Na Veronica Simba, Dodoma
Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, leo Mei 30, amefungua rasmi
maonesho ya madini katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma na kuipongeza Wizara
ya Madini kwa kuyaandaa.
Akitoa hotuba ya
ufunguzi, Ndugai alimpongeza Waziri mwenye dhamana, Angellah Kairuki pamoja na
watendaji wa Wizara, kwa juhudi kubwa za kutangaza na kulinda rasilimali ya
madini hapa nchini. Alisisitiza kuwa, anatumaini juhudi hizo zitaendelezwa ili
kuiwezesha sekta husika kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu.
Alisema kwamba Wizara
ya Madini inalo jukumu kubwa la kuufahamisha umma kuhusu sekta husika kupitia
njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari na maonesho mbalimbali.
“Maonesho haya
yamekuja wakati muafaka kwa sababu kipindi hiki nchi yetu iko katika mageuzi
makubwa katika sekta ya madini; na ninyi wizara mnawajibika kuifanikisha azma hii
kwa njia mbalimbali, hususan vyombo vya habari na maonesho kama haya.”
Aidha, Spika
aliwataka wadau mbalimbali wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na
taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na usalama wa wafanyakazi wao na kulipa kodi
za Serikali.
Kuhusu suala la
uongezaji thamani madini kabla ya kuyauza, Ndugai alisema kwamba hilo ni suala
muhimu sana kwa kuzingatia sera ya nchi ya kuwezesha uchumi wa viwanda. “Ni kwa
kufanya hivyo tu ndipo tutajenga viwanda ambavyo vitatoa fursa ya ajira kwa
watanzania na kuinua uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza.
Akizungumzia mchango
wa Bunge katika kukuza sekta ya madini, alisema Bunge limekuwa makini katika
kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta husika unakuwa wenye tija na manufaa kwa
pande zote; yaani Serikali, Taifa na wawekezaji.
“Tuliunda Kamati
mbalimbali za ufuatiliaji wa sekta ya madini. Nafurahi kuwaambia kwamba mambo
yamekuwa yakiboreka siku hadi siku. Nawasihi tuendelee hivyohivyo kwa manufaa
ya pande zote.”
Awali, akimkaribisha
Spika kufungua maonesho husika; Waziri Kairuki alisema kuwa, Wizara imeandaa
maonesho hayo kwa kuzingatia kuwa ni Wizara mpya hivyo inahitaji kutoa elimu
kwa umma kuhusu majukumu yake; yakijumuisha dhima na dira.
“Baada ya Bunge lako
tukufu kuifanyia marekebisho Sheria ya Madini Namba 14 ya Mwaka 2010, kupitia
marekebisho ya Sheria Namba 7 ya Mwaka 2017, Wizara yangu imekuwa na jukumu
kubwa la kutekeleza maelekezo ya Sheria hiyo.”
Maonesho hayo ya siku
tatu, yaliyoanza Mei 30 na kutarajiwa kuhitimishwa Juni Mosi; yameshirikisha
Taasisi mbalimbali za Serikali, Shirikisho la Wachimbaji Wakubwa (TCME) na
Kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji na uongezaji thamani madini.
No comments:
Post a Comment