Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki jana tarehe13 Agosti alikutana na Balozi wa Afrika Kusini
nchini Tanzania, Mheshimiwa Thami Mseleku. Katika mkutano huo, Balozi huyo alimueleza
Waziri Kairuki kuhusu utayari wa Nchi hiyo ya Afrika Kusini kuendeleza
ushirikiano na Tanzania katika sekta ya madini nchini.
Ujio wa Balozi Thami
Mseleku, Makao Makuu ya Wizara ya Madini, unafuatia ziara ya Kamati ya Jamii na
Masuala ya usalama ya Bunge ya Jimbo la Gauteng Pretoria- Afrika Kusini ambao
walifika nchini mwezi Juni mwaka huu kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa
namna sekta ya madini nchini inavyoendeshwa.
Aidha, wakati wa
ziara ya kamati hiyo ya Bunge hilo nchini, ilikubalika kuwa na haja ya kuwa na ushirikiano
katika masuala mbalimbali ya namna ya kusimamia sekta ya madini ikiwa ni pamoja
na shughuli za uchimbaji madini, kubadilishana uzoefu katika udhibiti wa
uchimbaji holela wa madini, usimamizi wa migodi na wachimbaji wadogo wa madini.
Maeneo mengine ni
pamoja na namna ya kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini kutoka katika uchimbaji
mdogo kwenda katika uchimbaji wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.
Pia, masuala ya
utafiti wa miamba ya uchimbaji madini, mafunzo kwa ajili ya wataalam,
kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa sekta ya madini, masuala ya umiliki wa
migodi na namna ya kuwawezesha wazawa kumiliki uchumi kupitia sekta ya madini.
Kwa upande wake,
Waziri Kairuki alimhakikishia Balozi Thami kuhusu nia ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya kumarisha na kukuza zaidi mahusiano baina ya nchi hizo mbili pamoja na
kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika sekta mbalimbali hususan katika
sekta ya madini ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki akimweleza jambo Balozi ya Afrika Kusini nchini Tanzania Thami
Mseleku (kushoto) wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri kairuki ofisini
kwake jijini Dodoma.
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Thami
Mseleku, wakijadiliana jambo ofisini kwa Waziri Kairuki, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment