Wednesday, February 27, 2019

Prof. Msanjila ashikilia msimamo wa serikali kuhusu mgodi wa North Mara


Na Issa Mtuwa, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini imesema bado imeshikilia msimamo wake kuhusu muda uliotolewa kwa Mgodi wa North Mara kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa kwenye kikao cha Januari 9, 2019 kuhusu Bwawa la kuhifadhi topesumu (Tailings Storage Facility -TSF).

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila Februari 26, 2019 wakati akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake Jijini Dodoma, mara baada ya kufungua kikao cha pamoja baina ya wajumbe kutoka serikalini na wajumbe kutoka Mgodi wa North Mara waliokutana kujadili kuhusu hatua zilizofikwa na Mgodi katika kutekeleza maagizo hayo.

Amesema serikali haitoongeza muda zaidi ya ule uliotolewa katika kikao cha awali, na kusema kuwa msimamo wa serikali utabaki kuwa hivyo.

 “Ndugu zangu katika kikao hiki kilenge kutoa majibu ya utekelezaji wa maagizo ya serikali kama yalivyowasilishwa kwenye kikao cha Januari 9, 2019, ni kwa kiasi gani mmetekeleza maagizo hayo,” alisema Prof. Msanjila.

Serikali kupitia kikao chake cha Januari 9, 2019 chini ya Makatibu Wakuu wa wizara saba (Madini, Makamu wa Rais Mazingira (NEMC), Ardhi, TAMISEMI, Afya, Fedha na Maji) kilitoa maagizo mbalimbali yakiwemo: Kujenga TFS mpya na Kukarabati TFS iliyopo kwa aajili ya kudhibiti mtiririko wa topesumu, maagizo ambayo mgodi ulipewa kuyatekeleza kwa muda wa miezi Nane (8) kuanzia Januari 9, 2019.

Akiongoza wakati wa mjadala wa uwasilishaji wa mada mbalimbali wa kikao hicho, chini ya Mwenyekiti wa kikao hicho Prof. Hudson Nkotaga aliwataka North Mara kueleza namna gani wametekeleza maagizo ya serikali kwa lengo la kupata mrejesho wa utekelezaji.

Kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo, Meneja Usalama, Afya na Mazingira Reuben Ngusaru, kutoka mgodi wa North Mara amesema mgodi umeanza kutekeleza maagizo hayo na bado wanaendelea kutekeleza maagizo hayo na hata kikao cha tarehe 26 Februari ikiwa ni moja mkakati wa kutekeleza maagizo hayo kwa ufanisi.

Akizungumzia kuhusu hatua zilizochukuliwa na mgodi kudhibiti uvujaji unaoendelea kwenye (TSF) mpaka kufikia siku ya kikao cha Februari 26, mambo yaliyotekelezwa ni pamoja na: Kuondoa mawe na kusafisha mtaro uliopo upande wa Kaskazini mwa TSF. Kuvukiza (evaporation) maji yaliyotokana na uchenjuaji wa mawe yanayotengeneza tindikali asili (PAF Rock) (leachate water) badala ya kuyapeleka yote kwenye TSF na Programu zote zilizokuwepo za kupunguza maji katika TSF bado zinaendelea.

Aidha, kuhusu utekelezaji uliofikiwa katika kutekeleza agizo la Serikali la kujenga TSF mpya (Construction of a new TSF) Reuben amesema mpaka kufika tarehe 26 Februari, mgodi umefanya utambuzi wa eneo linalofaa kwa ajili ya ujenzi wa TSF mpya (Site Identification) nau sanifu wa awali (Conceptual design) ambapo usanifu wa awali umefanyika na ujenzi wa TSF mpya unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani milioni 45 za tope sumu (tailings) kavu kwa kadirio la ongezeko la tani 8200 kwa siku.

Maagizo ya serikali kwa mgodi wa North Mara yalitokana na ukaguzi uliofanywa na serikali kwenye mgodi huo uliohusisha timu kutoka ofisi mbalimbali za serikali zikiwemo, NEMC, Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, na Wizara ya Afya, uliopelekea kutolewa kwa maagizo yaliyolenga kudhibiti uharibifu wa mazingira uliokuwa unafanywa na mgodi.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila mwenye tai katikati kushoto akisikiliza na kufuatilia maelezo ya baadhi ya wajumbe wa kikao hicho mara baadaa ya kukifungua rasmi jana Jijini Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila mwenye tai katikati kushoto akimsikiliza mmoja wa wajumbe wa kikao hicho wakati akichangia. 

Leseni za migodi mikubwa kutolewa karibuni


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini inakamilisha taratibu za utoaji wa Leseni kwa Migodi Mikubwa ambazo hazijawahi kutolewa nchini, huku migodi hiyo ikitarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila alipokutana na viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi ofisini kwake, jijini Dodoma.

Viongozi hao walikutana na Prof. Msanjila Februari 26, kwa lengo la kujitambulisha, kuelewa shughuli za serikali upande wa sekta ya madini, kupata uelewa kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Madini na namna pande hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika kuendeleza sekta husika.

Prof. Msanjila aliwakaribisha viongozi hao kwenye sekta ya madini huku akiwataka kuzishawishi kampuni mbalimbali kuwekeza nchini hususani katika shughuli za uongezaji thamani madini na kueleza kuwa, suala hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo serikali inayapa kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vinu vya kusafisha na kuyeyusha madini.

Akizungumzia Sheria Mpya ya Madini ya Mwaka 2017, Prof. Msanjila amesema hakuna tatizo lolote katika utekelezaji wa sheria na kueleza kuwa, serikali kupitia wizara ya madini inapokea wawekezaji wengi wenye utayari na nia ya kuwekeza nchini huku utekelezaji wa sheria hiyo ukiwa si kikwazo na kuongeza kwamba, “hakuna mahali ambapo serikali inatengeneza sheria kwa ajili ya kumkandamiza mfanya biashara”.

“Hakuna tatizo lolote kwenye sheria ya madini. Hata wageni huwa tunakaa nao tunawaelimisha na wanatuelewa vizuri.  Kama kuna dosari ni vitu ambavyo tunaweza kuvirekebisha na tayari tumekwishakufanya hivyo kwa baadhi ya maeneo,” alisema Prof. Msanjila.

Aidha, katika kikao hicho Prof. Msanjila alitoa ushauri kwa viongozi hao kujitangaza zaidi kuhusu kazi zao huku akiwataka kutafuta wasaa kwa ajili ya pande hizo mbili kukutana ili wizara iweze kutoa elimu zaidi kwa Jumuiya hiyo kuhusu sekta ya madini ikiwemo fursa za uwekezaji zilizopo.

Pia, Prof. Msanjila alisema kuwa suala la kuaminiana linaweza kujengwa huku akiwataka watanzania kuwa wazalendo na namna wanavyotumia fedha za umma. Prof. Msanjila alizungumzia jambo hilo baada ya mmoja wa viongozi hao kueleza kuwa, bado kuna hali ya kutokuaminiana baina ya serikali na taasisi binafsi.

Kwa upande wake, mmoja wa viongozi wa jumuiya hiyo, Francis Nanai ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited amemweleza Prof. Msanjila kuwa, kama viongozi wa umoja huo, wamezipokea changamoto zilizotolewa kwao na Prof. Msanjila ikiwemo ushauri wa kukutana na wizara kwa lengo la kupata ufafanuzi na elimu  zaidi  kuhusu sekta ya madini.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (kulia) akizungumza jambo wakati wa kikao baina yake na Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi. Kushoto ni mmoja wa viongozi hao. 

Mmoja wa Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi akizungumza jambo katika kikao hicho. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Wizara ya Madini, Godfrey Nyamrunda. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila  wakijadiliana jambo na baadhi Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi. 

Mmoja wa viongozi wa jumuiya Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi, Francis Nanai ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, akizungumza jambo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila katika picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi.

Tuesday, February 26, 2019

Prof. Msanjila aongoza wadau kujadili rasimu Kanuni Uanzishwaji wa Masoko ya Madini nchini


Na Nuru Mwasampeta,

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ameongoza kikao kilicholenga kupokea maoni juu rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wizara kimewakutanisha, Makamishna Wasaidizi wa Wizara, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina, viongozi wa shirikisho hilo pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo kutoka mikoa ya kimadini nchini.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa kikao, Prof. Msanjila alisema maoni ya wajumbe hao ni muhimu kwa watanzania na taifa kwa ujumla katika kuboresha kanuni hizo.

