Monday, December 31, 2018

Doto Biteko atoa maagizo mazito kwa wachimbaji kokoto Dodoma

Na Nuru Mwasampeta

Kufuatia ziara ya Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa  aliyoifanya hivi karibuni katika eneo la Ihumwa ambako ujenzi wa Mji wa Serikali unaendelea  na kubaini uhaba wa kokoto katika ujenzi huo,  leo Disemba 30, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko akifuatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana Anthony Mavunde wamefanya ziara ya kushtukiza kwenye maeneo yanayochimba kokoto hizo na kubaini madudu.

Naibu Mawaziri hao wamebaini machimbo ya kokoto yakiwa yamefungwa kwa madai kuwa wafanyakazi wako likizo, zikiwemo mashine za kusagia mawe hayo zikiwa  zimeharibika kwa takribani miezi mitatu na hivyo kupelekea uzalishaji kusimama.

Akizungumza katika eneo hilo la machimbo, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema anashangazwa kuona kuwa watumishi katika mgodi wa kokoto wanakwenda likizo wakati mahitaji ya kokoto ni makubwa  na soko la  uhakika.

“Mmechukua  zabuni  kwa ajili ya kusambaza kokoto kutoka kwa   Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),na  kampuni ya MZINGA wenye uhitaji mkubwa kwa ajili ya ujenzi wa mji wa Serikali unaoendelea halafu mnadai mko likizo,?” amehoji Biteko.

Akizungumza  kwa njia ya simu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Laroy Aggregate Co. Ltd , Biteko amemtaka  mkurugenzi huyo aliyefahamika kwa jina la Joel Mchovu kuhakikisha kuwa, ifikapo  Januari 2, 2019 kokoto ziwe zimezalishwa na kusambazwa kwa wahitaji kama walivyokubaliana ili ujenzi uendelee kwa kasi iliyokusudiwa.

Aidha, amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa ili kuzalisha kiasi kinachotosheleza mahitaji vinginevyo oda zitahamishwa na kupewa kampuni za zinazozalisha kokoto zilizopo Chalinze ambazo zinaonesha  uwezo mkubwa katika uzalishaji wa kokoto.
“Mfahamu kwamba endapo tutatoa oda kwa watu wa Chalinze maana halisi ya ujenzi wa mji wa Serikali kwa watu wa Dodoma haitakuwepo kwani hamtanufaika na ujenzi huu,” amesisitiza Biteko.

Biteko amewataka wananchi wa Dodoma kutambua kuwa, ujenzi wa mji wa Dodoma ni fursa kwao ya kuweza kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao binafsi hivyo, wanapaswa kuwajibika ili kupata manufaa hayo. “Fursa kubwa imepatikana na soko la uhakika lipo nitawashangaa kuona kuwa mnapoteza fursa hii,” amesisitiza.

Naye, Fundi wa Mitambo ya kuchoronga mawe katika mgodi wa WADI, Gao Peng, amesema kuwa, kampuni hiyo iko katika hatua za kutengeneza mashine iliyoharibika ili kuwawezesha kuendelea na uzalishaji wa kokoto hizo na kueleza kwamba mashine hiyo imeharibika kwa takribani kipindi cha  miezi mitatu sasa na hivyo kufanya uzalishaji wa kokoto hizo kusimama.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthony Mavunde, amesema anajisikia vibaya kuona kazi katika maeneo ya machimbo hazifanyiki na kuwataka wananchi wanaofanya shughuli hizo kuongeza nguvu, weledi na ufanisi ili  waweze kunufaika.

“Dodoma tumejaliwa kuwa na mawe mengi ya kuzalisha kokoto na madini mengine ya ujenzi, mahitaji ni makubwa kutokana na kasi ya ujenzi iliyopo lakini bado wana Dodoma mmelala,” amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Jonas Mwano amekiri kuwepo kwa leseni hai za uchimbaji wa madini ya kokoto 75 katika mji wa Chigongwe na leseni 66 zimekwisha tolewa kwa waliowasilisha maombi ya leseni hizo na hivyo kuwataka wamiliki wa leseni hizo kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni zao vinginevyo zitagawiwa kwa watu wengine.

