Saturday, August 18, 2018

Serikali kutoa eneo la Buhemba kwa wachimbaji ikiwa itanufaika


Na Asteria Muhozya, Mara

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema Wizara italigawa kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini eneo lote la mgodi wa Buhemba linalomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ikiwa Serikali itanufaika ipasavyo  na makusanyo kutokana na shughuli za wachimbaji hao.

Kauli ya Waziri Kairuki imekuja kufuatia maombi yaliyotolewa na Chama Cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara (MAREMA) kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Stephano Mseti ambaye alimuomba Waziri Kairuki kulitoa eneo lote la STAMICO kwa wachimbaji hao kwa kuwa wana uhakika wa kuchangia zaidi kodi za serikali ikiwa watamilikishwa eneo husika.

Aidha,  Mseti alimweleza Waziri Kairuki kuwa  wachimbaji katika eneo hilo wamejiandaa kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wanalipa kodi stahiki kwa kuwa, ndani ya mwezi mmoja waliopewa kufanya kazi katika eneo husika, wamekusanya kiasi cha shilingi milioni 107 kama mrahaba.

Katika hatua nyingine, wakati akisikiliza kero za wachimbaji hao, Waziri Kairuki aliiagiza Tume ya Madini na Wataalam kutoka Wizara hiyo kuchunguza kwa kina suala la migogoro ya migodi  yote iliyopo katika eneo la Buhemba iliyotolewa awali na STAMICO kwa wachimbaji hao  na kukamilisha kazi husika ndani ya kipindi cha wiki 3 ikiwemo  kutoa mapendekezo  aweze kujua hatua za kuchukua.

Akizungumzia mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Waziri Kairuki alieleza kuwa, tayari serikali imeanza kujenga kituo cha umahiri katika mkoa huo ili kuwezesha wachimbaji wadogo  kujifunza uchimbaji bora na kuwataka wachimbaji mkoani humo kukitumia kikamilifu kituo hicho mara baada ya kukamilika kwake.

Akizungumzia muda wa uhai wa leseni, alisema kuwa suala hilo limebainishwa kisheria kuwa ni ndani ya kipindi cha miaka saba na kufafanua kuwa, ipo haki ya kuhuisha  muda wa leseni na hivyo kuwataka wamiliki wote wa leseni kuzingatia muda husika uliowekwa kisheria.

Pia, aliwataka wachimbaji hao kutoa taarifa za kuwepo Maafisa Madini wanaomiliki leseni za uchimbaji madini au wanaomiliki leseni hizo kupitia  kwa kutumia majina tofauti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Akizungumzia kuhusu suala la migogoro, alisema kuwa Serikali haifurahishwi na migogoro inayotokea katika maeneo ya migodi na hususani ile inayohatarisha maisha na kuongeza kuwa, serikali haipendi kufunga migodi hiyo kutokana na umuhimu wa migodi hiyo kwa pande zote.

Pia, Waziri Kairuki alisisitiza kuhusu suala la uchimbaji salama  migodini na Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii na kuongeza kuwa, suala hilo ni lazima litekelezwe na wamiliki wote wa leseni wakiwemo wachimbaji wadogo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, alisema Mkoa huo umejipanga kuwa na Gold Exchange ili kuwezesha mkoa huo pia kunufaika na rasilimali hiyo.

Aidha, alisisitiza suala la uchimbaji salama wa madini ikiwemo utunzaji wa mazingira na kuwataka wachimbaji hao kubadilika kwa kuhakikisha wanafanya shughuli zao kisasa.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa, Serikali inawaona wachimbaji wadogo kwa jicho la kipekee na inajua kuwa, ikiwawezesha itapata fedha nyingi kutokana na rasilimali hiyo.

Alisema kuwa, mkoa huo una migogoro mingi ikilinganishwa na mingine na kumshauri Waziri Kairuki kupokea  vizuri malalamiko yote ya wanaolalamika kwani si wote wanalalamika kihalali.

Pia, aliwashauri Maafisa Madini nchini kuhakikisha kuwa, wanapotatua migogoro zawanavishirikisha Vyama vya Wachimbaji katika kutatua migogoro hiyo ikiwemo katika suala la ukusanyaji kodi za serikali.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Chama Cha Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, aliiomba  Serikali kuiwezesha Tume ya Madini ili iweze kuwafikia wachimbaji katika ngazi za chini.

Pia, aliwataka wachimbaji kuwa wakweli na kuacha ubifasi, na kueleza kuwa, kuna watu ndani ya umoja huo wananufaika pindi panapokuwa na migogoro na kuongeza kuwa, migogoro katika jamii ya wachimbaji ni mdudu anayekua kila siku.

Awali, akiwasilisha taarifa ya chama hicho, Katibu Mkuu wa MAREMA, Milele Mundeba, alisema Chama hicho kinakusudia uanzishaji wa biashara ya vifaa vya uchimbaji madini.

Mbali na wachimbaji mkutano huo uliofanyika tarehe 16 Agosti, ulihudhuriwa na benki ya CRDB, SIDO, Benki ya Posta Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya NMB, FINCA, Shirika la Bima la Taifa ( NHIF),  Mamlaka ya Maji, Musoma (MUWASA), Migodi ya Wachimbaji wa Kati ya CATA Mining, ACACIA na  Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akipokewa na viongozi mbalimbali MAREMA na FEMATA.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya pamoja  na Baadhi ya Viongozi na Wanachama wa MAREMA na Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini, ( FEMATA).



Waziri wa Madini Angellah Kairuki akizungumza jambo wakati wa mkutano na Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara (MAREMA).

No comments:

Post a Comment