Thursday, March 29, 2018

Tanzania yaendelea kutekeleza malengo ya ICGLR

Na Mohamed Saif,

Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kutekeleza malengo na makubaliano mbalimbali ya Mpango wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ili kuleta tija kwenye shughuli za madini kwa Nchi Wanachama.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema hayo Machi 27, 2018 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Kikanda wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu katika Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR Regional Gold Expert Meeting) uliofanyikia Jijini Arusha.

Gambo alisema Tanzania imekuwa Mwanachama rasmi wa ICGLR Mwaka 2008 na kwamba tangu wakati huo imeendelea kutekeleza malengo ya mpango wa ICGLR ili kufanikisha udhibiti wa uvunaji haramu wa madini na kuhakikisha manufaa ya pamoja ya rasilimali husika yanapatikana kwenye Nchi Wanachama.

Malengo ya ICGLR ni kuwianisha sheria za nchi wanachama ili kuweka uwiano katika sheria za kudhibiti uvunaji haramu wa madini, kuwa na hati moja ya usafirishaji madini ya Tin, Tantalum, Tungsten (3TG) na dhahabu ili kuhakikisha kuwa madini hayo yanachimbwa na kutumika kihalali na kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo.

Malengo mengine ya ICGLR ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uchimbaji madini, kuimarisha uwazi na uwajibikaji na kuwa na mfumo wa kanzidata utakaowezesha kufuatilia taarifa za uvunaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.

Katika kutambua malengo hayo, Gambo alisema Nchi Wanachama wanao wajibu wa pamoja kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanafikiwa kwa manufaa ya wanachama wote.

Gambo alizungumzia changamoto mbalimbali zinazozikabili Nchi Wanachama ambazo ni pamoja na uvunaji haramu wa madini, utoroshwaji wa madini, uharibifu wa mazingira, ukosefu wa teknolojia na baadhi ya Nchi kuwa na changamoto za Kiusalama.

Hata hivyo alisema changamoto hizo zisiwe sababu ya kurudi nyuma badala yake juhudi za pamoja, mshikamano wa dhati unahitajika ili kukabiliana nazo na kuhakikisha zinatatuliwa.
"Ni jukumu letu sote kwa pamoja kuhakikisha tunafikia malengo bila kurudi nyuma hasa ikizingatiwa changamoto tunazokabiliana nazo ni nyingi na hatupaswi kukata tamaa wala kurudi nyuma," alisema.

Akizungumzia hali ya uchimbaji dhahabu nchini, Gambo alisema hivi sasa Tanzania inashika nafasi ya Nne Barani Afrika na kwamba juhudi mbalimbali zinaendelezwa za kurasimisha uchimbaji mdogo. Hata hivyo alisema changamoto kuu iliyopo ni utoroshaji wa madini hayo ambayo Serikali inaendelea kukabiliana nayo.

Gambo alielezea mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kufanyika kwenye Sekta ya Madini nchini ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya Madini kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akifungua rasmi Mkutano wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakiendelea na majadiliano Jijini Arusha.

Wednesday, March 28, 2018

Wataalam wa madini ya dhahabu Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) wakutana Arusha


Na Mohamed Saif,

Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wamekutana Jijini Arusha ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu madini hayo kwa maslahi mapana ya nchi hizo.

Mkutano huo wa siku mbili ulifunguliwa jana Machi 27, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambapo alisisitiza kuwa Nchi Wanachama wa ICGLR wanao wajibu wa pamoja kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanafikiwa kwa manufaa ya wanachama wote.

Gambo alizungumzia changamoto mbalimbali zinazozikabili Nchi Wanachama ambazo ni uvunaji haramu wa madini, utoroshwaji wa madini, uharibifu wa mazingira, ukosefu wa teknolojia na baadhi ya Nchi kuwa na changamoto za Kiusalama.

