Thursday, May 31, 2018

Spika Ndugai afungua maonesho ya madini Bungeni Dodoma


Na Veronica Simba, Dodoma

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, leo Mei 30, amefungua rasmi maonesho ya madini katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma na kuipongeza Wizara ya Madini kwa kuyaandaa.

Akitoa hotuba ya ufunguzi, Ndugai alimpongeza Waziri mwenye dhamana, Angellah Kairuki pamoja na watendaji wa Wizara, kwa juhudi kubwa za kutangaza na kulinda rasilimali ya madini hapa nchini. Alisisitiza kuwa, anatumaini juhudi hizo zitaendelezwa ili kuiwezesha sekta husika kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu.

Alisema kwamba Wizara ya Madini inalo jukumu kubwa la kuufahamisha umma kuhusu sekta husika kupitia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari na maonesho mbalimbali.

“Maonesho haya yamekuja wakati muafaka kwa sababu kipindi hiki nchi yetu iko katika mageuzi makubwa katika sekta ya madini; na ninyi wizara mnawajibika kuifanikisha azma hii kwa njia mbalimbali, hususan vyombo vya habari na maonesho kama haya.”

Aidha, Spika aliwataka wadau mbalimbali wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na usalama wa wafanyakazi wao na kulipa kodi za Serikali.

Kuhusu suala la uongezaji thamani madini kabla ya kuyauza, Ndugai alisema kwamba hilo ni suala muhimu sana kwa kuzingatia sera ya nchi ya kuwezesha uchumi wa viwanda. “Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tutajenga viwanda ambavyo vitatoa fursa ya ajira kwa watanzania na kuinua uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza.

Akizungumzia mchango wa Bunge katika kukuza sekta ya madini, alisema Bunge limekuwa makini katika kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta husika unakuwa wenye tija na manufaa kwa pande zote; yaani Serikali, Taifa na wawekezaji.

“Tuliunda Kamati mbalimbali za ufuatiliaji wa sekta ya madini. Nafurahi kuwaambia kwamba mambo yamekuwa yakiboreka siku hadi siku. Nawasihi tuendelee hivyohivyo kwa manufaa ya pande zote.”

Awali, akimkaribisha Spika kufungua maonesho husika; Waziri Kairuki alisema kuwa, Wizara imeandaa maonesho hayo kwa kuzingatia kuwa ni Wizara mpya hivyo inahitaji kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake; yakijumuisha dhima na dira.

“Baada ya Bunge lako tukufu kuifanyia marekebisho Sheria ya Madini Namba 14 ya Mwaka 2010, kupitia marekebisho ya Sheria Namba 7 ya Mwaka 2017, Wizara yangu imekuwa na jukumu kubwa la kutekeleza maelekezo ya Sheria hiyo.”

Maonesho hayo ya siku tatu, yaliyoanza Mei 30 na kutarajiwa kuhitimishwa Juni Mosi; yameshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali, Shirikisho la Wachimbaji Wakubwa (TCME) na Kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji na uongezaji thamani madini.


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akitoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa maonesho ya madini katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Wengine pichani (kutoka kulia), ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila.


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (katikati), akiangalia aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini, alipotembelea Banda la Chuo cha Madini (MRI) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu.


Mjasiriamali anayejishughulisha na uongezaji thamani madini kwa kutengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali za urembo, Susie Kennedy (mwenye blauzi nyeupe), akimwonesha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, moja ya bidhaa anazotengeneza kutokana na madini; wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Kushoto ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akiangali bidhaa zinazozalishwa na Kampuni ya Tancoal, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Pamoja naye pichani ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof Simon Msanjila na Kamishna wa Madini Prof Shukrani Manya.

Thursday, May 24, 2018

Biteko aagiza Afisa Madini Mkazi Mererani aondolewe


Ø Ni kwa usimamizi dhaifu wa UKUTA

Na Veronica Simba, Manyara

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amemwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma kumwondoa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mererani, Fredrick Girenga kwenye wadhifa huo na kumweka Afisa mwingine atakayemudu vema usimamizi wa Ukuta wa Mererani unaozunguka machimbo ya Tanzanite.

Biteko alitoa agizo hilo jana, Mei 23, baada ya kufanya ziara kukagua shughuli zinazoendelea Mererani, hususan kwenye Ukuta na kubaini udhaifu katika uchukuaji  na utunzaji wa kumbukumbu za wahusika wanaoingia ndani ya eneo hilo na kutoka, pamoja na mali (madini) yanayotolewa kupitia getini.

“Mheshimiwa Rais amewekeza pesa nyingi sana hapa. Haiwezekani sisi watendaji tushindwe kujituma hata kwa mambo madogo kama haya ya kusimamia vema utekelezaji wa ulinzi wa rasilimali hizi; yaani tusubiri yeye aje tena mwenyewe kutuelekeza hata mbinu ndogo za udhibiti. Lazima tuwe wabunifu na wenye kujituma,” alisisitiza.

Alisema kwamba, yeyote atakayepangwa kufanya kazi ya usimamizi wa Ukuta huo ajue kwamba macho la Serikali yameelekezwa mahali hapo. “Hata usipomwona Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Kamishna wa Madini, ujue macho yetu yapo huku na usipotimiza wajibu wako kwa kiwango kinachoridhisha tutakuwajibisha mara moja.”

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuhitimisha ziara yake, Naibu Waziri alifafanua kuwa, udhaifu ulioonekana ni kwa upande wa Wizara ambapo alitoa mfano kuwa; hakuna rekodi yoyote inayoonesha nani anaingia, kwa muda gani, na nani amepangwa kufanya kazi ipi. Aliongeza kuwa, hata rekodi ya namna mzigo unavyotoka ndani kwenda nje ya migodi kupitia getini, haipo.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa ya kubadilishwa kwa Afisa Madini Mkazi anayesimamia eneo hilo; Biteko alifafanua kuwa, Wizara haiwezi kuruhusu mtu yeyote kuirudisha kwenye udhaifu wa usimamizi thabiti wa rasilimali za madini, hususan baada ya jitihada kubwa zilizofanywa kuisaidia sekta ya madini iweze kukua.

“Kusema kweli, hilo hatuwezi kukubaliana nalo. Ndiyo maana nimemwelekeza Kamishna wa Madini wa Kanda, tuangalie namna ya kubadilisha uongozi hapa Mererani ili tuweze kupata mtu ambaye anaweza kusimamia vizuri.”

Aidha, Naibu Waziri aliongeza kuwa, zipo taarifa kuhusu baadhi ya Maafisa wa Wizara waliopangwa kufanya kazi Mererani kutokutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kutokuwepo mahali pa kazi kwa muda wote wa kazi kama wanavyopaswa, badala yake wanakuwepo kwa muda mfupi na kuondoka.

“Hili jambo haliwezi kuvumiliwa kwenye Wizara yetu. Kwahiyo, tunataka tudhibitiane na tusimamiane vizuri ili maana halisi ya ndoto ya Rais wetu aliyokuwa nayo katika kudhibiti madini haya iweze kutimia.”

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambaye pia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya, akisisitiza kuhusu umuhimu wa udhibiti wa utoroshwaji madini, alisema kuwa, dhamira ya Serikali kujenga Ukuta husika ni kuhakikisha changamoto ya kutorosha madini inafika mwisho ili rasilimali hizo zinufaishe Taifa ipasavyo.

“Ziara hii imetufanya tubaini kuwa udhibiti wa utoroshaji madini uliopo unapaswa kuwekewa mkazo kwa kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanayotaka kila Idara husika kuweka mbinu zaidi za udhibiti, yanatekelezwa ipasavyo.”

Ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mererani, ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Aprili 6 mwaka huu; kufuatia agizo alilolitoa yeye mwenyewe kama njia ya kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo adhimu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kulia), akimsikiliza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mererani, Fredrick Girenga (katikati) kuhusu utaratibu unaotumika kuweka kumbukumbu za watu na mali/madini wanaoingia na kutoka katika migodi ya tanzanite. Hapo ni katika Lango/Geti la kuingilia na kutokea kwenye eneo la migodi hiyo lililozungushiwa Ukuta hivi karibuni kwa amri ya Rais John Magufuli. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi Mererani, Mei 23 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia), akizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa Madini ya Tanzanite wa Edward Zakayo, uliopo Kitalu D, Mererani, wakati wa ziara yake Mei 23 mwaka huu.


Matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, kwenye machimbo ya tanzanite, Mererani, Mei 23 mwaka huu.


Kiberenge maalum kinachobeba watu na malighafi yenye madini ya tanzanite, kikipita katika njia yake kushuka chini shimoni kunakochimbwa madini hayo, kama kilivyokutwa katika Mgodi wa Franone uliopo Kitalu D Mererani, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, Mei 23 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), akizungumza na maafisa mbalimbali wa Serikali waliopo Mererani (hawapo pichani), baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye machimbo ya tanzanite kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea, Mei 23 mwaka huu. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambaye pia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), akizungumza na maafisa mbalimbali wa Serikali waliopo Mererani (hawapo pichani), baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye machimbo ya tanzanite kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea, Mei 23 mwaka huu. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambaye pia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma.

Wizara ya Madini yafanya semina ya mabadiliko ya sheria ya madini kwa Kamati za Bunge


Na Samwel Mtuwa, Dodoma

Wizara ya Madini imefanya Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Kamati ndogo ya Sheria ya Bunge juu ya Mabadiliko ya  Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

Akizungumza katika semina hiyo, Katibu wa Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania, Casmir Kyuki, alieleza kuwa, semina hiyo imelenga kuwaelemisha Wabunge  kuhusu   Sheria  Mpya ya Madini ya mwaka 2017 baada ya kufanyika Marekebisho kadhaa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

Aidha, pamoja na kupata elimu kuhusu sheria hiyo, wajumbe  wa kamati hizo walipata fursa ya  kuelimishwa kuhusu  Kanuni Saba za  Sheria ya Madini ambazo ni Kanuni ya Umiliki wa madini; Kanuni ya Biashara ya madini; Kanuni ya uendeshaji wa wananchi Kanuni ya madini ya mionzi.

Kanuni  nyingine ni pamoja na Kanuni ya uongezaji thamani madini na Kanuni ya utafiti wa kijiolojia  na Kanuni ya hifadhi ya ukaguzi wa hesabu na kumbukumbu.

Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Flurence Luoga aliwaeleza wabunge  kuhusu sababu za maboresho  ya Sheria ya Madini ya  Mwaka 2010,  Sheria ilimpa mwekezaji uhuru mkubwa  ndani ya sekta ya madini.

"Uhuru huo ni  pamoja na uhuru wa kuchimba , kusafirisha , kufanya uchenjuaji nje ya nchi, pamoja na  kufanya tafiti bila kuwasilisha taarifa  za kijiolojia na madini,"alieleza Luoga.

Akielezea juu ya sababu za kuwepo kwa uhuru huo katika sekta ya madini kabla ya maboresho ya Sheria ya 2018, Gavana  Luoga alifafanua kuwa suala hilo lilitokana na Sheria zilizokuwepo tangu enzi za Serikali ya kikoloni.

Semina hiyo iliendeshwa na wabobezi  wa masuala ya sheria , fedha na madini ambapo walitoa mada mbalimbali  kuanzia  historia ya mikataba ya kisheria ya kitaifa na kimataifa juu ya sekta ya madini tangu enzi za serikali za kikoloni za Ujerumani na Uingereza.

Watoa mada Wakuu katika semina hii walikuwa  Mkurugenzi Mkuu wa  Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini Tanzania (GST), Profesa Abdulakarim Mruma Profesa Gavana wa  Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Florence Luoga na   Katibu wa Tume ya kurekebisha sheria Tanzania Casmir Kyuki.

