Na Nuru Mwasampeta,
Waziri wa
Madini Doto Biteko, amewataka Maafisa Madini wa mikoa kuepuka tuhuma za rushwa
na urasimu na kubainisha kuwa, hatamfumbia macho Mtumishi yeyote atakayebainika
kutekeleza majukumu yake kinyume na Sheria.
Aidha,
amewataka maafisa hao kuwabaini na kuwatambua wachimbaji wadogo waliopo katika
maeneo yao ya kazi.
Biteko
aliwaeleza maafisa hao kuwa wizara haita mfumbia macho mtumishi yeyote
asiyetekeleza majukumu yake na kukiri kuwa ni vema kufanya kazi na watu
wachache kuliko kufanya kazi na mamia ya watu wasiokidhi mahitaji na kasi ya
wizara katika kutekeleza majukumu yao.
Biteko
alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki alipofanya mkutano baina yake, Katibu
Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani
Manya pamoja na maafisa Madini wa Mikoa. Mkutano huo uliolenga kutoa msisitizo katika kutatua changamoto
zinazowakabili wachimbaji na wafanyabiashara wa madini katika maeneo yao ya
kazi.
“Tunao wachimbaji
wadogo wengi, wengi sana. Walio rasmi na wasio rasmi. Mwenye wajibu wa
kuwatambua wachimbaji hao ni ninyi. Lazima sasa hivi mkatengeneze data base kwenye mikoa yenu ili
kujua akina nani wanajihusisha na
shughuli za uchimbaji mdogo ili tutakapotaka kuwasaidia wachimbaji wadogo misaada hiyo
itolewe kwa wahusika kuliko kubahatisha,” alisisitiza Biteko.
“Tunataka
kuanzisha soko la madini, na Serikali itatoa nafuu (incentive) kwa wachimbaji wadogo, nafuu kwenye kodi, nafuu kwenye
ushuru, sasa hawa wachimbaji wadogo
watakaonufaika na punguzo hilo lazima tuwajue ni akina nani, lazima tuwe pro- active katika utendaji wetu wa kila
siku” alikazia.
Aidha,
Waziri Biteko aliwataka Maafisa hao kwenda kutekeleza na kusimamia Sheria
na kukataa kila aina ya maelekezo yanayotolewa kwao ambayo yanayokiuka sheria katika utekelezaji
wa majukumu yao.
Biteko
aliongeza kwa kuwataka Maafisa madini wa mikoa kuhakikisha wanafanya kazi na
kulifanya jina la Wizara ya Madini linakuwa zuri kuliko kuonekana kama watu wasiokuwa
na mwelekeo wa kiutendaji.
Biteko
alibainisha kuwa mpaka sasa wizara imehamisha watumishi 57 makao makuu ya
wizara ambao wizara imejiridhisha kuwa utendaji kazi wao hauridhishi na kwamba
zoezi hilo litaendelea kwa lengo la kuimarisha utendaji wizarani.
Zaidi ya hayo,
Biteko aliwataka Maafisa Madini hao kuhakikisha kuwa wanashirikiana na kamati
za ulinzi na usalama za mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya katika utekelezaji wa
majukumu yao ya kila siku na kuwataka kuwajibika kwao kwani ni wawakilishi wa Rais
na wanasimamia shughuli za Serikali.
Aliongeza
kuwa, wakuu wa wilaya ni wasimamizi wa Serikali katika maeneo hayo, ni
wawakilishi wa Rais katika wilaya na mikoa hiyo ni wasimamizi wa kazi zote za
serikali ikiwepo ya madini hivyo hawana budi kushirikiana nao.
Biteko aliwataka
maafisa Madini hao kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo ziwe ni za kibajeti
au vifaa ili waweze kusaidiwa na
kuwawezesha kutekeleza majukumu yao na kuwaagiza kumtumia Katibu Mkuu wa Wizara
Prof. Simon. Msanjila katika kutatua changamoto hizo.
Akizungumzia
suala la uanzishwaji wa vituo vya madini katika mikoa. Biteko alisema, Kanuni
za kusimamia vituo hivyo zimekwisha andaliwa na zitasainiwa wakati wowote na
kuwataka maafisa hao kutambua kuwa wao ni watu muhimu katika kusimamia vituo
hivyo.
Biteko alisema
anatamani ndani ya miezi sita sekta ya madini ibadilike, mtu akija aone kuna
maendeleo, aliwasihi kuhama kwenye majina ya kuitwa wala rushwa, tuhame kuitwa
warasimu tuhame kwenye sifa za watu wanaosimamia masuala ya madini pamoja na
kujihusisha na shughuli za uchimbaji jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Akihitimisha
kikao hicho, Biteko aliwataka maafisa hao kuhakikisha mapendekezo yote
yaliyotolewa katika mkutano wa kisekta kila mtu katika mkoa wake akayafanyie
kazi. Pia aliwaagiza kufanyia kazi
maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi wa wizara kwa nyakati tofauti ikiwa ni
pamoja na yale yaliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Kwa upande
wake Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya alieleza kufurahishwa na kukiri kwenda
kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kiongozi wa wizara hiyo.
Waziri wa Madini,
Mhe. Doto Biteko, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao baina ya
uongozi wa wizara na Maafisa Madini wa Mikoa kilichofanyika katika ofisi ndogo
za wizara jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment