Thursday, May 17, 2018

Waziri Kairuki asifu utendaji kazi wa GST


Veronica Simba na Samwel Mtuwa, Dodoma

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amefanya ziara katika Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) na kupongeza utendaji kazi wake.

Alifanya ziara hiyo Jumatano, Mei 16 mwaka huu katika Ofisi za Taasisi hiyo zilizopo Dodoma, akiwa amefuatana na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto Biteko.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, baada ya kukutana na Menejimenti ya GST na kutembelea sehemu mbalimbali kujionea shughuli zinazofanywa; Waziri Kairuki alisema kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake wa Wizara, wanafurahishwa na utendaji kazi wa Taasisi hiyo.

“GST wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya kuriarifu Taifa kuhusu uwepo wa aina mbalimbali za madini nchini; lakini pia katika upimaji wa matetemeko ya ardhi na shughuli nyingine za aina hiyo.”

Kuhusu upimaji wa matetemeko unaofanywa na GST, Waziri Kairuki alifafanua kuwa, Wizara imeielekeza Taasisi hiyo iendelee kutoa elimu zaidi kwa wananchi, hususan wanaojenga katika maeneo kunapotokea matetemeko ili wajue tahadhari za kiujenzi wanazopaswa kuchukua kuepukana na athari za majanga hayo.

Aidha, alisema kuwa Wizara yake itakutana na Wizara ya Ujenzi kujadiliana namna ambavyo wataalam wa pande hizo mbili wanavyoweza kushirikiana ili kuhakikisha majengo yote ya makazi na hata Taasisi mbalimbali, hususan yaliyopo katika maeneo yenye matetemeko ya ardhi, yanajengwa kwa kufuata ushauri wa kitaalam.

Kwa upande wa tafiti za kijiolojia zinazofanywa na GST, Waziri Kairuki alisema kuwa, baada ya ziara hiyo na kuzungumza na Menejimenti ya GST, yeye na viongozi wenzake wameona kuwa ipo haja ya kuipitia upya Sera ya Madini na kuiboresha zaidi, ili isaidie Taifa kupata mapato stahiki yatokanayo na rasilimali madini.

Akifafanua, alisema kuwa  kwa sasa, Sera ya Madini inaelekeza makadirio ya rasilimali-madini katika ardhi yetu yafanywe na sekta binafsi.

“Kuwaachia sekta binafsi kufanya makadirio kunampa mwekezaji nafasi nzuri zaidi ya Serikali wakati wa majadiliano ya uwekezaji, maana anakuwa na ufahamu zaidi wa rasilimali husika kuliko Serikali. Hivyo tumeona ni vema tuwe na ufahamu huo ili itusaidie kupata mapato zaidi.”

Waziri alitoa rai kwa wachimbaji wadogo wa madini kuwasilisha GST sampuli za madini wanazozipata katika maeneo yao, ili wapatiwe ushauri wa kitaalam zaidi kuhusu nini wanachotakiwa kufanya pindi wakianza shughuli za uchimbaji.

Aliwataka kutokuwa na wasiwasi, kwani Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele na mkazo kwa wachimbaji wadogo, kwa lengo la kuwawezesha kufikia hatua ya uchimbaji wa kati na hata uchimbaji mkubwa ili waweze kunufaika zaidi na kulinufaisha Taifa kwa ujumla.

Alisema, Serikali imetenga maeneo takribani 44 kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini na itaendelea kutenga maeneo zaidi. “Niendelee kuwasihi wachimbaji wetu wadogo wafuate kanuni na taratibu, nasi tunaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano na kipaumbele zaidi.”

Awali, wakizungumza wakati wa kikao na Menejimenti ya GST wakati wa ziara hiyo, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko pamoja na kupongeza utendaji kazi mzuri wa Taasisi hiyo, waliwataka watendaji wake kuendelea kumpa ushirikiano Waziri na Viongozi wengine ili kwa pamoja watimize majukumu yao ya kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha watanzania kwa kiwango stahiki.

Naye, Mtendaji Mkuu wa GST, Prof. Abdulkarim Mruma, alimshukuru Waziri na Naibu Mawaziri kwa kufanya ziara hiyo kwani imewawezesha kupata ufahamu zaidi kuhusu Taasisi husika.

Wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa GST kwa Waziri, pamoja na mambo mengine, Prof Mruma aliahidi kuwa yeye na watendaji wenzake wa Taasisi hiyo, wataendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha Taifa linanufaika ipasavyo kupitia rasilimali za madini.

GST ilipandishwa hadhi Julai 2017, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kuitwa Taasisi ya Jiolojia Tanzania. Awali, ilikuwa ikiitwa Wakala wa Jiolojia Tanzania.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) na Ujumbe wake, wakiangalia sampuli za miamba na madini mbalimbali yanayopatikana nchini, wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Jilojia Tanzania (GST) iliyopo Dodoma, Mei 16, 2018. Pamoja naye pichani ni Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto Biteko, Mtendaji Mkuu wa GST, Prof Abdulkarim Mruma, Mkurugenzi wa Kanzidata, Yokbeth Myumbilwa na Kaimu Meneja Uchoraji Ramani, Alphonce Bushi.


Mtendaji Mkuu wa GST, Prof Abdulkarim Mruma (katikati), akimwonesha Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (wa tatu kutoka kushoto) na Ujumbe wake, moja ya ramani ya kijiolojia iliyoandaliwa na Taasisi hiyo. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kwenye Taasisi hiyo, Mei 16 mwaka huu, pamoja na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo (kushoto kwa Waziri) na Doto Biteko (wa kwanza kushoto).


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (wa pili kushoto-mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST), baada ya ziara yake kwenye Taasisi hiyo Mei 16 mwaka huu. Pamoja naye (mstari wa mbele) kutoka kushoto ni Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, Mtendaji Mkuu wa GST Prof Abdulkarim Mruma na Naibu Waziri Doto Biteko.

No comments:

Post a Comment