Tuesday, May 8, 2018

Waziri Kairuki afungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini


Na Greyson Mwase,

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.

Katika mkutano huo Waziri Kairuki amewataka watumishi kuelekeza nguvu kwenye kutoa kipaumbele kwenye masuala muhimu kama vile kuendelea kutengeneza sera bora zinazosimamia rasilimali za madini na kuweka mfumo mzuri na ulio bora wa ukusanyaji wa mapato ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

Pia, amewapongeza watumishi kwa ukusanyaji wa maduhuli  hadi kuvuka lengo kwa asilimia 130 ya makusanyo ya lengo  lililokuwa limewekwa kwenye Sekta ya Madini.

Aidha, amewataka watumishi kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2017/2018 ili kufanya vizuri kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019.

Aidha amewaasa watumishi wote kuwa waadilifu katika utendaji kazi wa kila siku na kuagiza watumishi wote waelimishwe kuhusu maadili katika utumishi wa umma na wale ambao hawajajaza fomu za maadili kujaza mara moja.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Wizara imebeba matarajio makubwa ya wananchi na kuwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya.

Aidha,  amesema Wizara ya Madini ni miongoni mwa Wizara zinazowajibika kuchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa.

Waziri Biteko amesisitiza mahusiano mazuri baina ya vyama vya wafanyakazi na waajiri  ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na  umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa umma. Masuala mengine  yaliyojadiliwa ni pamoja na  mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017.

Mkutano huo umefanyika leo tarehe 07 Mei, 2018 katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki  (kushoto) akipokelewa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa RasilimaliWatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi (kulia) mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA)mjini Morogoro, kwa ajili ya kuzindua mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini tarehe 07 Mei, 2018.


Kutoka kushoto Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William (hayupo pichani) katika mkutano huo.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William akielezea majukumu ya chama hicho kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini (hawapo pichani) katika mkutano huo.


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko katika mkutano huo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko  akifafanua jambo katika mkutano huo.


Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini wakiimba wimbo maarufu wa mshikamano (solidarity forever) kwenye mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo.


Sekretarieti ya maandalizi katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akimkabidhi Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila nakala ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William nakala ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa nne kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la  Wizara ya Madini mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.

No comments:

Post a Comment