Na Asteria Muhozya,
Imeelezwa kuwa,
Wizara ya Madini itaendelea kusimamia Uanzishwaji wa Masoko ya Madini katika
maeneo mbalimbali nchini huku ikiendelea kufanya marekebisho ya Kanuni za
Uanzishwaji wa masoko hayo.
Waziri wa Madini Doto
Biteko ameysema hayo Machi 31, 2019 wakati akifunga Semina ya siku mbili
iliyoandaliwa na wizara kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati zenye uhusiano na Sekta ya
Madini.
Semina hiyo ililenga
kutoa elimu na kujenga uelewa wa pamoja kwa wabunge hao kuhusu sekta ya madini
ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa.
Mada zilizowasilishwa
ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini, mafanikio na changamoto ya
Shirika la Madini la Taifa STAMICO), elimu kuhusu majanga ya asili (hasa
matetemeko ya ardhi), ukaguzi migodini, biashara ya madini na shughuli
zinazofanywa na Taasisi ya Uwazi na uwajibikaji katika Rasiimali za Madini,
Mafuta na Gesi Asilia.
Waziri Biteko
aliongeza kuwa, Wizara itaendelea kuwaelea wadau wa madini huku akiwataka
kubadilika na kutenda matendo yenye manufaa kwa pande mbili na kuwaomba wabunge
hao kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa wadau wa madini ili waweze kuzingatia
na kufuata taratibu zilizowekwa.
Pia, alisema serikali
itaendelea kufanya kaguzi migodini kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji
wanachimba kwa usalama na kueleza kuwa, wizara imeomba kibali cha kuongeza
maeneo mengine ya ukaguzi wa madini na kusema,“ tumepanga kuongeza vituo
vingine 85”.
Aidha, alizungumzia
maeneo yenye wizi wa dhahabu katika maeneo ya kuchanjua madini hayo na kuyataja
kuwa ni Kahama na Chunya na kuwataka wahusika kuzingatia sheria.
Akizungumzia suala la
kupunguza zaidi kodi kwa uchimbaji mdogo wa madini, alisema serikali haitapunguza
tena kodi hizo kwa sasa mpaka hapo itakapoona manufaa yake.
Ikumbukwe kuwa, baada
ya mkutano wa Kisekta uliofanyika Januari 22 mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kuwashirikisha wadau
mbalimbali wa madini baada ya wadau hao kuwasilisha kero zao kubwa ikiwa kodi,
serikali ilifanya mabadiliko na kuondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo wa madini
kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT (18%) na
kodi ya zuio( withholding tax).
Mbali na wajumbe wa
kamati, wengine walioshiriki semina hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo
chini ya Wizara pamoja na Watendaji na Wataalam kutoka wizara na taasisi zake.
Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kushoto)
akifuatilia hoja zilizotolewa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa kamati nyingine wakati wa semina ya
wabunge iliyotolewa na wizara. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula, wa kwanza kushoto ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila na kwa kwanza kulia ni Katibu wa
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Omary Magwinza.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati nyingine wakifuatilia
uwasilishaji wa mada uliotolewa na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Taasisi
zake.
Baadhi ya
Watendaji na Wataalam kutoka Wizara na Taasisi zake wakifatilia uwasilishwaji
mada uliotolewa na Wataalam wa Wizara ya Madini na taasisi zake.
Baadhi ya
Watendaji na Wataalam kutoka Wizara na Taasisi zake wakifatilia uwasilishwaji
mada uliotolewa na Wataalam wa Wizara ya Madini na taasisi zake.
No comments:
Post a Comment