Thursday, November 29, 2018

Waziri Kairuki ataka kaguzi za mara kwa mara Migodini


Na Asteria Muhozya, Chunya

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amewataka Maafisa Madini nchini kuhakikisha wanafanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya wachimbji wadogo ikiwemo kutoa elimu ya uchimbaji, masuala ya afya na usalama kazini ili kuongeza tija katika shughuli hizo.

Waziri Kairuki aliyasema hayo Novemba 27, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Chunya kinachojengwa na Mkandarasi kampuni ya SUMAJKT.

Alisema, wachimbaji wadogo wanatakiwa kulelelewa ili watoke katika uchimbaji mdogo wa madini kwenda uchimbaji wa  Kati na hatimaye kuwa wachimbaji  wakubwa, na kueleza kuwa, ili kufikia azma hiyo  elimu ya mara kwa mara kwa wachimbaji ni muhimu  ikatolewa  kwani itawezesha serikali kupata mapato kutokana na kufuata uchimbaji sahihi.

Pia, aliwataka Maafisa hao kuhakikisha kuwa wanatatua migogoro katika maeneo yao kwani suala hilo litawezesha uzalishaji zaidi na kupelekea serikali kunufaika na shughuli hizo, ikiwemo ongezeko la ajira na ustawi wa jamii.

Vilevile, Waziri Kairuki alieleza kuwa, pamoja na kwamba katika Mwaka wa Fedha 2018/19 wizara yake imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 310, lakini kama anataka makusanyo hayo yafikie shilingi bilioni 500 na kuongeza kwamba, Maafisa madini watapimwa kutokana na ukusanyo huo wa maduhuli.

“ Sisi tumepangiwa kukusanya shilingi bilioni 310. Lakini na mimi nataka makusanyo hayo yafikie shilingi bilioni 500 na nitawapima maafisa madini kwa ukusanyaji wa maduhuli,” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine, amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashaurina na Wizara ya madini katika masuala yote yanayohusu kodi za madini kabla ya kuyatolea maamuzi kwa kuwa, isipofanyika  hivyo inachangia taasisi za serikali kukinzana katika utoaji wa maamuzi.

Alisema, wizara inaandaa utaratibu wa kukutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali   na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kulijadili suala la  kodi katika sekta ya madini.

Akizungumzia umuhimu wa Kituo cha Umahiri, alisema kuwa, kitawezesha wachimbaji kujua taratibu zinazotakiwa katika  utekelezaji wa majukumu yao katika sekta ya madini na kwamba, wizara inaangalia uwekezano wa kuwa na vituo hivyo katika kila mikoa ikiwemo ofisi za kisasa na vituo vya mafunzo ili kuwezesha  kuwepo na tija zaidi katika sekta ya madini.

“Tumeanza na vituo vya mahiri lakini upo umuhimu wa maafisa wetu kuwa na nyumba za kuishi lakini  pia kuhakikisha kwamba maafisa wetu hawakai katika eneo moja kwa kipindi kirefu,” alisema.  

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Wilaya ya Chunya Athumani Kwariko alimweleza Waziri Kairuki kuwa, leseni nyingi wilayani humo hazifanyiwi kazi kutokana na wamiliki wake kukosa mitaji na uwepo wa migogoro.  Hata hivyo amesema kuwa, tayari ofisi hiyo imewasiliana  na  wamiliki hao ili kuhakikisha kwamba wanaziendeleza leseni hizo.

Akizungumzia madini yanayopatikana  wilayani humo  hiyo  aliyataja kuwa ni  pamoja na   ya  dhdhabu, chuma,  bati, ulanga, chokaa na kokoto na mchanga.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Mkoa wa Mbeya Leonard Manyesha akielezea umuhimu wa kituo hicho alisema kwamba kitawawezesha  kupata maelekezo ya kitaalam kuhusu uchimbaji na hivyo kuwawezesha kupata mazao bora ya dhahabu na yenye tija.

