Na Greyson Mwase, Tunduru
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewataka wamiliki wa migodi nchini kuhakikisha
wanaweka mitambo ya kuchenjulia madini ili kuyaongezea thamani kabla ya
kusafirishwa nje ya nchi.
Naibu
Waziri Biteko ametoa wito huo kwenye mkutano wake na wachimbaji wadogo
alioufanya katika kijiji cha Mbesa kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma
mara baada ya kutembelea Mgodi wa Shaba wa Mbesa kama moja ya ziara yake ya
ukaguzi wa shughuli za madini katika mikoa ya Kusini ili kubaini changamoto
pamoja na kuzitatua.
Katika
ziara hiyo Naibu Waziri Biteko aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Madini,
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate
pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Tunduru.
Alisema
kuwa, wamiliki wa migodi wanatakiwa kuhakikisha wanaweka mitambo ya kuchenjulia
madini ili mbali na kuongeza mapato nchini watoe ajira kwa wananchi
wanaozunguka migodi.
Katika
hatua nyingine, Biteko aliwataka wamiliki wa migodi kununua bidhaa za ndani
badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi pamoja na kutoa ajira kwa wazawa ili
wananchi wanufaike na rasilimali za madini hayo.
Pia
aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanasajili mikataba yao kwenye Ofisi
za Wizara ya Madini kama Sheria ya Madini inavyotaka.
Awali
wakiwasilisha changamoto mbalimbali kwa Naibu Waziri Biteko, wachimbaji hao
walitaja kuwa ni pamoja na mitaji midogo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa
madini, vifaa duni vya uchimbaji pamoja na leseni za madini kulipiwa kwa fedha
za kigeni.
Walitaja
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa maabara za kupima madini
migodini na baadhi ya wachimbaji kufutiwa leseni zao.
Wakati
huo huo akielezea shughuli za uchimbaji madini ya shaba katika eneo la Mbesa
lililopo Tunduru mkoani Ruvuma, Afisa Madini wa Tunduru Mjiolojia Abraham
Nkya alisema Serikali ilitenga eneo la
Mbesa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 156.053 ambalo liko umbali wa takribani
kilometa 66 kutoka Tunduru Mjini.
Alisema
leseni nyingi zimekuwa hazifanyiwi kazi hali iliyopelekea leseni zaidi ya 1000
kufutwa.
Aliendelea
kufafanua kuwa kwa sasa Mbesa ina jumla ya leseni 441 za wachimbaji madini
wadogo ambazo kati ya hizo 158 ni hai na 283 zina makosa mbalimbali ikiwemo
kutokulipa ada ya pango, kutowasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa kila robo
mwaka n.k.
Akielezea
faida za uchimbaji madini ya shaba katika kijiji cha Mbesa Mjiolojia Nkya
alieleza kuwa ni pamoja na ulipaji wa kodi mbalimbali ikiwemo mrabaha, ajira
kwa vijana wa kijiji cha Mbesa pamoja na vijiji vya jirani.
Aliendelea
kutaja faida nyingine kuwa ni pamoja na uchangiaji wa shughuli za kijamii ikiwa
ni pamoja na ujenzi wa soko, uchimbaji wa kisima katika shule ya sekondari ya
Mbesa, hospitali na ajira kwa wakinamama wanaohudumia eneo la uchimbaji.
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (wa pili kulia) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara katika
Mgodi wa Shaba wa Mbesa uliopo katika
wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma tarehe 20 Julai, 2918.
|
Mkurugenzi
wa Mgodi wa Shaba wa Mbesa, Ziadi Igangula (kulia) akimwonesha Naibu Waziri wa
Madini, Dotto Biteko (kushoto) jiwe lenye madini ya shaba mara alipofanya ziara
kwenye mgodi huo.
|
Sehemu
ya wananchi wa kijiji cha Mbesa kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa
hadhara.
|
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kulia) pamoja na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma
Homera (kushoto) wakisikiliza kero ,mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na
wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
|
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto)
akiagana na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera (kulia) mara baada ya
kukamilika kwa ziara kwenye wilaya hiyo.
|
No comments:
Post a Comment