Thursday, April 25, 2019

Agizo la Waziri halijadiliwi, ni kutekeleza–Prof. Kikula


Na Issa Mtuwa, Ulanga Morogoro

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amewataka  Watumishi wa tume hiyo ofisi ya Morogoro na Ulanga kutambua kwamba agizo la Waziri linalowataka kufuta leseni zisizofuata utaratibu wa kisheria sio la kujadili bali ni kutekeleza.

Prof. Kikula ameyasema hayo Aprili 10, 2019 wilayani Ulanga wakati akizungumza na watumishi wa tume hiyo wakati wa ziara yake.

Taarifa iliyosomwa kwake na Afisa Migodi Mkazi ofisi ya Mahenge Ulanga, Tandu Jilabi inaonyesha kuwa wilaya ya Ulanga ina leseni za wachimbaji wadogo 221 kati ya hizo ni leseni 9 tu ndio zinazofanya kazi huku leseni za uchimbaji wa kati zikiwa 5 na leseni za utafiti wa madini 13.

Kufuatia hali hiyo, Afisa Migodi Mkazi ofisi ya Mahenge ameiomba tume ya madini kufuta leseni zisizofanya kazi ili wapewe wenye uhitaji ili waweze kuziendeleza. Kufuatia ombi hilo, Mwenyekiti wa tume amesema jukumu la kuzifuta leseni hizo ni la kwake pamoja na Afisa Madini Mkazi Morogoro na halina mjadala kwakuwa muongozo wa utekeleza wa suala hilo ulishatolewa na waziri wa Madini.

“Suala la leseni zisizofanya kazi sio la kujadili, hili ni agizo la Waziri na kazi yetu ni kutekeleza na wenye kuzifuta ni ninyi, fuateni taratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria katika kuzifuta na sio kuzifuta lazima wote waliozishikilia leseni hizo kwa muda wote walipe fidia na wasipo fanya hivyo taratibu za kisheria zifuatwe kwani katika kipindi hicho chote serikali imekosa mapato yake. Kuanzia leo pitieni leseni zote na ifikapo Juni 30 mwaka huu leseni zote zisizo hai ziwe zimefutwa”, amesema Prof. Kikula.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa tume amekutana na kuzungumza mwakilishi wa mwekezaji wa kampuni ya TanzGraphite (T) Ltd ambae ni Meneja Uhusiano wa Jamii na kuzungumzia kuhusu mgogoro uliopo baina ya mwekezaji huyo na baadhi ya wananchi wanaotakiwa kufanyiwa tathimini ili kupisha shuguli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo.

Prof. Kikula ameonyesha kusikitishwa na mgogoro huo ambao amesema ni wa muda mrefu sasa na unachelewesha maendeleo ya watu na kuikosesha serikali mapato.

Ameongeza kimsingi wananchi wanapaswa kuelewa kuwa “right surface” (haki ya kumiliki vitu vilivyo juu ya ardhi) inampa mwananchi haki  ya kulipwa fidia ya mali zilizo juu ya ardhi anayo miliki lakini watambue kuwa kuna “resource right” (haki ya kumiliki raslimali zilizo chini ya ardhi) ikiwemo madini ambayo mmiliki wake ni serikali, ndio maana inapohitaji raslimali hizo humuondoa na kumfidia mliliki wa mali za juu ya ardhi, hivyo wananchi wanapo ng’ang’ania wanatakiwa walitambue hilo.

Pia, amesema kuwa, kwa mpango ulioanishwa na mwekezaji huyo unaonyesha manufaa kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo (CSR) ambapo amebainisha kuwa mwekezaji ameahidi kuwalipa fidia, kuwajengea nyumba za kisasa wale wote walio ndani ya eneo.

Mambo mengine ni pamoja na kuwapatia chakula kwa muda wa miaka miwili wakiwa kwenye makazi mapya watakayo jengewa na kila kaya kusomesha mtoto mmoja kwenye vyuo vya veta na wakihitimu wataajiriwa na mgodi ili waweze kupata kipato cha kusaidia na kuendeleza kaya zao.

