Thursday, September 13, 2018

Mwenyekiti wa Tume ya Madini akutana na Balozi wa India nchini


Na Greyson Mwase, Dodoma

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo tarehe 13 Septemba, 2018 amekutana na Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya jijini Dodoma. Lengo la ziara ya Balozi Arya kwenye Ofisi ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini lilikuwa ni kujitambulisha pamoja na kufahamu majukumu ya Tume.

Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Kikula alieleza kuwa Tume ya Madini imejipanga kusimamia Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 na  kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya madini nchini.

Alisema Sheria ya Madini ina  matakwa yake kama vile  local content, utoaji wa huduma kwa jamii kwenye shughuli za uchimbaji madini (corporate social responsibility) na kiapo cha uadilifu kwenye shughuli za uchimbaji madini (integrity pledge).

Alisema kuwa Tume imejipanga pia kutoa leseni haraka iwezekanavyo na kuwasaidia wachimbaji wadogo.

Akizungumzia namna Tume ya Madini ilivyojipanga katika kutatua changamoto ya migogoro kwenye Sekta ya Madini Nchini, Profesa Kikula alisema kuwa Tume inaandaa mpango  wa kutatua migogoro kuanzia katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa migogoro mingi inatatulika katika mamlaka za Vijiji, Kata na Wilaya.

Aidha, Profesa Kikula alimwomba Balozi wa India kuendelea kutoa ufadhili kwa wataalam wa Tume ya Madini hususan  katika maeneo ya Uchimbaji wa Madini kwa kutumia teknolojia ya kisasa, Usimamizi wa Rasilimali Watu na maeneo  mengine ili  kukuza Sekta ya Madini Nchini.

“ Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, na kama Tume  kwa kushirikiana na  Wizara ya Madini tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na wataalam wenye weledi kwenye usimamizi  wa Sekta ya Madini. Hivyo basi mafunzo  kwa wataalam  tunayapa kipaumbele sana,” alisisitiza Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alimwomba Balozi wa India kuendelea kutangaza Sekta ya Madini Nchini na kusisitiza kuwa Tanzania ina maeneo mengi yenye madini yaliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Jiolojia na  Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali.

Wakati huo huo Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya alisema kuwa nchi ya India ipo  tayari kushirikiana na  Tume ya Madini hususan  katika Sekta ya Madini na kusisitiza kuwa wapo tayari kutoa ufadhili kwa watumishi wa Tume.

Aliendelea kusema kuwa nchi ya India imekuwa ikitoa mafunzo ya muda mrefu  hususan katika ngazi za Shahada za Uzamili na za Uzamivu katika vyuo bora na kusisitiza kuwa itaendelea na mpango wake wa kutoa mafunzo hususan kwenye masuala ya madini.

Katika hatua nyingine,  Balozi Arya alimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kwa kuteuliwa kuongoza Tume hiyo pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Tume ya Madini kwenye uboreshaji wa Sekta ya Madini Nchini.


Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Tume zilizopo jijini Dodoma 

Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili  kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Tume  ya Madini, Profesa Idris Kikula zilizopo jijini Dodoma 

Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (kushoto) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia)

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akielezea majukumu  ya Tume ya Madini kwa Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (hayupo pichani)

Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya akifafanua jambo kwenye kikao hicho

Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (kushoto) akiagana na  Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) mara baada kumalizika kwa kikao kilichofanyika kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Tume zilizopo jijini Dodoma

Serikali yakusudia kuondoa kodi vifaa vya uongezaji thamani madini


Na Asteria Muhozya, Arusha

Serikali imesema inaangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya vifaa vya uongezaji thamani madini  ikilenga kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini  kufanyika nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akijibu swali la mwanafunzi wa Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC) Rojer Mpele aliyeiomba Serikali kupitia Naibu Waziri kuangalia namna ya kupunguza kodi ya vifaa hivyo ili  kuwasaidia wanafunzi wanaojifunza ukataji na ung’arishaji madini katika kituo hicho kuweza kujiajiri baada ya kuhitimu.

Nyongo ameongeza kuwa, tayari Serikali imeanza kufanya taratibu za kupeleka maombi  kuhusu jambo hilo katika Mamlaka husika ili liweze kufanyiwa kazi kwani litahamaisha uwekezaji wa viwanda vya uongezaji thamani madini nchini ikiwemo kuongeza wigo wa ajira na mapato kupitia sekta ya madini.

