Na Issa Mtuwa,
Dodoma
Waziri wa Madini Doto
Biteko amekutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na makundi
mbalimbali ya wadau wa madini Aprili
3, 2019, Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Miongoni mwa aliokutana
nao ni pamoja na Kampuni ya MAGAL Security System inayojihusisha na ufungaji wa
mitambo ya usalama (security system) katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya
migodini.
Mkurugenzi wa
Biashara na Uendelezaji wa Masoko wa kampuni hiyo, Michael Gur Arie, amemweleza
Waziri kuwa, kampuni yake inataka kufanya kazi na Wizara ya madini katika
masuala ya ufungaji wa mitambo ya usalama kwenye migodi hususani Mirerani.
Amesema kuwa, kampuni
hiyo ina uwezo wa kufunga mitambo Mirerani na wizara ikawa na uwezo wa kufuatilia
kinacho fanyika kwenye eneo lote la mgodi huku shughuli nyingine za ofisi
zikiendelea.
Akizungumza katika
kikao hicho, Waziri Biteko ameishukuru kampuni ya MAGAL kwa kumtembelea na
kuzungumza nae kuhusu suala la usalama hususani Mirerani. Amesema suala la usalama
mirerani linapewa kipaumbele na uzito mkubwa katika kulinda raslimali hiyo ili
iwanufaishe Watanzania wote.
Ameongeza kuwa,
serikali imelipa kipaumbele suala la usalama katika eneo la Mirerani na Wizara
imekuwa na mpango wa awamu mbili katika kutekeleza suala hilo. Amesema, Awamu
ya kwanza ilikuwa ni kujenga ukuta kuzunguka eneo lote la migodi ya Mirerani na
kufunga kamera na awamu ya pili inasubiri ushauri wa namna ya kutekeleza huku
utekelezaaji wake ukitarajiwa kutafanyika baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara
kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, waziri Biteko
amekutana na Viongozi wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Nchini (FEMATA)
wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo, John Bina.
Bina na ujumbe wake
wamemtembelea Waziri Biteko kwa lengo la kukutana na kuzungumzia masuala
mbalimbali yanayohusu shirikisho hilo ukizingatia kwamba, tangu ateuliwe
kushika wadhifa huo hawajawahi kukutana na kufanya mazungumzo rasmi zaidi ya
kukutana kwenye ziara mbalimbali.
Pamoja na mambo
mengine, Bina amemweleza Waziri kuwa, Shirikisho lina laani vikali tukio la
udanganyifu uliotokea hivi majuzi huko Chunya na kuongeza kwamba, FEMATA
haikubaliana na udanganyifu unaofanywa na wachimbaji kwa kushirikiana na baadhi
watendaji wa serikali waliopewa dhamana na kwamba halipo tayari kuwalinda wala
kuwateteta.
Pia, Bina
amezungumzia kuhusu Mgodi wa Buhemba uliofungwa na serikali akimuomba waziri
kuufugua mgodi huo kwani wanachi wengi
walio katika eneo hilo wanategemea maisha yao kutokana na uwepo wa mgodi huo.
Aidha, amemwomba
Waziri maeneo mbalimbali yanayochukuliwa na serikali, afikirie kuwapatia
wawekezaji wazawa ili wayaendeleze kwa shughuli za uchimbaji. Bina ameongeza kuwa,
FEMATA ina mpango wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji (Miners Bank) kwa ajili ya
kuwahudumia wachimbaji nchini.
Kwa upande wake,
Waziri Biteko amemshukuru Rais wa FEMATA na ujumbe wake kwa kumtembelea.
Amesema FEMATA na Wizara ya Madini huwezi kutenganisha kwa kupiga mstari kwa kuwa
watu wa FEMATA ndio wadau wa wizara na kwamba hawajawahi kutofautiana na kuomba ushirikiano huo uendelee.
Vilevile, Biteko
amewashukuru FEMATA kwa kuunga mkono na kulaani kitendo cha udanganyifu
uliofanywa na wachimbaji kwa kushirikiana na watendaji wa wizara huko Chunya
kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu uzalishaji wa madini.
Kuhusu kufunguliwa
kwa mgodi wa Buhemba, Biteko amesema Wizara ina thamini maisha ya watu kuliko
shuguli za uchimbaji na kuongeza kwamba hivi sasa kuna timu ya wataalamu ambao
wamekwenda Buhemba kufuatilia
utekelezaji wa waliyokubaliana katika
kikao cha tarehe 6 Machi, 2019, na
ripoti hiyo inategemewa kuwa mwongozo wa
iwapo mgodi huo ufunguliwe au ufungwe.
Akizungumzia kuhusu
uanzishwaji wa Benki ya Wachimbaji amesema ni jambo zuri na kushauri kuanza na SACCOS
ili kupima imani ya uaminifu wa wanchama wake katika kurejesha amana watakazo
kuwa wanakopa.
Waziri Biteko
amewahakikishia FEMATA kuwa wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa
katika kutekeleza majukumu yake.
1 Waziri Doto Biteko akitoa ufafanuzi wa mambo
mbalimbali kwa Michael Gur Arie, Mkurugenzi wa Biashara na Uendelezaji wa
Masoko wa Kampuni ya MAGUL Security
System wa kwanza kushoto kwa Waziri alie ambatana na Idan Segev wa kwanza kulia walipo mtembelea
ofisini kwake Jijini Dodoma kwa mazungumzo
Ahasante kwa utekelezaji wa miongozo ya madini mungu akulinde mheshimiwa
ReplyDelete