Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Serikali
imesema inafanya utaratibu wa kuwa na Hati ya Utambulisho wa Kimataifa wa Madini
ya Tanzanite, ambayo yanapatikana katika nchi ya Tanzania pekee katika vilima
vya Mirerani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.
Hayo
yamebainishwa leo tarehe 25 Agosti na Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa
Semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
ambayo imefanyika Makao Makuu ya Wizara, jijini Dodoma.
Waziri
Kairuki amesema kuwa, serikali inataka kuona kuwa dunia inafahamu kuwa, madini
hayo yanapatikana Tanzania pekee na kuhakikisha kwamba yanajulikana zaidi.
Semina
ya wabunge imefanyika kufuatia maelekezo ya Kamati hiyo ambayo ilitaka kufahamu
kuhusu mwenendo mzima wa Madini ya tanzanite, biashara na udhibiti wa madini
hayo baada ya kujengwa kwa Ukuta wa Mirerani unaozunguka migodi ya madini ya
tanzanite, Muundo wa Wizara ya Madini, Tume ya Madini na majukumu yao.
Waziri
Kairuki amesema kuwa, Wizara imepata fursa ya kuwasilisha kwa Kamati hiyo
taarifa za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo mikakati ya serikali
katika kudhibiti utoroshaji wa madini hayo na mipango madhubuti ambayo serikali
inakusudia kuifanya ili kuhakikisha kwamba rasilimali madini inalinufaisha
taifa na hatimaye sekta ya madini iweze kufikia asilimia 10 ya machango wake
katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.
Ameongeza
ni kikao ambacho kimekuwa na manufaa kwa
upande wa Serikali kwa kuwa imetoa elimu kwa Kamati hiyo kuhusu yale ambayo
serikali imefanya na inayokusudia kufanya kuhusuiana na madini ya tanzanite lakini pia serikali imepata
wasaa wa kupokea maoni, mapendekezo na maelekezo kutoka kwa wabunge ambayo
yatawezesha kupeleka mbele sekta ya Madini.
Mbali
ya tanzanite, Waziri Kairuki amewaeleza wabunge hao kuhusu mkakati wa serikali
kuanzisha Mineral Exchange ambapo
amesema tayari wizara imeshaandaa timu ya wataalam ili kwenda kujifunza na
kufanya utafiti katika nchi nyingine ili suala hilo liweze kufanyika kwa ubora
.
Pia,
ameeleza kuwa, Wabunge wa Kamati hiyo, wamepata fursa ya kufahamu majukumu ya
Wizara baada ya kuundwa kwa Tume ya Madini, majukumu ya tume ya madini na mahusiano
ya kiutendaji kati ya Tume na Wizara.
Kwa
upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile, amesema kuwa,
kamati imebaini kuwa, Serikali imechukua hatua nyingi za kulinda na kudhibiti
madini ya tanzanite ikiwemo kudhibiti
utoroshaji wa madini hayo. “Kama kamati tumeona mnyororo mzima wa thamani ya
madini ya tanzanite, awali tulikuwa hatunufaiki kama taifa,” amesema
Ditopile.
Awali,
akiwasilisha mada kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti
utoroshaji wa madini ya tanzanite na usimamizi wa shughuli za uchimbaji na
biashara ya madini ndani ya ukuta, Afisa Madini Mkazi wa Mirerani Mhandisi David
Ntalimwa, amezungumzia sababu za kushuka kwa mapato na kueleza kuwa, kunategemea
kiwango cha ubora na sifa za madini husika.
Ameongeza
kuwa, kutokana na mazingira hayo, kiwango cha thamani ya madini na tozo ya
mrabaha kitakuwa tofauti kutegemea na mwezi na uzalishaji uliopo.
Akizungumzia
sababu za utoroshaji wa madini ya tanzanite, Mhandisi Ntalimwa amesema kuwa, zinatokana
na uwezo mdogo wa kusanifu na kuongeza thamani na kunga’risha madini ya vito na
hivyo watu kutamani kuuza tanzanite ghafi.
Pia,
amesema utoroshaji wa madini unatokana na kukwepa kulipa kodi na tozo
mbalimbali zinazotozwa na serikali ili kujipatia faida kubwa, kuwepo kwa raia
wa kigeni nchini wanaofanya biashara ya madini kinyume na sheria kwa
kushirikiana na wazawa na kukosekana kwa masoko ya uhakika ya kuuzia madini
yanayozalishwa.
Akizungumzia
hatua zilizochukuliwa na serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini baada
ya kujengwa ukuta amesema kuwa, serikali imeimarisha ulinzi na ukaguzi getini
kwa kutumia vikosi vya ulinzi na usalama, kuzuia magari kuingia na kutoka ndani
ya ukuta, watu kuingia ndani ya ukuta kwa vitambulisho maalum.
“Sasa watu wanaingia kwa utaratibu maalum tofauti na walivyozoea awali. Ukuta
umeleta utaratibu mzuri na si kero, kama baadhi ya watu wanavyodhani,”
amesisitiza Ntalimwa.
Amezitaja
hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuzuia Mabroker kwenda migodini na badala yake
kutakiwa kusubiria madini getini, uthaminishaji madini kufanyika ndani ya ukuta
na serikali kujenga jengo lenye ofisi ya ukaguzi, uthaminishaji na ukumbi wa
mabroker ndani ya ukuta.
Aidha,
pamoja na kushiriki semina hiyo, pia wabunge hao wamepata fursa ya kutembelea
Makumbusho ya Taifa ya Jiolojia na Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti
wa Madini Tanzania, (GST).
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini
wakifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali zilizotolewa kwa kamati ya Bunge.
|
![]() |
Afisa Madini Mkazi wa Mirerani,
Mhandisi David Ntalimwa, akieleza jambo wakati akiwasilisha mada kwa wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
|
Sehemu ya Maafisa Waandamizi wa Wizara
na Tume ya Madini wakifuatilia mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini.
|
Kamishna wa Madini Mhandisi David
Mulabwa, akieleza jambo wakati akiwasilisha mada kwa Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
|
No comments:
Post a Comment