Hata hivyo alisema changamoto hizo zisiwe sababu ya kurudi nyuma badala yake juhudi za pamoja, mshikamano wa dhati unahitajika ili kukabiliana na changamoto hizo na kuhakikisha ufumbuzi unapatikana kwa maslahi mapana ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Nchi Wanachama ni Tanzania, Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo (Kinshasa), Congo (Brazzaville), Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan Kaskazini, Uganda na Zambia.

Tanzania imekuwa Mwanachama rasmi wa ICGLR Mwaka 2008 na tangu wakati huo imeendelea kutekeleza malengo ya mpango wa ICGLR ili kufanikisha udhibiti wa uvunaji haramu wa madini na kuhakikisha manufaa ya pamoja ya rasilimali husika yanapatikana. 


Baadhi ya Waratibu wa Mkutano wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano huo Jijini Arusha. Kulia ni Mkurugenzi wa Demokrasia na Utawala Bora- ICGLR, Balozi Ambeyi Ligabo akifuatiwa na Mwenyekiti wa Mkutano, Service Julie kutoka Congo.

Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakiendelea na majadiliano.

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakifuatilia majadiliano

Mwenyekiti wa mkutano, Service Julie kutoka Congo (wa pili kulia) akizungumza wakati wa Mkutano wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR. 

Washiriki kutoka Tanzania wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano huo. Kutoka kulia ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma akimwakilisha Kamishna wa Madini, Prof. Shukran Manya na Mhandisi Fadhili Kitivai (kutoka Wizara ya Madini). 
Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakiendelea na majadiliano Jijini Arusha.

Naibu Waziri Biteko-Ukuta wa Mirerani utaweka rekodi Afrika


Na Asteria Muhozya, Mirerani

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Ujenzi wa Ukuta kuzunguka Migodi ya  Mirerani ni jambo la Kihistoria na kwamba linatarajiwa kuweka rekodi Barani Afrika.

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo tarehe 23 Machi, wakati wa kikao cha Maandalizi ya Uzinduzi wa Ukuta huo unaotarajiwa kuzinduliwa mapema mwezi Aprili na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John  Magufuli.

Aliongeza kuwa, ukuta huo ni jambo ambalo watanzania wamelisubiri kwa miaka mingi licha ya kuwepo kwa mapendekezo na sasa hatua zimechukuliwa na kutekelezwa.

Pia alilipongeza Jeshi kwa nidhamu kubwa ambayo limeonesha kwa ujenzi wa ukuta huo  wenye urefu wa kilomita 25.4  na ambao ujenzi wake umechukua kipindi cha miezi 3 tofauti na ilivyopangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, alilipongeza Jeshi kwa kazi ambayo imefanyika na kuwataka Wajumbe wa Kamati kukamilisha utekelezaji wa majukumu yote kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Simanjiro, Wizara ya Madini,  Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO - Manyara) na Wakala wa Barabara ( TANROAD)


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia), akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti mara baada ya kikao cha Maandalizi ya Uzinduzi wa Ukuta wa Mirerani.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Issa Nchasi, (wa pili kulia) wakibadilishana jambo na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya uzinduzi wa Ukuta wa Mirerani.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Issa Nchasi akimweleza jambo Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko mara baada ya kikao cha maandalizi.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa  wa Manyara na Wilaya ya Simanjiro wakibalishana jambo.

Monday, March 26, 2018

Madini ya ujenzi, viwanda yanachangia zaidi kwenye uchumi kupita mengine – Biteko


Ø Yachangia bilioni 7.1 mrabaha 2016/17

Ø Asema usimamizi mzuri unaweza kukuza mchango huo kufikia bilioni 15 kwa mwaka

Na Veronica Simba, Dodoma

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, amesema kuwa madini ya ujenzi na viwanda yanaipatia Serikali fedha nyingi kupita aina nyingine zote za madini yanayopatikana nchini.

Akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Dodoma, Machi 22 mwaka huu akiwa kwenye ziara ya kazi, Biteko alisema kuwa takwimu za makusanyo ya Serikali zinabainisha hayo.