Aidha, Mwano amekiri kuwa, awali wamiliki wengi wa leseni za madini ya kokoto walikuwa hawazalishi vya kutosha kwa madai kuwa soko lilikuwa adimu lakini sasa soko ni la uhakika na hivyo kuwataka wazalishe kokoto za kutosha ili kutoiangusha Serikali.

Pia, Mhandisi Mwano ameahidi kutembelea maeneo ya uchimbaji wa kokoto kila siku kufuatia maagizo ya Naibu Waziri Doto Biteko ili kuhakikisha kazi ya uzalishaji wa kokoto hizo unaridhisha na kutosheleza mahitaji ya ujenzi katika jiji la Dodoma.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto)  pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthon Mavunde (Kulia) wakiangalia moja ya kifaa kinachotumika katika kuchoronga mawe kwa ajili ya kokoto ambacho kwa sasa hakifanyi kazi kutokana na kuharibika. Katikati ni Fundi wa mashine katika mgodi wa WADI Gao Peng

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, akitoa tamko la Serikali kwa wachimbaji wa kokoto alipofanya ziara kujionea kinachoendelea katika machimbo hayo baada ya kubainika uhaba wa kokoto katika eneo la ujenzi wa ofisi za Serikali Ihumwa jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kutokea kushoto) akikagua eneo la uchimbaji wa kokoto katika kijiji cha Chigongwe alipofika kujionea ni kwa nini kokoto hazitoshelezi katika eneo la ujenzi wa mji wa Serikali Ihumwa. Kulia kwake ni fundi wa mashine katika mgodi wa WADI Gao Peng, akifuatiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthon Mavunde

 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni alipotembelea katika machimbo ya kokoto ya kampuni ya Laroy Aggregate Co. Ltd, Kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthon Mavunde na kushoto ni msaidizi wake Kungulu K. Masakala

Fundi wa mashine katika mgodi wa WADI Gao Peng (wa pili kushoto), akieleza jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (Wa pili kutoka kulia) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthon Mavunde (wa Kwanza kushoto) walipofanya ziara katika machimbo hayo ili kujionea kinachoendelea, wa kwanza kulia ni Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma mhandisi Jonas Mwano.

Miaka Mitatu ya Dkt. Magufuli ilivyoboresha sekta ya madini


Na Asteria Muhozya

Ni takriban Miaka Mitatu sasa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aingie madarakani kuliongoza Taifa la Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, Serikali anayoiongoza imefanya mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini kwa ajili ya kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinawanufaisha zaidi Watanzania.

Katika hatua za awali za kutekeleza mabadiliko hayo, Rais Magufuli Mwaka 2017, alianzisha Wizara mpya ya Madini baada ya kutenganishwa kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini kupitia Hati ya Majukumu (Instrument) Na.144 ya tarehe 22 Aprili, 2016 na Marekebisho yake ya tarehe 7 Oktoba, 2017.

Wizara hii ya Madini inaongozwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Naibu Mawaziri wawili, Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila.

Mbali na uundwaji wa wizara hii mpya, yamefanyika mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, utungwaji wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za nchi wa Mwaka 2017, na Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili za nchi wa Mwaka 2017.

Utungwaji wa Sheria hizo mpya na mabadiliko ya Sheria ya Madini na Kanuni zake kumeboresha ulipaji wa mrabaha wa Serikali kutoka asilimia nne (4) na kuwa asilimia sita (6) ya bei ya madini ghafi kwa madini ya metali na vito na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini ya kiasi cha asilimia moja (1).

Mabadiliko haya pia yanaiwezesha Serikali kuwa na umiliki wa asilimia zisizopungua 16 za hisa huru kwenye Migodi mikubwa na ya kati, kodi ya zuio ya asilimia tano ya thamani ghafi ya madini imeanzishwa kwa wachimbaji wadogo.

Akizungumza katika kipindi Maalum cha TUNATEKELEZA, Waziri wa Madini Angellah Kairuki anasema, Serikali imeweza kufanya majadiliano na wamiliki wa migodi ya ACACIA na TANZANITE ONE ambapo majadiliano hayo yameleta matokeo chanya kwa Acacia kukubali kuilipa Serikali kiasi cha Dola za Marekani Milioni 300.

