Na Greyson Mwase,
Kahama
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amefunga mitambo yote ya kuchenjulia madini ya dhahabu
Wilayani Kahama baada ya kubaini udanganyifu mkubwa kwenye uchenjuaji wa
madini.
Naibu Waziri Nyongo
amechukua hatua hiyo kwenye ziara yake aliyoifanya mapema leo tarehe 31 Machi,
2019 Wilayani Kahama yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji
wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara hiyo,
Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Kamishna
Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Saidi Ali, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian, wataalam kutoka Tume ya Madini,
wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.
Akiwa katika ziara
hiyo, alifanya ziara ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya
dhahabu ya Ng’ana Group inayomilikiwa na
Theogenes Zacharia pamoja na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Antidius na kubaini kampuni hiyo imekuwa
ikiwaibia wateja wake kupitia mfumo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.
Akiwa ameambatana na
msafara wake mara baada ya kuwasili katika kampuni hiyo alioneshwa na wataalam
kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini waliopewa kazi maalum ya kuchunguza
mfumo wa uchenjuaji wa dhahabu wa kampuni hiyo, sehemu ya mabomba ya mfumo
iliyoharibiwa kwa makusudi kwa lengo la kunasa kiasi cha dhahabu kabla ya kufikishwa
katika chombo maalum cha kupokelea kwa ajili ya mteja.
Alisema kuwa, kiasi
cha kaboni iliyokuwa na dhahabu iliyokamatwa ilipelekwa kwa ajili ya
kuchenjuliwa ili kubaini kiasi cha adhabu kilichokuwa kimeibiwa na kusisitiza
kuwa baada ya kuchenjuliwa kiasi cha gramu 102 kiligundulika kutaka kuibwa.
Katika hatua nyingine
mbali na kufunga mitambo ya kuchenjua madini ya dhahabu katika Wilaya ya
Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi
Macha kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya ya Kahama
kuhakikisha watuhumiwa wote wa kampuni ya Ng’ana Group wanakamatwa na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha, Naibu Waziri
Nyongo alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama na
uchunguzi kuanza mara moja.
Katika hatua nyingine,
Nyongo alisema kuwa maafisa madini wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Kimadini wa Kahama wataanza kufungua mtambo mmoja mmoja wa kuchenjua madini ya
dhahabu mara baada ya kujiridhisha na uendeshaji wake.
Awali akielezea siri
ya wizi unaofanywa na kampuni ya Ng’ana
Group, mmoja wa wateja kutoka kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Joseph Magunila & Partners, aliyepeleka kaboni
kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kupata madini ya dhahabu, Wema Shibitali alisema
kuwa, wakati zoezi la uchanjuaji likiendelea alishangaa kupata kiasi kidogo cha
dhahabu tofauti na kaboni iliyokuwa imewekwa.
Alisimulia kuwa
aliomba maafisa kutoka vyombo vya dola kufungua mfumo ili kubaini kama kuna
madini yamebaki na kuongeza kuwa mara baada ya mfumo kufunguliwa walibaini
kiasi kikubwa cha kaboni kilichokuwa kimebaki kwenye mfumo.
Aidha Shabitali
aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwatetea wachimbaji wadogo
kwa kuwa wamekuwa wakiibiwa na wachenjuaji wa madini ya dhahabu kwa muda mrefu.
Wakati huo huo
akizungumza katika msafara huo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha mbali
na kumpogeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutembelea Wilaya yake na kushughulikia
changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Madini, alisema kuwa ziara hiyo imewapa
mwanga zaidi wa mbinu zinazotumiwa na wachenjuaji wa madini na kusisitiza kuwa
ataendelea kusimamia kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Aliwataka wachimbaji
na wachenjuaji wa madini nchini kuunga juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya
Tano pamoja na Serikali yake, Dkt. John Pombe Magufuli katika kulinda
rasilimali za madini kwa kuwa waaminifu kwenye ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali
za Serikali.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na vyombo vya habari juu ya maamuzi ya
Serikali kuhusiana na udanganyifu uliofanywa na kampuni ya kuchenjua madini ya
dhahabu ya Ng’ana Group
|
No comments:
Post a Comment