“Mfano mwaka 2016/17, takribani tani milioni 15.6 za madini ya ujenzi zilizochimbwa, zilizalisha shilingi bilioni 230.6; ambapo katika hiyo, ulipatikana mrabaha wa shilingi bilioni 7.1,” alisema.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Biteko alieleza kuwa, idadi ya wachimbaji wa dhahabu na madini mengine nchi nzima ikijumlishwa, haiwezi kufika hata robo ya wale wanaofanya shughuli za madini ya ujenzi nchini.

Alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inaongeza vituo vya madini ya ujenzi na viwanda kutoka 85 vilivyopo sasa nchi nzima hadi kufikia 174. “Nina uhakika tukiviongeza vituo kufikia idadi hiyo, tutakusanya mrabaha wa zaidi ya shilingi bilioni 15 katika madini hayo pekee.”

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alitoa wito kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi mbalimbali hususan ya ujenzi wa barabara kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria ya madini inayomtaka kila mtu aliyepewa leseni kulipa tozo na kodi mbalimbali ambazo zimeelekezwa na sheria hiyo.

Alisema, Serikali haiwezi kukubali kuona mtu yeyote anafanya kazi ya ujenzi, amelipwa fedha na Serikali lakini yeye kwa upande wake hataki kulipa kiasi ambacho anapaswa kuilipa Serikali.

“Kama tuna watanzania ambao ni maskini na tunachukua mrabaha kwao, halafu kampuni kubwa yenye mtaji mkubwa, inayoendesha shughuli za ujenzi, iache kulipa kodi stahiki; hiyo haikubaliki,” alisisitiza.

Biteko alisema kuwa, Wizara ya Madini itaandaa utaratibu wa kukutana na kujadiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ambao ndiyo hupewa leseni kwa mujibu wa sheria, kuhusu namna bora ya kusimamia suala husika ili madeni yaliyopo yalipwe.

Maagizo hayo ya Naibu Waziri Biteko yalikuja kufuatia ripoti iliyosomwa kwake na Afisa Madini Mkazi Dodoma Silimu Mtigile, kuwa ofisi yake inakabiliwa na changamoto ya ukusanyaji mirabaha inayotokana na wakandarasi wa barabara.

“Katika miradi mikubwa ya barabara iliyopo Dodoma, ulipwaji wa mirabaha ya madini ujenzi kutoka kwa wakandarasi umekuwa wa kusuasua ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi 642,632,195.00 kimekusanywa, sawa na asilimia 33.11 kati ya jumla ya shilingi 1,941,177,853.23 zinazopaswa kulipwa,” alisema Mtigile.

Aliitaja miradi hiyo ya barabara kuwa ni barabara ya Dodoma kwenda Iringa, iliyotekelezwa na Kampuni ya CCCC, barabara ya Dodoma mjini hadi Mayamaya iliyotekelezwa na Kampuni ya Sinohydro; ambazo zote mbili zimekamilika pamoja na barabara kutoka Mayamaya hadi Mela inayotekelezwa na Kampuni ya CHICO inayotarajiwa kukamilika baada ya muda mfupi.

Naibu Waziri alisema kuwa, Wizara itaisimamia sheria ya madini katika kuhakikisha kila madau anatimiza wajibu wake ipasavyo. Aidha, aliiagiza Ofisi hiyo ya Madini Dodoma, kuhakikisha wanaendelea kufuatilia malipo husika na kutokuruhusu mitambo ya wakandarasi wanaodaiwa, iliyoko eneo la kazi, kuchukuliwa hadi pale watakapokamilisha malipo yao.

Aliwataka watumishi wote wa sekta ya madini kufikiria namna gani sekta hiyo itafanikiwa kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa. Pia, aliwakumbusha kuwa, mojawapo ya kazi kubwa ya Wizara ni pamoja na kuwalea wachimbaji wadogo waliopo ili wakue.