Aidha, Msanjila amebainisha kuwa, wadau wengine wamekwisha kutoa maoni yao katika makundi tofauti tofauti na pia maoni mengine yanaendelea kupokelewa kwa njia ya maandishi na kuwataka maoni hayo yakamilishwe ndani ya kipindi cha wiki moja.

Kabla ya kupokea maoni hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge aliwasilisha rasimu ya kanuni hizo ili kutoa uelewa wa kile wanachopaswa kuchangia katika kutoa maoni yao.

Akiwasilisha rasimu hiyo, Igenge alisema hii ni sheria ndogo inayotokana na sheria mama ya madini. “Kanuni hizo zinatungwa kwa mujibu wa kifungu cha 27 (C) kifungu kidogo cha pili pamoja na kifungu cha 129 cha sheria ya madini,” amesema Igenge.

Aidha, amesema mahala patakapo kuwa na soko la madini kutakuwa na huduma zote zinazotakiwa ili kurahisisha ubadilishwaji wa fedha na  madini kama vile mabenki, ofisi za mamlaka ya Mapato (TRA), ofisi za masuala ya ulinzi na usalama, pamoja na ofisi mbalimbali za serikali.

Igenge amesema baada ya kukamilika na kupitishwa kwa kanuni hizo zitatafsiriwa na kupatikana katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wote kuelewa kanuni na mwongozo wa masoko ya madini.

Akizungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo katika rasimu hiyo, Igenge alisema sehemu ya kwanza inahusika na utangulizi yenye vifungu 3 cha kwanza ni jina la kanuni ambapo litaitwa ‘Kanuni za masoko za mwaka 2019’, pili ni maelezo ya wapi kanuni hizo zitatumika na kuratibiwa na kipengele cha mwisho kitatoa tafsiri ya maneno mbalimbali yanayotumika ndani ya kanuni hizo.

Sehemu ya pili ya kanuni inahusika na uanzishwaji wa masoko yenyewe, ambapo masoko yataanzishwa katika maeneo yenye tawala za mikoa na kuipa maelekezo Tume ya Madini kuhakikisha wanashirikiana na tawala za mikoa katika kuanzisha masoko hayo.

Aidha, alielezea msingi wa kwanza ni msingi wa uwazi, msingi wa matangazo ili watu waweze kujua madini yanauzwa na kununuliwa wapi, msingi wa haki ambao utazuia manunuzi haramu ya madini, lakini pia msingi wa mwendelezo ikiwa na maana masoko hayo kuwa ni masoko ya kudumu na si ya msimu.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameiomba serikali kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wawakilishi wa wachimbaji wadogo ili kupata kitu kitakachokubalika na jamii nzima ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.

Aidha, alikiri kufurahishwa na ufafanuzi uliotolewa katika kila kipengele cha rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini na kukiri kwamba wanaamini kuwa serikali ina nia njema na wananchi wake.

Wajumbe wa mkutano wa kutoa na kupokea maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini wakifuatilia mada.

Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge akiwasilisha rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.

Katibu Mkuu wa Madini, Prof Simom Msanjila mbele (mwenye koti jeusi) akiongoza kikao cha kupokea maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini waliofika ili kutoa maoni yao juu ya rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini. Kulia kwa Katibu Mkuu ni Rais wa FEMATA John Bina na Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara Edwin Igenge

Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila akifafanua jambo wakati wa upokeaji wa maoni kutoka kwa wawakilishi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini.

Friday, February 22, 2019

Wachimbaji madini watakiwa kuwa na mpango wa ufungaji Mgodi


Na Greyson Mwase, Pwani

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini  ya ujenzi  aina ya kokoto katika mkoa wa Pwani kuwa na Mpango wa Ufungaji Mgodi utakaotumika kama mwongozo wa kuhakikisha mazingira yanaachwa yakiwa katika hali salama mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini hayo.

Profesa Kikula aliyasema hayo leo tarehe 21 Februari, 2019 katika nyakati tofauti alipofanya ziara yake katika migodi  inayojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi aina ya kokoto iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani yenye lengo la kutembelea wachimbaji wa madini hayo pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Profesa Kikula katika ziara hiyo akiwa ameambatana na Kamishna - Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, wataalam kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa Lugoba pamoja na waandishi wa habari, Profesa Kikula alitembelea migodi ya Sisti Mganga, Gulf Concrete Company Limited na  Yaate Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo.

Akizungumza katika nyakati tofauti mara baada ya kutembelea migodi hiyo, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mipango ya ufungaji migodi mapema badala ya kusubiri mpaka shughuli za uchimbaji madini zinapomalizika hivyo kufanya zoezi la ufungaji wa migodi kuwa gumu huku wakiacha mazingira yakiwa hatarishi. 

“Ninapenda kuwakumbusha kuwa suala la kuwa na Mpango wa Ufungaji wa Migodi ni la lazima kulingana na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, hivyo ninawataka kuhakikisha mnakuwa na mpango ili kuhakikisha mashimo hayaachwi wazi,” alisema Profesa Kikula.

Awali akiwa katika mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga Profesa Kikula  alielezwa mafanikio ya mgodi huo ikiwa ni pamoja na  kokoto za mgodi huo kutumika katika ujenzi wa daraja la Mto Wami uliopo mkoani Pwani,  reli ya kisasa ya standard gauge na utengenezaji wa marumaru kwa ajili ya soko la ndani ya nchi.

Katika hatua nyingine Mganga alitaja changamoto zinazoukumba mgodi huo kuwa ni pamoja na tozo kubwa kutoka katika halmashauri na tozo nyingine zinazotozwa na kijiji cha Kihangaiko  pasipo kuwa na risiti pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisasa.

Profesa Kikula alisema kuwa, suala la tozo litafanyiwa kazi kwa kuliwasilisha mamlaka za juu kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kusisitiza kuwa nia ya Serikali kupitia Tume ya Madini, ni kuhakikisha wachimbaji wa madini hususan wadogo wanafanya kazi katika mazingira mazuri yenye faida kubwa huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini pasipo vikwazo vyovyote.

Wakati huo huo, akiwa katika mgodi wa uzalishaji wa kokoto wa Gulf  Concrete Limited Profesa Kikula alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi huo kuhakikisha wanarekebisha kasoro ya mazingira kwa kuhakikisha vumbi linalotoka wakati wa shughuli za uchimbaji wa kokoto halisambai kwani linaathiri wananchi  wa vijiji vya jirani katika mgodi huo.

Alisema ni vyema wakazingatia Sheria ya Mazingira kwani vumbi mbali na kuathiri wananchi wanaoishi katika vijiji vya jirani linaweza kuathiri wafanyakazi wa mgodi huo.

Aidha, alituaka mgodi huo kuendelea kuhakikisha unatoa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo na kutumia huduma za ndani ya nchi kama vile bidhaa pamoja na ajira kwa wazawa.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula akiwa katika mgodi wa kuzalisha kokoto wa Yaate Co. Limited, mbali na kuupongeza mgodi kwa kuaminiwa na kupewa kazi ya kusambaza kokoto kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge unaotelekezwa na kampuni ya Yapi  Merkezi na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii inayouzunguka mgodi huo pamoja na ajira, aliutaka mgodi huo kuendelea kununua bidhaa/huduma kutoka kwa wananchi.

“Kutoa huduma bora kwa wananchi wanaozunguka mgodi kunaboresha mahusiano na kupunguza migogoro ya mara kwa mara inayoweza kujitokeza.

Awali akielezea mafanikio ya mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Yaate Co. Limited, Eugen Mikongoti alisema  mradi umenufaisha watanzania wengi kwa kuchangia maendeleo ikiwa ni pamoja na ulipaji  wa zaidi ya shilingi bilioni 1.31 ambazo zimelipwa kama ushuru wa madini  kati ya kipindi cha mwezi Juni, 2018 hadi Januari, 2019 na shilingi milioni 338.8 zilizolipwa kama mrabaha.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa za ajira kwa watanzania hususan vijana wanaozunguka mgodi na kuziwezesha kampuni zinazomilikiwa na wazawa kushiriki katika miradi mikubwa  hivyo kuzijengea uwezo wa kitaalam na kupata fursa.