Naibu Waziri Nyongo amekitembelea kituo hicho kilichopo jijini Arusha kwa lengo la kujifunza shughuli zinazofanyika kituoni hapo. Kituo cha TGC kipo chini ya Wizara ya Madini, kinatoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji madini ya vito lengo likiwa ni kuongeza thamani madini.

Ameongeza kuwa suala la uongezaji thamani madini nchini ni jambo ambalo  ni  kipaumbele cha serikali kutokana na Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017 na kwamba tayari serikali imezuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na badala yake inahamasisha shughuli hizo kufanyika hapa hapa nchini kwa kuwa, zitawezesha kuleta ujuzi, ajira, mapato zaidi ya serikali na kuyaongezea thamani madini hayo nchini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi.

“Bado Wizara inaweka msisitizo wa shughuli za uongezaji thamani zifanyike hapa nchini. Kwa hiyo napenda kuwaambia ninyi vijana mnajifunza kitu ambacho ni kipaumbele kwa wizara na serikali,” amesisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri amesema kuwa, serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) unaotekelezwa  chini ya wizara kutokana na mkopo wa Benki ya Dunia, tayari umeagiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha karakana ya shughuli za uongezaji thamani madini katika kituo hicho, karakana hiyo inalenga kutumiwa na wahitimu wa kituo husika ili kwawezesha kujiajiri pindi wanapohitimu mafunzo yao.

“Watakaohitimu hapa watalipia gharama ndogo sana za mashine watakazokuwa wakizitumia kufanya kazi zao katika karakana hiyo. Lakini pia, ili kuboresha shughuli za karakana hiyo, tutaendelea kujifunza kwa nchi nyingine namna wanavyoendesha karakana zao,” ameongeza Nyongo.

Katika jitihada za kuendelea kukiboresha kituo husika, Naibu Waziri Nyongo amemtaka Mratibu wa Kituo hicho, kuandaa  Mpango Mkakati wa namna ya kukiboresha na kukitanua kituo hicho ili kiweze kuwa bora na mfano kwa nchi  nyingine  barani Afrika.

“Imefika wakati ambapo tunataka TGC kuwa chombo ambacho kinatoa ujuzi wa hali ya juu katika uongezaji thamani madini. Lazima tutoe mafunzo kwa vijana wa kitanzania  na tuendelee kuangalia namna ya kuleta ujuzi au kwa kuwapeleka vijana wetu kujifunza kwa wenzetu na baadaye wawe wakufunzi katika kituo hiki.

Vilevile, Naibu Waziri Nyongo amesisitiza kuwa, Serikali kupitia wizara ya Madini itaendelea kusimamia kwa karibu kuhakikisha kuwa inatekeleza na kutimiza malengo ya uanzishwaji wa kituo hicho. “Lazima ifike mahali kituo kitoe mafunzo kwa jinsi ilivyokusudiwa, ameongeza Nyongo.

Kwa upande wake,  Kaimu Mratibu wa Kituo cha TGC, Eric Mpesa amesema kuwa, kituo hicho ni kituo pekee Afrika Mashariki kinachoendeleza taaluma ya uongezaji thamani madini ya vito na miamba.

Pia, amesema kuwa, kituo kinakusudia kutoa mafunzo ya Diploma ya Gem Jewelly technology ambapo mhitimu katika mwaka wa Kwanza atapatiwa cheti cha NTA Level 4, mwaka wa pili NTA Level 5 na mwaka wa tatu NTA Level 6.

“Kwa kuwa mafunzo yanayotolewa katika kituo hiki ni ya muda mrefu na mfupi, taratibu za kukisajili kwenye Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) zilifanywa na kwa sasa kituo kimepata usajili wa kudumu wenye Na. REG/SAT/003,” ameongea Mpesa.

Mpesa ameongeza kuwa, wizara iliamua kuwekeza katika Kituo hicho kwa lengo la kutoa mafunzo ya kuongeza thamani madini ya vito kwa wadau na wajasiliamali wa madini hayo hapa nchini.

Ameongeza kuwa, malengo mengine ni pamoja na kukuza na kuendeleza ujuzi na ufahamu wa kutambua madini ya vito, kuongeza thamani kipato na ajira kwa watanzania.

“ Hivi sasa kituo hicho kinatoa mafunzo ya muda mfupi ya ukataji na unga’rishaji wa madini ya vito na kinaendesha shughuli za uchongaji wa mawe ya miamba kwa kutengeneza  wanyama, ndege, samaki na vitu mbalimbali vya mapambo, amesema Mpesa.

Kituo cha Jemolojia Tanzania (Tanzania Gemological Center-TGC) kilianzishwa mwaka 2003 wakati serikali ikitekeleza mradi wa Maendeleo Sekta ya Madini (Mineral Sector Development Technical Assistance – MSD TA) ambao ulitekelezwa kati yam waka 1994 na 2005 kwa mkpo kutoka benki ya Dunia. Wakati huo lengo la kuanzissha kituo hicho lilikuwa ni kutekeleza Sera ya Madini ya Mwaka 1997 kuhusu uongezaji thamani madini nchini kwa kuanzia na kutoa mafunzo ya uchongaji wa vinyago vya miamba.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipata ufafanuzi juu ya utambuzi wa madini yaliyokatwa na kunga’rishwa na wanafunzi waliopata mafunzo  katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Kushoto ni  Mkufunzi katika Kituo hicho ambaye ni mhitimu katika kituo husika, Doricas Michael. 

Mmoja wa Wanafunzi wanaofanya mafunzo ya ukataji na unga’rishaji madini ya vito katika Kituo ch Jemolojia Tanzania (TGC). 

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipata ufafanuzi  kutoka kwa Mjiolojia na Mkufunzi wa Ukataji na Unga’rishaji wa madini ya vito kutoka katika  Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Ester Njiwa, kuhusu namna mashine ya kunga’risha madini inavyofanya kazi wakati alipokitembelea kituo hicho. Mkufunzi huyo aalipata mafunzo kutoka nchini Sri-Lanka. 

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipata ufafanuzi  kutoka kwa Mjiolojia na Mkufunzi wa Ukataji na Unga’rishaji wa madini ya vito kutoka katika  Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Ester Njiwa, kuhusu namna mashine ya kunga’risha madini inavyofanya kazi wakati alipokitembelea kituo hicho. Mkufunzi huyo aalipata mafunzo kutoka nchini Sri-Lanka. 

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiangalia moja ya Mashine zinazotumika kufanisi madini ya vito na miamba  wakati alipotembelea Kituo cha jemolojia Tanzania (TGC). 

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika picha ya panoja na Wanafunzi wanaopata mafunzo ya Ukataji na Unga’rishaji wa madini ya vito.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo  katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC).

Monday, September 10, 2018

Profesa Kikula atoa mwezi mmoja utatuzi wa mgogoro wachimbaji madini Winza


Na Greyson Mwase, Dodoma

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ametoa mwezi mmoja kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya kuhakikisha mgogoro katika machimbo ya madini aina ya rubi yaliyopo katika kijiji cha Winza kilichopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma unamalizika ili wachimbaji hao waendelee na shughuli zao za uchimbaji madini na kujipatika kipato.

Profesa Kikula ametoa agizo hilo mara baada ya kupokea kero za wachimbaji wadogo wa madini katika eneo hilo katika ziara yake katika wilaya ya Mpwapwa yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wadogo wa madini.

Katika ziara hiyo Profesa Kikula aliambatana na Makamishna wa Tume, Profesa Abdulkarim Mruma na Haroun Kinega, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya pamoja na waandishi wa habari.

Alimtaka Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto na  Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya kushirikiana kwanza kwa kuchukua alama za eneo (coordinates) ili kubaini maeneo yasiyo na leseni na kuwapatia wachimbaji hao ili wafanye uchimbaji bora wenye kufuata sheria na kanuni za madini.

Aliendelea kufafanua kuwa, kwa maeneo yenye leseni wachimbaji wadogo wa madini wanaweza kuangalia namna ya kushirikiana na wamiliki wa leseni kwa kuingia ubia na kujipatia kipato pasipo migogoro isiyo ya lazima.

