Wednesday, February 28, 2018

Nyongo awaahidi neema wananchi Kagera soko la madini bati


Na Veronica Simba, Kagera

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewaahidi wananchi wa Kagera kuwa Serikali inashughulikia kwa umuhimu mkubwa na kwa haraka suala la Soko kwa ajili ya Madini ya Bati yanayochimbwa wilayani Kyerwa, ili waendelee kunufaika nayo na nchi ipate faida kama ilivyo kwa majirani zetu wa Uganda na Rwanda.

Alitoa ahadi hiyo jana, Februari 27 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kazi mkoani humo.

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Naibu Waziri Nyongo alikiri kuwa wachimbaji wa Madini ya Bati hapa nchini, kwa sasa wana wakati mgumu kutokana na Serikali kusitisha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi; hata hivyo akasema kuwa hali hiyo itakoma hivi karibuni kwa kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa haraka.

Akifafanua zaidi, Nyongo alisema kuwa Tanzania ilichelewa kujiunga na Mkataba wa Kimataifa unaowezesha madini hayo kutambuliwa na kununulika kokote, hali iliyosababisha nchi jirani za Rwanda na Uganda ambazo zimeshajiunga na Mkataba huo, kutumia fursa hiyo kununua malighafi hiyo muhimu kutoka kwa wachimbaji wa hapa nchini kwa bei ya chini sana.

Alisema kuwa, ni kwa sababu hiyo Serikali iliamua kusitisha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi mpaka pale itakapokamilisha taratibu mbalimbali zitakazoiwezesha nchi na wananchi wote kunufaika ipasavyo kutokana na madini mbalimbali yanayopatikana nchini, ikiwemo kuharakisha mchakato wa kujiunga na Mkataba huo wa Kimataifa.

“Kwa hiyo, mimi nikuhakikishie kwamba, suala hilo tunalishughulikia kwa uharaka ili kuhakikisha nasi kama kama nchi tunatambulika katika Mikataba hiyo ya Kimataifa, ili nasi tuanze kuuza Bati yetu vizuri. Tunalichukulia suala hili kwa umuhimu wa kipekee.”

Aidha, Nyongo aliieleza pia Kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama kuhusu suala la utoaji Leseni za Madini nchini, kwamba utaendelea mapema iwezekanavyo mara tu baada ya Tume ya Madini itakapoanza kufanya kazi.

“Tume itaanza kufanya kazi muda wowote kuanzia sasa, mara tu Mheshimiwa Rais atakapofanya uteuzi wa Mwenyekiti wake. Na itakapoanza kazi tu, zoezi la utoaji na uhuishaji wa Leseni litaendelea.”
Vilevile, alifafanua kuwa, kufuatia kufutwa kwa iliyokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kuundwa Tume ya Madini; hakutakuwa tena na Ofisi za Madini za Kanda bali kutakuwa na Ofisi za Madini za Mikoa.

Kwa upande wa Madini ya Nickel ambayo pia yanachimbwa ndani ya Mkoa huo, Naibu Waziri alisema kuwa ni moja ya madini yanayoleta matumaini mapya ya kulinufaisha Taifa kutokana na umuhimu wake katika Soko la Dunia kwa sasa.

Alisema kuwa, kutokana na kukua kwa Teknolojia Duniani, Madini ya Nickel yanahitajika sana, hususan katika nchi zilizoendelea kwa ajili ya kutengeneza Betri maalum za Magari ambazo zinachajiwa na hivyo kutotumia mafuta.

“Sasa hivi nchi zilizoendelea wanataka kupunguza matumizi ya mafuta kwenye magari na ukienda Miji mikubwa ya Ulaya, wanataka kufikia 2040 wasitumie tena mafuta kwenye Magari yao, badala yake watumie Betri. Nickel ni madini muhimu sana katika utengenezaji wa Betri hizo na mitambo mingine inayohifadhi chaji za umeme kama vile kwenye Simu na kadhalika.”

Kuhusu uwekezaji katika Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold, unaomilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Naibu Waziri alieleza kuwa Serikali inajipanga upya kuona ni namna gani Mgodi huo uendeshwe ili kuhakikisha unaleta tija kwa Taifa na siyo kuleta hasara kama ilivyo sasa.

Alisema kuwa, baada ya Serikali kubaini kuwa hasara iliyopatikana katika Mgodi huo imesababishwa na Mgodi kutosimamiwa vizuri, ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasimamisha kazi wahusika pamoja na kutuma Timu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwenda kuhakiki madeni husika.

“Kwa hivyo, tumeamua kusimamisha shughuli zote pale, tujihakikishie yale madeni. Uchunguzi unaendelea na baada ya muda tutatoa msimamo wa Serikali kuhusu namna bora ya kuuendesha ule Mgodi.”
Baada ya kukutana na kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Uslama ya Mkoa, Naibu Waziri pia alitembelea Ofisi za Madini za Mkoa na kuzungumza na wafanyakazi.

Naibu Waziri anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo akiwa mkoani Kagera, anatarajiwa kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini ya Bati, kukagua maendeleo ya ujenzi wa Viwanda vidogo vya uongezaji thamani Madini hayo pamoja na kukagua Mradi wa Kabanga Nickel.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (katikati) pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, alipowasili mkoani Kagera kwa ajili ya ziara ya kazi, Februari 27 hadi 29 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Kagera, alipowatembelea akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo, Februari 27 mwaka huu. 


Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (katikati), akisoma Taarifa ya Sekta ya Madini ya Mkoa huo, mbele ya Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia kwake), alipomtembelea ofisini kwake akiwa katika ziara ya kazi Februari 27 mwaka huu.


Mjiolojia Samwel Shoo, kutoka Ofisi ya Madini Kagera (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, aina mbalimbali ya sampuli za madini yanayopatikana mkoani Kagera humo. Naibu Waziri alitembelea Ofisi ya Madini akiwa katika ziara ya kazi mkoani Kagera, Februari 27 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akisalimiana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera, alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, kueleza azma ya ziara yake mkoani humo Februari 27 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia), akisaini Kitabu cha Wageni katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera, Daniel Mapunda (kushoto), alipofika kumtembelea pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa Ofisi hiyo, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 27 mwaka huu.

Biteko autaka Mgodi wa Katavi & Kapufi kuajiri watanzania


Na Mohamed Saif

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameupa Siku 14 Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo Mkoani Katavi kuhakikisha uwe umepunguza wafanyakazi wa kigeni na kuajiri Watanzania kwenye nafasi wanazomudu kama Sheria inavyoelekeza.

Alitoa agizo hili jana Tarehe 24 Februari, 2018 alipofanya ziara kwenya mgodi huo ili kujionea shughuli zinazofanyika katika mgodi huo.

Taarifa ya mgodi iliyowasilishwa kwake ilibainisha kuwa jumla ya wageni 48 wameajiriwa na huku 36 kati yao wakiwa hawana ujuzi na wanafanya shughuli ambazo Watanzania wanamudu, ikiwemo ya ulinzi.

Biteko alisema dhamira ya Serikali ni kuona Watanzania wananufaika na Sekta ya Madini kwa namna mbalimbali ikiwemo ya kujipatia ajira kwenye migodi na kwamba suala hilo la kuajiri wageni kwenye nafasi wanazomudu Watanzania halivumiliki.

Alimuagiza Mkuu wa Wilaya na Afisa Madini kuhakikisha wanalifuatilia jambo hilo na liwe limemalizika baada ya wiki mbili kuanzia Tarehe 24 Februari, 2018 na apatiwe mrejesho wake.

“Mnawafanyakazi wengi ambao wanafanya kazi ambazo Watanzania wanaziweza. Hatuwabagui lakini tunataka manufaa ya madini yabaki kwa Watanzania,” alisema Biteko.

Biteko aliiagiza Idara ya Uhamiaji Nchini kufuatilia Wafanyakazi wakigeni waliopo migodini ili kukagua kama wanavyo vibali vya kufanya kazi hapa nchini. “Mnavyotoa vibali muwe makini, ili shughuli zinazokuja kufanywa na wageni ziwe kweli Watanzania hawazimudu,” alisisitiza.

Alihimiza migodi yote nchini kuepuka kuwanyanyasa wafanyakazi sambamba na kuwataka wafanyakazi waliaoajiriwa migodini kufanya kazi kwa uaminifu ili kulijengea Taifa heshima inayokubalika.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akisalimiana na Wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi mara baada ya kuwasili mgodini hapo kwa ajili ya kujionea shughuli zinazoendelea mgodini hapo na kuzungumza na wahusika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa mgodi huo.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akisalimiana na Wafanyakazi wa Kigeni (Wataalam wa Nje/expatriates) wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi mara baada ya kuwasili mgodini hapo kwa ajili ya kujionea shughuli zinazoendelea mgodini hapo na kuzungumza na wahusika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa mgodi huo ikiwemo hatua iliyofikiwa ya mgodi huo.



Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kulia) akitembelea Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi ili kujionea shughuli ziazoendelea mgodini hapo. 

Moja ya eneo la mitambo kwenye mgodi wa Dhahabu wa  Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi ili kujionea shughuli zinazoendelea mgodini hapo. Wa pili kulia ni Mbia na Makamu Mwenyekiti wa Mgodi wa Katavi & Kapufi Ltd, Sebastian Kapufi.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (katikati) wakati wa kukagua shughuli ziazofanyika kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Ltd uliopo Mkoani Katavi.

Watumishi wa umma wametakiwa kuacha kunyanyasa wachimbaji wadogo


Na Mohamed Saif

Serikali imesema itawachukulia hatua za kinidhamu watendaji wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyanyasa wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kujipatia kipato kinyume na taratibu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora.

Wakielezea changamoto zinazowakabili, wachimbaji wa machimbo hayo kwa nyakati tofauti walimueleza Biteko masikitiko yao juu ya unanyasaji wanayofanyiwa na baadhi ya Maafisa wa Serikali wasiowaaminifu wakiwemo Askari Polisi na Maafisa Madini.

Wachimbaji hao walisema kumekuwepo na tabia ya kushinikizwa kutoa rushwa ama kugawana faida kwa vitisho kuwa watazuiwa kuendelea kufanya shughuli zao kwenye maeneo yao.

“Kuna baadhi ya Maafisa Madini na Askari Polisi wamekuwa wakitulazimisha nao tuwape mgawo wa mawe tunayochimba vinginevyo watafukia maduara yetu,” alisema Alfred Kulwa mmoja wa wachimbaji kwenye machimbo hayo.

Kufuatia malalamiko hayo, Naibu Waziri Biteko alitoa onyo kwa watendaji wenye tabia hiyo kuacha mara moja na alimuagiza Afisa Madini kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya husika kuhakikisha wanafuatilia suala hilo na watakaobainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

“OCD, tendeni haki, hawa wawe salama. Askari atakayebainika ananyanyasa mchimbaji madini achukuliwe hatua za kinidhamu haraka bila kuchelewa,” aliagiza Naibu Waziri Biteko.

Biteko alisema Afisa yeyote anayehitaji kujishughulisha na biashara ya madini aache kazi ili ajikite katika biashara hiyo na sio kutumia cheo chake kuwanyanyasa wachimbaji.

Aliongeza kuwa hairuhusiwi Mtumishi wa Umma kutumia cheo kujinufaisha. “Marufuku watendaji wa Serikali ama wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kutumia madaraka yao vibaya. Kama unataka ingia uchimbe mwenyewe. Serikali hii ya Awamu ya Tano inatutaka tuondoe manyanyaso,” alisema Biteko.

Biteko alisema mchimbaji atakayenyanyaswa atoe taarifa Polisi na pia amfahamishe kwa njia ya simu kuhusiana na manyanyaso hayo ambapo alitaja namba zake za simu ili kukitokea hali ya sintofahamu wasisite kumfahamisha.

Hata hivyo, Biteko aliwataka wachimbaji hao kuacha kuwasilisha taarifa za uwongo ikiwemo kusingiziana na mara zote wasimamie haki ili kuepusha migogoro baina yao na Serikali.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda ya Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora. Biteko alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli zinazoendelea sambamba na kuzungumza na wachimbaji.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri wakiwa kwenye mkutano na wachimbaji wadogo wa machimbo ya dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani Sikonge, Mkoani Katavi.

Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) alipofika kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli wanazofanya pamona na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.

Baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) alipofika kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli wanazofanya pamona na kujadiliana nao masuala mbalimbali ikiwemo ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akiwasilikiza baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge wakiuliza maswali na kuelezea changamoto mbalimbali ziazowakabili kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mwenye kipaza sauti) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye machimbo ya Kitunda ya Wilayani Sikonge, Mkoani Tabora. Biteko alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli zinazoendelea sambamba na kuzungumza na wachimbaji.