Katika maelezo yake, Waziri Kairuki anaongeza kuwa, baada ya majadiliano na Kampuni ya Tanzanite One wamekubali kulipa fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali. “Tume maalum iliyoundwa na Rais inaendelea na majadiliano na makampuni yote makubwa yenye Mikataba na Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano, imedhamiria kuhakikisha rasilimali za madini zinasimimiwa ipasavyo ili ziweze kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Taifa na ustawi wa Watanzania,” anasema Waziri Kairuki.

Aidha, Kairuki anaeleza kuwa, Mabadiliko ya Sheria yamewezesha na kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi ili madini yaongezewe thamani hapa nchini. Aidha, Waziri Kairuki anasisitiza, mabadiliko hayo yanaifanya migodi ilazimike kutumia bidhaa na huduma za ndani ya nchi na kutoa uwezo wa usimamizi kisheria wa Sekta ya Madini kutakakoleta ufanisi mkubwa.

Akisisitiza suala hili katika moja ya mikutano yake na wadau wa sekta ya madini nchini, Waziri Angellah Kairuki anasema Serikali imeweka ZUIO la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi ikiwa na lengo la kuyaongezea thamani kabla ya kuyasafirisha. Katika kulisimamia hilo, anasema, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa Muswada wa Sheria ya uongezaji Thamani Madini, ili kuwezesha shughuli za Uongezaji Thamani madini kufanyika kwa kuzingatia Sheria na kusimamia vyema shughuli za uongezaji thamani madini nchini. 
Dhamira ya Serikali ni kujenga na kuendeleza Viwanda vya ndani, kuongeza Mapato ya Serikali kutoka Sekta ya Madini, na kurekebisha mapungufu yaliojitokeza katika utekelezaji wa Sheria zilizopo katika shughuli za uongezaji thamani madini hususani kwenye eneo la masonara,” anasisitiza Waziri Kairuki. 
Waziri Kairuki anaongeza kwamba, Wizara inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali. Pia, anafafanua kuwa, jumla ya maombi 27 ya uwekezaji kwenye smelters na refineries (ujenzi wa vinu (viwanda) vya uchenjuaji kwa ajili ya kusafisha na kuongeza thamani madini ya metali) yaliwasilishwa na uchambuzi unaendelea kufanyika ili kupata mwekezaji atakayekidhi vigezo. 
Akizungumzia ukuaji wa Sekta ya madini katika Awamu hii anasema, Sekta ya Madini ilikua kwa asilimia 17.5 Mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 9.1 Mwaka 2015. Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa uliongezeka na kufikia asilimia 4.8 Mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 4.0 Mwaka 2015.
Waziri Kairuki anasisitiza kuwa, Wizara imevuka malengo ya makusanyo ya maduhuli iliyopewa  mwaka 2017/18 ya Shilingi bilioni 194.66 na kuweza kukusanya Shilingi bilioni 298 sawa na asilimia 153.09. 
Pia anaongeza, kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa Sekta ya Madini kumetokana na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini; kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini; na usafirishaji wa madini nje ya nchi; kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017 na Kanuni zake.

Akizungumzia uundwaji wa Tume ya Madini, ambayo ni zao la Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka, 2010, baada ya kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (Tanzania Mineral Audit Agency–TMAA), Waziri Kairuki anasema kuundwa kwa Tume ya Madini, kumepelekea  usimamizi  wa karibu zaidi wa maeneo yenye uchimbaji wa madini. Aidha, uwepo wa ofisi za madini katika mikoa mbalimbali nchini unarahisisha ushughulikiaji wa maombi ya leseni, kupunguza migogoro na kuongeza makusanyo ya mrabaha.

“Pia, Tume imesimamia shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta wa Mererani ili kudhibiti utoroshwaji wa Madini ya Tanzanites na madini mengine ili kuimarisha ukusanywaji wa kodi za Serikali,” anasema Waziri Kairuki.