Profesa Kikula alisisitiza kuwa lengo la Serikali kupitia Tume ya Madini ni kuona wachimbaji wadogo wa madini wanafanya shughuli zao katika mazingira mazuri kwa kufuata kanuni na sheria za madini.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wachimbaji hao kuunda vikundi vidogo na kuomba leseni na kusisitiza kuwa Tume ya Madini ipo tayari  kuwasaidia kwa njia zote kupitia wataalam wake ikiwa ni pamoja na namna ya kuomba leseni za madini, elimu kuhusu kanuni na sheria za madini.

Wakiwasilisha kero zao kwa Mwenyekiti Kikula kwa nyakati tofauti, wachimbaji hao walisema kuwa wamekuwa wakifanya shughuli zao kwa muda mrefu pasipokuwa na leseni huku kukiwepo na watu wanaojitokeza na kudai kuwa ni wamiliki halali wa leseni za madini.

Awali akielezea historia ya ugunduzi wa madini aina ya rubi katika eneo hilo, mgunduzi ambaye ni mwenyeji wa kijiji hicho,  Shabani Kigelulye alisema kuwa, kati ya mwaka 2005 na 2006 akiwa shambani kwake katika eneo hilo aligundua mawe aliyohisi kuwa ni madini ya rubi.

Alieleza kuwa, katika harakati za utafiti wa  madini hayo mwaka 2007 alipeleka sampuli za mawe hayo aliyohisi kuwa ni madini ya rubi kwa ndugu wake walioko Dodoma Mjini na Arusha na kuelezwa kuwa yalikuwa ni madini ya rubi.

Aliendelea kueleza kuwa kwa kushirikiana na ndugu zake alipeleka sampuli hizo za mawe kwenye Ofisi za Madini na kushauriwa kuomba leseni na kupata.

Aliongeza kuwa  mwaka 2008 aliingia ubia na  wenzake Roja Sezinga, Johnson Kamara na Perfect Shayo na kuanza uchimbaji wa madini, na kusisitiza kuwa mwaka 2009 wakazi wengi wa kijiji hicho waliingia na kuanza kuchimba kiholela pasipokuwa na leseni hali iliyopelekea mgogoro.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula alitembelea eneo lililopangwa kujengwa mtambo wa kuyeyushia shaba na kukuta jengo lililotelekezwa tangu mwaka 2004

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto alimweleza Profesa Kikula na timu yake kuwa, kampuni ya Igozomo kutoka China ilipanga kujenga mtambo wa kuyeyushia shaba lakini baadaye walisitisha uwekaji wa mtambo huo baada ya kutoelewana na wazawa.

Profesa Kikula alishauri wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye shughuli za madini nchini kukutana na wenyeviti wa vyama vya wachimbaji madini ambao wanaweza kuwapa taratibu sahihi za uwekezaji nchini hivyo kuepuka kuingia kwenye mikono ya matapeli.

Wakati huohuo akiwa katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema kuwa suala ushiriki wa huduma za jamii (corporate social responsibility) kwa makampuni ya madini nchini si la hiari bali ni moja ya sheria.

Aliendelea kufafanua kuwa ni vyema kukawepo  mikataba kati ya wakuu wa wilaya na kampuni za madini kuhusu maeneo yanayohitaji katika uboreshaji wa huduma za jamii na kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na huduma zilizoainishwa kwenye mikataba na kupunguza migogoro.

“ Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka  mikakati ya kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za madini kupitia ushirikishwaji wananchi kwenye utoaji wa huduma kwenye kampuni za madini (local content) na kupata huduma bora za jamii kutokana na uwekezaji unaofanywa na kampuni za madini,” alisisitiza Profesa Kikula.

Akielezea mikakati ya kumaliza migogoro kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini nchini, Profesa Kikula alisema kuwa Tume ya Madini inaandaa rasimu ya mfumo wa utatuzi wa migogoro  kuanzia kwenye ngazi ya kijiji, kata na wilaya kabla ya kufikia ngazi ya tume.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba alimpongeza na kumshukuru Profesa Kikula pamoja na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutatua changamoto kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini na kutoa elimu kuhusu sheria na kanuni za madini

Aidha Komba aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kutoa taarifa za wavamizi wasiokuwa na leseni za madini ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma akizungumza katika mahojiano maalum na vyombo vya habari aliwataka wananchi wanaogundua madini kwenye maeneo yao kutoa taarifa kwenye ofisi za vijiji na vyama vyama vya wachimbaji madini na kufika kwenye Ofisi za Madini  kwa ajili ya utambuzi wa madini na  kuelekezwa namna ya kuomba leseni.

Alisema kutokana na wagunduzi wengi kuchimba bila kushirikisha uongozi wa kijiji, wilaya na vyama vya wachimbaji madini wamejikuta wakitoa mwanya kwa wajanja kuomba leseni hivyo kuzalisha migogoro isiyokwisha.

Alisema kuwa Serikali kupitia Tume ya  Madini imeweka utaratibu mzuri sana wa kumlinda mgunduzi wa madini tangu anapogundua madini hayo hadi kupata leseni.


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akisalimiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba (kulia) mara baada ya kuwasili kweye Ofisi ya Katibu Tawala huyo. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akielezea mikakati ya Tume ya Madini kwenye uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini nchini kwenye ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba. 

Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya kijiji cha Winza kilichopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. 

Jengo lililojengwa kwa ajili ya kusimikwa mtambo wa kuyeyushia shaba na kampuni ya Igozomo ya China lililopo katika kijiji cha Winza wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Winza yaliyopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. 

Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Winza yaliyopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Prof. Kikula aagiza kikundi cha wachimbaji madini kupewa leseni ndani ya mwezi mmoja


Na Greyson Mwase, Dodoma

Septemba 06, 2018

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amemwagiza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya kuhakikisha wanakipatia kikundi cha wachimbaji wadogo wa madini kijulikanacho  kwa jina la “Hapa Kazi Tu” kinachoendesha shughuli za uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika kijiji cha Suguta wilayani Kongwa mkoani Dodoma leseni ya uchimbaji madini ndani ya mwezi mmoja kwa kufuata kanuni na sheria za madini.

Profesa Kikula alitoa agizo hilo tarehe 05 Septemba, 2018 katika  machimbo ya madini hayo yaliyopo katika kijiji hicho kwenye ziara yake ya siku mbili katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.

Katika ziara hiyo, Profesa Kikula aliambatana na Makamishna wa Tume, Profesa Abdulkarim Mruma na Haroun Kinega, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya pamoja na waandishi wa habari.

Mara baada ya kusikiliza kero za wachimbaji wadogo hao Profesa Kikula mbali na kutoa  agizo hilo alimwelekeza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto, kuhakikisha anasaidia kikundi cha wachimbaji wadogo hao katika taratibu zote za usajili wa kikundi  kabla ya kuanza kushirikiana na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma katika upatikanaji wa leseni ndani ya mwezi mmoja.

Aidha, Profesa Kikula alimtaka Mwenyekiti huyo kuwasaidia wachimbaji hao katika usajili kwenye vyama vya  wachimbaji madini Tanzania pamoja na utafutaji wa masoko na bei elekezi kwenye masoko ya kimataifa.

“Kutokana na kuwa na mtandao mkubwa na uelewa kwenye masoko na bei elekezi za madini kwenye masoko ya kimataifa, nakuelekeza kama Mwenyekiti wa wachimbaji kuhakikisha unawasaidia wachimbaji hawa hususan kwenye maeneo ya masoko na bei elekezi ili uchimbaji wao uwanufaishe wao na Serikali kupata mapato stahiki,” alisema Profesa Kikula.

Profesa Kikula alisema Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia uboreshaji wa sheria na kanuni za madini pamoja na utoaji wa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu sheria na kanuni hizo.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wachimbaji wadogo nchini kuhakikisha kupitia viongozi wao kwenye vyama vya  wachimbaji madini wanashirikiana kwa karibu na viongozi wa vijiji, wilaya na ofisi za madini ili uchimbaji wao ulete tija zaidi kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Awali, wakiwasilisha kero mbalimbali wachimbaji hao walisema kuwa wamekuwa wakikutana na vikwazo mbalimbali kwenye usajili wa kikundi chao hali iliyopelekea ucheleweshwaji wa maombi ya leseni.

Akizungumza kwa niaba ya kikundi hicho, Job Pandila alisema awali waliwasilisha maombi yao kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya taratibu za usajili lakini kumekuwa na ugumu katika usajili wa kikundi chao kutokana na kutokuwa na uelewa wa namna bora ya kuwasilisha viambatisho kwenye maombi ya usajili wa kikundi.

