Na
Zuena Msuya, Pwani
Serikali imesema itazifutia
leseni za umiliki kampuni zote na wamiliki wa ardhi walioomba leseni za
uchimbaji madini ya ujenzi ikiwemo mchanga, kokoto pamoja na mawe kwa kushindwa
kuendeleza maeneo hayo kwa lengo lililokusudiwa.
Kauli hiyo
ilitolewa na Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya
kukagua migodi ya uchimbaji wa madini ya ujenzi
yaliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani pamoja na kuzungumza na
wakazi wa vijiji hivyo, Julai 24, 2018.
Nyongo alisema, kuna
baadhi ya wamiliki wa ardhi na kampuni mbalimbali zilizoomba leseni za uchimbaji madini ya ujenzi katika
maeneo tofauti nchini,miaka mingi iliyopita pasipo kuyaendeleza na hivyo
kusababisha maeneo hayo kuwa vichaka na kuwazuia wengine kuomba leseni za uchimbaji na kuendeleza maeneo hayo.
Aidha, alitoa onyo na
kuwataka baadhi ya watu wasiowaaminifu
kuacha mara moja tabia ya kuwahadaa wawekezaji wanaotaka kuomba leseni katika
maneo ya uchimbaji kwa kuwaeleza kuwa wanamiliki leseni za maeneo hayo na
kuwataka waingie nao ubia, jambo ambalo si kweli na kwamba tabia hiyo inachafua dhana halisi ya uwekezaji
nchini.
“Kuna mapori na
maeneo mengi nchini yanayofaa katika uchimbaji wa madini ya ujenzi, lakini mtu
akijitokeza kutaka kufanya kazi katika moja ya maeneo hayo anaalezwa kuwa eneo
hilo linamilikiwa na mtu na linaleseni ya uchimbaji, lakini eneo hilo
limeendelea kuwa pori au kichaka kwa miaka mingi, hili haikubaliki. Leseni za
aina hiyo lazima zifutwe na tutazifuta hivi karibuni”, alisema Nyongo.
Sambamba na hilo, aliwaagiza
maafisa madini wote kushirikiana na Serikali za Vijiji husika kukagua maeneo na
leseni zote za uchimbaji madini hayo, kubaini zilizohalali na zisizohalali ili ziweze
kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria ya madini.
Vilevile, aliwata
baadhi ya wamiliki wa migodi ya uchimbaji madini ya mchanga, wenye tabia ya
kutorosha madini hayo na kukwepa kulipa mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa
kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 na kufanyiwa Marekebisho 2017,
kuacha mara moja tabia hiyo na kwamba sheria itachukuwa mkondo wake kwa yeyote
atakayebainika.
"Nawaonya wale
wote wenye tabia ya kuchimba madini ujenzi, kwa maana ya kokoto, mchanga, mawe
kisha kuyatorosha na kukwepa kulipa mrabaha na tozo, pindi utakapokamatwa
serikali haitavumilia uhalifu huo kwani unaipoteza mapato,tutakufutia leseni na
kutaifisha vifaa vyako vyote", alisisitiza Nyongo.
Hata hivyo,
aliwaagiza maafisa madini kuangalia uwezekano wa kubadilisha vocha za ulipaji
mrabaha kuwa wa kieletroniki ili kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa
maduhuli ya serikali.
Akizungumzia suala la
ulipuaji wa miamba, lililolalamikiwa na wananchi, Nyongo aliwashauri wamiliki
wa migodi katika maeneo hayo, kuzungumza na wananchi wa maeneo husika ikiwezekana
kuwalipa fidia ili wananchi hao waweze kuondoka katika maeneo hayo kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Pia aliwashauri
wananchi hao kuwa, endapo watakubalina na wawekezaji hao, kuridhia kile watakachokubaliana
ili kuondoa migogoro na migongano ambayo hutokea mara kwa mara kati ya
muwekezaji na wananchi mara baada ya kulipwa fidia ama vinginenyo.
Mwaka 2017, serikali
kupitia Wizara ya Madini ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 8, ikiwa ni
mrabaha pamoja na tozo mbalimbali zilizotokana na sekta ya madini pekee.
akiwa wilayani
bagamoyo, nyongo alitembelea baadhi ya migodi ya uchimbaji madini ya mchanga
ukiwepo wa Suma JKT uliyoingia ubia na kampuni ya uwekezaji kutoka nchini
Uturuki, mgodi wa kampuni ya Ashraf, Mgodi wa kampuni ya uwekezaji ya Yaate ulioshinda
tenda ya kuzalisha kokoto za aina zote zinazotumika katika ujenzi wa reli ya
kisasa( Standard Gauge)kutoka Dar es salaam hadi Dodoma, mgodi wa kampuni ya
Tan-Turk, mgodi wa kampuni ya uwekezaji Even pamoja na mgodi wa kampuni ya
Kerai.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo,( pili kulia) akiwa katika chumba cha
mizani katika mgodi wa Suma JKT ulioingia ubia na kampuni ya uwekezaji ya
Uturuki,kukagua zoezi la upimaji wa uzito kwa magari yanayobeba madini ujenzi
kabla ya kutoka mgodini.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo( katikati) akitembelea Mgodi wa
SumaJKT ulioingia ubia na kampuni ya uturuki.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto)akipata maelezo juu
ya uchimbaji na uzalishaji wa madini ya ujenzi kutoka kwa Meneja Mtendaji wa
Kampuni ya uwekezaji ya Yaate,Mhandisi Eugen Mikongoti( katikati).
Mmoja wa mtambo wa mgodi wa madini ujenzi wa
kampuni ya ..... aliyoitembelea Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, akizungumza na wanakazi wa kijiji cha
kinzagu kata ya msata wilayani bagamoyo mkoani Pwani alipofanya ziara katika
migodi ya madini ujenzi iliyopo katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment