Tuesday, March 26, 2019

Wizara ya Madini yaieleza Kamati ya Bunge utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19


Ø YATAJA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA

Ø TUME YA MADINI YAPONGEZWA

Wizara ya Madini na Taasisi zake leo Machi 25, imewasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, kwa  kipindi  cha kuanzia  mwezi Julai 2018 hadi Februari, 2019.

Akiwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa ya utekelezaji wa Wizara, Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila pamoja na mambo mengine, ameelezea Mafanikio ya utekelezaji  wa bajeti kuwa ni pamoja na wizara kuvuka lengo la makusanyo ya maduhuli kwa asilimia 5.6 kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Februari 2019. Lengo la makusanyo kwa kipindi kinachorejewa lilikuwa shilingi 207,065,336,001 ambapo makusanyo halisi yamekuwa shilingi 218,650,392,234.

Pia, amesema Serikali imeondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la thamani (VAT 18), na kodi ya zuio
(Withholding tax  asilimia 5).

Pia, amesema kuzinduliwa kwa Soko la Madini katika mkoa wa  Geita ni juhudi za kuhakikisha uwepo wa masoko ya madini na bei inayoridhisha kwa wachimbaji wa madini hususan wachimbaji wadogo ili kudhibiti uuzaji holela na utoroshaji madini hayo.

"Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi soko hilo tarehe 17 Machi, 2019," amesema Prof. Msanjila.

Vilevile, ameeleza kwamba, kufuatia Kongamano lililofanyika nchini China lililojulikana kama China Tanzania Mining Forum, kampuni tatu zimewasilisha maombi ya miradi ya ubia (JV) kati ya watanzania na wageni Ofisi ya TIC Kanda ya Kati kwa ajili ya kupatiwa Cheti cha Vivutio vya Uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda vya kuchataka madini ya Graphite. Miradi hiyo inatarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 30 na kuzalisha ajira mpya 600 itakapokamilika.

Naye, Waziri wa Madini Waziri wa Madini Doto Biteko, akizungumza katika kikao hicho, ameishukuru Kamati hiyo kwa kuendelea kuisimamia na kuishauri vizuri na kueleza kwamba, Dira Kuu ya wizara ni kuongeza mchango kwenye uchumi wa nchi unaotokana na rasilimali madini.

Pia, Waziri Biteko ameiomba Kamati hiyo kuendelea kuishauri wizara ikiwemo kuikosoa kwa lengo la kuwezesha kuongeza tija zaidi kwenye sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula, amepongeza  jitihada zilizofanywa na wizara hususan kwa kuwezesha mkutano wa Kisekta baina ya serikali na wadau wa madini uliofanyika Januari 22 mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri wa Muungano  wa Tanzania Dkt. John Magufuli na kueleza kwamba, mkutano huo ulifungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau na hivyo kuutaka ushirikiano huo kuendelezwa ili uwezeshe kuendeleza sekta ya madini nchini.

Amesema matarajio ya Rais Magufuli kwenye sekta ya madini ni makubwa na hivyo kutaka jitihada zaidi kufanyika ili kukidhi maratajio hayo.

Aidha, wakichangia hoja kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Tume ya Madini kwa ukusanyaji maduhuli na kwa utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo ukaguzi migodini.

Monday, March 25, 2019

Biteko azitaka Taasisi za Madini kufikiri kibiashara


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini Doto Biteko amezitaka taasisi zilicho chini ya Wizara kufikiri kibiashara ikiwemo kutafuta njia zitakazowezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 23, jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) iliyoandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Aidha, amezitaka taasisi hizo kuhama katika mtindo wa kutegemea ruzuku ya serikali badala yake zijiendeshe kibiashara na kuwataka watendaji wa wizara na taasisi kuhakikisha wanafanya mageuzi yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia zaidi sambamba na kasi yake ya ukuaji kiuchumi.

“Serikali kwa upande wake imeshafanya mageuzi makubwa. Tunataka Idara, kitengo na taasisi zifanye mageuzi. Tuwe na taasisi ambayo mfanyakazi anaweza kueleza amefanya nini kipya,” amesisitiza Waziri Biteko.