Pandila aliendelea kusema kuwa uchelewaji wa usajili wa kikundi umepelekea kushindwa kuomba leseni ya madini na kuomba msaada katika usajili wa kikundi pamoja na maombi ya leseni ili waendelee na uchimbaji wa madini na kujipatika kipato.

Awali kabla ya kufika katika kijiji cha Suguta, Profesa Kikula alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembie na kuelezwa changamoto mbalimbali kwenye shughuli za uchimbaji madini zilizopo katika wilaya ya Kongwa.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembie alisema kumekuwepo na mgogoro kwenye eneo la Suguta lililopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma kutokana na wachimbaji wengi kutokuwa na leseni za uchimbaji madini pamoja na uelewa mdogo wa sheria na kanuni za uchimbaji madini.

Aidha,  Ndejembie alimpongeza Profesa Kikula na timu yake kwa kutembelea wilaya ya Kongwa na kusisitiza kuwa ziara hiyo mbali na kutoa elimu kwa wachimbaji madini, itapunguza migororo isiyo na lazima iliyokuwa ikijitokeza.

Wakati huo huo katika kikao chake na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Profesa Kikula aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kuandaa utaratibu wa utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji madini kuhusu sheria na kanuni za uchimbaji madini.

Katika ziara hiyo Profesa Kikula pamoja na ujumbe wake, walitembelea pia machimbo ya Rays Metal Corporation na Tambi Minerals Resources yaliyopo katika kijiji cha Tambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembie. Kushoto ni Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Deogratius Ndejembie (kulia) mara baada ya kumalizika kwa kikao kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo. 

Kutoka kushoto, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya, Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Deogratius Ndejembie na Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kikao hicho. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) na Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma (kulia) wakiangalia moja ya mawe ili kubaini madini yaliyomo kwenye machimbo ya Suguta yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (hayupo pichani) kwenye machimbo ya Suguta yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara kwenye kwenye machimbo ya Suguta yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

Mmoja wa watendaji wa migodi ya shaba ya Rays Metal Corporation na Tambi Minerals Resources iliyopo katika kijiji cha Tambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati). Kulia ni Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega. 

Sehemu ya mgodi wa shaba wa Rays Metal Corporation uliopo katika kijiji cha Tambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Thursday, September 6, 2018

Naibu Waziri Biteko afanya ziara ya kushtukiza mgodi wa MMG na kubaini madudu


·        Abaini raia wa kigeni 10 wasio na vibali vya kazi waliokuwa wamejificha ndani ya mgodi
·        Atoa wiki moja mikataba ya ajira kwa wafanyakazi

Na Greyson Mwase, Musoma

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko leo tarehe 29 Agosti, 2018 amefanya ziara ya kushtukiza katika Mgodi wa Dhahabu wa MMG unaomilikiwa na kampuni ya Waarmenia uliopo katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Mara baada ya kuwasili katika mgodi huo na kupata maelezo ya namna ya uendeshaji wa mgodi huo kutoka kwa Meneja Uendeshaji,  Sezgey Sazgyyan aliendelea na  ukaguzi wa mgodi na kubaini ukiukwaji wa  kanuni za usalama migodini ikiwa ni pamoja na watumishi kufanya  kazi katika mazingira hatarishi pasipokuwa na  vifaa vya usalama mgodini.

Mara baada ya kutoa maelekezo, Naibu Waziri Biteko alifanya kikao na uongozi wa mgodi pamoja na wafanyakazi wa mgodi huo lengo likiwa ni kusikiliza kero mbalimbali pamoja na kuzitatua.

Akitoa maelezo kuhusu idadi ya wataalam wa kigeni na wa kitanzania katika mgodi huo wakati wa uwasilishaji wa  taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mgodi huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 Afisa Utumishi wa mgodi huo,  Rose Masanja alisema mgodi mpaka sasa una wafanyakazi 126 wa kitanzania ambao ni pamoja na vibarua kutoka katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa mgodi na wataalam watatu kutoka nje ya nchi.

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Naibu Waziri Biteko alimbana Masanja na kumtaka kutoa taarifa sahihi kuhusu  idadi ya wataalam wa kigeni wanaofanya kazi kwa kuwa taarifa zote anazo kiganjani mwake kabla ya kufanya ziara katika mgodi huo.