Pamoja na hayo, mwekezaji huyo amemweleza mwenyekiti wa tume kuwa tayari wameshakubaliana kujengaa kituo cha afya, matundu ya vyoo kwa baadhi ya shule, kujenga shule na ukarabati wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali. Hata hivyo hakusita kuonyesha kusikitishwa kwake na watu wachache wanaogoma kuondoka kupisha shuguli za uchimbaji huku kila kitu ikiwemo mtaji wa shuguli hizo ukiwa tayari.

Katika mgogoro huo, kaya 347 zinatakiwa kuondoka kupisha mwekezaji huyo na kati ya hizo kaya 62 ndio zinazo goma kuondoka ili mwekezaji aanze kazi ya uchimbaji. Mwenyekiti amesikitishwa na hali hiyo na na kuuomba uongozi wa mkoa na wilaya kuzungumza na kaya hizo sambamba na Baba Askofu aliyeko ndani ya eneo hilo ili mradi huo uanze kwani ni wa muda mrefu na serikali inakosa mapato.

Amesema kwa sasa anaziachia juhudi za serikali ya mkoa na wilaya katika kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Mapema mwenyekiti alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya ambapo amemshukuru kwa ushirikiano anao utoa kwa viongozi na wafanyakazi wa tume ya madini wilaya ya Ulanga.

Amesisitiza suala la uadilifu kwa wafanyakazi wa tume na amesema hilo litakuwa jambo la kwanza kulisema kila aendapo sambamba na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.  Aidha, amesema kipimo kikubwa cha kila mkuu wa kituo cha tume ya madini kitakuwa ni ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 tume ilipangiwa kukusanya Bilioni 310 na mwaka wa fedha ujao tume imepangiwa kukusanya Bilioni 467.

Upande wake, Kamishna wa tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki amewakumbusha na kuwasisitiza watumishi wa tume na wachimbaji wa madini kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji na ulipaji wa tozo na stahiki zote za serikali kwa wakati.

Amesema kwa kufanya hivyo raslimali za madini zitakuwa na tija kwa taifa kama anavyo sisitiza Rais John Pombe Magufuli kuwa anataka raslimali za madini ziwanufaishe watanzania wote na namna za kuwanufaisha ni kulipa stahiki za serikali zinazo tokana na madini ili zikatumike kujenga uchumi wa taifa.

Prof. Kikula na Dkt. Macheyeki wanaendelea na ziara yao mkoani Morogoro kukagua shuguli za Tume katika Wilaya mbalimbali ambapo leo walitembelea eneo la wachimbaaji wadogo ipanko wilayani ulanga.

Kamishna wa Tume ya Madini  Dkt. Athanas Macheyeki kushoto akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula mara baada ya kuzunguka na kukagua eneo la wachimbaji lililopo Iponka eneo ambalo awali lilifungiwa kufanya shuguli za uchimbaji. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akionyesha jambo kwenye ramani ya mwekezaji wa Madini ya Graphite; TanzGraphite (T) Ltd. Wa tatu kushoto ni Meneja Uhusiano wa Jamii Bernad Mihayo, wa pili kushoto ni Kamishna wa Tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa pili kushoto akiwa katika eneo la wachimbaji wadogo Ipanko wilayani Ulanga akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Afisa Madini Mkazi Morogoro Mhandisi Emmanuel Shija alipotembelea kujionea namna shuguli za uchimbaji zinavyofanyika. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki.

Wednesday, April 10, 2019

Kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Mwakitolyo Wananchi watakiwa kumpisha mwekezaji kuchimba dhahabu


Na Greyson Mwase, Shinyanga

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga kumpisha mwekezaji  ambaye ni  mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu wa kampuni ya  Hanan Afro Asia Geo Engineering (T) Limited kutoka China  kuendelea na maandalizi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu, kwa kuwa ndiye aliyewekeza katika kijiji husika kwa kufuata sheria na kanuni zake.

Naibu Waziri Nyongo ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 03 Aprili, 2019 katika mkutano wake wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa wa Shinyanga yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Kamando, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba, Mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa, wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi wa habari.

Alisema kuwa, kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo na mwekezaji kutoka nchini China ambaye ni  kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited ambapo malalamiko yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Kahama Machi 10, 2018 ambapo alielezwa kuhusu unyanyasaji  uliofanywa wakati wa zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupisha uanzishwaji wa mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu.

Aliendelea kusema kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli Machi 11, 2018 aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitembelea eneo la Mwakitolyo linalolalamikiwa kwa lengo la kufanya mkutano na kusikiliza malalamiko ya wananchi ambapo baada ya kusikiliza malalamiko hayo aliahidi kwenda kufanyia kazi malalamiko yao na kuwapa mrejesho.

Aliendelea kueleza kuwa, iliundwa timu maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kulingana na hadidu rejea iliyokuwa imepewa ambayo iliitaka timu kukutana na viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya, kuainisha majina ya wananchi waliolipwa na ambao hawajalipwa fidia, vigezo vilivyotumika wakati wa uthaminishaji na ulipaji wa fidia pamoja na mapendekezo mbalimbali.

Nyongo aliendelea kufafanua kuwa, mara baada ya timu kumaliza kazi yake, ilibainika kuwa mwekezaji alilipa kiasi cha shilingi bilioni 1.63  kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo husika hivyo zoezi kukamilika kwa asilimia 99.6.

Alisisitiza kuwa pamoja na wananchi takribani 375 kulipwa fidia bado ilionekana kuwa wananchi wengi waliolipwa fidia sio wanakijiji wa Mwakitolyo na kuongeza kuwa wananchi 40 tu ndio walioonekana wamiliki halali wa mashamba pamoja na makazi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuharakisha upatikanaji wa maeneo mapya kwa ajili ya wanananchi 40 ambao ni wamiliki halali wa makazi na mashamba katika kijiji cha Mwakitolyo ili mwekezaji aweze kuanza shughuli za uchimbaji mara moja.
Aidha, Naibu Waziri Nyongo alimtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited kuhakikisha anadumisha mahusiano na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo na kumtaka kuhakikisha anashiriki katika uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, barabara kama Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake inavyofafanua.

Wakati huo huo Nyongo aliwataka wananchi kumpa ushirikiano mwekezaji ili kufaidi matunda ya uwekezaji  kwenye kijiji chao ikiwa ni pamoja na ajira kwa wazawa, utoaji wa huduma za vyakula, biashara, huduma za jamii hivyo kupaisha uchumi wa kijiji hicho.

Aliendelea kusema kuwa, madini ni mali ya watanzania wote, hivyo baada ya uwekezaji kuanza kampuni hiyo italipa kodi mbalimbali kwenye halmashauri na Serikali kuu hivyo kuboresha sekta nyingine kama vile miundombinu, afya, elimu n.k.

Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum akizungumza katika mkutano huo mbali na kumpongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutatua mgogoro huo, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii huku wakilinda amani ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited, Zhang Jiangho mbali na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kutatua mgogoro huo  uliodumu kwa muda mrefu, aliahidi kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kwa kuboresha  huduma za jamii na kulipa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara uliolenga kutatua mgogoro kati yao na mwekezaji ambaye ni kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited tarehe 03 Aprili, 2019. 

Kutoka kushoto mbele, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakinukuu kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara. 

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga  akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara. 

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga wakifuatilia ufafanuzi  uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara. 

Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo (hawapo pichani)

Thursday, April 4, 2019

Waziri Biteko akutana na kufanya mazungumzo na Wadau mbalimbali



Na Issa Mtuwa, Dodoma

Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na makundi mbalimbali ya wadau wa madini Aprili 3, 2019, Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Miongoni mwa aliokutana nao ni pamoja na Kampuni ya MAGAL Security System inayojihusisha na ufungaji wa mitambo ya usalama (security system) katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya migodini.

Mkurugenzi wa Biashara na Uendelezaji wa Masoko wa kampuni hiyo, Michael Gur Arie, amemweleza Waziri kuwa, kampuni yake inataka kufanya kazi na Wizara ya madini katika masuala ya ufungaji wa mitambo ya usalama kwenye migodi hususani Mirerani.

Amesema kuwa, kampuni hiyo ina uwezo wa kufunga mitambo Mirerani na wizara ikawa na uwezo wa kufuatilia kinacho fanyika kwenye eneo lote la mgodi huku shughuli nyingine za ofisi zikiendelea.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko ameishukuru kampuni ya MAGAL kwa kumtembelea na kuzungumza nae kuhusu suala la usalama hususani Mirerani. Amesema suala la usalama mirerani linapewa kipaumbele na uzito mkubwa katika kulinda raslimali hiyo ili iwanufaishe Watanzania wote.

Ameongeza kuwa, serikali imelipa kipaumbele suala la usalama katika eneo la Mirerani na Wizara imekuwa na mpango wa awamu mbili katika kutekeleza suala hilo. Amesema, Awamu ya kwanza ilikuwa ni kujenga ukuta kuzunguka eneo lote la migodi ya Mirerani na kufunga kamera na awamu ya pili inasubiri ushauri wa namna ya kutekeleza huku utekelezaaji wake ukitarajiwa kutafanyika baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, waziri Biteko amekutana na Viongozi wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Nchini (FEMATA) wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo, John Bina.

Bina na ujumbe wake wamemtembelea Waziri Biteko kwa lengo la kukutana na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu shirikisho hilo ukizingatia kwamba, tangu ateuliwe kushika wadhifa huo hawajawahi kukutana na kufanya mazungumzo rasmi zaidi ya kukutana kwenye ziara mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine, Bina amemweleza Waziri kuwa, Shirikisho lina laani vikali tukio la udanganyifu uliotokea hivi majuzi huko Chunya na kuongeza kwamba, FEMATA haikubaliana na udanganyifu unaofanywa na wachimbaji kwa kushirikiana na baadhi watendaji wa serikali waliopewa dhamana na kwamba halipo tayari kuwalinda wala kuwateteta.

Pia, Bina amezungumzia kuhusu Mgodi wa Buhemba uliofungwa na serikali akimuomba waziri kuufugua mgodi huo kwani  wanachi wengi walio katika eneo hilo wanategemea maisha yao  kutokana na uwepo wa mgodi huo.

Aidha, amemwomba Waziri maeneo mbalimbali yanayochukuliwa na serikali, afikirie kuwapatia wawekezaji wazawa ili wayaendeleze kwa  shughuli za uchimbaji. Bina ameongeza kuwa, FEMATA ina mpango wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji (Miners Bank) kwa ajili ya kuwahudumia wachimbaji nchini.

Kwa upande wake, Waziri Biteko amemshukuru Rais wa FEMATA na ujumbe wake kwa kumtembelea. Amesema FEMATA na Wizara ya Madini huwezi kutenganisha kwa kupiga mstari kwa kuwa watu wa FEMATA ndio wadau wa wizara na kwamba hawajawahi kutofautiana na  kuomba ushirikiano huo uendelee.

Vilevile, Biteko amewashukuru FEMATA kwa kuunga mkono na kulaani kitendo cha udanganyifu uliofanywa na wachimbaji kwa kushirikiana na watendaji wa wizara huko Chunya kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu uzalishaji wa madini.

Kuhusu kufunguliwa kwa mgodi wa Buhemba, Biteko amesema Wizara ina thamini maisha ya watu kuliko shuguli za uchimbaji na kuongeza kwamba hivi sasa kuna timu ya wataalamu ambao wamekwenda  Buhemba kufuatilia utekelezaji wa  waliyokubaliana katika kikao cha tarehe  6 Machi, 2019, na ripoti  hiyo inategemewa kuwa mwongozo wa iwapo mgodi huo ufunguliwe au ufungwe.

Akizungumzia kuhusu uanzishwaji wa Benki ya Wachimbaji amesema ni jambo zuri na kushauri kuanza na SACCOS ili kupima imani ya uaminifu wa wanchama wake katika kurejesha amana watakazo kuwa wanakopa.

Waziri Biteko amewahakikishia FEMATA kuwa wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake.


1   Waziri Doto Biteko akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa Michael Gur Arie, Mkurugenzi wa Biashara na Uendelezaji wa Masoko  wa Kampuni ya MAGUL Security System wa kwanza kushoto kwa Waziri alie ambatana na Idan   Segev wa kwanza kulia walipo mtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma kwa mazungumzo


Waziri Doto Biteko katikati akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kampuni ya MAGUL Security System wa pili kushoto ni Omary Rajabu alie ambatana na wageni hao.

      Waziri Doto Biteko akimsikiliza Rais wa Shirikisho la Wachimbaji nchini (FEMATA), John Bina kulia wakati wa mazungumzo yao ofisini kwake Dodoma. Kushoto ni Mtendaji mkuu wa Shrikisho hilo amabe pia ni Kamishna wa Tume ya Madini Haroun Kinega. 

Waziri Doto Biteko akiongea na Viongozi wakuu wa Shirikisho la Wachimbaji nchini (FEMATA) wakati wa mazungumzo yao ofisini kwake Dodoma. Kulia  ni Rais wa Shirikisho hilo John Bina na kushoto ni Mtendaji mkuu wa Shrikisho amabe pia ni Kamishna wa Tume ya Madini Haroun Kinega

Waziri Doto Biteko katikati akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Wachimbaji nchini (FEMATA) walipo mtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma kwa mazungumzo. Kulia  kwake ni Rais wa Shirikisho hilo John Bina na kushoto ni Mtendaji mkuu wa Shrikisho hilo amabe pia ni Kamishna wa Tume ya Madini Haroun Kinega

Wednesday, April 3, 2019

Waziri wa Madini Uganda afurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini Nchini


Na Greyson Mwase, Geita

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris amesema kuwa amefurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini nchini Tanzania na kusisitiza kuwa Uganda bado itaendelea kutuma wataalam wake pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania kwa ajili ya kujifunza namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Lokeris aliyasema hayo jana tarehe 02 Aprili, 2019 mara baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo na wa kati ya madini iliyopo Wilayani Geita Mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Tanzania yenye lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini hususan katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.

Akiwa ameongozana na  ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo aliwasili mkoani Geita na kupokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.

Ziara hiyo pia ilihusisha wataalam kutoka Wizara ya Madini. Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa pamoja na waandishi wa habari.

Akielezea hali iliyopelekea nchi ya Uganda kuichagua nchi ya Tanzania kama sehemu ya kujifunza kuhusu Sekta ya Madini, Lokeris alisema kuwa, baada ya kutanya  utafiti katika nchi za Aftika Mashariki, walibaini kuwa nchi ya Tanzania ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye usimamizi wa sheria na kanuni za madini hali iliyopelekea wananchi wengi kunufaika nayo hususan wachimbaji wadogo wa madini.

Aliendelea kusema kuwa, Sekta ya Madini Nchini Uganda ndio inaanza kukua, hivyo wameona ni vyema kuja Tanzania  kwa ajili ya kujifunza na kwenda kuimarisha Sekta ya  Madini ili baada ya miaka kadhaa angalau iwe inakaribiana na nchi ya Tanzania.

Akielezea mikakati ya matumizi ya uzoefu mkubwa ujumbe huo ilioupata kutoka kwa nchi ya Tanzania, Waziri Lokeris alisema hatua ya kwanza itakayofanywa na Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya  Madini ni kuhamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kuwapatia leseni.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kuwapatia leseni hatua itakayofuata itakuwa ni kuwaleta Tanzania kwa ajili ya mafunzo ambapo watajifunza kupitia wachimbaji wadogo wa madini wa Tanzania waliofanikiwa kwenye shugfhuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Aliendelea kueleza kuwa, nia ya Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na kuanza kuzalisha dhahabu na kuuza nyingine nje ya nchi na kujipatia mapato makubwa.

“Tumefurahishwa na usimamizi mzuri kwenye sekta ya madini hususan kwenye eneo la uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, tumeona namna wanavyochenjua madini huku wakizingatia sheria na kanuni za mazingira,”alisisitiza Waziri Lokeris.

 Naye Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo akielezea mafanikio ya sekta ya madini nchini alieleza kuwa, mafaniko yaliyopatikana ni pamoja na uboreshaji wa sheria mpya ya madini pamoja na kanuni zake inayotambua madini kama mali ya watanzania na kusisitiza kuwa wachimbaji wadogo wamekuwa wanufaika kwa kiasi kikubwa.

Aliongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeondoa tozo mbalimbali zisizo za lazima hali iliyopelekea wachimbaji wadogo kuzalisha madini kwa gharama nafuu na kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko nchini kama njia mojawapo ya kudhibiti utoroshwaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wa madini wanakuwa na soko la uhakika la kuuzia madini yao kwa bei yenye faida.

Naye mmiliki wa mgodi wa  dhahabu wa Blue Reef uliopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita mkoani Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Christopher Kadeo akizungumza na  ujumbe huo uliofanya ziara kwenye mgodi wake akielezea mchango  wa mgodi wake katika jamii iliyopo jirani alisema mgodi wake tangu ulipoanzishwa mwaka 1991 mpaka sasa umefanikiwa kuajiri watumishi  160 na vibarua takribani  200.

Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu, ulinzi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa mgodi umekuwa ukishirikiana kwa karibu zaidi na Tasisi nyingine za Serikali kama vile Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Chuo Cha Ufundi Dar es Salaam (DIT), Wizara ya Madini, Tume ya Madini na mashirika mengine ya kimataifa.

Aidha, aliongeza kuwa mgodi wake umewahi kupewa tuzo ya utunzaji bora wa mazingira na Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Akielezea mikakati ya mgodi wake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini  alisema mgodi wake unatarajia kufanya utafiti zaidi ili kugundua madini zaidi na kuunganisha leseni zake tano unazomiliki na kutoka kwenye uchimbaji wa kati hadi mkubwa.


Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo (katikati) wakiangalia namna kifusi cha mchanga kinavyotolewa kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Blue Creef  uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita unaomilikiwa na Christopher Kadeo tarehe 02 Aprili, 2019 

Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (wa pili kulia) akifafanua jambo kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Blue Reef  uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita unaomilikiwa na Christopher Kadeo mara baada ya yeye pamoja na ujumbe wake kufanya ziara kwenye mgodi huo. Katikati ni Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo. 

Mkurugenzi wa kampuni ya Tan-Discover Mineral Consultancy Co. Ltd, Peter Kaheshi (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (kulia) mara baada ya yeye pamoja na ujumbe wake kufanya ziara katika kituo cha mfano cha Rwamgaza kwa ajili ya kutoa mafunzo ya namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini kilichopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita Mkoani Geita. 

Mtaalam kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Busolwa uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita, Felix Adolf Ishebabi  (katikati) akielezea shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinavyofanywa na mgodi huo kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris, Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo. 

Afisa Migodi Mkazi wa Mkoa wa Geita, Ernest Maganga (kulia) akielezea namna biashara ya madini inavyofanyika kwenye Soko la Madini la Geita kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (kushoto) na Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo (katikati) pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo

Tuesday, April 2, 2019

Waziri Biteko awasimamisha kazi Maafisa Madini Ofisi ya Madini Chunya


Na Tito Mselem, Chunya

Waziri wa Madini Doto Biteko amewasimamisha kazi Maafisa Madini wote wa Ofisi ya Madini Chunya Mkoani Mbeya na kuteua Wajiolojia watakaokaimu nafasi hizo wakati wizara ikitafuta Maafisa wengine waaminifu watakaofanya kazi hizo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kugundua wizi mkubwa wa madini ya dhahabu unaofanywa na maafisa hao wakishilikiana na wamiliki wa kampuni ya uchenjuaji wa dhahabu.

Akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo wadogo pamoja na wamiliki wa makampuni ya uchenjuaji wa dhahabu Waziri Biteko, amesema udanganyifu unaofanywa na Maafisa hao wa Madini pamoja wenye  kampuni hizo za uchenjuaji ni mkubwa na  hahuitaji msamaha hata kidogo.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana katika sekta hii ya Madini ninawapenda sana wachimbaji ila nasikitika sana kwa wachimbaji na wenye makampuni ya uchenjuaji kutokuwa waaminifu,” amesisitiza Waziri Biteko

Ameongeza kuwa, Maafisa wa madini hao ndiyo wanaotoa mianya ya wizi wa dhahabu unaofanyika kwenye kampuni zaa uchenjuaji wa dhahabu  wilayani humo.

Aidha, katika ziara hiyo Biteko ameifunga kampuni ya   Ntorah Gold Company Ltd inayohusika na uchenjuaji wa dhahabu wilayani  humo baada ya kutoa taarifa za udanganyifu kwa serikali.

Pia, Waziri Biteko ameongeza kwamba, Wilaya ya  Chunya ndiyo sehemu pekee Tanzania inayoongoza kwa wizi wa dhahabu na kutoa taarifa za uongo za kampuni za uchenjuaji wa dhahabu ikifuatiwa na wilaya ya Kahama iliyopo Mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjla, amesema serikali imeondoa kodi zote kwa wachimbaji wadogo zilizokuwa zikilalamikiwa na wachimbaji pamoja na kampuni za uchenjuaji wa dhahabu lakini bado wizi unafanyika tena kwa kiwango kikubwa.  

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila amikiri kwamba hana elimu ya madini hivyo imekuwa vigumu kwake kudhibiti wizi huo   lakini anaamini wizi na udanganyifu upo tena kwa kiwango kikubwa.

“kiukweli sina elimu ya madini hasa kwenye upande wa uchenjuaji wa dhahabu, naamini kuna wizi mkubwa wa madini haya ya dhahabu na taarifa zisizo na ukweli”amesema  Chalamila.


Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Wizara ya Madini na Viongozi wengine wa Wilaya ya Chunya wakisikiliza maelezo ya namna wizi unavyofanyika katika mitambo ya kuchenjua dhahabu. 
Wachimbaji wadogo wadogo wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauli ya wilaya ya Chunya wakimsiliza Waziri wa Madini Doto Biteko


Waziri wa Madini Doto Biteko akitoa akieleza jambo wakati akitoa maelekezo ya namna ya kuifungia kampuni ya uchenjuaji dhahabu ya Ntorah Gold and Diamond Ltd wilayani Chunya

Monday, April 1, 2019

Wizara itaendelea kuanzisha masoko ya madini-Biteko


Na Asteria Muhozya,

Imeelezwa kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kusimamia Uanzishwaji wa Masoko ya Madini katika maeneo mbalimbali nchini huku ikiendelea kufanya marekebisho ya Kanuni za Uanzishwaji wa masoko hayo.

Waziri wa Madini Doto Biteko ameysema hayo Machi 31, 2019 wakati akifunga Semina ya siku mbili iliyoandaliwa na wizara kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati zenye uhusiano na Sekta ya Madini.

Semina hiyo ililenga kutoa elimu na kujenga uelewa wa pamoja kwa wabunge hao kuhusu sekta ya madini ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini, mafanikio na changamoto ya Shirika la Madini la Taifa STAMICO), elimu kuhusu majanga ya asili (hasa matetemeko ya ardhi), ukaguzi migodini, biashara ya madini na shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Uwazi na uwajibikaji katika Rasiimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia.

Waziri Biteko aliongeza kuwa, Wizara itaendelea kuwaelea wadau wa madini huku akiwataka kubadilika na kutenda matendo yenye manufaa kwa pande mbili na kuwaomba wabunge hao kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa wadau wa madini ili waweze kuzingatia na kufuata taratibu zilizowekwa.

Pia, alisema serikali itaendelea kufanya kaguzi migodini kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji wanachimba kwa usalama na kueleza kuwa, wizara imeomba kibali cha kuongeza maeneo mengine ya ukaguzi wa madini na kusema,“ tumepanga kuongeza vituo vingine 85”.

Aidha, alizungumzia maeneo yenye wizi wa dhahabu katika maeneo ya kuchanjua madini hayo na kuyataja kuwa ni Kahama na Chunya na kuwataka wahusika kuzingatia sheria.

Akizungumzia suala la kupunguza zaidi kodi kwa uchimbaji mdogo wa madini, alisema serikali haitapunguza tena kodi hizo kwa sasa mpaka hapo itakapoona manufaa yake.

Ikumbukwe kuwa, baada ya mkutano wa Kisekta uliofanyika Januari 22 mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa madini baada ya wadau hao kuwasilisha kero zao kubwa ikiwa kodi, serikali ilifanya mabadiliko na kuondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo wa madini kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT  (18%) na  kodi ya zuio( withholding tax).

Mbali na wajumbe wa kamati, wengine walioshiriki semina hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Watendaji na Wataalam kutoka wizara na taasisi zake.


Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kushoto) akifuatilia hoja zilizotolewa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa kamati nyingine wakati wa semina ya wabunge iliyotolewa na wizara. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula, wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila na kwa kwanza kulia ni Katibu wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Omary Magwinza. 

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati nyingine wakifuatilia uwasilishaji wa mada uliotolewa na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake. 

Baadhi ya Watendaji na Wataalam kutoka Wizara na Taasisi zake wakifatilia uwasilishwaji mada uliotolewa na Wataalam wa Wizara ya Madini na taasisi zake. 

Baadhi ya Watendaji na Wataalam kutoka Wizara na Taasisi zake wakifatilia uwasilishwaji mada uliotolewa na Wataalam wa Wizara ya Madini na taasisi zake.

Naibu Waziri Nyongo afunga mitambo yote ya kuchenjulia madini Kahama


Na Greyson Mwase, Kahama

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefunga mitambo yote ya kuchenjulia madini ya dhahabu Wilayani Kahama baada ya kubaini udanganyifu mkubwa kwenye uchenjuaji wa madini.

Naibu Waziri Nyongo amechukua hatua hiyo kwenye ziara yake aliyoifanya mapema leo tarehe 31 Machi, 2019 Wilayani Kahama yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Kamishna Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini,  Ali Saidi Ali, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian, wataalam kutoka Tume ya Madini, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.

Akiwa katika ziara hiyo, alifanya ziara ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group inayomilikiwa na  Theogenes Zacharia pamoja na mwenzake aliyejulikana kwa jina la  Antidius na kubaini kampuni hiyo imekuwa ikiwaibia wateja wake kupitia mfumo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

Akiwa ameambatana na msafara wake mara baada ya kuwasili katika kampuni hiyo alioneshwa na wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini waliopewa kazi maalum ya kuchunguza mfumo wa uchenjuaji wa dhahabu wa kampuni hiyo, sehemu ya mabomba ya mfumo iliyoharibiwa kwa makusudi kwa lengo la kunasa kiasi cha dhahabu kabla ya kufikishwa katika chombo maalum cha kupokelea kwa ajili ya mteja.

Alisema kuwa, kiasi cha kaboni iliyokuwa na dhahabu iliyokamatwa ilipelekwa kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kubaini kiasi cha adhabu kilichokuwa kimeibiwa na kusisitiza kuwa baada ya kuchenjuliwa kiasi cha gramu 102 kiligundulika kutaka kuibwa.

Katika hatua nyingine mbali na kufunga mitambo ya kuchenjua madini ya dhahabu katika Wilaya ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya ya Kahama kuhakikisha watuhumiwa wote wa kampuni ya Ng’ana Group wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama na uchunguzi kuanza mara moja.

Katika hatua nyingine, Nyongo alisema kuwa maafisa madini wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama wataanza kufungua mtambo mmoja mmoja wa kuchenjua madini ya dhahabu mara baada ya kujiridhisha na uendeshaji wake.

Awali akielezea siri ya wizi unaofanywa na kampuni ya  Ng’ana Group, mmoja wa wateja kutoka kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya  Joseph Magunila & Partners, aliyepeleka kaboni kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kupata madini ya dhahabu, Wema Shibitali alisema kuwa, wakati zoezi la uchanjuaji likiendelea alishangaa kupata kiasi kidogo cha dhahabu tofauti na kaboni iliyokuwa imewekwa.

Alisimulia kuwa aliomba maafisa kutoka vyombo vya dola kufungua mfumo ili kubaini kama kuna madini yamebaki na kuongeza kuwa mara baada ya mfumo kufunguliwa walibaini kiasi kikubwa cha kaboni kilichokuwa kimebaki kwenye mfumo.

Aidha Shabitali aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwatetea wachimbaji wadogo kwa kuwa wamekuwa wakiibiwa na wachenjuaji wa madini ya dhahabu kwa muda mrefu.

Wakati huo huo akizungumza katika msafara huo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha mbali na kumpogeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutembelea Wilaya yake na kushughulikia changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Madini, alisema kuwa ziara hiyo imewapa mwanga zaidi wa mbinu zinazotumiwa na wachenjuaji wa madini na kusisitiza kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Aliwataka wachimbaji na wachenjuaji wa madini nchini kuunga juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano pamoja na Serikali yake, Dkt. John Pombe Magufuli katika kulinda rasilimali za madini kwa kuwa waaminifu kwenye ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.


Kutoka kulia, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakiangalia steel wire iliyokuwa na mabaki ya kaboni yaliyonasa, kwenye ziara yake ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group tarehe 31 Machi, 2019.

Kutoka kushoto Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha wakishuhudia kaboni ikichomwa ili kupata dhahabu katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group tarehe 31 Machi, 2019.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na vyombo vya habari juu ya maamuzi ya Serikali kuhusiana na udanganyifu uliofanywa na kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group