Friday, May 18, 2018

GST, PanAfGeo, Umoja wa Ulaya watoa mafunzo ya urithi wa vivutio vya kijiolojia


Na Samwel Mtuwa, GST

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia ya Afrika, Taasisi ya Kijiolojia ya Ulaya, Umoja wa Ulaya pamoja na Muungano wa Afrika na Ulaya katika tasnia ya Jiosayansi wametoa mafunzo juu ya Urithi wa Kijiolojia (Geoheritage) kwa Mwaka 2018.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Jiolojia kutoka GST Maruvuko Msechu alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha na kuongeza ufahamu pamoja na ujuzi juu ya sekta ya madini barani Afrika hususani katika taasisi za jiolojia Afrika pamoja na kuvumbua vivutio vingi vya utalii wa kijiolojia kupitia urithi wa kijiolojia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Jiolojia kutoka GTS John Kalimenze, alisema lengo kuu la mafunzo hayo ilikuwa ni kupeana ujuzi na kuongeza uelewa kupitia uwasilishaji wa mada mbalimbali kama vile mafunzo juu ya upimaji wa ramani za jiosayansi, uchunguzi juu ya rasilimali madini, uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo na usimamizi wa mazingira katika uchimbaji madini.

Mmoja wa Waratibu na Msimamizi wa mafunzo hayo kutoka nchini Hispania Enriq Diaz alitoa mada juu ya utunzaji wa uzuiaji wa uchimbaji holela wa madini kwa lengo la kuonyesha njia bora za kutunza urithi wa vivutio vya kijiolojia duniani.

Mafunzo hayo yanayofanyika kila mwaka yalianza tarehe 14- 19 Mei, 2018 na kushirikisha washiriki kutoka nchi mbalimbali kutoka barani Afrika zikiwemo Liberia, Botswan, Sudani ya kaskazini, Nigeria, Commoro, Moroco, Zimbambwe, Namibia.


Washiriki wa mafunzo ya kuongeza uelewa na ujuzi juu ya kuongeza na kufumbua vivutio vya urithi wa kijiolojia (Geoheritage), wakiwa katika picha ya baada ya kufunguliwa mafunzo hayo. Watano kutoka kulia  ni  Mkurugenzi wa Idara ya Jiolojia kutoka GST Maruvuko Msechu ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa  GST  Prof. Abdukarim Mruma.

Waratibu na Wasimamizi wa Mafunzo yenye lengo la kuongeza uelewa na ujuzi katika Sekta ya jiosayans na vivutio vya kijiolojia iliyoendeshwa na GST kwa ushirikiano wa PanAfGeo na Umoja wa Ulaya. Wa kwanza kutoka kushoto ni Joshua Mwankunda kutoka NCAA, anayefuata ni John Kalimenze kutoka GST, Enriqu Diaz kutoka IGME.

Mratibu na Msimamizi wa mafunzo juu ya urithi wa kijiolojia kutoka Hispania Enriq Diaz aliyesimama upande wa kulia akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

No comments:

Post a Comment