Pia, ameongeza kuwa, ukataji madini ni suala ambalo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee kutokana na umuhimu wake katika biashara ya madini na hususan kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini ikiwemo kuhamasisha ujenzi wa viwanda hivyo.

Vilevile, amewataka washiriki wa kikao hicho kuwasilisha mawazo chanya yatakayosaidia kuboresha mkakati huo utakopelekea uboreshaji wa kituo cha TGC.

Aidha, amewataka watendaji wa Kituo cha TGC kuhakikisha wanakitangaza kituo hicho ikiwemo kuwafanya wachimbaji wadogo wa madini kuwa marafiki wa kituo hicho.

Kwa upande wake, Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, amesema serikali iliona umuhimu wa Kituo cha TGC hali ambayo imepelekea kuandaliwa kwa mikakati hiyo na kueleza kuwa uwepo wake unapaswa kutoa mabadiliko katika kituo hicho na hususan katika eneo la uongezaji thamani madini.

 Ameongeza kuwa, uongezaji thamani madini ni jambo ambalo serikali inaliangalia kwa umuhimu wake na kueleza kuwa ni miongoni mwa mambo  yaliyopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na 2017 ili taifa liweze kunufaika zaidi.

Ameeleza masuala mengine yaliyopelekea serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya madini ni pamoja na kutaka kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na madini, serikali kushiriki katika uchumi wa madini na kumiliki hisa, kushirikisha jamii katika miradi ya madini na kampuni za madini kushirikiana  na jamii.

Aidha, amewashukuru wataalam washauri Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutokana na ushauri wao walioutoa kwa wizara wakati wa kupitia Mikakati hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara yaMadini, Prof. Simon Msanjila amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha kila mmoja anaangalia eneo linalomhusu katika kituo hicho na kulifanyia kazi kikamilifu ili kufikia lengo linalotarajiwa.

Wizara ya Madini iliona umuhimu wa kukiimarisha Kituo cha TGC ili kijiendeshe kibiashara kutokana na fursa zilizopo katika sekta ya madini hususan kwenye ukataji wa madini. Pia, kutokana na fursa zilizopo katika ukataji wa madini ya vito na jimolojia kwa ujumla, wizara iliona TGC inaweza kujiendesha kibiashara na hivyo kuongeza mapato kwa serikali.

Kazi ya kuandaa Mikakati hiyo imetekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na  kuandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na kupitiwa kikamilifu na Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizarani na taasisi zake.


Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Wengine ni watendaji wa Wizara na Taasisi. 

Waziri wa Madini Doto Biteko katikati kipitia jambo wakati wa kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na kushoto ni Katibu Mkuu, Prof. Simon Msanjila. 

Viongozi Waandamizi wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa wizara na taasisi, Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu Cha Mzumbe na Wataalam Washauri kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. 

Mtaalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe  Dkt. George Mofulu akieleza jambo wakati akiwapitisha wajumbe wa kikao hicho katika mikakati  hiyo.

Viongozi Waandamizi Madini watembelea jengo la Wizara, Ihumwa


v Waziri Biteko asema wizara iko tayari kuwahudumia watanzania kutokea Ihumwa

v Mkandarasi aahidi kukamilisha ujenzi ndani ya siku Tano

Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini, wakiongozwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Machi 23, wametembelea Jengo la Wizara ya Madini lililopo mji wa Serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo, Waziri wa Madini Doto Biteko amewahakikishia watanzania wote pamoja na wadau wa madini kuwa, wizara iko tayari kuwahudumia kutokea eneo hilo la Ihumwa pindi itakapohamia na kuwataka watumishi kujiandaa kuhamia eneo hilo mara baada ya mkandarasi kukabidhi jengo kwa wizara.

Vilevile, Waziri Biteko amezitaka taasisi nyingine zenye uhitaji wa kutumia madini ya mawe yanayopatikana nchini ikiwa ni pamoja na mable, kuwa wizara iko tayari kuwasaidia kwa kuwaunganisha na wajeta wake.

