Thursday, July 26, 2018

Shughuli za uchimbaji madini ya Kaolin zasimamishwa mgodi RAK Kaolin


Na Zuena Msuya, Pwani

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amesimamisha shughuli za uchimbaji madini ya Kaolin katika mgodi unaomilikiwa na kampuni ya RAK Kaolin hadi pale wahusika watakapoeleza thamani halisi ya bei ya madini hayo yanayouzwa na kutumika viwandani, leseni ya mgodi, uchimbaji pamoja na umiliki ardhi.

Pia, alimtaka mmiliki wa leseni ya mgodi huo kuwasilisha wizara ya madini nakala ya mkataba walioingia kati yake na wachimbaji wa madini hayo katika mgodi huo, na namna ambavyo aliweza kumiliki eneo husika.

Nyongo alisimamisha shughuli za uchimbaji katika mgodi huo ulipo katika Kijiji cha Kimani wilayani Kisarawe mkoani Pwani, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini ya ujenzi Julai 25,2018.

Akizungumzia uamuzi wa kufunga mgodi huo ambao baadhi ya viwanda hutumia madini hayo kutengeneza bidhaa mbalimbali, Nyongo alisema kuwa, haridhishwi na shughuli za uchimbaji zinazofanya katika mgodi huo ikiwepo suala la umiliki wa ardhi, leseni ya mgodi, uchimbaji pamoja na biashara ya madini hayo viwandani.

Alifafanua zaidi kuwa, shughuli za uchimbaji na biashara ya madini katika mgodi huo hazionyeshi wazi taratibu wa ulipaji serikalini, mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho 2017.

“Shughuli za uchimbaji wa madini hapa nchini ni lazima ziwanufaishe watanzania na taifa kwa ujumla kwa kuwawekea mazingira mazuri wamiliki wa ardhi, wamiliki wa leseni pamoja na wachimbaji na siyo kuwanyonya, pia kulipa mrabaha na tozo mbalimbali kwa lengo la kuongeza mapato serikalini, sasa mgodi huu taarifa zake zinakinzana licha yakuwawepo kwa muwekezaji kufanya shughuli za uchimbaji na kuendelea na biashara ya madini,” alisisita Nyongo.

Aidha, aliiagiza ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kushirikiana na maafisa madini kufuatilia maeneo yote yenye madini ya Kaolin na kuhakiki leseni zilizopo pamoja na uhalali wake ili kufahamu idadi ya zilizokuwa hai na zilizomaliza muda wake.

Pamoja na mmbo mengine, aliendelea kusisitiza kuwa serikali itayafutia leseni zote sizoendelezwa na kuwa maeno hao wale wenye nia ya kuendeleza maeneo hayo kwa shughuli za uchimbaji madini.

Sambamba na hilo kuwataka wachimbaji na wamiliki wa migodi na wafanyabiashara ya madini kulipa mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 na kufanyiwa marekebisho 2017 pamoja na kushiriki shughuli za kimaendeleo na kijamii katika maeneo yanayowazunguka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happyness Seneda alimuhakikishia Naibu Waziri Nyongo kuwa, kwa kushirikiana na Wizara ya Madini,anaimani mapato yote yaliyokuwa yakipotea sasa yataingia serikalini.

Seneda aliwaonya wawekezaji uchwara, wamiliki wa leseni na wachimbaji wasiowaaminifu kuwa kuanzia sasa kuacha    kufanya udanganyifu au ujanja ujanja katika sekta ya madini baada ya sheria ya madini ya 2010 kufanyiwa marekebisho 2017, kwa lengo la kuifanya sekta hiyo kuwanufaisha watanzania na taifa kwa ujumla.

Mkoa wa Pwani hasa katika Wilaya ya Kisarawe unasifika zaidi kwa upatikanaji wa madini ya Kaolin yanayotumika viwandani kutengeza bidhaa mbalimbali zikiwepo,Malumalu (Tiles) zinazotumika katika shughuli za ujenzi, karatasi, rangi ya nyumba n.k.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akiongozana na mmoja wa wazee (katikati) katika kijiji cha Kimani wilayani Kisarawe baada ya kusimamisha shughuli za uchimbaji madini ya Kaolin katika mgodi unaomilikiwa na kampuni RAK Kaolin. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happyness Seneda.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia), akionyeshwa jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Happynes Seneda( wa pili kulia) wakati wakikagua migodi ya uchimbaji madini ya Kaolin wilayani humo.

Naibu Moja ya maeneo yaliyokuwa yakichimbwa madini ya Kaolin katika Wilaya ya Kisarawe ambayo uchimbaji wake umesimamishwa kutokana na kutofuata sheria ya uchimbaji wa madini

No comments:

Post a Comment