Tuesday, February 27, 2018

Biteko atangaza kiama kwa waliohujumu ruzuku


Serikali imetoa onyo kali kwa waliojinufaisha na kutumia ruzuku ya uchimbaji madini kinyume na makusudio yake ambao hadi sasa hawajarejesha licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa onyo hilo Februari 26, 2018 kwenye mkutano na wananchi na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Isanga, Kata ya Lusu Wilaya ya Nzega.

Awali kabla ya kutoa onyo hilo, wachimbaji hao waliiomba Serikali kuwapatia ruzuku ili iwasaidie katika shughuli zao za uchimbaji madini ndipo Naibu Waziri Biteko alipoweka bayana suala hilo la ruzuku.

Alisema Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini baada ya kubaini kwamba imeshindwa kuleta mafanikio yaliyokusudiwa na kwamba ilikwishaagiza wale wote waliojipatia ruzuku na kuitumia kinyume na makusudio wanapaswa kuirejesha mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

“Wapo ambao tayari wameanza kurejesha na wengine bado hawajafanya hivyo. Ninawahakikishia wale ambao bado, tutawachukulia hatua kali za kisheria,” alisema Biteko.

Alisema haiwezekani watu wachache wasiokuwa na huruma kwa wanyonge wakatumia fedha ya Watanzania kinyume na makusudio yake.

Biteko alisema kuwa lengo la Serikali la utoaji wa ruzuku lilikuwa ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini nchini wanaweza kuendeleza machimbo yao kwa kufanya shughuli zenye tija kwao na Taifa kwa ujumla hata hivyo, makusudio hayo hayakufikiwa kama ilivyotarajiwa.

Alibainisha kuwa Serikali inakuja na mpango mwingine wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata manufaa kutokana na shughuli zao lakini sio kuwapatia fedha kama ilivyokuwa hapo awali. “Tunanunua vifaa vya uchimbaji ambavyo vitatumika kuwasaidia na sio kuwapatia fedha,” alisema Biteko.

Aidha, Biteko aliwataka wachimbaji kote nchini kujiunga kwenye vikundi ili kujipatia manufaa mbalimbali ikiwemo urahisi wa kupata huduma za kifedha, kukopesheka na kuelimishwa njia bora na sahihi ya uchimbaji.

Alisema wachimbaji watakapojiunga wataweza kuwa na uchimbaji wenye tija na hivyo kutoa ajira nyingi kwa Watanzania wenzao, kulipa ushuru na tozo mbalimbali za Serikali na hivyo kujiletea maendeleo wao binafsi lakini pia maendeleo kwa Taifa kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Biteko aliambatana na mwenyeji wake Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala ambapo walitembelea maeneo ya Chuo cha Dodoma Kampasi ya Nzega (MRI) ambapo zamani palikuwa ni mgodi wa Reolute.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akikagua mazingira ya Chuo cha Madini Dodoma, Kampasi ya Nzega ili kujionea hali ya Kampasi hiyo.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Isanga, Kata ya Lusu Wilaya ya Nzega (hawapo pichani).

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akiongozana na mwenyeji wake Mbunge wa Nzega Vijijini na Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala (kulia) walipofanya ziara kwenye Chuo cha Madini Dodoma, Kampasi ya Nzega ili kujionesa hali ya Kampasi hiyo.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto) akikagua mazingira ya Chuo cha Madini Dodoma, Kampasi ya Nzega.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) alipotembelea Chuo Cha Madini Dodoma, kampasi ya Nzega.

Nyongo awataka wachimbaji wadogo kuwajibika


Na Veronica Simba, Geita

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini, kufahamu wajibu wao na kuutekeleza kikamilifu ili waendeshe shughuli zao kwa amani na tija.

Aliyasema hayo Februari 26 mwaka huu, alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa Lwamgasa, Bingwa, Musasa na Nyakafuru katika Wilaya za Mbogwe na Chato, Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa.

“Msiishie kulalamika tu. Jifunzeni kuwajibika kikamilifu katika nafasi zenu ili kazi zenu zilete tija na kuwanufaisha ninyi wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla.”

Alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi mahiri wa Rais John Magufuli, inawajali na kuwathamini sana wachimbaji wadogo lakini pia inawataka wawajibike ili mchango wao katika sekta husika uonekane.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri aliwataka wachimbaji hao kuhakikisha wanarasimisha shughuli zao kwa kuomba leseni ili wasajiliwe na kutambuliwa rasmi na Serikali, hivyo waweze kulipa kodi na tozo mbalimbali.

