Na
Zuena Msuya, Pwani
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo,
ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na maafisa madini nchini(
TRA) kuchunguza na fuatilia kiwanda cha Goodwill namna ya ulipaji wake wa
mrabaha na tozo mbalimbali
serikalini kutokana na aina mbalimbali ya madini wanayotumia yakiwemo Kaolin
katika uzalishaji wa bidhaa zake.
Madini ya Kaolin hutumika kwa kiasi kikubwa katika
kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwepo Malumalu( Tiles), rangi za nyumba,
karatasi, n.k.
Nyongo alitoa agizo hilo alipotembelea kiwanda
hicho cha Goodwill wakati akihitimisha ziara
yake ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi katika ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Julai 26,
2018 ambapo katika ziara hiyo alipata fursa ya kutembelea maeneo ya uchimbaji
chumvi na katika kiwanda cha kutengeneza chimvi aina ya NEEL.
Nyongo alieleza
kuwa , mara baada ya kutembelea kiwanda hicho, hakuridhishwa na majawabu
aliyokuwa akipewa na uongozi wa kiwanda hicho juu ya mahesabu ya manunuzi ya
madini kaolin, matumizi ya madini hayo katika uzalishaji wa bidhaa zake, pamoja
na uwazi wa ulipaji wa mrabaha na tozo mbalimbali zilizowekwa kwa mujibu wa
sheria ya madini, tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho mwezi April mwaka jana.
Hata hivyo aliweka wazi kuwa bei elekezi ya
serikali katika uuzaji wa madini ya ujenzi,hasa mchanga ni shilingi elfu kumi(
10,000) kwa tani.
Aidha, Nyongo alishangazwa na bei ya madini ya
Kaolin yanayotengeneza malumalu( tiles) kuwa ni shilingi elfu tatu (3,000) kwa tani na mrabaha unaolipwa
ni 3% ya bei kitu ambacho si sahihi, na
baada ya kupiga hesabu za haraka waligundua kuwa, tani moja ya Kaolin ilipaswa
kuuzwa shilingi 35,000, hivyo serikali
ingepata mrabaha wa shilingi 1,500 kutokana na ile 3% , tofauti na ilivyo sasa
serikali inapata mrabaha wa shilingi Tisini (90) katika kila tani ya kaolin
inayouzwa, kitu alichosema kuwa ni wizi.
Kutokana mkanganyiko huo aliwaagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwenda
kufanya mahesabu katika kiwanda cha Goodwill ili kufahamu wanunua au
waandika shilingi ngapi kwa tani ikiwa
ni gharama za uzalishaji wa malumalu ( tiles),ili ikifahamika bei halisi ya
tani moja, Wizara ya Madini itaanza kutoza mrabaha wa 3% katika kila mahesabu
waliokuwa wakiyapeleka TRA.
" unaweza kukuta wamepeleka mahesabu makubwa
TRA, lakini katika uchimbaji waandika wamenunua shilingi elfu 3 (3000) hii
haiingii akilini kabisa, kila mtanzania anajua Malumalu( tiles) zinauzwa kwa
bei juu sana na wakati mwingine watu wanaagiza kutoka nje kupunguza gharama,
halafu madini ya kaolin ambayo ni malighafi muhimu katika kuzitengeza malumalu
hizo yanauzwa shilingi elfu tatu kwa tani , huo ni wizi mkubwa na haiwezekani",
alisisitiza Nyongo.
Alisisitiza kuwa endapo kiwanda hicho
kitagundulika kukwepa kodi, kitalazimika kulipa fedha zote ambazo zimepotea
katika kipindi chote cha uzalishaji na endapo watashindwa kufanya hivyo,sheria
itachukuwa mkondo wake.
Tangu kiwanda hicho kianzishwe mwezi April mwaka
jana hadi sasa, kumbukumbu zinaonyesha kuwa wametumia tani elfu sabini( 70,000)
za madini ya Kaolin, kwa gharama ya shilingi milioni 6 na laki tatu, (6,300,000) tu, ila kwa bei haraka iliyopigwa pale na wataalam inaonyesha kuwa zaidi
ya shilingi milioni sabini ( 70,000,000,) zimepotea , hivyo wataalamu wa Wizara
ya Madini kwa kushirikiana na TRA wameagizwa
kufuatilia jambo hilo kwa haraka na umakini mkubwa ili kuipatia serikali mapato
stahiki.
Katika hatua nyingine, Nyongo alipiga marufuku
uchimbaji wa mchanga na vifusi katika jiji la Dar es salaam, na kuwaagiza
wachimbaji kwenda katika maeneo yalioanishwa katika Mkoa wa Pwani.
Alisisitiza kuwa Mkoa wa Pwani unamaeneo mengi
yenye madini ya ujenzi ambayo yakichimbwa yanatosheleza majitaji ya mchanga na
kokoto katika jiji la dar es salaam na mikoa mingine, hivyo wachimbaji
wazingatie sheria za uchimbaji madini hayo.
Sambamba na hilo aliwaagiza Wakuu wa Wilaya zote wenye
maeneo ya uchimbaji wa madini ujenzi pamoja na chumvi, kukamata wafanyabiashara
na wachimbaji wa madini hayo wnaofanya kazi hiyo bila kufuata sheria ya madini
ikiwemo kutosha madini hayo na kukwepa kulipa mrabaha na tozo mbalimbali
serikalini na katika halmashauri.
Vilevile, alisema kuwa kila lori litakalokuwa
limepakia madini mchanga lazima liwe na stakabadhi ya vocha inayoonyesha kuwa
madini hayo yamelipiwa stahili zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria ya
madini.
Pia aliwaagiza maafisa madini kuangalia utaratibu
bora utakaofaa kutumika katika kulipa tozo mbalimbali pamoja na mrabaha
ikiwezekana zilipwe kwa mfumo wa kieletroniki ili kukwepa wafanyabiashara wasio
waaminifu.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, akiwa
katika kiwanda cha goodwill.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akikagua chumvi iliyovunwa tayari kupelekwa kiwandani.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo,(katikati) akipata maelezo alipotembelea kiwanda cha
kuzalisha chumvi katika wilaya ya Mkuranga.
No comments:
Post a Comment