“Tusifanye kazi za kukamata tu. Tufanye kazi kubwa ya kuwalea watu hawa ili wafuate sheria. Ukiwafundisha wakafuata sheria, utatumia nguvu ndogo sana kuwakamata, kwa sababu watakuwa ni watu wenye uelewa tayari,” alisisitiza.

Katika taarifa yake kwa Naibu Waziri; Mtigile alibainisha mojawapo ya mafanikio makubwa ya Ofisi yake kuwa ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli mwaka hadi mwaka, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/17, lengo la kukusanya maduhuli lilikuwa jumla ya shilingi 1,200,000,000. Alisema Ofisi ilifanikiwa kutimiza lengo kwa kukusanya shilingi 1,444,100,922.00 sawa na asilimia 120.34.

Aidha, alibainisha kuwa lengo la mwaka 2017/18 ni kukusanya jumla ya shilingi 1,230,000,000.00; ambapo hadi kufikia Februari 28 mwaka huu, Ofisi yake imekusanya jumla ya shilingi 812,384,840.98 sawa na asilimia 66.05. Alisema kuwa, katika pesa hizo, makusanyo ya mirabaha ya madini pekee ni jumla ya shilingi 621,329,912.38 sawa na asilimia 76.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Biteko pamoja na kuipongeza ofisi ya madini Dodoma kwa jitihada na mafanikio iliyopata; alizungumzia makusanyo ya maduhuli kwa nchi nzima kuwa yanaleta matumaini baada ya mabadiliko ya sheria ya madini.

“Sheria hii tulipoibadilisha, imeongeza msukumo mkubwa kwenye usimamizi wa sekta na hivyo, kwa sasa ukusanyaji wa maduhuli umekuwa mzuri sana ukilinganisha na miaka iliyopita.”

Akitoa mfano, alisema kuwa, mathalani mwezi Februari mwaka huu, makusanyo yalikuwa zaidi ya asilimia 85. Alisema anaamini Wizara yake itavuka lengo ililowekewa la shilingi bilioni 250 kutokana na uwepo wa sheria hiyo nzuri inayosaidia kusimamia vizuri mapato ya serikali.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akisalimiana na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Dodoma, alipowasili katika Ofisi hiyo akiwa katika ziara ya kazi, Machi 22 mwaka huu.


Baadhi ya wafanyakazi katika Ofisi ya Madini Dodoma, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani), alipotembelea ofisi hiyo na kuzungumza na wafanyakazi Machi 22 mwaka huu. Kutoka kushoto ni Halima Kikoti, Affa Edward Affa na Betilda Kirway.


Shughuli za uchimbaji madini ya nakshi zikiendelea katika Mgodi uliopo Ntyuka Dodoma, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) mgodini hapo Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akikagua tarazo zilizotengenezwa na mawe ya nakshi katika mgodi uliopo Ntyuka Dodoma, wakati wa ziara yake Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na Ujumbe aliofuatana nao, wakikagua maeneo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu yaliyopo kijiji cha Nholi wilayani Bahi, Machi 22 mwaka huu.


Sehemu ya shehena ya mawe ya nakshi aina ya Graphite. Taswira hii ilichukuliwa Machi 22 mwaka huu wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) katika Mgodi uliopo Itiso wilayani Chamwino.

Biteko atoa wito kwa wadau kuzingatia sheria mpya ya madini


Na Veronica Simba, Dodoma

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya madini nchini, kuzingatia sheria mpya ya madini ambayo inaelekeza namna bora ya usimamizi wa sekta hiyo.

Alitoa wito huo jana, Machi 22 mwaka huu kwa nyakati tofauti, alipokuwa katika ziara ya Mkoa wa Dodoma, kukagua shughuli mbalimbali za madini.

 “Moja ya mambo muhimu ambayo sheria mpya ya madini inaelekeza ni kutunza rekodi za uzalishaji wa madini ili Serikali iweze kujua ni kitu gani kinazalishwa na hatimaye tuweze kujua kodi gani zinalipwa na wenye leseni husika,” alifafanua.

