Wednesday, November 22, 2017

Takukuru kuhakiki matumizi STAMIGOLD – Kairuki

Uchimbaji wa madini ya dhahabu ukiendelea katika moja ya mashimo  yanayomilikiwa na Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo mkoani Kagera. 

 Kaimu Meneja Uchimbaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo, Rashil Rulanga (kulia mbele) akielezea shughuli za uchimbaji zinavyofanyika katika mgodi huo kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto mbele) mara alipofanya ziara katika mgodi huo tarehe 27 Oktoba, 2017. Wa pili kushoto mbele ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo. 

 Shughuli za utafiti wa madini ya dhahabu zikiendelea katika Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo uliopo mkoani Kagera.

 Kutoka kushoto mbele ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Balozi Alexander Muganda,   Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Saada Malunde wakiendelea na ziara katika eneo la Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo. 

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja Uchenjuaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo, Joseph Kamishina (kulia mbele) katika ziara hiyo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akifafanua jambo katika ziara hiyo.


Kaimu Meneja Uchenjuaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo, Joseph Kamishina (katikati mbele) akimwongoza Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ( wa pili kulia) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kulia) kuelekea kwenye eneo la uchenjuaji katika mgodi huo. 

 Kaimu Meneja Uchenjuaji kutoka Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo, Joseph Kamishina(katikati) akielezea shughuli za uchenjuaji madini zinavyofanyika kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) katika ziara hiyo. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo

Mmoja wa wafanyakazi katika Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo, Sara Mkama akiwasilisha  kero yake kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ( hawapo pichani) mara Mawaziri hao walipokutana na watumishi wa mgodi huo kwenye ziara hiyo lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua kero zao.

Sehemu ya watumishi wa Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo, wakisikiliza maelezo  yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani)

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) wakisikiliza kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na watumishi mbalimbali wa Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo (hawapo pichani)
 
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameitaka Bodi ya  Wakurugenzi wa Shirika la  Madini la Taifa (STAMICO) kuwasilisha  taarifa zote za gharama za uendeshaji wa Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu  wa STAMIGOLD – Biharamulo  ili  kujiridhisha  pamoja na kuchukua hatua za kisheria iwapo kama kuna taratibu za manunuzi zimekiukwa.

Kairuki ameyasema hayo leo  tarehe 27 Oktoba, 2017 alipofanya ziara katika mgodi huo uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera lengo likiwa ni kufahamu shughuli za migodi ya serikali, binafsi na wachimbaji wadogo.

Alisema kuwa gharama  za uendeshaji wa shughuli za mgodi  huo zimekuwa ni kubwa mno pamoja na madeni hali inayopelekea shirika hilo  kujiendesha kwa  hasara badala ya kujiendesha kwa faida.
Aliendelea kusema kuwa STAMIGOLD  imekuwa ikitumia  gharama kubwa sana katika uendeshaji wa shughuli zake kwa kutumia mashine za kukodi na kutaka watendaji wa mgodi huo kuwa wabunifu  kwa kuibua mikakati mipya kupunguza matumizi na kuzalisha  faida kubwa ili  hatimaye waweze kutumia vifaa vyake badala ya kukodi.

“ Ukiangalia  gharama inayotumika kukodi mashine  za uchorongaji  na uchimbaji madini na nyinginezo utabaini kubwa sana ambapo kama STAMIGOLD ingejipanga ingekuwa na uwezo kabisa wa kununa mashine na mitambo yake yenyewe na kuepuka gharama kubwa za kukodi.
Aidha, Waziri Kairuki alielekeza Bodi ya  Wakurugenzi wa Shirika la  Madini la Taifa (STAMICO)  kwa kushirikiana  na menejimenti  ya Mgodi wa STAMIGOLD kuwasilisha mpango wa kibiashara wenye kuainisha gharama za uzalishaji, mapato na faida.

“ Tunataka kuanzia sasa STAMIGOLD uwe ni mgodi wa mfano wenye kuzalisha kwa faida Tanzania, badala ya kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki aliutaka Mgodi wa STAMIGOLD  kutumia Wakala wa Jiolojia  Tanzania (GST) kwenye tafiti zake za madini kwa kuwa  wakala huo una  wataalam na maabara za kutosha.

Alieleza kuwa kutokana na wakala huo kuwa na uzoefu katika utafiti wa madini ni muhimu kwa Mgodi wa STAMIGOLD kushirikiana nao kwenye utafiti wa madini kama njia mojawapo ya kuboresha  tafiti zake.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliitaka STAMIGOLD  kuwa wabunifu kwa kufanya utafiti na kubaini maeneo  yenye mashapo ya madini ya dhahabu ili kuwa na  miradi endelevu ya uchimbaji madini

Alisema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, hivyo inaanza na usimamizi wa karibu kwa migodi yote inayosimamiwa na serikali, binafsi na wachimbaji wadogo na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

alipongeza ujio wa Waziri na Naibu Waziri wa Madini katika mgodi huo na kuahidi kutekeleza kwa wakati maelekezo  yaliyokuwa yametolewa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Balozi Alexander Muganda
Alisema pamoja na mgodi kuwa na changamoto nyingi za kiuendeshaji kama bodi watahakikisha wanasimamia masuala ya kiutendaji kwa karibu zaidi, kushauri na kuwasilisha  ripoti za mara kwa mara kwa Waziri na Naibu Waziri wa Madini.

