Na
Greyson Mwase, Shinyanga
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani
Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga kumpisha mwekezaji ambaye ni mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya
dhahabu wa kampuni ya Hanan Afro Asia
Geo Engineering (T) Limited kutoka China kuendelea na maandalizi ya uchimbaji wa madini
ya dhahabu, kwa kuwa ndiye aliyewekeza katika kijiji husika kwa kufuata sheria
na kanuni zake.
Naibu Waziri Nyongo
ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 03 Aprili, 2019 katika mkutano wake wa
hadhara na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa
wa Shinyanga yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa
madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake
Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta
Mboneko, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Kamando,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba, Mbunge wa Jimbo
la Solwa, Ahmed Salum, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa,
wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi wa habari.
Alisema kuwa,
kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo
na mwekezaji kutoka nchini China ambaye ni
kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited ambapo malalamiko
yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe
Magufuli katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Kahama Machi 10, 2018 ambapo
alielezwa kuhusu unyanyasaji uliofanywa
wakati wa zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia kwenye maeneo hayo kwa ajili ya
kupisha uanzishwaji wa mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu.
Aliendelea kusema
kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli Machi 11, 2018 aliyekuwa Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko alitembelea eneo la Mwakitolyo linalolalamikiwa
kwa lengo la kufanya mkutano na kusikiliza malalamiko ya wananchi ambapo baada
ya kusikiliza malalamiko hayo aliahidi kwenda kufanyia kazi malalamiko yao na
kuwapa mrejesho.
Aliendelea kueleza
kuwa, iliundwa timu maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kulingana na hadidu
rejea iliyokuwa imepewa ambayo iliitaka timu kukutana na viongozi kuanzia ngazi
ya mkoa hadi wilaya, kuainisha majina ya wananchi waliolipwa na ambao
hawajalipwa fidia, vigezo vilivyotumika wakati wa uthaminishaji na ulipaji wa
fidia pamoja na mapendekezo mbalimbali.
Nyongo aliendelea
kufafanua kuwa, mara baada ya timu kumaliza kazi yake, ilibainika kuwa
mwekezaji alilipa kiasi cha shilingi bilioni 1.63 kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo
husika hivyo zoezi kukamilika kwa asilimia 99.6.
Alisisitiza kuwa
pamoja na wananchi takribani 375 kulipwa fidia bado ilionekana kuwa wananchi
wengi waliolipwa fidia sio wanakijiji wa Mwakitolyo na kuongeza kuwa wananchi
40 tu ndio walioonekana wamiliki halali wa mashamba pamoja na makazi.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri Nyongo aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
kuharakisha upatikanaji wa maeneo mapya kwa ajili ya wanananchi 40 ambao ni
wamiliki halali wa makazi na mashamba katika kijiji cha Mwakitolyo ili
mwekezaji aweze kuanza shughuli za uchimbaji mara moja.
Aidha, Naibu Waziri
Nyongo alimtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co.
Limited kuhakikisha anadumisha mahusiano na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo
na kumtaka kuhakikisha anashiriki katika uboreshaji wa huduma za jamii kama
vile afya, elimu, barabara kama Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake inavyofafanua.
Wakati huo huo Nyongo
aliwataka wananchi kumpa ushirikiano mwekezaji ili kufaidi matunda ya
uwekezaji kwenye kijiji chao ikiwa ni
pamoja na ajira kwa wazawa, utoaji wa huduma za vyakula, biashara, huduma za
jamii hivyo kupaisha uchumi wa kijiji hicho.
Aliendelea kusema
kuwa, madini ni mali ya watanzania wote, hivyo baada ya uwekezaji kuanza
kampuni hiyo italipa kodi mbalimbali kwenye halmashauri na Serikali kuu hivyo
kuboresha sekta nyingine kama vile miundombinu, afya, elimu n.k.
Naye Mbunge wa Solwa,
Ahmed Salum akizungumza katika mkutano huo mbali na kumpongeza Naibu Waziri
Nyongo kwa kutatua mgogoro huo, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii huku
wakilinda amani ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa
Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited, Zhang Jiangho mbali na
kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu, aliahidi
kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kwa kuboresha huduma za jamii na kulipa kodi na tozo
mbalimbali za Serikali.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo
kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga (hawapo pichani) kwenye
mkutano wa hadhara uliolenga kutatua mgogoro kati yao na mwekezaji ambaye ni
kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited tarehe 03 Aprili, 2019.
Kutoka kushoto mbele,
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko na Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo wakinukuu kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wananchi
wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga
(hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Mmoja wa wananchi wa
kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Sehemu ya wananchi wa
kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga
wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa
unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye
mkutano wa hadhara.
Mbunge wa Solwa,
Ahmed Salum akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo (hawapo
pichani)
CV Sourcing | Top Resourcing | Recruitment Support On Demand
ReplyDeleteWe are experts at finding top tier candidates with particular skills and abilities appropriate for a wide range of industries and specific job roles. We search relevant online job boards and forums and analyse job seekers from other digital network platforms to ensure we find the most suitable candidates
http://topresourcing.co.uk/