“Serikali inategemea kodi zenu ili iweze kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa Taifa ikiwemo kutoa elimu bure kama inavyofanyika sasa, kujenga miundombinu, kuwezesha utoaji wa huduma za afya na nyinginezo. Hivyo basi, ni lazima mlichukulie suala la uwajibikaji kwa umuhimu mkubwa,” alisisitiza.

Aidha, aliwasisitiza kuunda vikundi na kufanya shughuli zao ndani ya vikundi hivyo, ili iwe rahisi kwa Serikali kuwatambua na kuwapa huduma mbalimbali zitakazowasaidia kuboresha kazi zao.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina, aliwasisitiza wachimbaji hao kujali afya zao na kuzingatia suala la kutumia vizuri mapato yao ili wajiletee maendeleo.

Naibu Waziri Nyongo anaendelea na ziara ya kazi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Wananchi mbalimbali katika Migodi ya Nyakafuru, Musasa na Bingwa wakitoa maoni yao mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake katika maeneo hayo, Februari 26 mwaka huu. Naibu Waziri yuko katika ziara ya kazi kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Sehemu ya umati wa wananchi katika Machimbo ya Madini Bingwa, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake inayoendelea Kanda ya Ziwa kukagua shughuli za madini.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akizungumza na wananchi na wachimbaji madini wadogo katika Mgodi wa Musasa uliopo Chato, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia Shimo la Uchimbaji katika Machimbo ya Madini ya Nyakafuru wilayani Mbogwe, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi.


Wananchi mbalimbali katika Migodi ya Nyakafuru, Musasa na Bingwa wakitoa maoni yao mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake katika maeneo hayo, Februari 26 mwaka huu. Naibu Waziri yuko katika ziara ya kazi kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Wananchi mbalimbali katika Migodi ya Nyakafuru, Musasa na Bingwa wakitoa maoni yao mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake katika maeneo hayo, Februari 26 mwaka huu. Naibu Waziri yuko katika ziara ya kazi kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akisalimiana na wachimbaji madini wadogo waliopo Nyakafuru, wilayani Mbogwe, Mkoa wa Geita, baada ya kuwasili hapo kukagua shughuli zao na kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa.

Monday, February 26, 2018

Mkutano mkubwa wa wadau wa madini wafanyika Mwanza


Ø Waazimia hakuna tena utoroshaji wa madini

Ø Wapendekeza Soko la pamoja kwa madini ya dhahabu

Ø Kamati yaundwa kuandaa taratibu

Na Veronica Simba, Mwanza

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameongoza Mkutano mkubwa wa wadau wote wa madini katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa uliojadili namna ya kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa pamoja na udhibiti wa utoroshaji wa madini.

Mkutano huo uliofanyika jana Februari 25 jijini Mwanza, uliazimia kwa sauti moja kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi.

Aidha, Mkutano ulipendekeza kuwepo na Mnada au Soko la pamoja la Madini ya Dhahabu ili kuweka mazingira wezeshi na yenye tija kwa wadau wote wa sekta hiyo.

Kufuatia maazimio hayo, Mkutano uliunda Kamati yenye wajumbe 14 kutoka kada mbalimbali za sekta husika, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa sasa wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina na Katibu ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria – Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba.

Akiwasilisha Hadidu za Rejea kwa Kamati husika ambayo imeahidi kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya siku 30 kuanzia jana Februari 25, Mwenyekiti wa Mkutano ambaye ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alizitaja kuwa ni pamoja na kuainisha utaratibu utakaotumika kuanzisha Soko hilo la Dhahabu katika Jiji la Mwanza kama ilivyopendekezwa.

Alitaja kazi nyingine inayopaswa kufanywa na Kamati hiyo kuwa ni kubainisha mbinu zitakazotumika kupata washiriki wa Mnada huo ikiwa ni pamoja na wauzaji na wanunuzi.

Vilevile, alisema Kamati husika itatakiwa kuainisha miundombinu ya Mnada mzima kwa maana ya mpangilio wa wote watakaohusika katika Mnada huo kama vile watu wa kodi, Benki mbalimbali na wengineo. “Kwa ufupi watapaswa kuainisha shughuli zote ambazo zitaendana na Mnada zifanyike vipi.”