Aidha, Naibu Waziri aliwataka wenye leseni kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kunufaika kupitia kazi wanazofanya. “Kwa maneno mengine, asitokee mtu wa kumnyanyasa mchimbaji mdogo eti kwa sababu tu ana leseni,” alisisitiza.

Akizungumza na wamiliki wa leseni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini wa dhahabu katika eneo la Nholi wilayani Bahi, Naibu Waziri alipongeza uamuzi wao wa kuanzisha kampeni ifikapo Aprili mwaka huu, kupanda miti kwenye maeneo yao ili kurejesha hali nzuri ya mazingira.

Vilevile, aliwaagiza kuweka wigo kuzunguka mashimo yaliyo wazi ili kuonyesha hali ya tahadhari kuwa eneo hilo ni hatari na linaweza kusababisha ajali, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuzingatia usalama migodini.

Akizungumzia changamoto kuu iliyowasilishwa kwake na wachimbaji wa mawe ya nakshi aina ya Granite na Dorelite Dyke katika maeneo ya Itiso wilayani Chamwino na Ntyuka Wilaya ya Dodoma Mjini, kuhusu vibali vya kusafirisha mawe hayo nje ya nchi, Biteko alisema kuwa awali Serikali ilisimamisha utoaji vibali hivyo kuzuia usafirishaji wa mawe ghafi nje ya nchi.

“Changamoto iliyokuwepo awali, ni kuwa wako watu walikuwa wanasafirisha madini nje ya nchi yakiwa ghafi, yanaongezwa thamani huko kasha tunarejeshewa sisi tununue bidhaa hizo.”

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, jambo linalotia moyo ni kwamba uongezaji thamani madini hivi sasa umeanza kufanyika nchini kwa kiwango kinachotakiwa kusafirishwa nje ya nchi. Alisema, jambo hilo hilo litaleta manufaa kwani thamani, ajira na teknolojia vyote vitabaki ndani na manufaa yatabaki ndani ya nchi pia.

Alipongeza wachimbaji wa mawe ya nakshi wa Itiso na Ntyuka ya kudhamiria kujenga mitambo ya uongezaji thamani mawe hayo katika maeneo husika.

Alisema kiu ya Serikali ni kuona madini yanayochimbwa Tanzania, yanaongezwa thamani nchini na hatimaye kusafirisha bidhaa zinazotokana na madini hayo na kuziuza katika nchi nyingine mbalimbali na siyo vinginevyo.

Aidha, Naibu Waziri aliwasisitiza wamiliki wote wa leseni za madini kufanya kazi zao huku wakizingatia kujenga mahusiano mema na jamii zinazowazunguka.

Alisema kuwa kmujibu wa kanuni mpya iliyopo hivi sasa, mwenye leseni anapaswa kuwasilisha mpango wake wa utoaji huduma kwa jamii (CSR) kwenye Halmashauri husika ili iuthibitishe mpango huo kabla ya utekelezaji wake.

“Ule utaratibu wa mtu anajifungia ofisini, anasema nitawajengea shule pasipo Serikali ya Kijiji au Wilaya kujua, tumeufuta kwa sababu mwanzo ulikuwa unatengeneza matatizo mengi,” alifafanua Biteko.

Alisema, Serikali itafanya kazi ya kuangalia na kuthibitisha thamani halisi ya fedha zitakazotumika katika mpango huo, ili kujiridhisha.

Naibu Waziri alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Dodoma Silimu Mtigile kuandaa na kuendesha semina siku ya Jumatatu, Machi  26 mwaka huu, kwa ajili ya wachimbaji wa eneo la Nholi kuhusu sheria mpya ya madini, kufuatia maombi waliyowasilisha kwake alipokuwa akizungumza nao.

