Monday, March 18, 2019

Majaliwa atoa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa kukamilisha masoko ya madini


Nuru Mwasampeta na Greyson Mwase, Geita

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa hususan mikoa yenye utajiri mwingi wa madini ya metali na vito nchini kuhakikisha wanakamilisha na kufungua masoko ya madini ili kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuwa na soko la uhakika la madini hayo.

Majaliwa alitoa  agizo hilo kwenye uzinduzi wa Soko la Madini la Geita tarehe 17 Machi, 2019 uliofanyika katika viwanja vya Soko Kuu mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa kiserikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya.

Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, watendaji kutoka Tume ya Madini, Wakuu wa Mikoa, wabunge, madiwani, viongozi wa dini, waandishi wa habari pamoja na wananchi kutoka katika mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya  jirani.

Alisema kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini ni  sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa tarehe 22 Januari, 2019 kwenye mkutano wake na wachimbaji wa madini nchini uliofanyika jijini Dar Es Salaam. 

“Ninawataka wakuu wa mikoa kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kabla ya mwaka wa fedha kumalizika Juni 30, 2019,” alisema Majaliwa.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwanufaisha watanzania wote, Serikali kupitia Wizara ya Madini ilianza kwa kuboresha Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Aliongeza kuwa, serikali imeamua kuondoa tozo mbalimbali zilizokuwa mzigo kwa wachimbaji wa madini uli uchimbaji wao uwe na faida kubwa na kuwawezesha kulipa kodi mbalimbali za Serikali.

Alisema kuwa, kufutwa kwa kodi na tozo mbalimbali kutapunguza kwa kiwango kikubwa utoroshwaji wa madini nje ya nchi na Serikali kujipatia pato kubwa linalotokana na shughuli za madini nchini.

Akielezea umuhimu wa masoko ya madini, Majaliwa alieleza kuwa mbali na kupunguza utoroshwaji wa madini, hakutakuwepo na dhuluma kwa wachimbaji wadogo wa madini kwani watakuwa na sehemu yenye uhakika ya kuuzia madini hayo kulingana na bei elekezi iliyotolewa na Serikali.

Aliendelea kueleza kuwa, soko la madini  litarahisisha huduma za uuzaji na ununuzi wa madini ambapo huduma zote zitatolewa ndani ya jengo moja hivyo kuokoa muda wa wauzaji na wanunuzi wa madini.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alitoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa, atakayekamatwa anatorosha madini atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.

Pia aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali  kuhusu sekta ya madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje ya nchi.

Aidha, aliitaka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara na Taasisi nyingine za Serikali  zinazohusika na maendeleo ya sekta ya madini kuheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

“Wizara ya Madini, ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hilo ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini,” alisisitiza Majaliwa.

Aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na maendeleo ya  sekta ya madini ambapo utekelezaji  wa dhamira hiyo unakwenda sambamba na kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha kuimarika kwa sekta ya madini nchini.


Jiwe la Msingi kwenye viwanja vya Soko la Madini Geita mara baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto) akielezea namna Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita ilivyojipanga kwenye usimamizi wa  Soko la Madini Geita kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kabla ya kuanza kwa shughuli za uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kabla ya kuzindua Soko la Madini  Geita tarehe 17 Machi, 2019. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) akizugumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Soko la Madini la Geita kufanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Soko la Madini Geita kabla ya uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa hotuba ya uzinduzi wa Soko la Madini Geita kwa wananchi na watendaji waandamizi wa Serikali (hawapo pichani) tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo kwenye uzinduzi huo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Simon Msanjila akitoa taarifa ya uzalishaji wa madini nchini kwenye uzinduzi huo.

Tutaendelea kuiunga mkono Wizara ya Madini-Mwenyekiti wa Kamati


Na Issa Mtuwa, Songea

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mariam Ditopile Mzuzuri amesema kamati yake inaipongeza na itaendelea kuiunga mkono Wizara ya Madini kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Akiongea na waandishi wa habari mbele ya kamati yake Machi 13, 2019 mjini songea baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha umahiri (Centre of excellence) kwa mkoa wa ruvuma, Mzuzuri amesema kamati yake inaridhishwa na kazi za Wizara ya Madini na wataendelea kuiunga mkono (support) hasa swala la wachimbaji wadogo.

“Tunawapongeza sana Wizara ya Madini, mnafanya kazi nzuri na sisi kama kamati niseme tutaendelea kuwaunga mkono (support) hasa hili la wachimbaji wadogo” alisema Mzuzuri.