Aidha, alipongeza kwa hatua ya serkali ya kutaka kuhamasisha Mikoa kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishaji wa masoko ya madini na kueleza kuwa, uwepo wa masoko hayo utasaidia tatizo la wachimbaji kuficha mapato kuisha.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia ramani ya jengo la Kituo cha Umahiri Chunya litakavyokuwa mara baada ya kukamilika kwake. Jengo hilo linajengwa na Mkandarasi SUMAJKT. 

Sehemu ya jengo la  Kituo cha Umahiri Chunya  likiwa katika maendeleo ya ujenzi wake. 

Sehemu ya viongozi wa Wilaya, viongozi wa  Ofisi za Madini Mbeya na Chunya pamoja na wadau wa madini wilayani humo wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani). 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akisikiliza jambo kutoka kwa Mkandarasi SUMAJKT  alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Chunya. Wengine ni Wataalam kutoka Ofisi za Madini Mbeya na Chunya, wataalam kutoka Wizara ya Madini, na uongozi wa Wilaya ya Chunya.

Wednesday, November 28, 2018

Serikali haijaruhusu uchimbaji madini Mto Muhuwesi-Kairuki


Na Asteria Muhozya, Songea

Serikali imesema haijaruhusu uchimbaji wa Madini katika Mto Muhuwesi na kwamba tayari Wizara ya Madini ilikwishakutoa maelekezo  yapatayo matano ambayo wahusika wanatakiwa kuyafanyia kazi ili itoe  maamuzi.

Hayo yalielezwa na  Waziri wa Madini Angellah Kairuki  wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Songea, wakati akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina  Mndeme ambaye   alimwomba Waziri asimamishe uchimbaji huo na kwamba tayari  Mkoa  umezuia  shughuli hizo kuendelea  kwa kuwa  ndiyo chanzo cha maji mkoani humo na kwamba, alifanya hivyo ili kulinda miundombinu ya barabara.

Waziri Kairuki alimweleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa, wizara ilitoa maelekezo kwa  wahusika kwamba wanatakiwa  kuwasilisha barua ya ridhaa ya Waziri wa Maji, ridhaa ya Wakala wa Barabara nchini (TANROAD), ridhaa ya Bodi ya Bonde la Mto Ruvuma/Pwani na Kusini ili wizara ijiridhishe kabla ya kutoa maamuzi.

“Tunataka tujiridhishe na approval kutoka katika maeneo hayo na vikipatikana vyote, nitafanya uamuzi. Kwa sasa ipo ridhaa ya bodi ya bonde la mto Ruvuma,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Pia, akifafanua  kuhusu kusimama kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya Uranium unaofanywa na Kampuni ya  Mantra Tanzania Limited, waziri Kairuki  alisema  kuwa,  kampuni hiyo iliomba kusisitisha shughuli zake  kwa kipindi cha miaka mitano kutokana na bei ya madini hayo kushuka katika soko la dunia na kwamba , suala hilo bado linafanyiwa kazi kitaalam na kiuchumi hivyo, bado serikali haijatoa majibu kuhusu suala husika.

Kuhusu  upatikanaji wa masoko kwa wachimbaji wa madini, Waziri Kairuki  alieleza kuwa,   tayari  serikali imepanga kuanzisha masoko ya madini  katika maeneo mbalimbali nchini, na hivyo  kutoa rai kwa  Wakuu wa Mikoa nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishwaji wa masoko hayo. Waziri Kairuki  alitoa ufafanuzi kwa  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina ambaye alitaka kujua ni namna gani serikali inawasaidia wachimbaji wadogo kupata masoko ya kuuzia madini madini yao.

“Mhe. Waziri Mkoa wetu umejaliwa kuwa na madini ya aina mbalimbali na madini haya yamekuwa ni kichocheo cha uchumi. Sasa, bado wachimbaji wetu wanapata changamoto ya masoko kwa ajili ya kuuza madini yao,” alisema Mkuu wa Mkoa Mndeme.

Akizungumzia  ujenzi wa Vituo vya Umahiri, Waziri Kairuki alisema, ujenzi wa vituo vya umahiri vinavyojengwa maeneo mbalimbali nchini vinagharimu takribani  Bilioni 11 ambao ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Aliongeza kuwa,   Songea ni eneo  ambalo serikali inaliangalia kwa ajili ya  kuanzisha shughuli za ukataji na uongezaji thamani madini.

Alisema kuwa, serikali iliona umuhimu wa kuwepo na vituo hivyo kutokana na wananchi  wengi kutamani kuingia katika shughuli za uchimbaji  lakini bado  uchimbaji wao umekuwa si salama na wenye tija hivyo, uwepo wa kituo hicho utawezesha kutoa elimu ya uchimbaji sahihi na wenye tija.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Christina Mndeme akizungumzia uwepo wa kituo hicho alisema, kukamilika kwa kituo hicho kutawezesha shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika mkoani humo, kupanua wigo wa shughuli za uchimbaji na wachimbaji kuchimba kwa faida.

Aliongeza kwamba, wachimbaji watapata taarifa sahihi wa mahali gani wauze madini yao  na pia uwepo wake  utawezesha kutangaza aina ya madini yanayopatikana mkoani huo.

Vilevile, alisema kuwa, kituo hicho kitawezesha kupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa kwani kitawezesha kupata taarifa sahihi za wapi wachimbe madini.

Naye, Afisa Madini Mkoa wa Ruvuma Abraham Nkya alisema kuwa, ujenzi wa kituo hicho utawezesha kurahisisha upatikanaji wa takwimu za madini za mkoa huo, wachimbaji kupata elimu ya utaalamu wa uchenjuaji bora wa madini, elimu ya ujasiliamali wa shughuli za madini, afya na usalama mahali pa kazi.

Pia, aliongeza kuwa, uwepo wa kituo hicho chenye nafasi kubwa, kitaweza kuwahudumia wachimbaji wengi zaidi.

Waziri Kairuki alitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Songea Novemba 26.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) na Mkuu wa MKoa wa Ruvuma Christina Mdeme  (kulia ) wakichanganya kokoto katika Kituo ch Umahiri Songea  wakati wa ziara Kairuki kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho 

Sehemu ya jengo la Kituo cha Umahiri Songea katika hatua zake za  ujenzi 

Afisa Madini Mkazi wa Songea   Abraham Nkya akieleza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Madini Angellah Kairuki alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho. 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki  kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mdeme (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Songea Ploliti Mgema wakijadiliana jambo wakati  Waziri Kairuki alipomtembelea Mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake. 

Baadhi ya Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri Songea. 

Waziri wa Madini ANgellah Kairuki akiteta jambo na AFisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma Abraham Nkya wakati wa ziara ya Waziri Kairuki kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Songea. Wa Pili Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mdema , Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi  Msaidizi Wizara ya Madini Gladness Mkambaita na wa kwanza kulia ni Meneja wa Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini, Andrew Eriyo. 

Tuesday, November 27, 2018

Biteko atembelea wachimbaji wadogo Mbogwe, Geita


Na Greyson Mwase,

Leo tarehe 26 Novemba, 2018 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amefanya ziara katika machimbo ya  dhahabu ya wachimbaji wadogo yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali  zinazowakabili wachimbaji wadogo. Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Augustino Masele, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Christopher Bahali, na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita, Christopher Kadeo.

Wengine ni pamoja na  Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick Mwanjisi, Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mbogwe pamoja na waandishi wa habari.

Mara baada ya kukamilisha ziara yake katika migodi ya kuchenjua dhahabu ya Isanja Badugu, na Magimi Gold Partners iliyopo katika eneo la Buluhe wilayani Mbogwe mkoani Geita, Naibu Waziri Biteko alielekeza migodi husika kuhakikisha inahifadhi nyaraka zote mgodini kama sheria ya madini inavyotaka.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika mgodi wa dhahabu wa Nyakafulu uliopo Wilayani Mbogwe Mkoani Geita unaomilikiwa na  kikundi cha Isanja Badugu na kufanya mkutano wa hadhara ulioshirikisha wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli  za uchimbaji madini katika eneo la mgodi huo na kutatua kero zao hapo hapo.

