Na
Asteria Muhozya
Waziri wa
Madini Angellah Kairuki amesema anatamani kuona ifikapo mwezi Disemba mwaka huu,
Serikali kupitia Wizara ya Madini inaanzisha Soko Huria la Madini nchini (Tanzania Mineral Exchange).
Waziri Kairuki
aliyasema hayo tarehe 24 Julai, 2018, wakati wa kikao cha Menejementi ya Wizara
ya Madini na Taasisi zake ambapo Wataalam kutoka Kampuni ya Tanzania Mecantile
Exchange PLC (TMC) waliwasilisha mada
juu ya Elimu ya Soko la Bidhaa Tanzania.
Aidha, Waziri
Kairuki aliishukuru kampuni hiyo kwa kutoa wasilisho hilo ikiwemo utaalam wao
katika masuala ya soko huria la madini na kuongeza kuwa, anatamani kuona suala
hilo linafanikiwa na kufanyika mapema kwa kuwa, litawezesha Watanzania kumiliki
uchumi wa madini hata wale wenye kipato cha chini.
“Natamani
kuona ndani ya kipindi cha miezi sita vinavyowezekana kufanyika vinaanza
kufanyika. Lakini tutazingatia sheria, taratibu na utalaam kuhakikisha kwamba
suala hili linafanikiwa,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Akiwasilisha
mada, Mtaalam mwelekezi kutoka kampuni hiyo, Girish Raipurie, alieleza faida za
soko huria la madini kwa Tanzania, huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa kutolewa
mafunzo kwa wadau na elimu ya kutosha kuhusiana na suala hilo.
Pia, alieleza
kuhusu namna ambavyo Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo
zinafanya vizuri katika suala hilo huku akielezea mazingira wezeshi ambayo
yanawezesha Tanzania kufanikiwa katika uanzishaji wa soko hilo, huku akijaribu
kufananisha na mazingira ya nchini India ambayo mfumo wa soko hilo unafanya
vizuri.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMC, Godfrey Marekano, alitoa mada kuhusu Mpango wa
uwekezaji katika Soko huria na pia amegusia kuhusu masuala ya kisheria na namna
ambavyo Sheria ya Madini kama ilivyorekebishwa Mwaka 2017 inavyoweza kusimamia
uanzishaji wa suala husika.
Naye, Naibu
Waziri wa Madini Doto Biteko, alimpongeza Waziri Kairuki kwa kuanzisha wazo
hilo ambalo litawezesha kuleta mageuzi katika Sekta ya Madini na kuwataka
wataalam katika Wizara ya Madini na Tume ya Madini kulichukulia suala hilo kwa
uzito ili utekelezaji wake uweze kufanyika kama ilivyopangwa.
“Kuna maelekezo
mengi kwenye Sheria ambayo tunahitaji kuvipitia na kuyafanyia kazi. Maarifa
tuliyoyapata ni makubwa. Rai yangu ni kwa wataalam kuhakikisha wanalichukulia
suala hili kwa uzito mkubwa lisibaki mikononi mwa Waziri tu, alisisitiza Biteko”.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akifuatilia
uwasilishaji wa mada juu ya Elimu ya Soko la Bidhaa Tanzania katika kikao
kilichowashirikisha wizara na taasisi.
Mtaalam Mwelekezi kutoka kampuni ya, Girish
Raipurie, Tanzania Mecantile Exchange PLC
(TMC) akiwasilisha mada wakati wa kikao cha Waziri na Wataalam kutoka
Wizara ya Madini na Taasisi zake.
Mkurugenzi Mkuu wa TMC, Godfrey Marekano
akizungumza jambo wakati akiwasilisha mada kwa menejimenti ya Wizara na
Taasisi.
Baadhi ya Wataalam kutoka Wizara na Taasisi
wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kutoka kwa Wataalam wa kampuni ya Tanzania
Mecantile Exchange PLC (TMC).
|
No comments:
Post a Comment