Naibu Wziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo ameiambia kamati kuwa wizara yake imejipanga katika kukamilisha ujenzi wa vituo vyote vya umairi kikiwemo cha Songea kwa kuzingatia ubora. Amesema ujenzi wa vituo vyote unakwenda vizuri, hata hivyo kituo cha songea kilichelewa ujenzi wake tofauti na vituo vingine kwa sababu mbalimbali ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa kokoto tatizo ambalo lilisha tatuliwa na kwa sasa ujenzi unaendelea kwa kasi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekusudia kukamilisha ujenzi wa kituo hiki na vingine kwa wakati na kama nilivyo tangulia kusema zile changamoto zimesha tatuliwa na tuaendelea vizuri. Naishukuru kamati yako kwa kutuunga mkono na ushauri wote uliotolewa tutauzingatia.” Alisema Nyongo.

Nae Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Prof. Riziki Shemdoe akiongea kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo amewambia wajumbe wa kamati kuwa ni kweli kuna kipindi mkoa wa Ruvuma ulikumbwa na changamoto za upatikanaji wa kokoto na miradi mingi ya serikali ilisimama kutokana na kuwa na kampuni moja tu ya uzalishaji wa kokoto mkoa nzima, mara baada ya mitambo yake kuharibika na uzalishaji kusimama upatikanaji wa kokoto ulikuwa ni tatiizo.

Kituo cha Umahiri Songea ni miongoni mwa vituo mbalimbali vinavyo jengwa hapa nchini katika maeneo mbalimbali kama vile, kituo cha Bukoba, Simiyu, Tanga, Chuya kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo kujifunza na kupata uelewa wa masuala mbalimbali madini.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alie mbele akikagua na kutoa maelekezo kwa Meja Atupele Mwamfupe Meneja wa Ujenzi SUMA JKT Kanda ya Kusini kulia kwa Meja ni Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali watu  wa Wizara ya Madini Issa Nchasi kabla ya kuwasili kwa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini 

Meneja wa Kanda ya Ujenzi SUMA JKT, Meja Atupele Mwamfup akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa kituo na kutafsiri michoro mbalimbali ya jengo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Wizara ya Madini Issa Nchasi, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Makamu Mwenyekiti Mhe. Mriam Mzuzuri na wajumbe wengine.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akitoa maelezo ya ujenzi wa kituo cha umahiri songea kwa Makamu Mwenyekiti wa kamati Mhe. Mariam Mzuzuri kushoto kwake. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Wizara ya Madini Issa Nchasi na Meja Atupele Mwamfupe Meneja wa Ujenzi SUMA JKT Kanda ya Kusini.  

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Mariam Mzuzuri akimueleza jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wa kulia kwake mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha umairi. 

Friday, March 15, 2019

Waziri Kairuki amkabidhi rasmi Wizara Biteko


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki amemkabidhi rasmi Majukumu ya Uwaziri wa Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko katika kikao kilichohudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Waziri Kairuki amemshukuru Waziri Biteko kwa ushirikiano aliompatia kwa kipindi chote alichokuwa Waziri wa wizara hiyo na kueleza kwamba, kabla ya makabidhiano hayo, wamepata wasaa wa kupitia kwa pamoja majukumu na vipaumbele vya wizara ikiwemo maeneo muhimu yanayotakiwa kupewa msukumo.

Naye, Waziri Biteko, akizungumza mara baada ya kukabidhiwa majukumu hayo, amemshukuru Waziri Kairuki na kumwelezea kuwa ni Waziri aliyekuwa mwalimu mzuri kwake kwa kipindi chote alichokuwa Naibu Waziri.

Ameongeza, Waziri Kairuki hakuwahi kumnyima nafasi ya kujifunza ikiwemo kumtuma kutekeleza majukumu mbalimbali nafasi ambayo ilimkomaza.

“ Waziri hakuwahi kuninyima fursa, alinituma popote na nitaendelea kuhitaji ushauri wake katika kutekeleza majukumu yangu,” amesisitiza Biteko.

Makabidhiano hayo yamefanyika Machi 12, ofisini kwa Waziri Biteko Jijini Dodoma.

Waziri Biteko aliteuliwa Januari 8, 2019 kushika wadhifa huo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali. Waziri Biteko alichukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.


Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, akimkabidhi Nyaraka za majukumu ya Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko.Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, akimkabidhi Nyaraka za majukumu ya Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko.Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Madini Doto Biteko na Waziri Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, wakifurahia jambo mara baada ya makabidhiano. Katikati anayeshuhudia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Thursday, March 14, 2019

Acacia yazungumza na Serikali kunusuru Mgodi usifungwe


Na Issa Mtuwa, Dodoma

Uongozi wa Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa North Mara umezungumza na Serikali kuelezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa kudhibiti maji yenye sumu ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Waziri wa Madini Doto Biteko, atangaze kufunga shuguli za mgodi huo endapo utashindwa kudhibiti maji ya sumu yanayotiririka kwenye makazi ya watu, ifike Machi 30 mwaka huu.

Tamko hilo la serikali limeifanya kampuni ya Acacia kuchukua hatua za haraka za kudhibiti maji hayo ili kukwepa rungu la serikali la kuufunga mgodi huo.  Machi 12, uongozi wa Acacia North Mara ulikutana na Waziri Biteko ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kueleza hatua iliyofikiwa ya kutekeleza agizo la serikali.

Uongozi wa kampuni hiyo ukizungumza katika kikao hicho, ulieleza kuwa, tayari mgodi huo umechukua hatua za haraka tangu kutolewa kwa agizo na kwamba hadi sasa suala la kudhibiti maji yenye sumu limeshetekelezwa na hakuna maji yanayotiririka kuelekea kwenye makazi ya watu.

Aidha, ulimweleza kuwa, pamoja na kudhibiti maji hayo kupitia bwawa la kuhifadhia maji yenye sumu yajulikanayo kitaalam kama “topesumu” (Tailings Storage Facility- TSF) mgodi umeanza kuchukuwa hatua za kujenga TSF mpya.

“Mhe. Waziri tumekuja kutoa mrejesho wa utekelezaji wa agizo lako, tunafurahi kukuambia kuwa tumetekeleza agizo hilo na kwa sasa hakuna maji yanayotiririka. Pamoja na hatua hiyo mgodi umeanza mchakato wa ujenzi wa bwawa jipya (TSF) la kuhifadhia topesumu,” walieleza.

Aidha, ulimweleza Waziri Biteko kuhusu hujuma za uharibifu wa miundombinu ya bomba la maji yenye sumu unaofanywa kwa maksudi na wakazi wanaozunguka mgodi ili kufifisha juhudi zao za kudhibiti maji hayo wakiwa na lengo la kuufanya mgodi uonekane haujachukuwa hatua kudhibiti jambo hilo, ambapo walionesha picha mbalimbali ya namna bomba lilivyo pasuliwa ili maji yatiririke kuelekeka kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko alieleza kuwa, amepokea taarifa ya kampuni husika na kuwapongeza kwa hatua zilizochukuliwa na kusema kuwa, ukweli wa jambo hilo atauthibitisha mara baada ya kupata ripoti ya wataalam watakaokwenda kuhakikisha kuhusu utekelezaji wa agizo hilo na kuongeza,“katika hili sitanii juu ya kuufunga mgodi ikiwa utashindwa kudhibiti tope sumu,”.

 “Naomba nirudie tena katika hili sitanii, sitabadilisha msimamo wangu kama serikali na utaendelea kubaki pale pale dawa pekee ni kutekelezwa kwa agizo hilo. Lakini niseme ukweli, nasikitishwa sana na kitendo hiki cha wananchi kupasua bomba, kwa hili sikubaliani nao na siwaungi mkono.

 Pia, aliongeza kuwa, atawasiliana na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuona namna ya kudhibiti hali hiyo ili wale watakao bainika wachukuliwe hatua.

Waziri Biteko alilitoa agizo hilo   Machi 6, alipoutembelea mgodi huo hapo kwa ziara ya kikazi  pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime.


Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa.

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa. 

Kamati ya Bunge yaipongeza Wizara ya Madini


Na Issa Mtuwa, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kwa utekelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Taaluma la chuo cha Madini Dodoma (MRI) na Ujenzi wa Jengo la Ofisi za Wizara ya Madini lilipo eneo la Mji wa Serikali Ihumwa, Jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa  Machi 13, 2019 na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa kikao cha majumuhisho kilichofanyika kwenye jengo la wizara ya Madini Ihumwa, mara baada ya kukagua majengo yote mawili na kupewa taarifa ya ujenzi wake.

Wakiwa kwenye jengo la taaluma la chuo cha madini, wajumbe wamepongeza na kuridhishwa na  hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kupongeza SUMA JKT  kujenge jengo hilo.

Jengo la Taaluma ni la ghorofa tatu lenye ofisi, vyumba vya kufundishia na ukumbi wa mikutano. Ujenzi huo utagharimu jumla ya shilingi 2, 863, 161, 369.00 hadi kukamilika kwake  na unatekelezwa chini ya chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Raslimali Madini (SMMRP) kwa mkopo kutoka Benki ya  Dunia. 

Akizungumzia ujenzi wa jengo la Wizara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amewaeleza wajumbe wa kamati kuwa, ujenzi huo ulianza tarehe 4/12/2018 na ulitakiwa kukamilika tarehe 31/01/2019, hata hivyo mkandarasi hakuweza kukamilisha ndani ya muda huo kutokana na sababu mbalimbali. Prof. Msanjila ameongeza kuwa, kwa kuzingatia ushauri wa msimamizi wa ujenzi huo, walifikia makubaliano ya kumuongezea muda mkandarasi hadi kufikia tarehe 28/02/2019.

Prof. Msanjila ameongeza kuwa, mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 80 na mwezi ujao wizara itakuwa tayari kuhamia. Amesema ujenzi huo umegharimu Jumla ya shilingi Milioni 975,360,028.10 zitatumika katika ujenzi huo.

Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko ameiambia kamati kuwa, mkandarasi wa ujenzi huo, alipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha ujenzi wake ili wafanyakazi wa Wizara hiyo waanze kulitumia. Waziri emeleza kuwa wizara inaridhishwa na kasi ya mkandarasi katika ujenzi huo.

Biteko ameongeza kuwa, wizara imedhamiria kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuthibitisha hilo wizara imemteuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimaliwatu, Nsajigwa Kabigi ambae yupo muda wote wote eneo la ujenzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula amesema pamoja na wabunge kuipongeza wizara kwa kazi nzuri, ameishauri wizara na mkandarasi wa ujenzi huo, Mzinga Holdings Company kujielekeza kwenye manunuzi ya vifaa vinavyopatikana hapa nchini.

Wakichangia wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Musukuma na Ally Keissy wakichangia wakati wa majumuhisho waliipongeza wizara na mkandarasi, hata hivyo, walishangaa muda waliopewa na hatua iliyofikia, msukuma alisema ni kazi ya kupongeza na  wameeleza pamoja na mkandarasi kutokamilisha kazi yake kwa wakati bado utendaji wake wa kazi unaridhisha na kasi  yake inaonekana.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo aliwaambia wajumbe wa kamati kuwa, ujenzi wa jengo hilo la wizara unafanana ramani na wizara nyingine ikiwemo kiasi cha fedha zilizotolewa na serikali zote zikiwa na kiwango cha shilingi Bilioni moja.

Amesema muda uliotolewa ulilenga kutimiza azma ya wizara kuhamia eneo hilo kwa wakati. Aliwashukuru wajumbe kwa ushauri wao na kueleza kwamba kama wizara watauzingatia.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa na viongozi wa juu wa wizara ya madini wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jingo la Wizara Ihumwa Dodoma.  
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Danstan Kitandula wa kwanza kushoto akisikiliza maelezo ya ujenzi wa jengo la taaluma la chuo cha Madini (MRI) kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Fredrick Mangasini wa kwanza kulia na wapili yake ni Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteo. 


Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Danstan Kitandula wa kwanza kushoto akimueleza jambo Waziri wa Madini Doto Biteko, anae mtazama na wa kwanza kushoto ni Issa Nchasi Mkurugezi wa Utawala na Raslimali Watu Wizara ya Madini. 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na viongozi wa Wizara ya Madini wakiwa kwenye kikao cha majumuisho baada ya kutembelea miradi

Wednesday, March 13, 2019

Waziri Biteko azitaka nchi za Maziwa Makuu kudhibiti rasilimali ardhi


Na Issa Mtuwa Dodoma

Nchi Wanachama wa Maziwa Makuu zimetakiwa kushikamana kuunganisha nguvu katika kulinda na kusimamia matumizi ya raslimali ardhi ikiwemo madini ili kunufaisha nchi hizo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifungua mkutano wa Kimataifa wa nchi Wanachama wa Maziwa Makuu (International Conference on the Great Lakes Region - ICGLR) unaofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 11-12 Machi 2019 katika Hotel ya Morena jijini Dodoma.

Biteko amezitaka nchi hizo kuunganisha nguvu ya pamoja katika kudhibiti raslimali ardhi ikiwemo madini na kujiwekea utaratibu utakao dhibiti shughuli za uzalishaji na biashara ya madini ili raslimali hizo zinufaishe mataifa yao na zisitumike vibaya.

“Unganisheni nguvu kwa pamoja, wekeni utaratibu utakao wafanya nchi wanachama kunufaika na raslimali ardhi/madini. Jitahidini kuhakikisha raslimali hizo hazitumiki vibaya kama ilivyo kubaliwa kwenye itifaki, hivyo lazima kuwe na utaratibu na sheria kwa kila nchi namna ya kudhibiti uzalishaji na biashara ya madini,” amesema Biteko.

