Tuesday, January 30, 2018

Serikali yasisitiza uwazi shughuli za madini

Na Mohamed Saif,

Kampuni za Madini nchini zimetakiwa kufanya shughuli zake kwa uwazi sambamba na kufuata Sheria za nchi ili kuepuka migongano.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Januari 29, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kwenye mkutano na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles aliyeambatana na Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson.

Ujumbe huo ulimtembelea Katibu Mkuu Msanjila kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali kwenye Sekta ya Madini ikiwemo suala la Sheria ya Madini, masuala ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) yanayofanywa na kampuni mbalimbali zikiwemo za kutoka nchini Canada na matarajio ya Serikali kwa kampuni (wawekezaji).

Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazofanya shughuli zake nchini zinalazimika kufuata taratibu na sheria za nchi ili kujijengea mazingira rafiki ya utekelezaji wa shughuli husika.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa kwa ujumla sambamba na wawekezaji na alibainisha kwamba lengo hilo litafikiwa ikiwa kampuni husika zitatekeleza wajibu wake kwa uwazi kulingana na matakwa ya sheria.

“Kampuni zinazojihusisha na shuguli za madini zinapaswa kufanya shughuli zake kwa usahihi na uwazi,” alisisitiza Profesa Msanjila.

Aidha, Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za madini nchini, zinapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwa Wataalam waliopo Serikalini ili kupata mwelekeo sahihi wa dhamira ya Serikali.

“Kampuni zinatakiwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo sahihi ili kufanya shughuli zake kwa usahihi,” alisisitiza Profesa Msanjila.

Profesa Msanjila vilevile alizungumzia dhamira ya Serikali ya kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa nje ili kukuza uchumi wa Taifa.

“Madini yakiongezwa thamani hapa nchini, faida ni nyingi ikiwemo ajira na pia mapato yataongezeka kwani tutakuwa tumeelewa thamani halisi ya madini husika, kabla hayajasafirishwa,” alisema.

Ili kufikia dhamira hiyo, Profesa Msanjila alisema Serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni zilizoonyesha nia ya kujenga viwanda vya kuyeyusha na kusafisha madini (smelting and refining).

Mbali na hilo, Profesa Msanjila alizungumzia suala la uwezeshaji wachimbaji wadogo wa madini ambapo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba wananufaika ipasavyo na shughuli zao sambamba na mchango wao kwenye pato la Taifa kuonekana.

Alielezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuwawezesha wachimbaji wadogo ikiwemo uanzishaji wa vituo vya mafunzo vya mfano (centre of excellence) ambavyo alivitaja baadhi yake kuwa ni Kituo cha Tanga, Geita na Mtwara.

Kwa upande wake Balozi Myles alisema ni muhimu Serikali, Wawekezaji na Jamii kwa ujumla kushirikiana na pia kuwa na lengo la wazi la namna ya kunufaika kutokana na Sekta ya Madini.

Naye Davidson aliahidi kuzungumza na kampuni za Canada kuelezea matarajio ya Serikali kwao kwa namna mbalimbali ikiwemo suala la sheria, uwajibikaji kwa jamii, mazingira na michango mbalimbali ya kampuni kwa maendeleo ya jamii.

“Nitawakumbusha kwamba wanawajibika si kwa wanahisa wao peke yake bali pia kwa jamii wanapofanyia shughuli zao,” alisema Davidson.

Mkutano wa Katibu Mkuu wa Madini na Balozi wa Canada nchini ulihudhuriwa na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini akiwemo Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (wa pili kulia) mara baada ya kumalizika kwa mkutano na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Ian Myles (katikati). Kulia ni Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya. Kutoka kushoto ni Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson na Kamishna wa Biashara Ubalozi wa Canada nchini, Anita Kundy.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (katikati) akizungumza jambo wakati wa mkutano na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles (kulia) na Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson (kushoto).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (kulia) akimsikiliza Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson (katikati). Kushoto ni Balozi wa Canada nchini, Ian Myles (kulia).
Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano wa Katibu Mkuu Madini na Balozi wa Canada (hawapo pichani). Kushoto ni Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya na kulia ni Kamishna wa Biashara Ubalozi wa Canada nchini, Anita Kundy. Wengine ni Maafisa kutoa Wizara ya Madini.

Monday, January 22, 2018

Kiwanda cha Dangote chaagizwa kuwalipa kwa wakati wachimbaji wa jasi

Na Asteria Muhozya,

Kampuni ya Saruji ya Dangote imetakiwa kuwalipa kwa wakati Wachimbaji wa Madini ya Jasi ili kuwawezesha kulipa kodi zao kwa Serikali kulingana na taratibu zilizopo.

Hayo yamesemwa tarehe 19/01/2018 na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alipotembelea kiwandani hapo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Naibu Waziri amesema kuwa, lazima Wachimbaji Wadogo wapate malipo yao kwa wakati baada ya kuuza madini ili kuwawezesha kulipa kodi za Serikali pamoja na kurejesha mikopo yao kwa wakati katika Benki walizokopa.

Pia, Naibu Waziri Biteko ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuandaa rasimu ya Mkataba ndani ya kipindi cha wiki mbili na kueleza kuwa, kuwepo kwa mkataba huo ambao kutawawezesha Wachimbaji wadogo wa madini ya Jasi kutatua changamoto zilizopo baina yao na Kiwanda husika.

“Andaeni rasimu ya mkataba ili kila moja auze madini yake kwa bei inayoeleweka bila kuoneana na kila moja apate faida anayostahili,” amesema Biteko.

Ameongeza kuwa zipo changamoto za Wachimbaji wadogo kutokuwa na umoja na hivyo kuwataka kuwa na umoja ili waweze kufanikiwa katika shughuli zao ikiwemo kuwepo na bei moja ya madini yao.

Aidha, Naibu Waziri Biteko amewataka wananchi na Wachimbaji wadogo kuacha tabia ya wizi ambayo imelalamikiwa na uongozi wa Kiwanda hicho. 

Kwa upande wake, Mkurugezi Mtendaji wa Mitambo ya uzalishaji wa katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Hemendra Raithatha amesema kuwa kulikuwepo na tatizo la malipo isipokuwa hivi sasa tatizo limeshughulikiwa,  na kuahidi  kuwa wachimbaji wa madini watalipwa kwa wakati.

Pia, Raithatha ameongeza kuwa, kiwanda hicho kipo tayari kufanya kazi na Wachimbaji wa Jasi kwa kuwa mali ghafi nyingi za kutengeneza Saruji zinatoka kwa wachimbaji hao jambo ambalo linaimarisha mahusiano kati ya pande husika.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa Mahusiano mazuri kati yake na Kiwanda hicho na pia amemshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea kiwanda hicho. 

 Mbali na Naibu Waziri, ziara hiyo imehudhuriwa pia na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mayigi Makolobela, Watumishi wa Wizara ya  Madini, Uongozi wa Halmashauri ya Mtwara, Uongozi wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi na Kamati ya Ulinzi na Usalama.


Naibu Waziri amefanya ziara yake ya siku tatu katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo ililenga kukutana na wadau wa sekta hiyo na kukagua shughuli zinazofanyika ikiwemo kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto) akisaini kitabu cha wageni katika ukumbi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote wakati alipofanya ziara yake kiwandani hao.  Wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mayigi Makolobela.  Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mitambo ya Uzalishaji Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Hemendra Raithatha.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (mbele) akiongoza kikao baina yake na Uongozi na Wafanyakazi  wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Wafanyakazi wa Wizara ya Madini, pamoja na Uongozi wa Wachimbaji wa Madini ya Jasi.

Eneo la uzalishaji Kitalu Na. 1   katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.
Na Rhoda James, Lindi

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka Wachimbaji wa Madini ya Jasi kuungana ili kuweza kuandaa Kanuni ndogo ndogo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto katika utekelezaji wa shughuli zao ikiwemo ya Bei ya Madini ya Jasi.

Aliyasema hayo tarehe 17 Januari, 2018, wakati alipowatembelea   Wachimbaji Wadogo katika ziara ambayo inalenga kutatua migogoro iliyopo katika sekta husika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Naibu Waziri alisema kuwa bei ya madini ya Jasi imekuwa ikitofautiana kutokana na kukosekana kwa umoja baina ya wachimbaji wa madini hayo.
“ Jiungeni pamoja mpange bei ya kuuza Jasi kwa pamoja na mkiwa kitu kimoja changamoto hizi hazitakuwepo,” amesisitiza Biteko.