Mara baada ya kusikiliza na kutatua  kero mbalimbali zilizowasilishwa na wachimbaji wadogo hao, Naibu Waziri Biteko alitoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya  Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha inafanya uchunguzi dhidi wizi uliofanywa na  mmoja wa viongozi wa kikundi cha Isanja Badugu na kuchukua hatua za kisheria, wachimbaji wadogo kuhakikisha wanalipa kodi za madini Serikalini,  wamiliki wa machimbo kuhakikisha hawawanyanyasi wachimbaji wadogo na kufanya nao kazi kwa mikataba na wamiliki wa machimbo kuhakikisha hawatoi rushwa.

Kero zilizowasilishwa na wachimbaji wadogo hao awali ni pamoja na  baadhi ya wachimbaji wa madini kufanya kazi pasipokuwa na mikataba rasmi, ukosefu wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendeshea mitambo na baadhi ya wachimbaji wadogo kutokulipwa mara baada ya kusimamishwa kazi.


Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda (kushoto) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita, Christopher Kadeo (kulia) kabla ya kuanza kwa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye machimbo ya dhahabu ya wachimbaji wadogo yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita. Katikati ni Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick Mwanjisi. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akikagua nyaraka katika mgodi wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na kikundi cha Isanja Badugu, uliopo Wilayani Mbogwe mkoani Geita. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto mbele) pamoja na msafara wake akiendelea na ziara katika mgodi wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Magimi Gold Partners uliopo wilayani Mbogwe mkoani Geita. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akitoa maelekezo kwa mkurugenzi  wa mgodi wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Magimi Gold Partners, Juma Galehe (hayupo pichani). Wengine kutoka kulia ni  Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akimsikiliza mmoja wa wachimbaji wa madini ya dhahabu katika machimbo ya Nyakafulu yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akisalimiana na mmoja wa wachimbaji wadogo kwenye machimbo ya Nyakafulu yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na sehemu ya wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika machimbo ya Nyakafulu yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita.

Monday, November 26, 2018

Naibu Waziri Biteko atembelea Mgodi wa Buzwagi


Na Greyson Mwase

Leo tarehe 25 Novemba, 2018 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amefanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali  zinazoukabili mgodi huo. Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko aliambatana na  Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,  Anderson Msumba, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timothy Ndaya,  Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Mhandisi Abdulrahman Milandu, Afisa Mgodi Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Modest Tarimo, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick Mwanjisi,wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi wa habari.

 Mara baada ya  kufanya ziara na kupokea taarifa ya hatua za kufunga mgodi wa Buzwagi, Naibu Waziri Biteko alitoa  maagizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na:- mgodi kuwasilisha upya mpango wa ufungaji wa shughuli zake kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ili aweze kuwasilisha kwenye Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi  kwa ajili ya kuidhinishwa ili  utekelezaji wake uanze mara moja, pawepo na utaratibu wa kupitia upya kiwango cha fedha    zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa mazingira (rehabilitation bond) na kuweka mkakati wa kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi za wakazi wanaozunguka mgodi huo haziathiriki na ufungaji wa mgodi husika.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliutaka uongozi wa mgodi huo kufuata sheria na kanuni za ufungaji wa mgodi kwa wakati na kuepuka kufanya kazi kwa zimamoto.

Meneja Mkuu wa Migodi ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Buzunzu alisema kama mgodi wamepokea maelekezo na kuahidi kuwa watayafanyia kazi.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akimsikiliza Afisa Mgodi Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Modest Tarimo ( wa pili kulia) mara alipowasili kwenye ofisi yake iliyopo katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga. Kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Mhandisi Abdulrahman Milandu. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kulia mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga. 

Mtaalam kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi, Jonathan Joseph (kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto). 

Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga. 

Meneja Mkuu wa Migodi ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Buzunzu (kushoto) akielezea mikakati ya Mgodi wa Buzwagi kwenye ufungaji  wa shughuli zake kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia). 

Uchimbaji wa wazi wa dhahabu (open pit) ukiendelea katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.

Biteko atatua mgogoro sugu madini


  • ·        Ni baada ya kruhusu wananchi  kijiji cha Mhandu kuendelea na  uchimbaji dhahabu

Na Greyson Mwase, Shinyanga

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameruhusu wananchi  wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga kuendelea na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la utafiti wa madini hayo lililokuwa linamilikiwa na Menan Sanga kwa kushirikiana na kampuni ya  Lion Town.

Biteko aliyasema hayo leo tarehe 24 Novemba, 2018 katika mkutano wa hadhara ulioshirikisha wananchi  wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa  huo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za wachimbaji wa madini.

Katika ziara hiyo, Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Wataalam kutoka Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari.

Biteko alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini  haiwezi kuruhusu mwekezaji kumiliki eneo pasipo kuliendeleza, kutokulipa kodi inayohitajika Serikalini  huku wananchi wenye nia ya kuchimba katika eneo husika wakiendelea kuteseka.

Alisema kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli imeweka mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja marekebisho ya Sheria ya Madini inayotambua madini kama rasilimali za watanzania wote.

“Madini ni mali ya watanzania wote, na sisi kama Serikali tumejipanga katika kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kwa kiasi kikubwa katika umiliki wa rasilimali za madini, hivyo ninawaomba endeleeni kufanya kazi ya uchimbaji katika eneo hili wakati taratibu nyingine zikiwa zinaendelea,” alisema Biteko huku akishangiliwa na wananchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini waliopo katika eneo hilo pamoja na kuwapatia leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini ili wawe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta ya madini.

Pia alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga kuandaa orodha ya wachimbaji wote wa madini pamoja na taarifa za uzalishaji wa madini  yanayozalishwa na wachimbaji wa madini ikiwa  ni pamoja na kodi mbalimbali wanazolipa Serikalini.

Aliwataka wachimbaji wadogo hao kufuata sheria na kanuni za madini ikiwa ni pamoja na ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali zinazohitajika Serikalini na kusisitiza kuwa, Serikali haitasita kufuta leseni za madini pale watakapokiuka sheria na kanuni za madini.

Awali wakizungumza katika nyakati tofauti wananchi  wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga walisema kuwa awali eneo hilo lilikuwa likimilikwa kampuni ya Lion Town tangu mwaka 1989 kabla ya kukabidhiwa kwa Menan Sanga ambaye amekuwa  haendelezi uchimbaji katika eneo hilo  huku akiwafukuza wananchi ambao wamekuwa wakichimba madini ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji hao Innocent Deus alisema kuwa wachimbaji wadogo wa madini wanaochimba madini katika eneo hilo wamekuwa wakitishiwa maisha ikiwa ni pamoja na kupigwa mara kwa mara na walinzi waliowekwa na mmiliki wa eneo  hilo Menan Sanga.

Deus alisema awali kikundi kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo kijulikanacho kwa jina la BMS kiliundwa na kuomba leseni ya uchimbaji wa madini katika Wizara ya Madini kupitia ofisi yake iliyopo mkoani Shinyanga lakini walishangaa kuambiwa kuwa leseni husika imeshaombwa na kutolewa kwa Menan Manga.

Aliomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuwapatia sehemu ya eneo hilo kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini huku taratibu nyingine zikiendelea ikiwa ni pamoja na urasimishaji na utoaji wa leseni ili waweze kuchangia kwenye pato la Taifa.

Naye Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige mbali na kutoa pongezi kwa Naibu Waziri wa Madini kwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu aliiomba Wizara ya Madini  kuwapatia maeneo yenye  madini kwa ajili ya uchimbaji hususan katika eneo husika kwa kuwa madini ni tegemeo pekee kwenye uchumi wao.

