Thursday, May 24, 2018

Biteko aagiza Afisa Madini Mkazi Mererani aondolewe


Ø Ni kwa usimamizi dhaifu wa UKUTA

Na Veronica Simba, Manyara

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amemwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma kumwondoa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mererani, Fredrick Girenga kwenye wadhifa huo na kumweka Afisa mwingine atakayemudu vema usimamizi wa Ukuta wa Mererani unaozunguka machimbo ya Tanzanite.

Biteko alitoa agizo hilo jana, Mei 23, baada ya kufanya ziara kukagua shughuli zinazoendelea Mererani, hususan kwenye Ukuta na kubaini udhaifu katika uchukuaji  na utunzaji wa kumbukumbu za wahusika wanaoingia ndani ya eneo hilo na kutoka, pamoja na mali (madini) yanayotolewa kupitia getini.

“Mheshimiwa Rais amewekeza pesa nyingi sana hapa. Haiwezekani sisi watendaji tushindwe kujituma hata kwa mambo madogo kama haya ya kusimamia vema utekelezaji wa ulinzi wa rasilimali hizi; yaani tusubiri yeye aje tena mwenyewe kutuelekeza hata mbinu ndogo za udhibiti. Lazima tuwe wabunifu na wenye kujituma,” alisisitiza.

Alisema kwamba, yeyote atakayepangwa kufanya kazi ya usimamizi wa Ukuta huo ajue kwamba macho la Serikali yameelekezwa mahali hapo. “Hata usipomwona Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Kamishna wa Madini, ujue macho yetu yapo huku na usipotimiza wajibu wako kwa kiwango kinachoridhisha tutakuwajibisha mara moja.”

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuhitimisha ziara yake, Naibu Waziri alifafanua kuwa, udhaifu ulioonekana ni kwa upande wa Wizara ambapo alitoa mfano kuwa; hakuna rekodi yoyote inayoonesha nani anaingia, kwa muda gani, na nani amepangwa kufanya kazi ipi. Aliongeza kuwa, hata rekodi ya namna mzigo unavyotoka ndani kwenda nje ya migodi kupitia getini, haipo.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa ya kubadilishwa kwa Afisa Madini Mkazi anayesimamia eneo hilo; Biteko alifafanua kuwa, Wizara haiwezi kuruhusu mtu yeyote kuirudisha kwenye udhaifu wa usimamizi thabiti wa rasilimali za madini, hususan baada ya jitihada kubwa zilizofanywa kuisaidia sekta ya madini iweze kukua.

“Kusema kweli, hilo hatuwezi kukubaliana nalo. Ndiyo maana nimemwelekeza Kamishna wa Madini wa Kanda, tuangalie namna ya kubadilisha uongozi hapa Mererani ili tuweze kupata mtu ambaye anaweza kusimamia vizuri.”

Aidha, Naibu Waziri aliongeza kuwa, zipo taarifa kuhusu baadhi ya Maafisa wa Wizara waliopangwa kufanya kazi Mererani kutokutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kutokuwepo mahali pa kazi kwa muda wote wa kazi kama wanavyopaswa, badala yake wanakuwepo kwa muda mfupi na kuondoka.

“Hili jambo haliwezi kuvumiliwa kwenye Wizara yetu. Kwahiyo, tunataka tudhibitiane na tusimamiane vizuri ili maana halisi ya ndoto ya Rais wetu aliyokuwa nayo katika kudhibiti madini haya iweze kutimia.”

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambaye pia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya, akisisitiza kuhusu umuhimu wa udhibiti wa utoroshwaji madini, alisema kuwa, dhamira ya Serikali kujenga Ukuta husika ni kuhakikisha changamoto ya kutorosha madini inafika mwisho ili rasilimali hizo zinufaishe Taifa ipasavyo.

“Ziara hii imetufanya tubaini kuwa udhibiti wa utoroshaji madini uliopo unapaswa kuwekewa mkazo kwa kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanayotaka kila Idara husika kuweka mbinu zaidi za udhibiti, yanatekelezwa ipasavyo.”

Ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mererani, ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Aprili 6 mwaka huu; kufuatia agizo alilolitoa yeye mwenyewe kama njia ya kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo adhimu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kulia), akimsikiliza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mererani, Fredrick Girenga (katikati) kuhusu utaratibu unaotumika kuweka kumbukumbu za watu na mali/madini wanaoingia na kutoka katika migodi ya tanzanite. Hapo ni katika Lango/Geti la kuingilia na kutokea kwenye eneo la migodi hiyo lililozungushiwa Ukuta hivi karibuni kwa amri ya Rais John Magufuli. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi Mererani, Mei 23 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia), akizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa Madini ya Tanzanite wa Edward Zakayo, uliopo Kitalu D, Mererani, wakati wa ziara yake Mei 23 mwaka huu.


Matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, kwenye machimbo ya tanzanite, Mererani, Mei 23 mwaka huu.


Kiberenge maalum kinachobeba watu na malighafi yenye madini ya tanzanite, kikipita katika njia yake kushuka chini shimoni kunakochimbwa madini hayo, kama kilivyokutwa katika Mgodi wa Franone uliopo Kitalu D Mererani, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, Mei 23 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), akizungumza na maafisa mbalimbali wa Serikali waliopo Mererani (hawapo pichani), baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye machimbo ya tanzanite kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea, Mei 23 mwaka huu. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambaye pia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (katikati), akizungumza na maafisa mbalimbali wa Serikali waliopo Mererani (hawapo pichani), baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye machimbo ya tanzanite kukagua shughuli mbalimbali zinazoendelea, Mei 23 mwaka huu. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ambaye pia ni Kamishna wa Madini Tanzania, Profesa Shukrani Manya na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma.

No comments:

Post a Comment