Pia, Naibu Waziri alisema kuwa, ameelezwa kuwa ipo changamoto ya miundombinu ya barabara na hivyo kuitaka Halmashauri ya Kilwa kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo   kwa kuwa  itatumka kwa  shughuli mbalimbali.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mayigi   Makolobela alisema kuwa Jasi inayochimbwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara ina ubora wa asilimia 89-95 na iko juu ukilinganisha na Jasi inayopatikana nchi  jirani.

Vilevile, Makolobela ameeleza kuwa kiwango cha Jasi kilichochimbwa katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Desemba, 2017 kilikuwa Tani 44,500 na gharama yake ilikuwa Shilingi bilioni 4.6.

Aliongeza kuwa, katika kiasi hicho cha Jasi kilichopatikana Serikali imekusanya Mrabaha wa shilingi milioni 138 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2017.

Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Jasi Mkoa wa Lindi, Peter Ludvick alimweleza Naibu Waziri kuwa ikiwa Serikali itawasaidia  suala la miundombinu hususan barabara wachimbaji watazalisha mara tatu ya kiwango wanachokizalisha hivi sasa.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi, Peter Ludvick (wa tatu kushoto). Naibu Waziri amemweleza  mwenyekiti huyo kuhusu umuhimu wa kuandaa Kanuni ndogo ndogo ambazo zitawasaidia wachimbaji wa madini hayo kukabiliana na changamoto ya Bei ya Madini ya Jasi.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika kijiji cha Hotel Tatu katika eneo ambalo Madini ya Jasi yanahifadhiwa kwa muda tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwenye viwanda mbalimbali nchini. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Kanda ya Kusini, Mayigi Makolobela (wa pili kushoto), wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai na Wengine katika picha Watumishi wa Madini pamoja na wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo.

Biteko aitaka STAMICO kujitathmini

Na Rhoda James, DSM

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amelitaka Shirika la Madini la Taifa  (STAMICO) kujitathmini ili kujua kama linatakiwa kuendelea kuwepo.

Naibu Waziri wa Madini, Biteko ameyasema hayo tarehe 16 Januari, 2018, wakati wa ziara yake Makao Makuu ya STAMICO ambayo ililenga kufahamiana na Bodi, Menejimenti pamoja na Watumishi wa shirika hilo.

Biteko amesema Serikali ililenga kulitumia shirika hilo ili kuhakikisha kuwa linasimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya madini nchini ukiwemo Mgodi wa Buckreef. “Mnazungumzia mradi wa Buckreef mmefanya nini kuhusu mradi huu? amehoji Biteko.

Vilevile, Biteko katika kikao hicho ameitaka STAMICO kuhakikisha inadhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite nchini kwa kuhakikisha kuwa inaweka mikakati madhubuti ya kudhibiti utoroshaji huo.

“STAMICO ni mbia katika Kampuni ya TanzaniateOne ni lazima muweke mikakati ya namna gani ya kudhibiti utoroshwaji wa madini haya,” amesema Biteko.
Aidha, amewataka watumishi wa STAMICO kufikiria namna ambayo itawezesha shirika husika kuchangia katika Pato la Taifa kwa kuwa mchango wa Sekta ya Madini bado ni kidogo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji anaye Kaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Alex Rutagwelela akitoa taarifa ya shirika hilo amesema kuwa lengo kuu la STAMICO ni kuhakikisha kuwa inarudi kama ilivyokuwa hapo awali.

Rutagwelela amemweleza Naibu Waziri kuwa, Shirika linafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali, kutoa ushauri kwa wachimbaji wadogo pamoja na biashara ya kukodisha mitambo ya Uchorongaji.

Ameongeza kuwa, STAMICO inaendelea na uchimbaji wa Makaa ya Mawe katika eneo la Kiwira – Kabulo, Kukarabati maabara ya Makaa ya Mawe ya Kiwira ambayo itatumika kupima ubora wa makaa hayo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda amemweleza Naibu Waziri Biteko kuwa, watayafanyia kazi maagizo yote na kumshukuru kwa kutembelea shirika hilo katika ziara ambayo imelenga kuboresha utendaji, kuongeza ubunifu ili  shirika hilo liweze kuchangia zaidi katika pato la Taifa.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kulia) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika Makao Makuu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na Bodi, Uongozi na Watumishi wa shirika hilo. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Balozi Elexander Muganda, Kamishna wa Madini, Profesa Shukrani Manya ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji, Alex Rutagwelela.
Kamishna wa Madini, Profesa Shukrani Manya ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini akifafanua jambo katika kikao hicho.
  Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akisikiliza mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa utafiti na Uchorongaji, Alex Rutagwelela wakati wa kikao hicho. Wengine ni Uongozi na Watumishi wa Shirika la STAMICO.