Mara baada ya kauli ya Naibu Waziri Biteko, Masanja alieleza kuwa kuna wafanyakazi wa kigeni takribani 10 wasio na vibali vya kazi na wamejificha ndani ya vyumba na kuelekeza kwenye vyumba walivyojificha.

Naibu Waziri Biteko akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Anney, Meneja Uendeshaji wa Mgodi huo, Sezgey Sazgyyan  alielekea kwenye vyumba walivyojificha na kufanya msako na kubaini watumishi wa kigeni wasio kuwa na vibali wamejificha kwenye vitanda.

Aidha, Biteko alibaini baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo waliokuwa wamefungiwa chooni kwa takribani masaa matatu na uongozi ili kuficha aibu ya kutokuwa na vifaa usalama migodini. 

Biteko alimwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Anney kuwachukulia hatua za kisheria wafanyakazi hao ambapo bila kusita Mkuu wa Wilaya huyo alielekeza Ofisi ya Wilaya ya Uhamiaji kufika muda huohuo kuwakamata na kuwafikisha kwenye ofisi hizo kwa ajili ya kutoa maelezo.

Katika hatua nyingine, Biteko alisikiliza kero mbalimbali za watumishi wa mgodi huo ambapo alielezwa kuwa watumishi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya shida ikiwa ni pamoja na kukosa huduma zote muhimu kama maji salama na matibabu.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake,  Afisa Usalama wa Mgodi huo,  Stephen Wambura alisema watumishi wa kitanzania wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira yasiyo salama bila kuwa na mikataba ya ajira na pale alipokuwa akiushauri uongozi wa mgodi kutatua changamoto hizo alikuwa akiambulia matusi.

“Mheshimiwa Naibu Waziri, tunashukuru sana kwa kufanya ziara katika mgodi huu kwani tumekuwa tukifanya kazi kama watumwa huku tukikosa huduma muhimu hali inayohatarisha usalama wa afya zetu,” alisema Wambura.

Naye Zuwena Swedi ambaye ni muuguzi wa kituo cha huduma ya kwanza cha mgodi huo aliongeza kuwa amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kutopewa muda wa kutosha kupumzika hasa ikizingatiwa kuwa ni mama wa mtoto mchanga.

Wakati huo huo akihitimisha kikao hicho, Naibu Waziri Biteko alitoa wiki moja kwa uongozi wa Mgodi kuhakikisha umesaini mikataba na watumishi.

Alisema kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji kufanya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini, hivyo wawekezaji wanaowekeza nchini wanatakiwa kufuata sheria na kanuni za utafiti na uchimbaji wa madini.

“Ni lazima wawekezaji wakahakikisha kuwa wanafuata kanuni na sheria za madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watumishi wa kitanzania wanafanya shughuli za utafutaji na uchimbaji madini katika mazingira yaliyo salama kwa afya na kupata stahiki zao kwa wakati,” alisisitiza Biteko.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaongeza mchango wake kwenye pato la taifa, serikali imeboresha sheria na kanuni za madini ambazo zitakuwa na manufaa kwa watanzania na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mara, Vicent Anney akizungumza katika kikao hicho aliwataka watumishi wa mgodi kutoa taarifa zozote za ukiukwaji wa sheria na kanuni za nchi na madini na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kwa ajili ya kuwatetea.

Pamoja na ziara katika mgodi huo, Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika machimbo ya wachimbaji wadogo yaliyopo katika eneo la Ikungwi, Musoma Vijijini  na kuwataka wachimbaji hao kutotumia zebaki katika uchenjuaji wa madini.


Meneja Uendeshaji wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG, Sezgey Sazgyyan (kulia) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) mara  baada ya kuwasili kwenye mgodi huo kwa ajili ya ziara yake tarehe 29 Agosti, 2018. 

Sehemu ya watumishi wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG wakisikiliza maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) katika kikao chake na uongozi na watumishi hao. 

Afisa Usalama wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG, Stephen Wambura akiwasilisha kero yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani). 

Sehemu ya raia wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa MMG pasipokuwa na vibali vya kazi nchini.
Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa MMG uliopo wilayani Musoma mkoani Mara.