Na
Zuena Msuya, Pwani
Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaangalia namna
bora ya kuimarisha soko la chumvi inayozalishwa nchini yenye uwezo wa kukidhi
mahitaji ya ndani na ziada, kwa kuzuia ile inayoingizwa kutoka nchi za nje.
Nyongo alisema hayo,
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Julai 23, 2018, baada ya kutembelea Mgodi wa kuzalisha
chumvi wa kampuni ya Stanley and Sons ulioanzishwa mwaka 1948/49 uliopo katika Kijiji
cha Kitame wilayani humo.
Akizungumzia
uzalishaji chumvi, Nyongo alitolea mfano mgodi pekee wa Stanley kuwa, huzalisha
chumvi kati ya tani 4000 hadi 6000 kwa mwaka kulingana na hali ya hewa, licha
ya kuwepo migodi mingi ya uzalishaji chumvi katika baadhi ya Mikoa nchini ambapo
mara nyingi wazalishaji wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa soko la chumvi
wanayozalisha.
Alitaja baadhi ya Mikoa
iliyokuwa na migodi ya kuchimba na kuzalisha chumvi kuwa ni pamoja Pwani yenye
zaidi ya mgozi mmoja, Kigoma katika eneo la Uvinza, Lindi pamoja na Mtwara.
" Tanzania ina migodi
mingi ya kuchimba na kuzalisha chumvi bora, ya kutosha na yenye kukidhi
mahitaji ya ndani na kuuza nje, hivyo ni wakati sasa, serikali kuangalia namna
bora ya kulinda soko la ndani la chumvi kwa kuzuia ile inayoingizwa kutoka nje,
ili wazalishaji waweze kupata soko la uhakika", alisisitiza Nyongo.
Aidha aliwaagiza
wachimbaji na wazalishaji wa chumvi nchi, kusindika chumvi hiyo katika ubora
unaotakiwa na kukidhi viwango vya soko la Kimataifa kwa kuzingatia kuwa, Tanzania
inazalisha chumvi iliyobora.
Sambamba na hilo, alieleza
kuwa kwakuwa chumvi ni bidhaa mtambuka inayotumika kama chakula, dawa, pamoja
na kuwa ni madini hivyo, aliwataka wachimbaji na wazalishaji wa chumvi, kusindika
chumvi hiyo katika ujazo tofauti na kwa bei nafuu ili kila mmoja aweze kumudu
gharama za kununua chumvi hiyo kwa matumizi husika ikiwemo majumbani, viwandani
na hata katika mifugo.
Pia, alisema
wazalishaji wakubwa wawasaidie na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wa chumvi
ili na wao waweze kuuza na kusambaza chumvi hiyo ili iwafikie watumiaji wa aina
mbalimbali kwa urahisi zaidi na kukidhi mahitaji ya walaji kwa wakati.
" Watumiaji
wengi wa chumvi majumbani wananunua na kutumia iliyosindikwa katika ile mifuko
midogo ya robo au nusu kilo, sasa ninyi wachimbaji na wazalishaji wa chumvi
muangalie namna ya kuwafikia watumiaji wote wa chumvi hapa nchini, hii italeta
tija kwa watanzania kutangaza na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini",
alisema Nyongo.
Nyongo aliendelea
kusisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za wachimbaji na
wazalishaji wa chumvi nchini kwa kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha
kufanya kazi hiyo katika kiwango kikubwa na ubora unaotakiwa.
Pamoja na mambo
mengine, alisema kuwa, tayari serikali imewafutia wachimbaji na wazalishaji
chumvi, kodi kumi na moja ambazo zilikuwa kero kubwa kwao, na kwamba serikali
inaendelea kushughulikia vikwazo vingine vinavyokwamisha shughuli zao.
Aidha alitaja baadhi
ya nchi zinazonunua chumvi ya Tanzania kuwa ni pamoja na Jamuhuri ya Watu
Congo, Malawi, Msumbiji,pamoja na Uganda na kusema kuwa lengo ni kufikia nchi
nyingi zaidi duniani.
Aliwaagiza wachimbaji
na wazalishaji wote wa chumvi nchini kulipa mirabaha na tozo mbalimbali na
kushiki katika shughuli za kijamii zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya madini,
kwa lengo la kuongeza pato la taifa kwa manufaa ya watanzania.
Mmoja wa Wakurugenzi
katika Mgodi wa Chumvi wa Kampuni ya Stanley and Sons, Richard Stanley aliiomba
serikali kuboresha miundombinu ya barabara itakayorahisisha usafirishaji ya
chumvi hiyo, kwa kuwa katika kipindi cha wa mvua hakuna vyombo vya usafiri
vinavyoweza kufika katika eneo hilo.
Vilevile, Richard
aliiomba serikali kuwapelekea huduma ya umeme katika kijiji hicho ili kupunguza
gharama za uzalishaji ambapo kwa sasa hutumia mafuta mazito kuendeshea mashine
za uzalishaji.
Hata hivyo, Naibu
Waziri Nyongo aliwahakikisha wawekezaji hao kuwa changamoto zote
zitashughulikiwa katika kipindi kifupi kijacho kwa kuwa nia ya serikali ni
kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje waweze kufanya shughuli zao katika
mazingira mazuri na rafiki ili kuunga mkono azma ya serikali ya kuwa tanzania
ya viwanda kutokana na rasilimali zilizopo nchini.
Naibu Waziri
Stanslaus Nyongo, (katikati) wakijadiliana hatua za uzalishaji chumvi,
katika mgodi wa chumvi wa kampuni ya Stanley and Sons, wa pili kushoro ni mmoja
wa Wakurugenzi wa mgodi huo, Richard Stanley.
Baadhi ya vitalu vya kuzalisha chumvi katika mgodi
wa kampuni ya Stanley and Son, uliopo katika Kijiji cha Kitame wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani.
|
Moja ya mashine za kuvuna chumvi katika mgodi wa
kampuni ya Stanley and Sons.
|
No comments:
Post a Comment