Aidha, Kamati imetakiwa kuandaa na kuwasilisha Mkakati utakaobainisha utaratibu mzima au mbinu sahihi zinazopaswa kutumika katika zoezi zima la kuanzia ununuzi hadi upatikanaji wa kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi kwa kutumia muda mfupi.

Kazi nyingine ya Kamati husika ni kupambanua faida na hasara za uwepo wa Soko hilo ili kuleta uelewa kwa wadau wote wanaohusika.

Awali, akizungumza katika Mkutano huo, Naibu Waziri alisema kuwa kwa niaba ya Serikali, ameafiki mapendekezo ya wajumbe na utayari wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kutoa eneo katika Jiji lake kwa ajili ya kufanyikia kwa Mnada husika.

“Wazo mlilopendekeza la kuwa na Kituo kimoja nchini cha kuuza Dhahabu ni jema sana. Naliunga mkono. Sisi kama Serikali tutakuwa tukitangaza wanunuzi wakubwa waje kwenye Mnada ili wanunue pale Dhahabu. Tupunguze chaneli ya madalali hapa katikati ili kusudi mkutane na wanunuzi wakubwa uso kwa uso na kufanya biashara,” alibainisha Nyongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alimhakikishia Naibu Waziri na wadau wote kuwa Ofisi yake iko tayari kutoa eneo zuri na salama kwa ajili ya kuendeshea Mnada husika.

Akizungumza katika Mkutano huo, Rais wa FEMATA, John Bina aliwaasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia haki na wajibu wao kama sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya madini zinavyoelekeza ili kufanikisha maazimio ya Mkutano huo kuhakikisha suala la utoroshaji madini linakoma.

“Sote tumekiri ukweli kwamba tunaiba, hatuchangii mapato, wengine hatujarasimishwa katika sekta, tujiulize tunafanya nini?! Tumejipanga vipi? Lazima tulijue hilo,” alisisitiza.

Awali, akizungumzia lengo la kuandaa Mkutano huo, Kamishna Msaidizi wa Kanda, Mhandisi Samamba alibainisha kuwa ni kutokana na changamoto ambayo imeibuka ya utoroshaji wa madini.

“Kwa hiyo, Wizara kupitia kwa Naibu Waziri wa Madini Nyongo, imeona iitishe Mkutano mkubwa na wadau wote wa uchimbaji ili kujadiliana pamoja tatizo liko wapi na kuja na suluhisho la kudhibiti utoroshaji huu wa madini kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.”
Kabla ya kufikia maazimio husika, asilimia kubwa ya wajumbe wa Mkutano huo walikiri kuwa utoroshaji wa madini upo ambapo kwa madai yao, hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na utozwaji wa kodi na tozo mbalimbali stahiki.

Waliiomba Serikali ipunguze kodi na tozo zilizopo ili waweze kumudu kuzilipa na hivyo kuachana na udanganyifu wa aina mbalimbali unaoendelea katika sekta hiyo.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Mhandisi Samamba alifafanua kuwa, suala la kulipa kodi limekuwa ni changamoto kwa wachimbaji wengi kutokana na kushindwa kutunza kumbukumbu zao hivyo kulazimika kulipa zaidi tofauti na wale wanaomudu kutunza kumbukumbu zao ambao hujikuta wanalipa kodi kidogo.

Vilevile, walitaja changamoto ya Soko la uhakika linalosababishwa na wengi wao kutokufahamu bei halisi ya dhahabu na ndiyo sababu wengi wakapendekeza kuanzishwa kwa Soko la Pamoja.

Hivi karibuni, akiwa ziarani Geita, Naibu Waziri alipokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Luhumbi kuhusu masuala ya utoroshaji wa madini ambapo aliahidi kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuitafutia suluhisho changamoto husika.

Aidha, Naibu Waziri alitoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na utoroshaji madini kuacha mara moja vinginevyo, wataadhibiwa vikali pindi wakibainika.

Naibu Waziri anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya madini pamoja na kuzungumza na wananchi.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, akizungumza na wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.

Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria-Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba, akizungumza wakati wa Mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina akizungumza wakati wa Mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.



Sekretarieti, wakichukua kumbukumbu za Mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.

Baadhi ya wadau wa sekta ya madini kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakichangia mada wakati wa Mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, uliofanyika jana, Februari 25 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kujadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini nchini.

Baadhi ya wadau wa sekta ya madini kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakichangia mada wakati wa Mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, uliofanyika jana, Februari 25 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kujadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini nchini.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela na kulia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina.