Na Greyson Mwase,
Geita
Waziri wa Madini
Nchini Uganda, Peter Lokeris amesema
kuwa amefurahishwa na usimamizi wa sekta ya madini nchini Tanzania na
kusisitiza kuwa Uganda bado itaendelea kutuma wataalam wake pamoja na
wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania kwa ajili ya kujifunza namna bora
ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Lokeris aliyasema
hayo jana tarehe 02 Aprili, 2019 mara baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji
wadogo na wa kati ya madini iliyopo Wilayani Geita Mkoani Geita, ikiwa ni
sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Tanzania yenye lengo la kujifunza namna
Tanzania ilivyofanikiwa katika Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini hususan
katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.
Akiwa ameongozana
na ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka
Serikali ya Uganda pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo aliwasili mkoani
Geita na kupokelewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya
ya Geita pamoja na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.
Ziara hiyo pia
ilihusisha wataalam kutoka Wizara ya Madini. Tume ya Madini, vyombo vya ulinzi
na usalama vya mkoa pamoja na waandishi wa habari.
Akielezea hali
iliyopelekea nchi ya Uganda kuichagua nchi ya Tanzania kama sehemu ya kujifunza
kuhusu Sekta ya Madini, Lokeris alisema kuwa, baada ya kutanya utafiti katika nchi za Aftika Mashariki,
walibaini kuwa nchi ya Tanzania ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye usimamizi
wa sheria na kanuni za madini hali iliyopelekea wananchi wengi kunufaika nayo
hususan wachimbaji wadogo wa madini.
Aliendelea kusema
kuwa, Sekta ya Madini Nchini Uganda ndio inaanza kukua, hivyo wameona ni vyema
kuja Tanzania kwa ajili ya kujifunza na
kwenda kuimarisha Sekta ya Madini ili
baada ya miaka kadhaa angalau iwe inakaribiana na nchi ya Tanzania.
Akielezea mikakati ya
matumizi ya uzoefu mkubwa ujumbe huo ilioupata kutoka kwa nchi ya Tanzania,
Waziri Lokeris alisema hatua ya kwanza itakayofanywa na Serikali ya Uganda
kupitia Wizara yake ya Madini ni
kuhamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kuwapatia leseni.
Aliongeza kuwa, mara
baada ya kuwapatia leseni hatua itakayofuata itakuwa ni kuwaleta Tanzania kwa
ajili ya mafunzo ambapo watajifunza kupitia wachimbaji wadogo wa madini wa
Tanzania waliofanikiwa kwenye shugfhuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Aliendelea kueleza
kuwa, nia ya Serikali ya Uganda kupitia Wizara yake ya Madini ni kuhakikisha sekta
hiyo inakua kwa kasi na kuanza kuzalisha dhahabu na kuuza nyingine nje ya nchi
na kujipatia mapato makubwa.
“Tumefurahishwa na
usimamizi mzuri kwenye sekta ya madini hususan kwenye eneo la uwezeshaji wa
wachimbaji wadogo, tumeona namna wanavyochenjua madini huku wakizingatia sheria
na kanuni za mazingira,”alisisitiza Waziri Lokeris.
Naye Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania,
Stanslaus Nyongo akielezea mafanikio ya sekta ya madini nchini alieleza kuwa,
mafaniko yaliyopatikana ni pamoja na uboreshaji wa sheria mpya ya madini pamoja
na kanuni zake inayotambua madini kama mali ya watanzania na kusisitiza kuwa
wachimbaji wadogo wamekuwa wanufaika kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa,
Serikali kupitia Wizara ya Madini imeondoa tozo mbalimbali zisizo za lazima
hali iliyopelekea wachimbaji wadogo kuzalisha madini kwa gharama nafuu na
kulipa kodi na tozo mbalimbali serikalini.
Alieleza mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko nchini kama njia mojawapo ya
kudhibiti utoroshwaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wa madini wanakuwa
na soko la uhakika la kuuzia madini yao kwa bei yenye faida.
Naye mmiliki wa mgodi
wa dhahabu wa Blue Reef uliopo katika
eneo la Rwamgaza Wilayani Geita mkoani Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha
Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), Christopher Kadeo akizungumza
na ujumbe huo uliofanya ziara kwenye
mgodi wake akielezea mchango wa mgodi
wake katika jamii iliyopo jirani alisema mgodi wake tangu ulipoanzishwa mwaka
1991 mpaka sasa umefanikiwa kuajiri watumishi
160 na vibarua takribani 200.
Alieleza mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii kama vile afya, elimu,
ulinzi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa mgodi umekuwa
ukishirikiana kwa karibu zaidi na Tasisi nyingine za Serikali kama vile Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Chuo Cha Ufundi Dar
es Salaam (DIT), Wizara ya Madini, Tume ya Madini na mashirika mengine ya kimataifa.
Aidha, aliongeza kuwa
mgodi wake umewahi kupewa tuzo ya utunzaji bora wa mazingira na Rais wa Awamu
ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Akielezea mikakati ya
mgodi wake kwenye shughuli za uchimbaji wa madini alisema mgodi wake unatarajia kufanya utafiti
zaidi ili kugundua madini zaidi na kuunganisha leseni zake tano unazomiliki na
kutoka kwenye uchimbaji wa kati hadi mkubwa.
Waziri wa Madini
Nchini Uganda, Peter Lokeris na Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania,
Stanslaus Nyongo (katikati) wakiangalia namna kifusi cha mchanga kinavyotolewa
kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Blue Creef
uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita unaomilikiwa na Christopher Kadeo
tarehe 02 Aprili, 2019
Waziri wa Madini
Nchini Uganda, Peter Lokeris (wa pili kulia) akifafanua jambo kwenye Mgodi wa
Dhahabu wa Blue Reef uliopo Wilayani
Geita Mkoani Geita unaomilikiwa na Christopher Kadeo mara baada ya yeye pamoja
na ujumbe wake kufanya ziara kwenye mgodi huo. Katikati ni Naibu Waziri wa
Madini Nchini Tanzania, Stanslaus Nyongo.
Mkurugenzi wa kampuni
ya Tan-Discover Mineral Consultancy Co. Ltd, Peter Kaheshi (kushoto) akitoa
ufafanuzi kwa Waziri wa Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris (kulia) mara baada
ya yeye pamoja na ujumbe wake kufanya ziara katika kituo cha mfano cha Rwamgaza
kwa ajili ya kutoa mafunzo ya namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini
kilichopo katika eneo la Rwamgaza Wilayani Geita Mkoani Geita.
Mtaalam kutoka Mgodi
wa Dhahabu wa Busolwa uliopo Wilayani Geita Mkoani Geita, Felix Adolf
Ishebabi (katikati) akielezea shughuli
za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinavyofanywa na mgodi huo kwa Waziri wa
Madini Nchini Uganda, Peter Lokeris, Naibu Waziri wa Madini Nchini Tanzania,
Stanslaus Nyongo pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo.
Afisa Migodi Mkazi wa
Mkoa wa Geita, Ernest Maganga (kulia) akielezea namna biashara ya madini
inavyofanyika kwenye Soko la Madini la Geita kwa Waziri wa Madini Nchini
Uganda, Peter Lokeris (kushoto) na Waziri wa Madini Nchini Tanzania, Stanslaus
Nyongo (katikati) pamoja na wajumbe kutoka Uganda na Tanzania kwenye ziara hiyo
No comments:
Post a Comment