Mikongoti alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya wanachi wanoishi karibu na mgodi kupitia huduma za jamii ambapo mpaka  sasa mgodi huo  unaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi na kuhudumia wananchi katika zahanati iliyopo mgodini.

Katika hatua nyingine Mikongoti alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na Tume ya Madini chini ya Mwenyekiti wake Profesa Kikula ikiwa ni pamoja na kuwatembelea, kuwapa elimu na kutatua changamoto mbalimbali.


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) pamoja na Kamishna-Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki (katikati) wakiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga uliopo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani tarehe 21 Februari, 2019 ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji. Kushoto ni mmiliki wa mgodi huo, Sisti Mganga. 

Mmoja wa watendaji wa mgodi wa kuzalisha kokoto wa Gulf Concrete Company Limited,  ulipo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, Ramesh Annlahamadu (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji tarehe 21 Februari, 2019. Kulia mbele ni Kamishna – Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki.

Monday, February 18, 2019

Waziri Biteko ataka Jengo la kituo cha pamoja cha biashara kukamilika ifikapo Aprili mwaka huu


Ø ASEMA ATAKAYEKAMATWA NA TANZANITE MARUFUKU KUINGIA TENA NDANI  YA UKUTA.

Ø ATAKA MINADA YA TANZANITE ILIYOSIMAMISHWA SASA IANZE.

Ø SUMA JKT msitucheleweshe,
ifikapo Aprili mwaka huu jengo liwe limekamilika. Jengo hili la Kituo cha Pamoja cha Biashara ya Madini litajengwa na SUMA JKT kwa gharama ya shilingi 1,148, 259,500.

Ø Tunafunga CCTV camera kuzunguka ukuta. Lengo la uwekaji wa mitambo hii ni kuimarisha ulinzi kwa ajili ya rasilimali na watu  waliomo na wanaoingia ndani ya ukuta. Tunataka tukiwa Dar es Salaam na Dodoma tuwaone. Rai yangu kwenu ni kila mtu awe mlinzi wa rasilimali madini na kwa upande wafanyabiashara wapende kununua katika mkondo sahihi madini yao ili kuepuka usumbufu.

Ø Tarehe 30 Januari 2019 nilisaini Kanuni za Mirerani Controlled Area. Nakuagiza Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Kamati ianze kazi tuanze kusimamia Kanuni hizi.

Ø Tumekuja kumkabidhi mkandarasi site  hakuna kulala mpaka madini yalinufaishe taifa.

Ø Mkandarasi wa CCTV nakukabidhi kazi hii nataka ufanye kazi yenye ubora na kumaliza ndani ya Mkataba tuliokubaliana bila kuongeza hata sekunde.

Ø Tulieni tunakuja na utaratibu wa mashine. Wizi ni lazima  tuutoe kwenye fikra zenu.

Ø Wakati ukuta huu unajengwa  kulikuwa na siasa nyingi. Wapo waliouita jela lakini leo mapato yameongezeka mnalipa kodi vizuri. Tunakwenda kuondoa vikwazo kwenye biashara ya madini. Mtalipa mrabaha usiozidi asilimia 7. Deni limebaki kwenu.

Ø Suala kujengwa ukuta lilikuwepo tangu mwaka 2002 lakini haukujengwa. Ametokea mzalendo Rais Magufuli tumejenga. Asingekuwa yeye ingebaki hadithi nyingine.

Ø Nitawashangaa sana baada ya jitihada hizi tunazozifanya mapato yakishuka. Mkuu wa Mkoa wasimamieni hawa  huku mkiwalea.

Ø Jengo la biashara ya madini limejengwa mahususi ili kurahisisha uthaminishaji wa madini pindi yanapovunwa hapa ndani.Ma broker tumewajengea nyumba hii hapa tuheshimu taratibu.