Akizungumza katika Mkutano baina ya Waziri Kairuki na Wafanyabiashara wa Madini ya Tanzanite jijini Arusha, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Sam Mollel anasema ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya Tanzanite Mirerani umeongeza Imani kubwa kwa walaji wa madini hayo zikiwemo nchi za Marekani na Ulaya huku akisisitiza kuwa, ukuta wa Mirerani umedhibiti ajira za watoto migodini na kuondoa wizi wa vifaa migodini.

Haya ni baadhi tu ya mafanikio yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Madini. Kwa hakika watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada hizi zinazofanywa na Serikali ambazo zinalenga kuhakikisha kwamba rasilimali madini zinalinufaisha taifa na watanzania wote.

Aidha, katika kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika pato la Taifa na ukuaji wa uchumi, Waziri Kairuki anasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, lengo la wizara ni kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia zaidi katika pato la Taifa ili hadi ifikapo mwaka 2025 sekta husika iweze kuchangia hadi kufikia asilimia kumi (10%).


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza mmoja wa Wachimbaji wa Madini ya Bati katika moja ya ziara zake za kukagua shughuli za uchimbaji madini, Kyerwa mkoani Kagera.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia bidhaa za mapambo zilizotokana na madini yanayopatikana nchini baada ya kuongezwa thamani.

Wanafunzi wa Shule za Sekondari jijini Arusha wakiangalia Madini ya Tanzanite wakati wa Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito na Usonara ya Arusha (AGF) yaliyofanyika Mwezi Mei,2017.

Monday, December 24, 2018

Kituo cha Jemolojia Tanzania-Nafasi za mafunzo kwa ngazi ya diploma na cheti kuanzia mwezi Januari, 2019


Profesa Kikula aongoza kikao cha kazi Tume ya Madini


Na Greyson Mwase, Dodoma

Leo tarehe 21 Desemba, 2018 Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ameongoza kikao cha kazi cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kilishirikisha makamishna wa Tume ambao ni Mtendaji  Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Nchini (FEMATA), Haroun Kinega, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Dorothy Mwanyika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Florence Turuka na  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa.

Wengine ni Dkt. Athanas Macheyeki, Profesa Abdulkarim Mruma Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji wa Tume ya Madini.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Tume na Mpango Mkakati wa Tume wa miaka mitano (2019/20 -2023/2024). Katika kikao hicho kati ya masuala yaliyokubaliwa ni pamoja na leseni ambazo hazifanyiwi kazi kufutwa na tathmini ya kina kufanyika kwa waombaji wa leseni ili kubaini kama wanakidhi vigezo kama vile uwezo wa kifedha na utaalam.


Kamishna kutoka Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma (kushoto) akifafanua jambo katika kikao cha Tume ya Madini kilichofanyika Desemba 21, 2018 jijini Dodoma. Wengine kutoka kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula.



Kutoka kushoto makamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega na Dkt. Athanas Macheyeki wakifuatilia majadiliano mbalimbali yaliyokuwa yanaendelea katika kikao hicho. 

Kutoka kushoto mbele makamishna wa Tume ya Madini  ambao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Dorothy Mwanyika, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Florence Turuka wakifuatilia ufafanuzi  uliokuwa unatolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (hayupo pichani) 

Sehemu ya wajumbe kutoka Tume ya Madini wakifuatilia majadiliano yaliyokuwa yanaendelea katika kikao hicho. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akifafanua jambo katika kikao hicho

Tuesday, December 18, 2018

Prof. Msanjila akutana na ujumbe wa Serikali ya India

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amekutana na Ujumbe   wa Serikali kutoka nchini India pamoja na Kampuni ya National India Development Corporation (NMDC) jijini Dodoma, katika kikao ambacho pia kimeshirikisha watendaji kutoka Wizarani, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Tume ya Madini.