 Wakati huo huo Waziri Kairuki pamoja na Naibu wake Nyongo, walikutana na wafanyakazi  wa Mgodi wa STAMIGOLD Biharamulo ili kusikiliza kero mbalimbali na kuzitatua.
Katika kikao hicho Waziri Kairuki ameelekeza Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la STAMICO pamoja na  uongozi wa Mgodi wa STAMIGOLD Biharamulo kuzingatia maslahi ya watumishi  ikiwa ni pamoja na kupata mishahara kwa wakati, kuwa na bima za afya, kufuata utaratibu wa manunuzi na  kuwepo kwa uwazi kwenye uzalishaji.

Katika kikao hicho ameagiza  bodi hiyo,  kumsimamisha kazi aliyekuwa afisa manunuzi, January Kinunda kwa kushindwa kusimamia mkataba wa ukodishaji wa mashine kwa ajili uchorongaji.
Awali ilielezwa katika kikao hicho kuwa mashine hizo mbili zililetwa kwa dharura huku zikiwa si mpya  ambapo zimekuwa zikiharibika mara kwa mara na kufikia hatua  ya moja kufanya kazi mara moja kwa wiki na kukwamisha uzalishaji katika

Waziri Kairuki, Nyongo Wakutana Na Femata Geita


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (mbele katikati) wakiongoza kikao na baadhi ya  wawakilishi kutoka Shirikisho la  Vyama vya  Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) mkoani Geita 

 Rais wa Shirikisho la  Vyama vya  Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) Taifa,  John Bina (kulia) akieleza jambo katika kikao hicho. Kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo 

 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akifafanua jambo katika kikao hicho 

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wamekutana na wawakilishi kutoka Shirikisho la  Vyama vya  Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA) mkoani Geita lengo likiwa ni kubaini changamoto zao pamoja na kuzitatua. Kati ya maombi yaliyowasilishwa na wawakilishi hao ni pamoja na uwepo wa siku ya maadhimisho ya madini nchini, elimu kuhusu kanuni na sheria mpya za madini, maeneo zaidi kwa ajili ya uchimbaji madini na fidia kwa wananchi waishio ndani ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)

Wanaodai fidia mgodi wa Buckreef kuhakikiwa

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef, Peter Zizhou (kulia) akielezea teknolojia ya zamani ya  uchenjuaji wa dhahabu kwa  Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo uliopo mkoani Geita kwa ajili ya kujionea maendeleo ya shughuli zake tarehe 27 Oktoba, 2017. Kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akimshukuru  Kaimu Afisa Mtendaji kutoka Kampuni ya  Tanzanian Royalty Exploration, Jeffrey Duval (katikati) mara baada ya kampuni  hiyo kupitia Mgodi wa Buckreef ulioko mkoani Geita kutoa mchango wa madawati 105 yenye thamani ya shilingi milioni saba kwa ajili ya shule ya sekondari moja na shule za msingi nne zilizopo katika kata ya  Busanda wilayani Geita mkoani Geita. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Busanda,  Justa Mabala. 

Mmiliki wa Mgodi wa Busolwa Mining Limited, Christopher Kadeo (wa pili kulia mbele) akielezea shughuli zinazofanywa na mgodi huo kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ( kushoto mbele) mara walipofanya ziara katika mgodi huo.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema Serikali inatarajia kuwasilisha majina ya wananchi 1062 waliofanyiwa  tathmini katika eneo la Kiseme wilayani Geita ili kulipwa fidia  kwa ajili ya kupisha shughuli za uchimbaji madini za Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kufanyiwa uhakiki na kubaini uhalali wa umiliki wake kabla ya kuanza kwa taratibu za malipo.

Waziri Kairuki aliyeambatana na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameyasema hayo mapema leo  katika Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef uliopo wilayani Geita mkoani Geita  mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku moja katika mgodi huo ili kujionea maendeleo  ya mgodi huo na kutatua changamoto zake.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara zake pamoja na Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo katika migodi ya serikali, binafsi na wachimbaji wadogo katika mikoa ya  Kagera na Geita ili kufahamu kwa undani  mafanikio na namna ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta  ya madini.
Alisema kuwa, kabla ya kuanza kwa ulipaji wa fidia, ni lazima Wizara ya Madini ihakikishe majina ya wanaodai fidia yanafikishwa katika  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki na wataalam wa wizara hiyo  ili kuepuka udanganyifu kwenye umiliki wa ardhi.

Aliendelea kusema kuwa katika sekta ya madini kumekuwepo na migogoro mingi hususan katika  madai ya fidia kutokana na wamiliki wengi  wasiokuwa halali kujitokeza na kudai  fidia  hali inayochangia  wawekezaji kushindwa kulipa kutokana na gharama kuwa kubwa.