Hata hivyo, alisema kuwa semina za aina hiyo zitaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini kote ili kuwajengea uelewa wa sheria hiyo mpya wadau wa madini waweze kufahamu haki na wajibu wao.
Akizungumzia suala la baadhi ya watu kueneza propaganda kuhusu sheria hiyo kuwa ni kandamizi; Biteko aliwataka watanzania kupuuza kauli hizo kwani sheria husika imelenga kuwanufaisha watanzania na siyo kinyume chake.

“Kama kuna bepari anadhani kwamba tunaweza kurudi nyuma katika hili, amekwama. Heri tuwe na wawekezaji wachache wanaofuata sheria kuliko kuwa nao wengi wenye kutaka tu kuchuma mali na kuondoka.”

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Biteko aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Dodoma Silimu Mtigile, wataalam kutoka wizarani na ofisi ya madini Dodoma pamoja na viongozi wa Wilaya na Halmashauri akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na Ujumbe aliofuatana nao, wakikagua migodi mbalimbali ya uchimbaji wa madini ya dhahabu na mawe ya nakshi  katika vijiji vya Nholi, Itiso na Ntyuka, wakati wa ziara yake ya kazi mkoani Dodoma, Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na Ujumbe aliofuatana nao, wakikagua migodi mbalimbali ya uchimbaji wa madini ya dhahabu na mawe ya nakshi  katika vijiji vya Nholi, Itiso na Ntyuka, wakati wa ziara yake ya kazi mkoani Dodoma, Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na Ujumbe aliofuatana nao, wakikagua migodi mbalimbali ya uchimbaji wa madini ya dhahabu na mawe ya nakshi  katika vijiji vya Nholi, Itiso na Ntyuka, wakati wa ziara yake ya kazi mkoani Dodoma, Machi 22 mwaka huu.


Mashine maalum ikikata jiwe la nakshi aina ya Dorelite Dyke katika Mgodi unaochimba mawe hayo uliopo Itiso wilayani Chamwino Mkoa wa Dodoma. Picha hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko mgodini hapo, Machi 22 mwaka huu.


Shughuli za uchimbaji zikiendelea katika Mgodi wa mawe ya nakshi aina ya Granite uliopo Ntyuka Dodoma wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) mgodini hapo, Machi 22 mwaka huu.


Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma, Silimu Mtigile (kulia) akifafanua jambo kwa wananchi wa Kijiji cha Nholi wilayani Bahi, wanaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu; wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto), Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na Ujumbe aliofuatana nao, wakikagua migodi mbalimbali ya uchimbaji wa madini ya dhahabu na mawe ya nakshi  katika vijiji vya Nholi, Itiso na Ntyuka, wakati wa ziara yake ya kazi mkoani Dodoma, Machi 22 mwaka huu.

Thursday, March 22, 2018

UDSM yaridhia kukilea Chuo cha Madini


Na Veronica Simba, Nzega

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umeridhia kukilea Chuo cha Madini Dodoma (MRI) baada ya kuombwa na Wizara ya Madini ambayo ndiyo inamiliki Chuo hicho.

Dhamira hiyo iliwekwa wazi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilipotembelea na kukagua Kampasi ya Chuo cha Madini iliyopo Nzega mkoani Tabora, Machi 17 mwaka huu.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa alisema kuwa UDSM ina uzoefu wa kutosha katika kulea vyuo mbalimbali hivyo iko tayari kufanya kazi hiyo.

“Sisi tunataka kuthibitisha kwamba tuko tayari kukilea hiki Chuo, kama tutapewa jukumu hilo. Hii ni kwa sababu tunao uzoefu wa kutosha uliotokana na kulea vyuo vingine mbalimbali vikiwemo SUA, Muhimbili, Mzumbe na vingine kadhaa,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa, katika Mpango-Kazi walioundaa na kuuwasilisha wizarani, umebainisha kuwa udahili wa wanafunzi utaanza mapema mwakani.

“Mwaka huu tumepanga uwe wa maandalizi lakini mwakani tunapanga kuanza udahili wa wanafunzi wa UDSM wanaosomea Kampasi ya Nzega na Dodoma.”

Awali, akiwasilisha taarifa ya Chuo cha Madini kwa Kamati hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Mpango wa Serikali ni kuifanya MRI kuwa kitovu cha mafunzo ya kozi mbalimbali za madini hapa nchini.

“Wizara iliunda kamati  kwa ajili ya kupitia kitaalam miundombinu yote iliyoko kampasi ya Nzega na Dodoma pamoja na kuangalia uwezekano wa kuimarisha taaluma katika Chuo hiki; kuimarisha uendeshaji wa Chuo; uanzishaji wa kozi mpya na hasa kukiwezesha Chuo kuwa cha mfano na kitovu cha mafunzo ya kozi zote za madini nchini,” alifafanua.

Alisema kuwa, Wizara imeshapokea taarifa ya Kamati husika na inaifanyia kazi ili kuangalia uwezekano wa UDSM kukilea Chuo hicho.

Aidha, Profesa Msanjila alieleza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Kampasi ya Nzega ni kuongeza wataalam wa kada ya kati katika sekta ya madini. Hivyo, pamoja na shughuli nyingine za taaluma, Kampasi hiyo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo katika fani za jiolojia na utafutaji wa madini, uhandisi wa uchimbaji madini, uhandisi wa uchenjuaji madini, usimamizi wa mazingira migodini na upimaji wa ardhi na migodi.

Vilevile, alieleza lengo jingine kuwa ni kukipanua Chuo hicho kiweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi zaidi, mathalani Kampasi ya Nzega ambayo ina migodi itakayowezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

Chuo cha Madini kilianzishwa rasmi mwaka 1982 kwa lengo la kutoa mafunzo ya kada ya kati katika sekta ya madini. Chimbuko la wazo hilo lilitokana na mahitaji ya watendaji wa kada hiyo.

Jumla ya wanafunzi 542 wamedahiliwa na Chuo kufanya mafunzo ya muda mrefu kwa nadharia na vitendo katika fani mbalimbali za madini.


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa akielezea utayari wa UDSM kukilea Chuo cha Madini, kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (hawapo pichani), walipotembelea Kampasi ya Nzega ya Chuo hicho wakiwa katika ziara ya kazi, Machi 17 mwaka huu.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua majengo mbalimbali ya Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua majengo mbalimbali ya Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua Mgodi wa Madini (Pit) uliopo katika Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu.

Kamati ya Bunge yatembelea Mgodi wa Buhemba na CATA Mining


Na Veronica Simba, Mara

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea na kukagua Mgodi wa Buhemba na ule wa CATA Mining Ltd iliyopo mkoani Mara ikiwa katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.

Katika Mgodi wa Buhemba, Kamati ilielezwa kuwa, Serikali iliukabidhi Mgodi huo wa dhahabu kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2011 ili iuendeleze, kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Kampuni ya Meremeta Limited.

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, aliieleza Kamati kuwa Shirika limekamilisha upembuzi yakinifu katika mabaki ya dhahabu yaliyoachwa kipindi cha nyuma ambapo umebaini kuwapo takribani tani 796,400 za mabaki ya mchanga wa dhahabu yenye wastani wa kilo 852 za dhahabu.

“Aidha, upembuzi huo ulibaini kuwa mabaki hayo ya mchanga yatachenjuliwa kwa kutumia teknolojia ya Carbon in Leach (CIL). Mtambo unatarajiwa kuchakata mabaki ya mchanga wa dhahabu kiasi cha tani 246,240 kwa mwaka,” alisema.

Aliongeza kuwa, tathmini ya kiuchumi ya mradi imeonesha gharama za uwekezaji zinakadiriwa kufikia Dola milioni 3.96 na kwamba gharama za uendeshaji kwa mwaka zinakadiriwa kufikia Dola milioni 4.46 na kutarajiwa kuingiza faida inayofikia Dola milioni 3.45 kwa mwaka.

Kuhusu tathmini ya mashapo katika miamba migumu, Kamati ilielezwa kuwa taarifa za kitaalam zinaonesha kwamba wakati Kampuni ya Meremeta inafunga uzalishaji katika mgodi, kiasi cha wakia 600,000 zilisalia kwenye miamba migumu.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa STAMICO imeamua kufanya upya tathmini ya mashapo hayo ili kujiridhisha. “Hadi sasa kiasi cha mashapo yenye wakia 441,772 kimethibitika kuwemo kwenye miamba migumu kutoka katika migodi ya wazi. Ukadiriaji wa mashapo unaendelea,” alisema.

Vilevile, ilielezwa kuwa Shirika lilifanikiwa kuchoronga shimo moja katika eneo la Nyasanero ili kutathmini mkanda mpya wa dhahabu. Tathmini kamili ya kiasi cha dhahabu kilichopo kwenye mwamba itakamilika mara baada ya kupokea majibu ya maabara.

Akieleza zaidi, alisema kuwa Januari mwaka huu, Shirika lilitangaza zabuni ya kumpata mbia wa kushirikiana naye katika kuendesha mradi kwa njia ya ushindani. Alisema, tayari Kampuni tatu zimenunua zabuni husika na kwamba uchambuzi wa zabuni hizo unaendelea.

Katika Mgodi wa CATA Mining Company Limited, Kamati ilielezwa kuwa Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania, Mahuza Mumangi na Raia wa Canada Stefan Nagy kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50.

Akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Mgodi huo, Kamishna Msaidizi wa Madini, Ofisi ya Madini Musoma, Samwel Mayuki alisema kuwa Kampuni inamiliki leseni sita za uchimbaji mdogo katika eneo la Kataryo ambapo kuna miundombinu mbalimbali ikiwemo mitambo ya kusaga na kuchenjua madini.

“Kuanzia Julai 2016 hadi Juni 2017, Mgodi umezalisha kilo 241.3 za dhahabu zenye thamani ya Dola 8,880,240.57 sawa na wastani wa shilingi bilioni 19.5 za Tanzania. Mrabaha uliolipwa ni Dola 355,209.66 sawa na shilingi milioni 781 za Tanzania,” alisema Mayuki.
Aidha, Kamishna Mayuki aliongeza kuwa, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Novemba 2017 Mgodi umezalisha kilo 62.4 za dhahabu zenye thamani ya Dola 2,239,659.86 sawa na shilingi bilioni 4.9 za Tanzania. Kiasi cha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini kilicholipwa ni Dola 134,388.56 na Dola 22,396.57 sawa na wastani wa shilingi milioni 295.7 za mrabaha na milioni 49.3 za ada ya ukaguzi.

Vilevile, alisema Mgodi umeajiri jumla ya wafanyakazi 351 ambao kati yao 318 sawa na asilimia 91 ni watanzania.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa changamoto kubwa inayoukabili Mgodi kwa sasa ni kusimamishwa kwa shughuli za Mgodi kuanzia Juni 2017 kutokana na mgogoro baina ya wawekezaji husika na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao ni wamiliki wa eneo hilo la uchimbaji.

“Hali hiyo imesababisha hasara mbalimbali ikiwemo kusimama kwa ajira za watanzania 318, kushindwa kurejesha mikopo ya Benki na hasara ya kupoteza mapato ya mamilioni ya shilingi kutokana na kusimama kwa uzalishaji.”

Kamati iliiagiza Wizara kuhakikisha inasaidia katika kushughulikia mgogoro huo ili shughuli za uzalishaji katika Mgodi zirejee mapema.

Viongozi mbalimbali wa Wizara walishiriki ziara hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ambaye aliahidi kwa niaba ya Wizara kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Kamati.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia) akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, mambo kadhaa kuhusu Mgodi wa Dhahabu wa CATA Mining uliopo Mara, walipotembelea Mgodi huo wakiwa katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila (kushoto) wakishiriki katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, katika Mgodi wa CATA Mining mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.


Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.


Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.


Wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.