Ø Jengo hili la biashara na uthaminishaji litatumika kuwakutanisha wafanyabiashara wadogo na wenye madini ili kuweza kufanya biashara sehemu salama na  kwa uwazi. Kama alivyosema Katibu Mkuu, jengo hili limegharimu shilingi milioni 85.

Ø Tanzania Tumegeuka kuwa darasa kwa jirani zetu  na nchi nyingine kutokana na namna tunavyosimamia Sekta ya madini. Watu wa mataifa wanakuja kujifunza lakini pia Tunapata mialiko mingi kutoka nchi mbalimbali ili tuwaeleze namna tunavyosimamia rasilimali hii.

Ø Tutumie madini yetu kubadilisha maisha yetu. Tunataka siku moja watoto wa Simanjiro wasome kwenye shule nzuri, watumie barabara nzuri, akina mama wapate huduma za afya sehemu nzuri. Haya ndiyo mambo tunayoyataka. Siasa nyingine siyo agenda ya watanzania.

Ø Tanzania ni nchi ya 3 Afrika kwa kuzalisha dhahabu, ya pili Afrka kwa madini ya vito na ya 18 duniani kwa kuzalisha dhahabu lakini utajiri huu wa madini na maisha ya watanzania havifanani.

Ø Minada ya Tanzanite iliyosimamishwa sasa ianze.

Ø Chama Cha MAREMA unganeni,tukigundua hamna msaada tutawaacha.

Ø Hatutaki kukwamishana,tunataka kusimamia sekta..Wachimbaji acheni majungu, toeni taarifa za kweli.

Ø Hatutawatoza fedha nyingi lakini mtatuonesha vitambulisho. Natoa maelekezo kuanzia leo tozo za kiingilio zitatozwa kwa wale wanaofanya kazi. Ndani ya mgodi watalipa shilingi elfu 50,000 kwa mwaka, Mabroker watalipa shilingi elfu 30,000 kwa mwaka na wana Appolo, wafanyabiashara wadogo kama wachekechaji, mama lishe watalipa shilingi 20,000 kwa mwaka.

Ø Naomba Wizara ya Kazi kupitia Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi  ( WCF) na  Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuja kujifunza na kutengeneza muundo ambao unaendana na aina ya kundi hili ili kuweza kulihudumia kundi hili la wachimbaji wadogo wa madini.

Ø Katika mkutano wa wadau wa tarehe 22 Januari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli  pamoja na mambo mengine alisisitiza kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara ya Madini Tanzania na pia kuimairisha usalama. Tuliagizwa kiualisia kuanza mara moja kuweka mifumo ya kidigitali kuzunguka ukuta.

ALIYOYASEMA MKUU WA MKOA WA MANYARA ALEXANDER MNYETI

Ø Mkoa wa Manyara ni mkoa mkubwa wenye Tanzanite ambayo haipo  popote duniani. Unapokuwa Mkuu wa Mkoa kama huu lazima uweze kudhibiti Tanzanite. Nataka nikamwambie Mhe. Waziri  tuna madini mengi zaidi ya Tanzanite.

Ø Kwenye madini lazima nibanane na wewe. Nisipodhibiti sina cha kumwambia Mhe. Rais. Tutapambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha kodi zinapatikana. Babati tuna rubi ya kutosha. Nataka nikwambie ifanye Babati kuwa Makao Makuu ya Madini nchi nzima.

Ø Mhe. Waziri kazi yetu ni kusimamia mnayoyapitisha juu ili yasipotoshwe na yatekelezwe kwa Mujibu wa Sheria.

Ø Mhe. Rais alituelekeza tupitie na kukubaliana kuweka mazingira mazuri ya kuboresha Tanzania kupitia sekta hii. Tulikaa kujadili mabadiliko makubwa. Nina hakika mabadiliko makubwa yanakuja.

Ø Mhe. Waziri tumeshakubaliana na wadau hawa mambo mengi. Tunataka kuona mengi kutoka kwao.

Ø Ni matarajio yangu kuwa shughuli nyingi zitafanyika ndani ya jengo la Kituo cha Biashara.

Ø Nakipongeza Chama Cha Marema kwa kufanya kazi nzuri. Ukipingana na Serikali hakuna unachoweza kufanya. Hakuna aliye juu ya serikali.