Ujumbe huo umefika wizarani kwa lengo la kuonana na uongozi wa Wizara kwa ajili ya kufanya majadiliano juu ya nia yao ya kufanya uwekezaji kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kupata maeneo mapya ya uchimbaji. Awali kampuni hiyo ilikutana na Shirika la STAMICO na kufanya majadiliano kuona ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana katika utekelezaji wa malengo yao kupitia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Desemba 18, Katibu Mkuu Prof. Msanjila amewakaribisha na kuwapongeza kwa nia yao ya kufanya uwekezaji nchini na kuueleza ujumbe huo kuwa, kampuni ya NMDC inayo fursa ya kuchagua kuwekeza ikiwa kama kampuni inayojitegemea ama kwa kuingia ubia na Shirika la Madini la Taifa la (STAMICO).

Aidha, ameuleza ujumbe huo kuwa, wizara inazo taasisi ambazo zinasimamia masuala yanayohusu leseni na shughuli za utafiti na kuusisitiza kujadiliana na Kamishna wa Madini, Mkurugenzi wa Sheria na Tume ya Madini kwa ajili ya kupata taratibu zinazotakiwa kisheria kuhusu masuala ya leseni na mahitaji mengine wanayotakiwa kutekeleza kabla ya kuwasilisha mpango huo kwenye ofisi yake. Aidha, aliutaka ujumbe huo kujadiliana na GST kwa masuala yanayohusu shughuli za utafiti wa madini.

Pia, Prof. Msanjila ameishauri kampuni husika kukata leseni ya utafiti kwanza ili kufanya utafiti katika maeneo waliyoyakatia leseni na kuwasilisha taarifa hizo katika ofisi ya GST ndipo waendelee na utaratibu wa kupata leseni ya uchimbaji. Vilevile, ameutaka ujumbe huo kuwa tayari kuwasiliana na wizara pindi unapohitaji kupata ufafanuzi wa masuala yote ya yanayohusu uwekezaji katika sekta husika.


Kampuni ya NMDC inajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa
 madini ya chuma na iko chini ya Wizara inayoshughulikia madini ya 
chuma ya India.  Pia kampuni hiyo pia inajishughulisha na utafiti wa 
madini mbalimbali kama vile madini ya chuma, shaba, phosphate, nk.
katika nchi mbalimbali na barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akieleza jambo katika kikao kati yake na ujumbe wa Serikali ya India na Kampuni ya National India Development Corporation  (NMDC)

Sehemu ya ujumbe kutoka Serikali ya India na Kampuni ya NMDC pamoja na watendaji wa wizara wakifuatilia kikao hicho.

Sehemu ya Watendaji kutoka Tume ya Madini, Taasisi na Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia kikao hicho.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiongoza kikao baia yake na ujumbe kutoka Serikali ya India kilichoshirikisha pia Watendaji kutoka Wizarani, Tume ya Madini na GST.

Mgodi wa Wachimbaji Wadogo Mahenge Wafunguliwa


Ø Ni baada ya kufungwa kwa miezi Mitano
Ø Biteko azidua Ofisi ya Madini Ulanga

Na Rhoda James, Mahenge

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameufungua mgodi wa Wachimbaji Wadogo wa Mahenge baada ya kufungwa kwa takribani miezi Mitano tangu   Julai 10, 2018.

Mgodi huo wa madini ya Vito aina ya Spino uliopo Wilayani Ulanga ulisimamishwa kutokana na kukiukwa kwa taratibu za uchimbaji wa madini ikiwemo  kutolipa kodi za Serikali.

Akizungumza katika mkutano kati yake na wachimbaji Biteko alisema kuwa, Sekta ya Madini haipo kwa ajili ya kufunga migodi, na kuongeza kuwa, hakuna mchimbaji yeyote atakayeruhusiwa kuchimba katika eneo hilo hadi pale atakapokuwa amelipa madeni yake angalau ya awamu ya kwanza.

Pia, alisema kuwa, ikiwa kuna mchimbaji ambaye atakiuka taratibu za uchimbaji, atachukuliwa hatua za kisheria  na si kwa kufungiwa mgodi tu bali atapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

 “Nyie ni wadau muhimu katika sekta ya maendeleo, na mkilipa kodi, ikaonekana imefanya nini, hata wawekezaji hawatakwepa kulipa kodi,” alisema Biteko.

Aliwataka Wachimbaji Wadogo wa Mahenge kubadilika na kufuata taratibu zilizowekwa kisheria na kusema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitaki rushwa hususan kwenye Sekta ya Madini.

Aidha, pamoja na kufuungua mgodi huo, Biteko pia alizidua Ofisi ya Afisa  Madini Mkazi wa Mahenge, ikiwa ni mojawapo ya mahitaji ya awali ili shughuli za uchimbaji madini katika Mji wa Mahenge ziende  kama inavyotakiwa.

Pia, Biteko alimtaka Afisa Mkazi wa Mahenge, Tandu Jirabi kuhakikisha leseni za dealers zinasainiwa ili  pamoja na kutoa utaratibu kwa wadau hao kuhusu namna ambavyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kabla ya  kupatiwa leseni.

“Mzawa lazima awe na mashinetano na mwekezaji kuwa na mashine 30,” alisema Biteko.

Aidha, Biteko alitoa wito kwa viongozi wa Halmashauri ya Mahenge kuhakikisha kuwa fedha zinazolipwa kama kodi zinatumika ipasavyo katika kuwezesha huduma mbalimbali za jamii ikiwemo kujenga Zahanati, Shule, Barabara na kadhalika.

Kwa Upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mahenge Goodluck Mlinga alimshukuru Naibu Waziri Biteko kwa kufugua mgodi huo wa wachimbaji wadogo na kuwataka wananchi wa Mahenge kufuata taratibu zinazotakiwa ili kuepusha usubufu kama huo uliojitokeza hapo awali.

Mlinga alisisitiza kuwa, kodi inayolipwa na Wachimbaji Wadogo lazima itekeleze majukumu yaliyopangwa na kumwakikishia Naibu Waziri kuwa wachimbaji watalipa kodi kwa kishindo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya alisema kuwa Rais Magufuli anataka kila mwananchi afaidike na rasilimali za madini, hivyo, kuwataka wananchi na Wachimbaji wote wa Mahenge  kufuata taratibu zilizopo ili kila mmoja wao afaidike na rasilimali hiyo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja baada ya kuzidua Ofisi ya Madini Wilayani Ulanga katika Mji wa Mahenge uliofanyika tarehe 14 Desemba, 2018. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Mahenge Goodluck Mlinga na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akikata utepe kuashiria uziduzi wa Ofisi ya Madini Wilayani Ulanga katika Mji wa Mahenge uliofanyika tarehe 14 Desemba, 2018. 

Mbunge wa Jimbo la Mahenge Goodluck Mlinga akiwahutubia wananchi pamoja na wachimbaji wadogo wa madini (hawapo pichani) wilayani Ulanga katika mji wa Mahenge, wakati wa ziara ya Naibu Waziri Biteko. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akimtambulisha Afisa Mkazi mpya wa Madini wa Mahenge kwa wananchi (hawapo pichani) baada ya kuzidua Ofisi ya Madini ya Mahenge tarehe 14 Desemba, 2018. 

Wananchi wa Mahenge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) wakati alipofanya mkutano wa hadhara katika mji wa Mahenge wilayani Ulanga. 

Wananchi wa Mahenge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) wakati alipofanya mkutano wa hadhara katika mji wa Mahenge wilayani Ulanga. 

Kamshina wa Madini, Dk. Athenes Macheyeki akitia saini katika kitabu cha Afisa Mkazi wa Madini Mahenge baada ya kuziduliwa kwa Ofisi hiyo tarehe 14 Desemba, 2018. Wanaoshuhudia ni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko aliyekaa na Mbunge wa Jimbo la Mahenge, Goodluck Mlinga kulia.