Naye, Mtaalam kutoka Wizara ya Madini, Mhandisi Assah Mwakilembe amesema Mkutano huo unalenga kujadili na kupitia mfumo wa udhibitisho wa mnyororo wa madini kwa lengo la kudhibiti uzalishaji na biashara ya madini katika nchi za maziwa makuu kufuatia kuwepo tetesi zilizo kuwa zinahusisha raslimali ardhi (Madini) na ufadhili wa vita katika nchi za aaziwa makuu. (Region Certification Manual).

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu marekebisho ya Sheria Madini ya Mwaka 2017 Mkurugenzi wa Idara ya Sheria kutoka Wizara ya Madini, Edwin Igenge amesema kwa upande wa Tanzania, imetekeleza itifaki ya pamoja ya nchi wanachama wa Maziwa Makuu kama ilivyo kubaliwa.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa itifaki kwa Tanzania ni pamoja na marekebisho ya sheria ya Madini ya Mwaka 2017 yaliyopelekea kuundwa kwa Tume ya Madini ambapo shuguli zote za usimamizi wa raslimali madini zimepewa Tume ya Madini ambapo kabla ya hapo shuguli hizo zilikuwa chini ya Kamishna wa Madini.

Igenge amesema kuanzishwa kwa itifaki katika nchi za maziwa makuu kulitokana na tetesi za uwepo wa matumizi mabaya ya raslimali ardhi ikiwemo madini ambapo kipato cha raslimali hizo inasadikika kuwa zilikuwa zinatumika kufadhili shuguli za za kivita katika nchi za maziwa makuu, hivyo kupelekea kuanzishwa kwa itifaki ya pamoja kwa lengo la kudhibiti.

Mkutano huo wa kimataaifa unahudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania, Burundi, Rwanda na wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Sekretariati ya nchi wanachama wa Maziwa Makuu. Kwa upande wa  Tanzania inawakilishwa na Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Shirikisho la Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Chama cha Wanunuzi  na Wauzaji wa  Madini Tanzania  (TAMIDA), Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa  Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST).

Katika mkutano huo, Waziri Biteko aliambatana na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Kamishna wa Madini Mhandisi Daivid Mulabwa, Mkurugenzi wa Sheria kutoka Wizara ya Madini Edwin Igenge na baadhi ya maafisa kutoka wizara ya Madini. 
Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akiongea na wajumbe wa mkutano wa kimataaifa wa nchi wanachama wa Maziwa Makuu jijini Dodoma.
Mjumbe kutoka Burundi Gerard Nayuburundi akiwasilisha mada kwenye mkutano wa kimataifa wa nchi wanachama wa Maziwa Makuu kwenye Hotel ya Morena Jijini Dodoma.

Tuesday, March 12, 2019

Waziri Biteko ateta na wenye nia ya kuwekeza nchini


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer ambaye amemweleza Waziri Biteko kuhusu ujio wa kampuni zipatazo 3 kutoka mataifa mbalimbali zenye nia ya kuwekeza katika sekta ya madini.

Dkt. Gollmer amesema kampuni hizo zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini hususan katika masuala ya utafiti na uchimbaji wa madini kutokana na ushawishi unaofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Urusi Meja Jenerali Mstaafu Simon Mumwi  ambaye amekuwa akihamasisha watu wa mataifa mbalimbali nchini humo kuwekeza nchini.

Pia, ameeleza kwamba, kampuni hizo hazina shaka ya kuwekeza Tanzania kutokana na mazingira tulivu ya kisisasa yaliyopo nchini pamoja na utajiri wa rasilimali madini ambayo Tanzania imejaliwa kuwa nayo.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko amemweleza Dkt. Gollmer kuwa kikao hicho ni muhimu na kwamba milango kwa ajili ya wawekezaji wenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini iko wazi na kuongeza kuwa, kama wizara inaratajia kukutana na kampuni hizo.
Wengine walioshiriki kikao hicho ni Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, Mkurugeni wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal na Katibu wa Waziri Kungulu Kasongi.


Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. 

Kamishna wa Madini David Mulabwa akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya Waziri wa Madini Doto Biteko na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. Anayefuatilia ni Mkurugenzi wa Ssera na Mipango Wizara ya Madini, Augustine Ollal. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akiteta jambo na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. Kulia wanaofuatilia ni Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Katibu wa Waziri, Kungulu Kasongi.