Katika hatua nyingine, Kairuki alitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lenye umiliki wa asilimia 45 katika mgodi  huo kwa niaba ya  Serikali kuhakikisha linafanya tathmini ya vifaa vyote vinavyotumika katika uchimbaji na uchenjuaji madini pamoja na mikataba  kati yake na mbia wake ambaye ni kampuni ya Tanzam 2000 mwenye asilimia 55.

“Mkumbuke kuwa mmepewa dhamana  na Serikali ya kusimamia mgodi huu, hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanaangaliwa huku mkifanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu  ili uchimbaji ulete tija,” alisema Kairuki.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza  katika kikao na  uongozi na wafanyakazi wa mgodi wa  dhahabu wa Busolwa Mining Limited, alisema kuwa Serikali ipo tayari kuwasaidia wachimbaji wadogo ili uzalishaji wao  ulete manufaa kwenye uchumi wa nchi.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wa madini hususan wazawa wanafanya  shughuli zao katika mazingira rafiki na kupata faida kubwa na kutoka kwenye lindi la umaskini

Alisisitiza wachimbaji wa madini kufuata kanuni na sheria katika shughuli zao na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutoa elimu kuhusu kanuni na sheria za madini.

Wachimbaji madini Maswa, waomba kufanyiwa utafiti


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akijibu kero mbalimbali za wakazi wa kitongoji cha Mwanguhi kilichopo wilayani Maswa mkoani Simiyu (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.

Sehemu ya wakazi wa kitongoji cha Mwanguhi kilichopo wilayani Maswa mkoani Simiyu wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara

 Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini, Sylivester Fundikira akiwasilisha kero yake mbele ya Naibu  Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (hayupo pichani). 

Wachimbaji wa madini ya  dhahabu katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu  wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kufanya utafiti wa madini katika maeneo yao ili waweze kuwa na uhakika wa  uchimbaji wa madini na uzalishaji wao kuwa na tija.

Wameyasema hayo leo  tarehe 29 Oktoba, 2017 katika ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu yenye lengo la kukusanya kero za wananchi mbalimbali hususan katika shughuli za uchimbaji madini.

Akizungumza kwa niaba yao, Sylivester Fundikira alisema kuwa wameunda jumla ya vikundi 30 ambapo kila kikundi kina mashimo yake na kueleza kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya upatikanaji   wa madini ya  uhakika kutokana na maeneo yao kutofanyiwa utafiti kwa muda mrefu.
Akijibu kero hiyo Naibu  Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa Wizara ya Madini kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imekuwa ikifanya  tafiti sehemu mbalimbali nchini na kusisitiza  kuwa Serikali  kupitia Wizara ya Madini ipo tayari kuwasaidia.

Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo wa madini na kuongeza kuwa imeweka mikakati ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwapatia  vifaa kupitia ruzuku ili uchimbaji wao uwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“ Tuna mpango wa kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinakuwa na mchango mkubwa sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo  tutahakikisha tunasimamia ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa mazingira ya uchimbaji madini yanakuwa rafiki,” alieleza Naibu Waziri Nyongo.

Katika hatua nyingine, Nyongo alisema kuwa kazi yake pamoja na  Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakua kwa kasi na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa sekta ya madini imekuwa na changamoto kubwa hususan katika upotevu wa mapato  kutokana na wawekezaji wasio waaminifu na kukwamisha juhudi za serikali katika ukusanyaji wa mapato. Aliendelea kusema kuwa tangu Rais John Magufuli ameanza kupambana na wezi wa rasilimali za madini kumekuwa na mabadiliko makubwa kwa kuwa uzalishaji na mapato umebadilika kutokana na Serikali kuhakikisha kiwango sahihi kinapatikana na kulipiwa kodi serikalini.
Alisema Serikali imeweka Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017 na kuwataka wachimbaji madini nchini kufuata sheria hiyo pamoja na kanuni zake.

Monday, November 20, 2017

Katibu Mkuu Mpya Madini Ahimiza Uwajibikaji



Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, amewataka watumishi wa Wizara kuwajibika katika nafasi zao ili wananchi wanufaike na matunda ya kazi zao kama inavyopaswa.
Profesa Msanjila aliyasema hayo jana, Oktoba 30, 2017 baada ya kuwasili rasmi Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma na kupata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi.
Alifafanua kuwa, uwajibikaji hupimwa kwa matokeo. “Tutakuuliza umefanya nini katika nafasi yako ili tuweze kupima utendaji wako.”

Aidha, Profesa Msanjila alisisitiza ushirikiano baina ya viongozi na wafanyakazi wote ili kupata matokeo chanya, hivyo kuleta manufaa katika sekta ya madini.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara ya Madini, Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, aliahidi ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi na uwajibikaji katika nafasi zao kama alivyoasa Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu Msanjila, alipokelewa na watumishi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Lusias Mwenda.