Monday, December 17, 2018

Nyongo aitaka Tume ya Madini kuchunguza chanzo cha mgogoro wa wachimbaji madini, Kilwa


Na Greyson Mwase, Kilwa

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameitaka Tume ya Madini kufanya uchunguzi kuhusu mgogoro kati ya kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya Kizimbani inayomilikiwa na Seleman Mohamed na wananchi wa kijiji cha Hotel Tatu kilichopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Naibu Waziri Nyongo ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Desemba, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho wakati wa utatuzi wa mgogoro huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Lindi yenye lengo la kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Alisema kuwa, baada ya kusikiliza pande zote mbili imeonekana kuna haja ya  Tume ya Madini kufanya uchunguzi ili kubaini namna utoaji wa leseni ya uchimbaji wa madini ya jasi kwa kampuni ya Kizimbani ulivyofanyika kabla ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa sheria na kanuni za madini.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo alisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini haitasita kuwaondoa maafisa madini wakazi wa mikoa watakaobainika kuwa ndio chanzo cha migogoro kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini.

“Kama Serikali tunataka kuhakikisha leseni za utafiti na uchimbaji wa madini zinatolewa kwa kufuata sheria na kanuni za madini bila kuwepo kwa migogoro ya aina yoyote, aidha hatutasita kumwondoa afisa madini mkazi yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha migogoro kwenye shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini,” alisema Naibu Waziri Nyongo huku akishangiliwa na wananchi.

Awali wakielezea mgogoro huo kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa walikuwa na mgogoro wa muda mrefu kati yao na Seleman Mohamed aliyedai kuwa mmiliki halali wa eneo husika hali iliyopelekea mgogoro kuwasilishwa kwenye Ofisi ya Madini Mtwara, ambapo  mtaalam kutoka ofisi hiyo alifika kwa ajili ya kuchukua alama za eneo husika kwa ajili ya kwenda kuhakiki umiliki wa eneo husika.

Waliendelea kusema kuwa, walifika katika Ofisi hiyo baada ya siku mbili na kuelezwa kuwa eneo hilo lilishaombewa leseni na kutolewa kwa mmiliki wa kampuni ya Kizimbani, Seleman Mohamed.

Walisema kuwa tangu kuzuka kwa mgogoro huo mwaka 2013, wamekwenda katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Mkoa pasipo mafanikio yoyote na kusisitiza kuwa wanahitaji eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya jasi kwa kutumia mwekezaji na  kujipatia kipato pamoja na kulipa kodi Serikalini.

Kwa upande wake mmiliki wa leseni hiyo, Seleman Mohamed alidai kuwa aliomba leseni kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kupatiwa leseni yake.

Wakati huo huo akizungumza katika nyakati tofauti kupitia mikutano na wazalishaji wa chumvi iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi na katika eneo la Kilwa Masoko Wilayani Kilwa mkoani Lindi, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini inatambua mchango wa wazalishaji wa chumvi hususan katika mkoa wa Lindi kwenye Sekta ya Madini hivyo imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasaidia.

Alieleza mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuondoa tozo mbalimbali tisa kisheria zilizokuwa zinatozwa na halmashauri ili uzalishaji wao uwe na tija na kuinua uchumi wa mkoa wa Lindi.

Alieleza kuwa mikakati mingine kuwa, ni pamoja na kuendelea kushughulikia changamoto zilizopo kwenye uzalishaji chumvi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chumvi katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi mara baada ya kupata eneo na fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini. (SMMRP) uliopo chini ya Wizara ya Madini.

Aliendelea kusema kuwa mahitaji ya chumvi nchini ni takribani tani laki tatu na nusu kwa mwaka ambapo asilimia 70 ya chumvi inaagizwa kutoka nje ya nchi  na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imejipanga katika uboreshaji wa uzalishaji wa chumvi nchini.

“Kama Wizara ya Madini tunataka ifike mahali tuzalishe chumvi bora ya kutosha na kuuza ya ziada nje ya nchi na kujiingizia fedha za kigeni,” alisema Naibu Waziri Nyongo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliwataka wazalishaji wa chumvi hao kufuata sheria na kanuni za madini.

Wakizungumza katika nyakati tofauti wazalishaji wa chumvi mkoani Lindi waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na tozo zilizoondolewa kisheria kwenye madini ya chumvi kuendelea kutozwa na halmashauri, ukosefu wa mitaji pamoja na masoko.

