Na Asteria Muhozya,
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amemsimamisha kazi Fundi Sanifu wa Madini,
Asheni Daudi wa Ofisi ya Madini Dodoma baada ya kuagizwa na Waziri wa Madini
Doto Biteko.
Hatua hiyo
ilifikiwa Januari 30, 2019, baada ya Waziri Biteko akiongozana na Katibu Mkuu
na Wataalam wengine wa wizara vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kufanya
ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Dhahabu cha Umoja kilichopo eneo la Viwanda la Kizota (Industrial
Area) na kubaini mapungufu makubwa katika utendaji kazi wa wataalamu hususan
uandaaji wa tarifa za uzalishaji wa madini.
Akizungumza
katika eneo hilo, Waziri Biteko alisema wizara ilipata taarifa kutoka kwa raia
wema kuhusu mienendo inayoendelea katika eneo hilo ambapo wahusika ambao ni Maafisa
Madini wamekuwa hawatoi taarifa halisi za uzito na ubora wa dhahabu
zinazozalishwa baada ya kuchenjuliwa, hivyo, serikali kukosa mapato stahiki.
Waziri Biteko aliongeza
kuwa, tayari anayo majina yote ya wanaofanya michezo ya ujanja ujanja kwenye
viwanda vya kuchenjua dhahabu, huku akieleza kuwa, hatua madhubuti zitachukuliwa
kwa wote wanaofanya vitendo hivyo na kuongeza kwamba, zoezi hilo litakuwa
endelevu kwa lengo la kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwataka
maafisa madini kuwa makini.
Aidha, alimwagiza
Kamishna wa Madini kufanya kaguzi katika viwanda vyote vya kuchenjua dhahabu
kwa lengo la kubaini utendaji wa kazi wa viwanda hivyo, ikiwemo taarifa za
uzalishaji zinazotolewa na kusema “Lazima tufike mahali tuheshimu taratibu, madini
haya ni mali ya nchi”, alisisitiza Biteko.
Wakati huo
huo, Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkoa wa Dodoma kujitathmini kutokana
na mambo yanavyokwenda katika eneo lake la kazi na kumtaka kuwasilisha kwa
Kamishna wa Madini na kwa Waziri wa Madini taarifa za uzalishaji madini ya dhahabu
kwa kipindi cha miezi sita.
Pia, katika
ziara yake, Waziri Biteko alibaini mnunuzi wa madini ya dhahabu katika eneo la Kizota
aliyefahamika kwa jina la Matondo Michembe ambaye anafanya shughuli hizo bila kuwa
na leseni ya biashara ya madini hayo. Hivyo, alimwagiza Michembe kuwasilisha
taarifa za utendaji wake kwa Kamishna wa Madini na Waziri wa Madini hususan soko analouzia madini hayo ya dhahabu.
Kwa upande
wake, Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila alieleza kuwa, kiutaratibu ilikuwa
lazima taarifa za uzalishaji na kiasi kilichozalishwa kujazwa katika vitabu
maalum ndani ya kiwanda hicho lakini jambo hilo halikufanyika kama
inavyotakiwa.
Aliongeza
kuwa, Afisa huyo amesimamishwa ili kupisha uchunguzi na endapo itabainika,
taratibu za kiutumishi zitachukuliwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati
alipotembelea kiwanda cha kuchenjua madini ya dhahabu cha Umoja eneo la Viwanda
la Kizota wakati wa ziara yake ya kushtukiza. Katikati kulia ni Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, wengine ni Watumishi wa kiwanda hicho
kushoto, Katikati mwenye suruali ya blue ni Afisa aliyesimamishwa kazi, Fundi
Sanifu Asheni Daudi, anayefuatia ni Afisa Madini wizara ya madini, Mhandisi
Assah Mwakilembe.
Waziri wa Madini Doto Biteko akitafakari jambo
wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika eneo ambalo shughuli za uuzaji wa madini zinafanyika bila kuwa na leseni.
Mbele ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila. Wengine ni
Maafisa wa Wizara.
Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati
akimhoji Munuzi wa Madini Matondo Michembe (wa pili kulia) ambaye alikutwa
akifanya shughuli hizo bila kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo. Wa kwanza
kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila.
No comments:
Post a Comment