Saturday, August 18, 2018

Serikali kuleta timu jumuishi ya wataalamu utafiti wa madini Muheza


Na Zuena Msuya, Mheza Tanga

Serikali imesema itawaleta wataalam kutoka kituo cha Utafiti wa Miamba(GST), Wizara ya Maliasili  na  Mazingira kwenye eneo walilokuwa wakitumia wachimbaji wadogo kwa shughuli za madini, ambalo pia linadaiwa kuwa liko katika chanzo cha maji, kufanya utafiti na kujiridhisha kama eneo hilo liruhusiwe kuendeleza na shughuli za uchimbaji madini  ama laa. 

Hayo yalisemwa na Naibu waziri wa Madini Dotto Biteko alipotembelea katika kijiji cha Sakale katika Kata ya Mbomole Tarafa ya Amani wilayani Mheza mkoani Tanga, wakati akizungumza na wananchi waliomuelezea kero yao ya kuzuiwa na serikali kutokuchimba madini eneo hilo licha ya kuwatokuwepo na viashiria vya uharibifu wa mazingira na misitu kama serikali inavyosema.

Naibu Waziri Biteko, alisema kuwa kiu ya serikali ni kuwapatia maeneo ya uchimbaji wachimbaji wadogowadogo ili waweze kubadilisha maisha yao kupitia uchumi wa madini, hii ni kutokana Rais kubadilisha sheria za nchi kwa upande wa madini kutoka kuwanufaisha wageni na sasa kuwanufaisha watanzania.

“Serikali yenu ni sikivu,Mheshimiwa Rais amebadilisha sheria ya madini ili kuwanufaisha watanzania badala ya wageni ,hapa leo tumekuja kuangalia kwa macho ili tufanye uamuzi sahihi …siwezi kumiambia mchimbe sasa hivi ila tutaleta wataalamu wetu wa GST,maliasili na mazingira kwa pamoja ili waje kuona uwezekano wa kupewa eneo la kuchimba ikiwa hapa au kwengine”alisema.

Aidha aliongeza kuwa wananchi lazima wafundishwe kufuata sheria za madini haswa katika kuhama  matumizi ya zebaki katika kuchenjua madini ambayo yana athari kubwa kwenye mazingira na miili ya binadamu kutumia madini ya Sayayi ambayo hayana madhara. 

Kwa upande wa wananchi wa eneo hilo, walimueleza naibu waziri huyo kuwa madini katika eneo hilo yaligunduliwa mwaka 2013 na yanapatikana kwenye miamba na siyo kwenye chanzo cha mto kama serikali inavyosema lakini walizuiwa kwa tahadhari ya uharibifu wa mazingira na misitu ya asili.

Walisema kuwa kutoka uliopo mwamba unaosadikiwa kuwa na madini na chanzo cha maji ni zaidi ya mita sitini na ilipo hifadhi ya msitu wa asili wa Amani ni zaidi ya mita 3,000 lakini wamekuwa wavumilivu kusubiri hatima ya serikali.

“Mheshimiwa Naibu Waziri uchumi tunao lakini tunakufa maskini…hapa madini yapo lakini serikali imetuzuia kwa hatari ya uharibifu wa mazingira ..sisi tunakuhakikishia hakuna uharibifu wowote wa mazingira  utakaotokea,” alisema Shetwai.

Naye diwani wa kata hiyo Anord Mlowe alisema kuwa wataalamu walikuja kupima mwamba  na baadae ukaanza kutoa madini lakini baadae kukaanza mabishano kati ya watu wa maliasili,maji na mazingira kuhusu usafishaji wa madini kwa kutumia zebaki lakini mkuu wa wilaya  ya Muheza  aliyepita Subira Mgalu alijiridhisha kuwa hakuna madhara lakini serikali ikaweka zuio.

Alimuomba waziri kuwaruhusu ili waweze kuchimba kutoka maeneo yalipo mmwamaba wa madini ni mashamba ya wananchi na sio eneo la hifadhi kutokana wameyarithi kutoka kwa mababu zao.                    

Akizungumzia eneo hilo,  mbunge wa jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu alimuomba Naibu Waziri , Biteko kuleta wataalamu wa madini kuja kupima ili kuona kama madini hayo yanatoka milimani au yapo kwenye mto ili kuona namna ya kuwasaidia kupewa eneo la uchimbaji.

“Mheshimiwa naibu waziri pale mwamba uko pembeni kutoka chanzo cha maji na wananchi wa Sakale kata ya Mbomole wametunza msitu wa asili wa Amani….hivyo wakipewa eneo la uchimbaji wataweza kutunza msitu bila ya kuathiri  chanzo cha maji” alisema.

Aliongeza “kwa niaba yao tuma wataalamu wako waje ili wakuletee taarifa ili wananchi hawa waweze kuchimba”.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo akisoma taarifa ya zuio la uchimbaji wa madini eneo hilo, alisema lengo ni kulinda mazingira na chanzo cha maji licha ya sheria katika maeneo hayo matatu ya madini, mazingira na maliasili kukinzana jambo ambalo linaleta ugumu kwa watendaji kuwadhibiti wachimbaji hao.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, (mwenye Tshit nyekundu) na Mbunge wa Mheza Balozi Rajab Adad (mbele) wakielekea eneo lililokuwa likitumiwa na wachimbaji wadogo kuchimba madini pia likidaiwa kuwa chanzo cha maji katika hifadhi ya misitu wa asili wa amani, mheza Tanga. 

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko,( katikati) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sakale, Mheza mkoani Tanga, waliokuwa wakiomba kuruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji madini katika eneo linalodaiwa kuwa ni chanzo cha maji yanayotumika Mkoa wa Tanga.

No comments:

Post a Comment