Changamoto nyingine ni pamoja na miundombinu duni kwenye maeneo yenye uzalishaji wa chumvi, madini joto yanayotumika kwenye uzalishaji wa chumvi kuuzwa kwa gharama kubwa na kutotambuliwa katika halmashauri na taasisi  nyingine za kifedha.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, kabla ya kuanza ziara yake katika Wilaya ya Kilwa yenye lengo la kukagua shughuli za madini pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wazalishaji wa madini ya chumvi mara baada ya kumalizika kwa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akielekeza jambo kwenye sehemu ya kukusanya madini ya jasi iliyopo katika eneo la Hoteli Tatu Wilayani Kilwa mkoani Lindi. Kushoto mbele ni Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia Omari.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Hoteli Tatu kilichopo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi wakifuatilia ufafanuzi  uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya kijiji hicho na mmiliki wa kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya Kizimbani, Seleman Mohamed.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia madini ya chumvi katika eneo la Jangwani kwa Chinja lililopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Wachimbaji madini Namungo waomba vifaa


Na Greyson Mwase, Ruangwa

Wananchi katika kijiji cha Namungo kilichopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuwapatia vifaa bora ili kuboresha  uchimbaji wa madini na kuchangia kwenye pato la taifa kupitia Sekta ya Madini.

Wameyasema hayo leo  tarehe 14 Desemba, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanywa katika kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya  ziara ya siku mbili ya  Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo mkoani Lindi yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Dickson Baltazary ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu alisema kuwa, wamekuwa wakichimba madini kwa kutumia zana duni hali inayowasababishia kushindwa kufikia malengo yao kwenye uzalishaji.

Baltazary aliongeza kuwa, iwapo watapata fedha kupitia mikopo na ruzuku Serikalini kupitia Wizara ya Madini wataweza kufanya shughuli zao za uchimbaji wa madini kwa ufanisi na kuchangia zaidi kwenye mapato ya Serikali.

Akizungumza na wachimbaji hao mara baada ya kupokea kero mbalimbali, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia wachimbaji wadogo ambapo mpaka sasa maeneo yameanza kutengwa kwa ajili ya uchimbaji madini.

Aliendelea kusema kuwa Serikali inaangalia utaratibu mzuri utakaowawezesha kupata ruzuku.

Wakati huohuo, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nangurugai Wilayani Ruangwa mkoani Lindi Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi kuunga mkono uwekezaji wa uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) unaotarajiwa kufanya na kampuni ya utafiti wa madini hayo ya Chilalo Graphite Mine.

Aidha, aliwapongeza wananchi hao kwa kuunga mkono uwekezaji huo kwa kuwa na subira wakati wa tathmini iliyofanywa miaka miwili iliyopita na kuitaka kampuni ya Chilolo kurudia tathmini kwani thamani ya mali imebadilika.

Akielezea manufaa ya mradi huo, Nyongo alieleza kuwa ni pamoja na ajira 480 kutolewa wakati wa ujenzi wa mgodi na ajira 250 kutolewa mara baada ya uendeshaji wa mgodi kuanza.

Alieleza manufaa mengine kuwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wa Wilaya ya Ruangwa kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na uzalishaji wa madini hayo.

“Madini ya kinywe yana soko kubwa duniani  kutokana na kampuni nyingi kutumia madini hayo katika utengenezaji wa betri za magari, ni vyema mkachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi,” alifafanua Nyongo.

Katika hatua nyingine, Nyongo aliutaka mgodi huo kuhakikisha unatoa ajira kwa wananchi wenye sifa wanaozunguka karibu na mgodi kabla ya kufikiria kuajiri wageni kutoka katika mikoa mingine.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akifafanua jambo alipofanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Namungo uliopo Wilayani Ruangwa mkoani  Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali. Katikati ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia Omari. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo kuhusiana na shughuli zinazofanywa na kampuni  inayojishughulisha na utafiti  wa madini ya Kinywe ya Ngwena Limited iliyopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akizungumza na  wananchi wa kijiji cha Nangurugai kilichopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi. 

Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Namungo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akikagua shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu  katika Mgodi wa Dhahabu wa Namungo uliopo Wilayani Ruangwa mkoani  Lindi.