Naibu Waziri Biteko atoa changamoto Chuo cha Madini

Na Veronica Simba, Dodoma

Naibu Waziri mpya wa Madini Dotto Biteko ametembelea Chuo cha Madini (MRI) na kutoa changamoto kadhaa kwa Menejimenti na wafanyakazi wote, ili kiwe na tija stahiki kwa Taifa.

Akizungumza baada ya kutembelea sehemu mbalimbali za Chuo hicho kilichopo Dodoma, Januari 15 mwaka huu, Naibu Waziri alieleza kutokuridhishwa kwake na utekelezaji hafifu wa masuala kadhaa muhimu na hivyo kutoa changamoto kwa uongozi wa Chuo kuyafanyia kazi mapema.

Moja ya mambo muhimu aliyoelekeza yatekelezwe ni pamoja na matumizi mazuri ya rasilimali za Serikali kwa manufaa ya Taifa. Aliwataka kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais John Magufuli anayetaka rasilimali kidogo inayopatikana nchini itumike vizuri na kuleta matokeo.

“Mathalani, viko vifaa vya mamilioni ya shilingi katika baadhi ya maabara zenu na havijawahi kufanya kazi kwa muda wa miezi Sita sasa. Vinachakaa na kuharibika tu. Akija aliyetufadhili kununua vile vifaa, atatushangaa. Tutaonekana wote hatuna uwezo wa kufikiri kumbe ni watu wachache tu wanaosababisha,”alisema.
Kufuatia suala hilo, Naibu Waziri aliagiza maabara zote zenye vifaa ambavyo havifanyi kazi zirekebishwe na zianze kufanya kazi kufikia mwisho wa mwezi huu wa kwanza.

Changamoto nyingine aliyoitoa Naibu Waziri ni kwa Chuo kufanya tafiti ili kuisaidia Serikali kujua mahitaji halisi ya rasilimali watu kwenye sekta ya madini.
“Ninyi ni tofauti kabisa na taasisi nyingine zinazofanya biashara. Mkifanya vizuri, maafisa wetu wa madini kule mikoani na kwingineko kwenye kanda watafanya kazi rahisi sana. Kwa sababu ninyi mtakuwa mmeshafanya utafiti kwa niaba ya Wizara kugundua mahitaji ya rasilimali watu kwenye sekta ya madini.”

Akifafanua zaidi, alisema kwamba Wizara inategemea kupata chemchemi ya fikra kutoka kwenye taasisi hiyo ya Chuo. Alisema, Chuo kinatarajiwa kuzalisha wataalam wazuri ambao watakwenda kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenda kufundisha wachimbaji wadogowadogo namna nzuri ya kuchenjua madini kwa kuzingatia usalama wa mazingira na kupata tija ili kupandisha hadhi ya mavuno ya rasilimali wanayopata.

Aidha, aliongeza kuwa haipendezi kuona Chuo kikifundisha vijana wengi wa kitanzania lakini kwenye migodi kunakuwa na wafanyakazi wa kigeni wakifanya kazi ambazo watanzania wanaweza kufanya.

“Changamoto kwenu kama Chuo, je, vijana wetu mnawanoa kiasi cha kutosha kushindana katika soko la ajira? Ninyi ni taasisi ya kitaaluma, mnatakiwa kuyaona mambo ya kesho leo. Na mambo ya jana yawasaidie kuboresha kesho ya nchi hii.”

Vilevile, aliwataka kuachana na utamaduni wa kulalamika kwa masuala mbalimbali badala yake wahakikishe wanatimiza wajibu wao ipasavyo na matokeo ya kazi yao yaonekane. Alisema, matokeo mazuri ya kazi ndiyo yatakayoihamasisha Serikali kuona umuhimu wa kuboresha yale wanayoyalalamikia ikiwemo suala la maslahi.


Hii ni ziara ya kwanza ya Naibu Waziri Biteko katika Chuo cha Madini tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo na kuapishwa na Rais John Magufuli Januari 8 mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Chuo cha Madini (MRI) kilichopo Dodoma, alipowatembelea hivi karibuni. 
Sehemu ya wafanyakazi wa Chuo cha Madini (MRI) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati alipowatembelea hivi karibuni kujitambulisha kwao na kujionea utendaji kazi wa Chuo hicho. 


Mkutubi Msaidizi wa Chuo cha Madini (MRI), Rachel Lugoye (kulia) akimweleza Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko na Ujumbe wake (kulia) utendaji kazi wa Maabara katika Chuo hicho, wakati wa ziara ya Naibu Waziri Januari 15 mwaka huu.

Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko akikagua sehemu mbalimbali za Chuo cha Madini (MRI), alipofanya ziara ya siku moja kujitambulisha na kujionea utendaji kazi wa Chuo hicho, Januari 15 mwaka huu.

Naibu Waziri Biteko atamani madini yachangie zaidi pato la Taifa

Na Veronica Simba, Dodoma

Naibu Waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko ameeleza kuwa anatamani kuiona sekta ya madini ikichangia zaidi ya ilivyo sasa katika Pato la Taifa.

Ameyasema hayo mapema leo, Januari 15 mjini Dodoma, alipowasili rasmi katika Ofisi yake ya Makao Makuu na kupokelewa na viongozi mbalimbali pamoja na watumishi wa Wizara ya Madini na wa Wizara ya Nishati.

Amesema kuwa, sekta ya madini inaweza kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa kutoka asilimia Nne ya sasa na kuweza kufikia asilimia 10 au zaidi ikiwa kutakuwa na ushirikiano baina ya wafanyakazi wote na viongozi wa Wizara huku kila mmoja akijituma kutimiza wajibu wake ipasavyo.

“Tujiulize hivi ni kwanini hadi leo sekta hii inachangia asilimia Nne tu katika Pato la Taifa badala ya kupanda hadi asilimia 10 au zaidi. Tubainishe ni madini yapi yanayotupatia fedha nyingi zaidi na ni mbinu gani tutumie ili tuweze kupanda zaidi,” amesisitiza.

Hata hivyo, Naibu Waziri Biteko alibainisha kuwa ujio wake wizarani haulengi kubadili au kugeuza mambo bali ni kuongeza nguvu zaidi kwa watangulizi wake katika kutekeleza yale ambayo yameagizwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli kwa niaba ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Tuombeane kwa Mungu atupe kibali, hekima na uwezo wa kuyaona matatizo lakini zaidi sana atupe uwezo wa kutekeleza majukumu yetu ili sekta hii ya madini iwe sekta ambayo ina mchango mkubwa kwa Taifa letu.”

Aidha, amesema kuwa falsafa yake ya utendaji kazi ni kwa kila mmoja kuheshimu nafasi ya mwenzake bila kujali nafasi aliyonayo. “Binafsi ninaamini hakuna mkubwa kwenye kufanya kazi. Ukubwa wako unaonekana kwenye matokeo ya kazi unayofanya. Kwa hiyo tushirikiane wote. Mimi ninaamini katika nguvu ya ushirikiano,” amesisitiza.

Viongozi mbalimbali waliompokea Naibu Waziri Biteko akiwemo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Madini Profesa Simon Msanjila, wamemwahidi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wote wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga amempongeza Naibu Waziri kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na kueleza kwamba wafanyakazi wanayo imani kubwa kuwa atasimamia vema utekelezaji wa majukumu katika sekta husika.

“Hii ni kwa sababu tunaamini unaifahamu vema sekta ya madini kutokana na kuwa umekuwepo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa muda mrefu na umeweza kuisimamia vizuri.”

Wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati wana uhusiano wa karibu kikazi kutokana na kufanya kazi kwa pamoja kwa muda mrefu katika iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini kabla ya kutenganishwa na kuwa Wizara mbili tofauti. Hii ndiyo sababu wangali wanashirikiana katika mambo mbalimbali kama hafla hii ya kumpokea Naibu Waziri.


Naibu Waziri Biteko aliteuliwa katika nafasi hiyo Januari 6 mwaka huu na kuapishwa tarehe 8 Januari na Rais John Magufuli.

Naibu Waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko akisalimiana na watumishi mbalimbali wa Wizara ya Madini, Wizara ya Nishati na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), alipowasili Makao Makuu ya Wizara, Dodoma mapema leo Januari 15, 2018.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akifurahia jambo na Naibu Waziri mpya wa Madini Dotto Biteko (kushoto kwa Waziri) alipofika ofisini kwake kumsalimu mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Wizara Dodoma. Wengine pichani ni viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (kushoto) akizungumza, wakati wa hafla fupi ya kumpokea Naibu Waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko (katikati) Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Januari 15 mwaka huu. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo.

Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati, wakimsikiliza Naibu Waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma Januari 15 mwaka huu.

Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati, wakimsikiliza Naibu Waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma Januari 15 mwaka huu.

Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati, wakimsikiliza Naibu Waziri mpya wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma Januari 15 mwaka huu.

Mgodi wa Buhemba wafunguliwa rasmi

Na Mohamed Saif,

Hatimaye Serikali imefungua Migodi ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo iliyopo katika eneo la Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara baada ya kujiridhisha hali ya usalama katika migodi hiyo.

Migodi hiyo imefunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Januari 13, 2018 na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi.

Akizungumza katika tukio hilo, Nyongo alisema jumla ya migodi 10 imefunguliwa kati ya 16 baada ya kujiridhisha usalama wake.

Alifafanua kwamba eneo la Buhemba lina jumla ya Migodi ya Dhahabu 16 ambayo inamilikiwa na Wachimbaji Wadogo hata hivyo iliyokidhi vigezo vya kiusalama ni Migodi 10 pekee ambayo imeruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Alisema Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea vifo vya Wachimbaji Saba na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.

Alibainisha kuwa Mwezi Desemba mwaka jana alifanya ziara kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao ambapo aliagiza shughuli za ukaguzi zikamilike ifikapo Mwezi huu wa Januari ili migodi ifunguliwe.

"Kama mtakumbuka nilifanya ziara hapa na niliagiza kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba uwe umekamilika ili shughuli za uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe; tumejiridhisha mashimo kumi ni salama na sasa tunafungua rasmi," alisema Naibu Waziri Nyongo.

Alisema shughuli hiyo ya Ukaguzi kama alivyokua ameagiza ilifanyika kwa umakini na kwamba maduara Kumi (Migodi Kumi) yameruhusiwa na mengine Sita hayatoruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.

Aliongeza kuwa baada ya kufika kwenye eneo hilo kwa mara ya kwanza alisikitishwa kuona wananchi wengi wakiwa wamekosa shughuli za kufanya kutokana na migodi hiyo kufungwa na ndiyo sababu ya kuagiza ukaguzi wake ukamilike haraka.

“Nilivyotembelea hapa Mwezi Desemba mwaka jana nilisikitishwa kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea ajali,” alisema.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwaagiza Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya migodi ili kukagua hali ya usalama pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji salama kwa wachimbaji hususan wadogo lengo likiwa ni kuepusha ajali.

“Ninawaagiza kwa mara nyingine Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili kuepusha ajali,” aliagiza Naibu Waziri.

Naibu Waziri Nyongo vilevile aliwaagiza wachimbaji madini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji ili kuepusha ajali migodini na wakati huohuo kunufaika ipasavyo na shughuli zao bila kupata usumbufu.

Aidha, Naibu Waziri alizungumzia ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali ambapo aliwaagiza wachimbaji hao kuhakikisha wanalipa kwa mujibu wa sheria na alionya kwamba mgodi utakaoshindwa kulipa inavyostahili, utafungiwa.

"Tumewafungulieni migodi yenu tukiamini kwamba nanyi mtatimiza wajibu wenu wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria. Mkishindwa kulipa, hatutosita kuifungia," alibainisha Nyongo.


Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Mara kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa migodi na kuzungumza na wachimbaji wadogo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akizungumza wakati wa ufunguzi wa migodi ya wachimbaji wadogo ya Buhemba, Mkoani Mara.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akifungua rasmi migodi ya Buhemba ya wachimbaji wadogo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akishuhudia tukio hilo.

Serikali yaitaka Stamigold ijiendeshe kibiashara

Ø  Katibu Mkuu Madini atoa siku 14 kwa uongozi kuwasilisha mpango mkakati

Na Veronica Simba, Biharamulo

Serikali imetoa siku 14 kwa kampuni ya Stamigold, inayomiliki Mgodi wa Dhahabu uliopo Biharamulo mkoani Kagera, kuandaa mpango mkakati wa kibiashara, utakaobainisha namna itakavyojiendesha pasipo kuitegemea Serikali.
Agizo hilo lilitolewa jana, Januari 6, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alipotembelea Mgodi huo na kuzungumza na Menejimenti pamoja na wafanyakazi wake.

Profesa Msanjila alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, ni kuona Kampuni tanzu hiyo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), inajiendesha kibiashara na kiushindani ili ipate faida stahiki na kulinufaisha Taifa kama ilivyo dhamira ya kuanzishwa kwake, na siyo vinginevyo.

“Menejimenti ya Kampuni, Bodi pamoja na Menejimenti ya STAMICO, nawapa hadi tarehe 21 mwezi huu, kila upande uwe umewasilisha mapendekezo ya kimkakati yanayobainisha namna gani Stamigold itaweza kusimama yenyewe na kujiendesha kiushindani kama zilivyo kampuni nyingine za kibiashara. Kwa upande wetu, Kamishna wa Madini na mimi Katibu Mkuu pia tutakuja na mapendekezo yetu.”

Akifafanua zaidi, Katibu Mkuu alisema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kampuni ya Stamigold hivyo haitakubali kuona mgodi huo unaendeshwa kwa hasara. “Kila mtu awajibike kwenye eneo lake,” alisisitiza.

Alisema, pamoja na kuwa Stamigold ni kampuni ya Serikali lakini imesajiliwa na Taasisi inayotoa leseni za biashara ya Brela, hivyo inapaswa kujiendesha kama kampuni nyingine za kibiashara. “Kampuni ya serikali ambayo haifanyi biashara haiendi kujiandikisha Brela. Ninyi mnafanya biashara hivyo lazima mfanye kazi kibiashara.”

Aidha, Profesa Msanjila aliutaka uongozi wa kampuni kuhakikisha unaweka wazi taarifa zote za mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote ili waelewe wanazalisha kiasi gani, wanapata faida kiasi gani, matumizi ni kiasi gani na kama kuna hasara ibainishwe wazi.

Alifafanua kuwa utaratibu wa kuweka wazi mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote utaondoa manung’uniko kwani utaratibu wa kibiashara unamtaka mwajiri amlipe mfanyakazi kulingana na mapato. “Huwezi kumlipa mtu mshahara hata pale ambapo hazalishi. Hii siyo sawa kibiashara maana lazima utapata hasara. Huu ndiyo ukweli ndugu zangu. Tubadilike. Hakuna hela ya kuchezea.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Mhandisi John Nayopa alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa ndani ya muda alioelekeza. Aidha, aliwataka wafanyakazi wa Stamigold kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni na ushauri wao wakati wa kuandaa mpango mkakati huo utakaoiwezesha Kampuni kujiendesha kibiashara.


Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu aliambatana na viongozi wengine wa Wizara akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu, Miriam Mbaga, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahaya Samamba, Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kagera, Paschal Bundala na Mhandisi Migodi kutoka wizarani, Kungulu Kasongi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na msafara wake wakitembelea kukagua sehemu mbalimbali za Mgodi wa Dhahabu Stamigold unaomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera, alipokuwa katika ziara ya kazi Januari 6, 2018.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na msafara wake wakitembelea kukagua sehemu mbalimbali za Mgodi wa Dhahabu Stamigold unaomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera, alipokuwa katika ziara ya kazi Januari 6, 2018.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na msafara wake wakitembelea kukagua sehemu mbalimbali za Mgodi wa Dhahabu Stamigold unaomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera, alipokuwa katika ziara ya kazi Januari 6, 2018.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Stamigold, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake hivi karibuni.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Stamigold, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake hivi karibuni.

Wafanyakazi mbalimbali wa Kampuni ya Stamigold wakitoa maoni yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (hayupo pichani) alipowatembelea hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kampuni ya Stamigold alipowatembelea hivi karibuni.