeza  kwa muda mrefu bila ya kuendeleza shughuli zozote na wananchi wengi ambao shughuli zao kubwa ni uchimbaji waliokuwa wakiingia eneo hilo walifanyiwa vitendo vya visivyokuwa vya kibinadamu ikiwemo kupigwa risasi,kubakwa na askari aliowaweka kulinda eneo hilo.

Diwani huyo alikwenda mbali zaidi kuwa mwekezaji huyo huwa anatumia eneo hilo kama dhamana ya kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha na alimpa mwenzake anaitwa Najim  kuendesha mgodi huo kinyemela bila ya serikali kuwa na taarifa.

“Huyu mwekezaji leseni yake ilikwisha tangu mwaka 2001,wananchi wakaomba leseni ya uchimbaji na yeye akaomba ,lakini baadae  akaingia mkataba na mfanyabiashara anayeitwa Najim halafu yeye akajitoa kabisa na huyo Najim hachimbi bali anafanya shughuli zake za biashara ya utalii na huyu Amazon anatumia eneo hili kukopea fedha kwenye taasisi za fedha ”alisema.

Aliongeza “Serikali ya kijiji ilifanya mapendekezo matatu na kuyapeleka katika baraza la madiwani na baadae tukayandika kuyaleta katika ofisi yako,mapendekezo haoy ni eneo hilo litafutwe mwekezaji mwenye sifa ya uwekezaji,nyumba zilizopo eneo la mgodi  zirudishwe serikalini ambazo waasisi wake ni STAMICO na wananchi wakatiwe eneo ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi za uchimbaji”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwasi, Loronyotu Lakaney alimueleza Naibu Waziri kuwa mbali na mgodi huo kutelekezwa na mwekezaji huyo pia madini yanatorosha kwa njia za panya na  kuuzwa Voi nchini Kenya.

“Mheshimiwa Naibu waziri mbali na mgogoro huo pia wachimbaji wengi wadogowadogo wakishapata madini wanakwenda kuyauza Voi mpakani mwa Kenya na Tanzania upande wa hapa Tanga kutokana hakuna udhibiti  na hakuna minada ya madini inayoendeshwa kama serikali ilivyoagiza”alisema.

Naye mwekezaji huyo alimueleza Naibu waziri kuwa alichelewa kulipa hiyo kodi kutokana Kutokupewa taarifa yoyote ya kuendeleza mgodi wala kudaiwa kodi.

“Mheshimiwa Naibu waziri mimi ni kweli kwa muda mrefu sijapaendeleza hapa baada ya leseni yangu kwisha mwaka 2011 sijapewa leseni nyingine wala sijapata hiyo barua ya kulipa hiyo kodi ya pango”alisema.

Taarifa ya ofisi ya Afisa Madini  Mkazi mkoa wa Tanga amabayo gazeti hili inayo nakala yake  ilishapendekeza kwa kamishna wa madini leseni hizo nane za mwekezaji ziandikiwe hati ya makosa(default notice) na hatimaye zifutwe kwa mujibu wa sheria ya madini mwaka 2010,lakini kwenye mfumo wa flexicadastre leseni hizo zinaonesha zipo hai(active in default) ingawa zilishaisha muda wake tangu Septemba 30,2011.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, akikagua Mabaki ya mgodi wa Amazon,ambao umesitisha uchimbaji kwa miaka mingi kutokana na Matatizo mbalimbali.

Naibu waziri wa madini, Dotto Biteko (aliyesimama) akizungumza na wachimbaji wadogo wa eneo la Kilalani, baada ya kutembelea eneo hilo.