Alisema kuwa, wananchi wengi wanaishi katika maisha magumu huku wakiwa na rasilimali za madini ya kutosha ambazo zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuwanufaisha na kuimarisha huduma nyingine za jamii kama vile miundombinu ya barabara, umeme na maji.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu ulioko katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani Shinyanga  lengo likiwa ni kuona shughuli za uchimbaji madini na kufuatilia  utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki tarehe 24 Aprili, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Biteko aliutaka mgodi huo kuhakikisha unamaliza mgogoro kati yake na wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa mchanga wa marudio ambao ni mali ya wananchi  wanaozunguka mgodi huo waliouacha wakati wakipisha shughuli za uchimbaji kwa mgodi huo kwa kufuata sheria na taratibu.

Aidha, aliutaka mgodi kuandika barua kwenda Tume ya Madini kwa ajili ya kuomba mwongozo  wa namna ya kutoa mchanga wa marudio na kuwakabidhi wananchi ambao ndio wamiliki wa awali wa mchanga huo wakati wakiendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo.

Aidha, Naibu Waziri Biteko  alikerwa na kitendo cha mgodi huo kutokulipa kodi ya mapato kwa takribani miaka 19 na kuendesha shughuli zake kwa kusuasua  kwa kisingizio cha kuwa mgodi umeamua kupunguza gharama za uendeshaji.

“Haiwezekani kama mgodi mnaamua kupunguza gharama za uzalishaji pasipo kushirikisha Serikali huku mkibadilisha umiliki wa leseni ya baruti wa kampuni nyingine na ni jambo ambalo halikubaliki kabisa,” alisisitiza Biteko.

Alielekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Sinyanga kuangalia iwapo kuna taratibu zimekiukwa ili taratibu za kisheria zichukuliwe.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga tarehe 24 Novemba, 2018 ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye mkoa huo yenye  lengo la kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini. 

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia mbele) akiendelea na ziara katika  eneo la uchimbaji wa chini ya ardhi kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani Shinyanga. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akipata maelezo jinsi  shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu  zinavyofanyika chini ya ardhi katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na msafara wake pamoja na watendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu kabla ya kushuka chini ya ardhi ili kujionea uchimbaji wa madini unavyofanyika. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara  katika Mgodi  wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Waziri Kairuki aahidi kusaidia uendelezaji madini ya nikel na chumvi Simiyu


Na Asteria Muhozya, Bariadi

Waziri wa Madini Angellah Kairuki  ametembelea Kituo cha Umahiri cha Bariadi ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kumhaidi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka kuwa, Wizara  ya Madini itaangalia namna ya kuusaidia mkoa huo katika uendelezaji wa madini ya Nikel na chumvi yanayopatikana mkoani humo.

Pia, Waziri Kairuki ametoa pongezi kwa Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo hicho  kwa kazi iliyofanyika na kumtaka mkandarasi huyo kuzingatia muda wa kukamilisha ujenzi na ubora wake.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuridhia kuondoa tozo 9 kati ya 16 zilizokuwa zikitozwa na Taasisi mbalimbali  za serikali  katika Sekta ya Madini.

Amesema uwepo wa kituo hicho mkoani humo, utawezesha wachimbaji wadogo  wa madini kuchimba kwa tija.

Pia, ametoa rai kwa wananchi walio tayari kuwekeza katika Sekta ya Madini kuwekeza mkoani humo pamoja na maeneo mengine nchini.

Vilevile, amewataka wale wenye leseni za madini kutoshikilia leseni hizo bila  kuziendeleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka, ameishukuru Wizara kwa kuuchagua mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa ambayo vituo hivyo vya umahiri vinajengwa.

Amesema  kuwa, uwepo wa kituo hicho utawezesha wachimbaji kupata mafunzo ya uchimbaji bora wenye tija  ikiwemo kupata mahali sahihi ambapo shughuli za uendelezaji Sekta ya Madini utafanyika.

Aidha, ameleeza pia, kituo hicho kitatumika kama sehemu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi ikiwemo  taarifa kuhusu bei elekezi ambazo wizara kupitia Tume ya Madini imekua ikitoa kila mwezi.

Vituo vya Umahiri vinajengwa na mkandarasi kampuni ya SUMAJKT maeneo mbalimbali nchini, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia.

 Vituo hivyo vya umahiri vinalenga kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.

Pia, vinalenga katka kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo bora za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.

Mbali na Bariadi, kituo kama hicho kinachojengwa Bukoba, Mara, Chunya, Handeni, Songea, na Chuo Cha Madini Dodoma.

Wakati huo huo, Waziri Kairuki jana alitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Handeni. Akiwa kituoni hapo, Waziri Kairuki alisema wizara inaendelea kuweka jitihada kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika pato la taifa  na hivyo kuwataka watumishi katika sekta husika kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa weledi na kuongeza kuwa,“ mjue kuwa kosa moja mtakalofanya katika sekta hii, linawakosesha watanzania wote manufaa.

Aliongeza kuwa, hatosita kumwondoa afisa yoyote atakayekwamisha  kazi ya serikali na watanzania na kueleza kuwa, bado analikumbushia suala hilo kwa kuwa ni wajibu wake na kusema kuwa, ni vema watumishi katika sekta ya madini kuongeza nguvu  katika utendaji kazi na kuhakikisha kuwamba wanatoa kipaumbele kwa rasilimali hiyo ya madini.

“ Mwaka huu tumewekewa malengo ya kukusanya shilingi bilioni  310, natamani tufike makusanyo ya shilingi bilioni 500. Nitawapima Maafisa Maadini kwa hayo. Sitasita kuchukua hatua kwa wanaolegalega,” alisisitiza Waziri Kairuki. 

Pia, alizungumzia kuhusu wamiliki wa leseni na kueleza kuwa, wote wanaomikili leseni hizo wanapaswa kuziendeleza badala ya kuzihodhi bila kuzifanyia kazi na kusema kuwa “ lengo letu ni kuhakikisha kwamba leseni zinachangia  katika upatikanaji wa mapato,” alisema Kairuki.

Aidha, alieleza kwamba, Serikali kupitia Wizara ya madini inaandaa Jukwaa la uwekezaji kati ya nchi ya China na Tanzania ambalo linatarajiwa kufanyika mwezi Disemba na hivyo kutoa wito kwa wadau wa sekta ya madini kuchangamkia fursa hiyo.

Pia, aliendelea kusisitiza kuhusu wadau wa sekta ya madini kufuata sheria na kuzingatia taratibu zilizopo wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, alisema kuwa, uwepo wa kituo hicho katika wilaya hiyo kutakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi wilyani humo na hivyo kutoa wito kwa wale wenye ni ya kufanya biashara ya madini wilayani humo kutosita kufanya hivyo.

Alisema Wilaya hiyo itasimamia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kutokana na manufaa yake kwa wilaya hiyo na kueleza kuwa, wilaya hiyo ni mzalishaji mkubwa wa madini ya viwandani hivyo uwepo wa kituo hicho kitahamasisha wawekezaji zaidi kuwekeza wilayani humo.

Mwisho alimtaka Mkandarasi SUMAJKT kuharakisha ujenzi huo kabla ya msimu wa mvua na kumwomba Waziri Kairuki kuhakikisha  kusaidia upatikanaji wa haraka wa fedha za ujenzi.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia matofali yanayotumika kujenga Kituo cha Umahiri cha Bariadi, alipokitembelea kituo hicho ili kukagua maendeleo ya ujenzi wake. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka. 

Sehemu ya jengo la Kituo cha Umahiri Bariadi katika hatua zake za ujenzi. 

Waziri wa Madini  Angellah Kairuki na Mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka wakimsikiliza Mkandarasi  SUMAJKT (hayupo) akieleza maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Umahiri cha Simiyu. Waziri Kairuki alitembelea kituoni hapo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo husika. 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo cha Umahiri cha Handeni akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho. Anayefuatilia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe , uongozi wa Mkoa, watalaam wa Ofisi ya Madini Handeni na Tanga na watalaam kutoka Wizara ya Madini. 

Mafundi wa SUMAJKT wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Handeni. 

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, akimtambulisha waziri wa Madini Angellah Kairuki kwa viongozi wa Wilaya alipofika wilayani humo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri kinachojengwa Handeni. 

Mafundi wa SUMAJKT wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Handeni.