ALIYOYASEMA MWENYEKITI WA  KAMATI YA KUDUMU YA  BUNGE YA NISHATI NA MADINI, DUSTAN KITANDULA

Ø Mhe. Rais ameonesha uungwana, mpira uko kwenu. Hisani pekee kwake ni ninyi kulipa kwa kuonesha kwa vitendo. Yale yaliyokuwa yakiwakwaza yameondoka, mlipe kodi.

Ø Tumewaona mkiwa katika maandamano ya kumuunga mkono Rais. Kikao cha Januari 22 kilionesha dhamira ya Rais na aliahidi kutekeleza  kero zenu ndani ya kipindi kifupi. Tuliletewa miswada kufanya mabadiliko.

Ø Nampongeza Rais kwa kuondoa vikwazo kwa wachimbaji wadogo. Serikali imedhamiria kuhakikisha sekta hii inalinufaisha taifa.

ALIYOYASEMA MBUNGE WA SIMANJIRO JAMES OLLE  MILLYA

Ø Kuwepo kwa ukuta huu hakumaanishi hakuna majirani. Kwa mujibu wa Sheria na  taratibu zake  nakuomba  Mhe  Waziri migodi hii isaidie jamii. Wanaofanya uchimbaji wakumbuke vijiji vya jirani.

Ø Baada  ya kujengwa ukuta bado wanapanga mistari mirefu. Wanaongia ndani wakaguliwe mapema.

Ø Bado kuna changamoto kwako Mhe. Waziri na  Katibu Mkuu ikiwezekana muwaletee maji.

ALIYOYASEMA MWENYEKITI WA MAREMA, JUSTIN NYARI

Ø Mhe. Rais ameweka alama ambayo haitapotea, alama ambayo itakumbukwa kwa vizazi na vizazi.

Ø Ujenzi wa kituo cha pamoja cha biashara ni  mwanzo mzuri kwetu na mkoa wetu na nchi yetu, wachimbaji wako tayari kushirikiana na serikali.


Waziri wa Madini Doto Biteko akiweka Jiwe la Msingi katika Kituo Cha Pamoja Cha Biashara ya Madini. Pamoja naye ni Mbunge wa Simanjro, James Ole Millya , Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof.Simon Msanjila na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula.

Waziri wa Madini Doto Biteko akifuatilia jambo baada ya kuweka Jiwe la Msingi Kituo cha Pamoja Cha Biashara, eneo la Mirerani. Wengine wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula. Kulia ni mwanzo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila.

Waziri wa Madini Doto Biteko akizindua Jengo la Biashara na Uthaminishaji wa Madini, Mirerani. Wengine wanaoshuhudia ni Viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wizara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Waziri wa Madini Doto Biteko Sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti pamoja na wageni waloshiriki hafla ya uzinduzi wa Jengo la Biashara na Uthaminishaji Madini, wakielekea mahali kunakojengwa Kituo cha Pamoja Cha Biashara ya Madini.

Wadau wa Tanzanite Mirerani waandamana kumpongeza Rais Magufuli


Ø NI KUFUATIA KUPUNGUZA KODI ZA MADINI NA KUSIKILIZA KERO ZAO

Ø WAAHIDI KULIPA KODI

Maandamamo hayo yaliyofanyika Februari 16, yalihusisha wadau wote wa madini ya Tanzanite wanaofanya shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta wakiwemo wachimbaji wadogo, wa Kati na Wakubwa, yakilenga kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kupunguza kodi za madini, kusisitiza suala la uanzishwaji wa masoko ya madini na  mwongozo wa uongezaji thamani madini

v ALIYOYASEMA MKUU WA MKOA WA MANYARA, ALEXANDER MNYETI
 Mhe. Rais ametuagiza mlipe kodi kwa hiari. Msipofanya hivyo mtalipa kwa nguvu. Lipeni kodi.

Ø Nimepokea maandamano yenu na tutaandaa barua Maalum kwenda kwa Mhe. Rais kufikisha salam zenu. 

Ø Mnajua safari ya tulikotoka, tulipofika na tunaweza kutengeneza njia nzuri ya tunakotaka kufika. MAREMA inakwenda vizuri.

Ø Mirerani acheni umbeya, kuna uongo mwingi, punguzeni uongo taarifa zenu zinatupotosha. 

Ø Mnajichonganisha wenyewe na serikali. Waajiri mnawatelekeza wafanyakazi wenu wakiugua wanakuwa mzigo wa serikali.

ALIYOYASEMA MWENYEKITI WA MAREMA, MKOA WA MANYARA, JUSTIN NYARI

Ø Maandamano haya yanalenga kutoa pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuondo kodi ambazo hazikuwa rafiki kwa wachimbaji.Tunampongeza Mhe. Rais kwa  kupeleka bungeni Muswada kwa hati ya dharura, ujenzi wa masoko  ya madini na mwongozo wa uongezaji thamani madini.

Ø Wachimbaji wako tayari  kushirikiana na serikali kukuza uchumi kupitia sekta ya madini.

ALIYOYASEMA MBUNGE WA SIMANJIRO, JAMES OLLE MILLYA

Tunampongeza Rais kwa kuondoa VAT ya asilimia 18 kwenye sekta. Ameacha asilimia 7 tu huu ni upendo wa pekee.

Baada ya Januari 22 Mkuu wa Mkoa aliitisha kikao Januari 25 na migodi yote imeanza kufanya kazi na matunda yameanza kuonekana.

ALIYOYASEMA MKUU WA WILAYA YA SIMANJIRO, MHANDISI ZEPHANIA CHAULA

Ø Kama Mhe. Rais amewaheshimu na ninyi mumheshimu, heshima hiyo ni kulipa kodi.

ALIYOYASEMA MWAKILISHI WA TANZANITE AFRIKA KWA NIABA YA WACHIMBAJI WA KATI, WILFRED MUSHI

Ø Tunampongeza Mhe.Rais, kwa mara ya kwanza ameondoa kero za wachimbaji wa  Kati ambazo hazipishani sana na wachimbaji wadogo.

Ø Nuru ya Tanzanite imenga'rishwa,
Mirerani sasa inakwenda kutengeneza  tanzanite mpya.

ALIYOYASEMA MWAKILISHI WA TANZANITE ONE, FEISAL SHABHAI

Ø Tunampongeza Rais Magufuli kwa kutambua uwepo wetu, kusikiliza kilio chetu na kuondoa changamoto zetu.
Ø Tunatambua maendeleo yanayotarajiwa kutokana na rasilimali hii ambayo lengo ni kuwanufaisha watanzania na vizazi vijavyo viweze kuishi katika mazingira salama.

ALIYOYASEMA MWAKILISHI WA TAMIDA, HUSSEIN GONGA 

Ø Tulikuwa na tashwishi kubwa juu ya kufanya biashara ya madini. Mhe Rais alisikia kilio cha wachimbaji na dealers.

Ø Hawezi kuwepo mnunuzi bila mchimbaji, tulikuwa na changamoto ya kusafirisha madini ghafi.

Ø Rais Magufuli ameondoa kodi ya VAT ya asilimia 18, ilikuwa kero kubwa.

Ø Mhe. Rais hajapoteza, mafanikio  atayaona tunamhakikishia. Biashara ya madini  sasa inakuwa nzuri.

ALIYOYASEMA MWAKILISHI WA BROKER,
Ø Tunampongeza Rais kwa suala la ujenzi wa masoko ya madini nchi nzima, serikali itakusanya kodi ya kutosha.

Ø Niwaombe Ma broker, kufanya uthamini wa madini, sitamwombea radhi broker yoyote atakayevunja sheria.

ALIYOYASEMA MWAKILISHI WA WANA APOLLO

Ø Tunampongeza Rais Magufuli kwa kututambua wana Appolo na kutupa nafasi ya kuwasilisha kero zetu. Tunaahidi kushirikiana katika nyaja zote. Wana Appolo ndiyo wachimbaji wa tanzanite.

Ø Tunayo sababu ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, leo wana Appolo tunapewa vipaza sauti. Kwa muda mrefu wana Appolo hawakuwa na sehemu ya kuzungumza.