Ø Aitaka Wizara ya Madini kutoa
Mwongozo wa Usafirishaji Madini Nje.
Ø Waziri Biteko asema, Rasimu ya Kwanza
imekamilika.
Ø Asisitiza Masoko yaanze mwezi
Februari.
Asteria Muhozya na
Samwel Mtuwa, Dodoma
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Madini kuharakisha
ukamilishaji wa Kanuni za Uanzishwaji Masoko ya Madini nchini, ikiwemo kuhakikisha
masoko hayo yaanza haraka.
Waziri Mkuu
Majaliwa ameyasema hayo Januari 26, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha
Mawaziri kutoka wizara mbalimbali, Wakuu wa Mikoa yote nchini, Wizara ya madini,
Makatibu Tawala wa Mikoa, Taasisi mbalimbali zikiwemo Tume ya Madini, Benki Kuu
ya Tanzania na Kituo cha Uwekezaji Nchini, (TIC).
Amesema kikao hicho
ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli aliyayotoa Januari 22 wakati akifungua Mkutano wa Kisekta
uliowashirikisha wachimbaji na wadau wa madini nchini ambapo Rais Magufuli
alisisitiza juu ya kuanzishwa kwa masoko ya madini.
Aidha, ameipongeza
Wizara ya Madini kwa kikao hicho na kusema kwamba, kimelenga katika kujenga
uelewa wa pamoja kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Maafisa Madini
wa Mikoa kuhusu kanuni na namna ya kuendesha Masoko hayo.
Akisisitiza kuhusu
usimamizi wa masoko ya madini, Waziri Mkuu amesema kuwa, Wakuu wa Mikoa kwa
kushirikiana na Maafisa Madini ndiyo watakuwa wasimamizi wakuu wa masoko hayo na kuongeza kuwa, katika ngazi ya Wilaya,
masoko hayo yatasimamiwa na wakuu wa wilaya na kueleza “kwenye wilaya msimamizi
ni mkuu wa wilaya, wakuu wa wilaya mkaripoti kwa wakuu wa mikoa wawasaidie,”.
Pia, ametaka pindi
kanuni hizo zitakapokamilika kuzifikisha kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na
Halmashauri za Wilaya na katika maeneo
yote yenye machimbo wakiwemo wachimbaji na Wafanyabiashara ikilenga kuwezesha
wadau hao kufikiwa na kanuni hizo na kuwa na uelewa wa kutosha na hatimaye
ziweze kusimamiwa kikamilifu kwa kushirikiana
na Tume ya Madini.
Katika kuhakikisha
kwamba masoko hayo yanaendeshwa kwa
usalama, ameitaka mikoa kuhakikisha kunakuwa na na hali ya ulinzi na usalama
kwenye maeneo hayo ili kuwahakikishia wafanyabiashara,
wachimbaji na wananchi kwa ujumla usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini
hayo katika masoko yatakayoanzishwa.
Akizungumzia
mwongozo wa usafirishaji madini nje ya nchi, ameitaka wizara
ya madini kutoa mwongozo huo mapema na kueleza kuwa, baada ya serikali
kutafakati kwa kina, imetoa mwongozo wa kusafirisha baadhi ya madini nje ya
nchi na hivyo kuitaka wizara kutoa mwongozo huo kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa, tayari
rasimu ya kwanza ya Kanuni hizo imekamilika na kueleza
kuwa, kikao kazi kinalenga jambo ambalo halikuwahi kufanyika tangu nchi ya
Tanzania ipate uhuru na hivyo kuwataka wakuu wa mikoa kulifanya kuwa jambo
linalowahusu wote.
Amesema
kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalum
wanayoweza kufanyia biashara ya madini hali ambayo inachangia kuwepo
utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Ameongeza,
ili kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati
iliyojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo
Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara,
Benki Kuu na Tume ya Madini.
Amesema
kuwa, Kamati hiyo iliundwa ili kuandaa rasimu ya Kanuni za kuanzisha na kusimamia
Masoko ya Madini Nchini na kuongeza kuwa katika kuandaa kanuni hizo, jina la
Kanuni linalondekezwa The Mining (Mineral and Gem House) Regulations,
2019," amesema Waziri Biteko.
Ameongeza kuwa,
Marekebisho ya sheria yaliyofanyika mwaka 2017 katika sheria ya Madini ya Mwaka
2010 yalilenga kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha sekta ya madini
inachangia ipasavyo katika kukuza na kuimarisha mchango wa sekta katika pato la
Taifa na kuongeza kwamba, si kweli kwamba marekebisho hayo yamefukuza
wawekezaji bali yameongeza idadi ya wanaotaka kuwekeza katika sekta ya madini.
Katika hatua
nyingine, Waziri Biteko amewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha masoko ya madini
yanaanza mara moja wakati kanuni hizo zinaendelea kuboreshwa na kusisitiza
wakuu hao wahakikishe yaanza ifikapo mwezi Februari mwaka huu.
“Lazima Wakuu wa
Mikoa tuanze. Wakuu wa Mikoa tutaanza na Kanuni hizi, hizi. Tutaendelea
kuziboresha lakini lazima tuanze. Na kanuni hizi zikipita, lazima kila
anayehusika atafanya biashara kupitia kanuni hizi,” amesisitiza Waziri Biteko.
Halikadhalika,
amewataka washiriki wa kikao hicho kuhakikisha wanazipitia kanuni hizo kwa
lengo la kufanya maboresho na kutoa mapendekezo yatakayowezesha kuwa na kanuni
zitakazowezesha taifa kunufaika na rasilimali hiyo na kuongeza, “ hizi kanuni
zikiwa mbovu itakuwa yetu wote,”.
Pia, amewaomba
Wakuu wa Mikoa, Maafisa Tawala wa Mikoa, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na
Wadau kwa ujumla kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kutimiza ndoto za muda
mrefu za Wachimbaji wadogo Wafanyabiashara wa Madini, Wadau na Watanzania wote
kwa ujumla za kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika taifa
na inalinufaisha.
Naye, Waziri , Ofisi
ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo amesema
kuwa, Waziri Biteko ameanza vizuri na
kueleza kuwa, kikao hicho
kitasaidia kupata mambo mbalimbali yatakayosaidia katika uanzishwaji wa masoko
hayo na kueleza kuwa, timu yake ya mikoa iko tayari.
“Mhe. Waziri
nimefurahi sana namna wakuu wa mikoa walivyozungumza wakati wa majadiliano ya
kuboresha Kanuni hizi. Tunakwenda kuona namna ya kuanzisha masoko haya,”.
Aidha, amewataka
wakuu wa mikoa kulichukulia jambo hilo kama matarajio ya Rais Magufuli
anavyotaka kuona kwamba madini yanalinufaisha taifa.
No comments:
Post a Comment