Semina ilifanyika tarehe 19 Mei 2018, katika ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya ukumbi mdogo wa Pius Msekwa  na kuhudhuria na  kutoka Vyama mbalimbali vya siasa, Watendaji wa Wizara na Watalaam wa  Sheria na Madini  kutoka wizara ya  Madini.

Baadhi ya Wabunge  na Watendaji wa Wizara wakifuatilia semina  kuhusu Sheri ya Madini ya Mwaka 2017.
Baadhi ya Wabunge  na Watendaji wa Wizara wakifuatilia semina  kuhusu Sheri ya Madini ya Mwaka 2017.


Baadhi ya Wabunge  na Watendaji wa Wizara wakifuatilia semina  kuhusu Sheri ya Madini ya Mwaka 2017.

Baadhi ya Wabunge  na Watendaji wa Wizara wakifuatilia semina  kuhusu Sheri ya Madini ya Mwaka 2017.

Baadhi ya Wabunge  na Watendaji wa Wizara wakifuatilia semina  kuhusu Sheri ya Madini ya Mwaka 2017.

Baadhi ya Wabunge  na Watendaji wa Wizara wakifuatilia semina  kuhusu Sheri ya Madini ya Mwaka 2017.

Friday, May 18, 2018

GST, PanAfGeo, Umoja wa Ulaya watoa mafunzo ya urithi wa vivutio vya kijiolojia


Na Samwel Mtuwa, GST

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia ya Afrika, Taasisi ya Kijiolojia ya Ulaya, Umoja wa Ulaya pamoja na Muungano wa Afrika na Ulaya katika tasnia ya Jiosayansi wametoa mafunzo juu ya Urithi wa Kijiolojia (Geoheritage) kwa Mwaka 2018.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Jiolojia kutoka GST Maruvuko Msechu alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha na kuongeza ufahamu pamoja na ujuzi juu ya sekta ya madini barani Afrika hususani katika taasisi za jiolojia Afrika pamoja na kuvumbua vivutio vingi vya utalii wa kijiolojia kupitia urithi wa kijiolojia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Jiolojia kutoka GTS John Kalimenze, alisema lengo kuu la mafunzo hayo ilikuwa ni kupeana ujuzi na kuongeza uelewa kupitia uwasilishaji wa mada mbalimbali kama vile mafunzo juu ya upimaji wa ramani za jiosayansi, uchunguzi juu ya rasilimali madini, uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo na usimamizi wa mazingira katika uchimbaji madini.

Mmoja wa Waratibu na Msimamizi wa mafunzo hayo kutoka nchini Hispania Enriq Diaz alitoa mada juu ya utunzaji wa uzuiaji wa uchimbaji holela wa madini kwa lengo la kuonyesha njia bora za kutunza urithi wa vivutio vya kijiolojia duniani.

Mafunzo hayo yanayofanyika kila mwaka yalianza tarehe 14- 19 Mei, 2018 na kushirikisha washiriki kutoka nchi mbalimbali kutoka barani Afrika zikiwemo Liberia, Botswan, Sudani ya kaskazini, Nigeria, Commoro, Moroco, Zimbambwe, Namibia.


Washiriki wa mafunzo ya kuongeza uelewa na ujuzi juu ya kuongeza na kufumbua vivutio vya urithi wa kijiolojia (Geoheritage), wakiwa katika picha ya baada ya kufunguliwa mafunzo hayo. Watano kutoka kulia  ni  Mkurugenzi wa Idara ya Jiolojia kutoka GST Maruvuko Msechu ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa  GST  Prof. Abdukarim Mruma.

Waratibu na Wasimamizi wa Mafunzo yenye lengo la kuongeza uelewa na ujuzi katika Sekta ya jiosayans na vivutio vya kijiolojia iliyoendeshwa na GST kwa ushirikiano wa PanAfGeo na Umoja wa Ulaya. Wa kwanza kutoka kushoto ni Joshua Mwankunda kutoka NCAA, anayefuata ni John Kalimenze kutoka GST, Enriqu Diaz kutoka IGME.

Mratibu na Msimamizi wa mafunzo juu ya urithi wa kijiolojia kutoka Hispania Enriq Diaz aliyesimama upande wa kulia akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Thursday, May 17, 2018

Waziri Kairuki asifu utendaji kazi wa GST


Veronica Simba na Samwel Mtuwa, Dodoma

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amefanya ziara katika Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) na kupongeza utendaji kazi wake.

Alifanya ziara hiyo Jumatano, Mei 16 mwaka huu katika Ofisi za Taasisi hiyo zilizopo Dodoma, akiwa amefuatana na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto Biteko.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, baada ya kukutana na Menejimenti ya GST na kutembelea sehemu mbalimbali kujionea shughuli zinazofanywa; Waziri Kairuki alisema kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake wa Wizara, wanafurahishwa na utendaji kazi wa Taasisi hiyo.

“GST wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya kuriarifu Taifa kuhusu uwepo wa aina mbalimbali za madini nchini; lakini pia katika upimaji wa matetemeko ya ardhi na shughuli nyingine za aina hiyo.”

Kuhusu upimaji wa matetemeko unaofanywa na GST, Waziri Kairuki alifafanua kuwa, Wizara imeielekeza Taasisi hiyo iendelee kutoa elimu zaidi kwa wananchi, hususan wanaojenga katika maeneo kunapotokea matetemeko ili wajue tahadhari za kiujenzi wanazopaswa kuchukua kuepukana na athari za majanga hayo.

Aidha, alisema kuwa Wizara yake itakutana na Wizara ya Ujenzi kujadiliana namna ambavyo wataalam wa pande hizo mbili wanavyoweza kushirikiana ili kuhakikisha majengo yote ya makazi na hata Taasisi mbalimbali, hususan yaliyopo katika maeneo yenye matetemeko ya ardhi, yanajengwa kwa kufuata ushauri wa kitaalam.

Kwa upande wa tafiti za kijiolojia zinazofanywa na GST, Waziri Kairuki alisema kuwa, baada ya ziara hiyo na kuzungumza na Menejimenti ya GST, yeye na viongozi wenzake wameona kuwa ipo haja ya kuipitia upya Sera ya Madini na kuiboresha zaidi, ili isaidie Taifa kupata mapato stahiki yatokanayo na rasilimali madini.

Akifafanua, alisema kuwa  kwa sasa, Sera ya Madini inaelekeza makadirio ya rasilimali-madini katika ardhi yetu yafanywe na sekta binafsi.

“Kuwaachia sekta binafsi kufanya makadirio kunampa mwekezaji nafasi nzuri zaidi ya Serikali wakati wa majadiliano ya uwekezaji, maana anakuwa na ufahamu zaidi wa rasilimali husika kuliko Serikali. Hivyo tumeona ni vema tuwe na ufahamu huo ili itusaidie kupata mapato zaidi.”

Waziri alitoa rai kwa wachimbaji wadogo wa madini kuwasilisha GST sampuli za madini wanazozipata katika maeneo yao, ili wapatiwe ushauri wa kitaalam zaidi kuhusu nini wanachotakiwa kufanya pindi wakianza shughuli za uchimbaji.

Aliwataka kutokuwa na wasiwasi, kwani Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele na mkazo kwa wachimbaji wadogo, kwa lengo la kuwawezesha kufikia hatua ya uchimbaji wa kati na hata uchimbaji mkubwa ili waweze kunufaika zaidi na kulinufaisha Taifa kwa ujumla.

Alisema, Serikali imetenga maeneo takribani 44 kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini na itaendelea kutenga maeneo zaidi. “Niendelee kuwasihi wachimbaji wetu wadogo wafuate kanuni na taratibu, nasi tunaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano na kipaumbele zaidi.”

Awali, wakizungumza wakati wa kikao na Menejimenti ya GST wakati wa ziara hiyo, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko pamoja na kupongeza utendaji kazi mzuri wa Taasisi hiyo, waliwataka watendaji wake kuendelea kumpa ushirikiano Waziri na Viongozi wengine ili kwa pamoja watimize majukumu yao ya kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha watanzania kwa kiwango stahiki.

Naye, Mtendaji Mkuu wa GST, Prof. Abdulkarim Mruma, alimshukuru Waziri na Naibu Mawaziri kwa kufanya ziara hiyo kwani imewawezesha kupata ufahamu zaidi kuhusu Taasisi husika.

Wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa GST kwa Waziri, pamoja na mambo mengine, Prof Mruma aliahidi kuwa yeye na watendaji wenzake wa Taasisi hiyo, wataendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha Taifa linanufaika ipasavyo kupitia rasilimali za madini.

GST ilipandishwa hadhi Julai 2017, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kuitwa Taasisi ya Jiolojia Tanzania. Awali, ilikuwa ikiitwa Wakala wa Jiolojia Tanzania.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) na Ujumbe wake, wakiangalia sampuli za miamba na madini mbalimbali yanayopatikana nchini, wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Jilojia Tanzania (GST) iliyopo Dodoma, Mei 16, 2018. Pamoja naye pichani ni Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto Biteko, Mtendaji Mkuu wa GST, Prof Abdulkarim Mruma, Mkurugenzi wa Kanzidata, Yokbeth Myumbilwa na Kaimu Meneja Uchoraji Ramani, Alphonce Bushi.


Mtendaji Mkuu wa GST, Prof Abdulkarim Mruma (katikati), akimwonesha Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (wa tatu kutoka kushoto) na Ujumbe wake, moja ya ramani ya kijiolojia iliyoandaliwa na Taasisi hiyo. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kwenye Taasisi hiyo, Mei 16 mwaka huu, pamoja na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo (kushoto kwa Waziri) na Doto Biteko (wa kwanza kushoto).


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (wa pili kushoto-mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST), baada ya ziara yake kwenye Taasisi hiyo Mei 16 mwaka huu. Pamoja naye (mstari wa mbele) kutoka kushoto ni Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, Mtendaji Mkuu wa GST Prof Abdulkarim Mruma na Naibu Waziri Doto Biteko.

Friday, May 11, 2018

Waziri Kairuki akutana na Balozi wa Japan nchini


Na Samwel Mtuwa, Dodoma

Waziri wa Madini,  Angellah Kairuki leo amekutana na  balozi wa Japani nchini, Masaharu Yoshida mjini  Dodoma lengo likiwa ni kujadiliana namna ya kushirikiana kwenye uwekezaji wa madini nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki alisema lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili maandalizi ya Jukwaa la Uwekezaji  katika Sekta ya Madini kati ya  Tanzania na  Japan.

Alisema kupitia jukwa hilo, wadau kutoka nchi zote mbili watafahamu  fursa za uwekezaji  katika sekta ya madini kama vile uongezaji  thamani ya madini yapatikanayo nchini na namna ya kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo.

Kairuki aliongeza kuwa mbali na fursa mbalimbali katika sekta ya madini jukwaa hilo litaangalia namna ya kuongeza ajira kwenye sekta hiyo kwa kuwajengea uwezo wadau wa madini nchini.

Balozi Yoshida aliambatana na Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya uwekezaji katika sekta  ya madini.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) akibadilishana mawazo na Balozi wa Japan Nchini Masaharu Yoshida (kulia) ofisini kwake mjini Dodoma mapema leo tarehe 09 Mei, 2018.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) akiagana na Balozi wa Japan Nchini Masaharu Yoshida (kulia) mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.


Waziri wa Madini,  Angellah Kairuki (wa pili kutoka kulia) na Balozi wa Japan Nchini Masaharu Yoshida ( wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa  Japan mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.

Tuesday, May 8, 2018

Naibu Waziri Nyongo afunga mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini


Na Greyson Mwase,

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefunga mkutano wa kwanza wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini uliofanyika mjini Morogoro leo tarehe 07 Mei, 2017.

Akifunga baraza hilo, amesema sekta ya madini ni muhimu katika kuinua uchumi wa nchi na kuwataka watumishi kutoa kipaumbele kwenye uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini nchini.

Naibu Waziri Nyongo amewataka watumishi kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma ili kuleta tija kwenye utendaji kazi.

Aidha, amewataka wajumbe wa baraza na watumishi kwa ujumla kutekeleza maazimio waliyojiwekea katika mkutano huo ili kuboresha utendaji kazi wa Wizara na kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Madini.

Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo ni pamoja na  wachimbaji wadogo wa madini wawezeshwe kwa kuwekewa mazingira mazuri ya utendaji kazi, taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ziunde mabaraza na  watumishi wote ambao hawajajaza fomu za maadili watekeleze wajibu huo.

Kikao kingine cha baraza hilo kimependekezwa kufanyika mjini Morogoro baada ya mwaka mpya  wa fedha 2018/2019.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akifunga mkutano wa kwanza wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini uliofanyika mjini Morogoro leo tarehe 07 Mei, 2017. 


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati waliokaa mbele), Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila ( wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya  Wizara ya Madini.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati waliokaa mbele), Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila ( wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati waliokaa mbele), Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila ( wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini.


Kutoka kulia Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa RasilimaliWatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila na Katibu wa TUGHE mkoa wa Dodoma, Mchenya John wakiwa katika picha ya pamoja.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati waliokaa mbele), Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila ( wa nne kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na madereva wa wizara hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

Waziri Kairuki afungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini


Na Greyson Mwase,

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.

Katika mkutano huo Waziri Kairuki amewataka watumishi kuelekeza nguvu kwenye kutoa kipaumbele kwenye masuala muhimu kama vile kuendelea kutengeneza sera bora zinazosimamia rasilimali za madini na kuweka mfumo mzuri na ulio bora wa ukusanyaji wa mapato ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

Pia, amewapongeza watumishi kwa ukusanyaji wa maduhuli  hadi kuvuka lengo kwa asilimia 130 ya makusanyo ya lengo  lililokuwa limewekwa kwenye Sekta ya Madini.

Aidha, amewataka watumishi kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2017/2018 ili kufanya vizuri kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019.

Aidha amewaasa watumishi wote kuwa waadilifu katika utendaji kazi wa kila siku na kuagiza watumishi wote waelimishwe kuhusu maadili katika utumishi wa umma na wale ambao hawajajaza fomu za maadili kujaza mara moja.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Wizara imebeba matarajio makubwa ya wananchi na kuwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya.

Aidha,  amesema Wizara ya Madini ni miongoni mwa Wizara zinazowajibika kuchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa.

Waziri Biteko amesisitiza mahusiano mazuri baina ya vyama vya wafanyakazi na waajiri  ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na  umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa umma. Masuala mengine  yaliyojadiliwa ni pamoja na  mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017.

Mkutano huo umefanyika leo tarehe 07 Mei, 2018 katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki  (kushoto) akipokelewa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa RasilimaliWatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi (kulia) mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA)mjini Morogoro, kwa ajili ya kuzindua mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini tarehe 07 Mei, 2018.


Kutoka kushoto Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William (hayupo pichani) katika mkutano huo.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William akielezea majukumu ya chama hicho kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini (hawapo pichani) katika mkutano huo.


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko katika mkutano huo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko  akifafanua jambo katika mkutano huo.


Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini wakiimba wimbo maarufu wa mshikamano (solidarity forever) kwenye mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo.


Sekretarieti ya maandalizi katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akimkabidhi Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila nakala ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William nakala ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa nne kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la  Wizara ya Madini mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.