Pia, amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutokana na msukumo alioutoa kuhakikisha ujenzi wa majengo ya serikali unakamilika kwa wakati.

Aidha,  amempongeza Mkandarasi kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd kutokana na kuongeza kasi ya ujenzi ikiwemo kuzingatia ubora nakuongeza kwamba, wizara imeridhika na ujenzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ameeleza kuwa, wizara imepanga kulifanya eneo la ofisi hiyo kuwa kijani kwa kuhakikisha inapanda miti ya aina mbalimbali na kuhakikisha kwamba eneo hilo linawekewa mazingira mazuri ya kuvutia.

Naye, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila Amesema Mkandarasi Kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd imeahidi kuikabidhi Wizara jengo hilo ndani ya kipindi cha siku Tano zijazo “awali ujenzi ulianza kwa kusuasua lakini sasa uko katika hatua nzuri na mkandarasi amezingatia ubora,” amesema Prof. Msanjila.

Akizungumzia mahitaji ya ofisi na idadi ya watumishi, amemsema kwa idadi ya watumishi wa wizara Makao Makuu ofisi zilizopo katika jego hilo zinatosheleza mahitaji na kuongeza kuwa, kwa kuanza Idara zote na Vitengo vya Wizara vinatarajia kuhamia katika eneo hilo isipokuwa Idara ya fedha kutokana na masuala ya mfumo wa kifedha.

Pia, ameeleza kuwa, wizara imetumia malighafi inayopatikana nchini yakiwemo madini ya mable ambayo yamepatikana kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa kampuni hiyo   Hamisi Msangi ameihakikishia wizara kuwa , ndani ya siku tano zijazo, jengo hilo litakabidhiwa rasmi kwa wizara hiyo.

Muonekano wa Jengo la Wizara ya Madini linalojengwa katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko, (mwenye koti) Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto) na Prof. Simon Msanjila (mwenye tisheti nyekundu) wakikagua maeneo maeneo mbalimbali ya jengo la Wizara


Waziri wa Madini Doto Biteko (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto ) na Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila, wakijadiliana jambo wakati wakikagua maeneo mbalimbali ya jengo la Wizara, eneo la Ihumwa.

Waziri wa Madini Doto Biteko  katikati na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakiangalia kitu wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara, Ihumwa. 

Monday, March 18, 2019

Majaliwa atoa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa kukamilisha masoko ya madini


Nuru Mwasampeta na Greyson Mwase, Geita

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa hususan mikoa yenye utajiri mwingi wa madini ya metali na vito nchini kuhakikisha wanakamilisha na kufungua masoko ya madini ili kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuwa na soko la uhakika la madini hayo.

Majaliwa alitoa  agizo hilo kwenye uzinduzi wa Soko la Madini la Geita tarehe 17 Machi, 2019 uliofanyika katika viwanja vya Soko Kuu mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa kiserikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya.

Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, watendaji kutoka Tume ya Madini, Wakuu wa Mikoa, wabunge, madiwani, viongozi wa dini, waandishi wa habari pamoja na wananchi kutoka katika mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya  jirani.

Alisema kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini ni  sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa tarehe 22 Januari, 2019 kwenye mkutano wake na wachimbaji wa madini nchini uliofanyika jijini Dar Es Salaam. 

“Ninawataka wakuu wa mikoa kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kabla ya mwaka wa fedha kumalizika Juni 30, 2019,” alisema Majaliwa.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwanufaisha watanzania wote, Serikali kupitia Wizara ya Madini ilianza kwa kuboresha Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Aliongeza kuwa, serikali imeamua kuondoa tozo mbalimbali zilizokuwa mzigo kwa wachimbaji wa madini uli uchimbaji wao uwe na faida kubwa na kuwawezesha kulipa kodi mbalimbali za Serikali.

Alisema kuwa, kufutwa kwa kodi na tozo mbalimbali kutapunguza kwa kiwango kikubwa utoroshwaji wa madini nje ya nchi na Serikali kujipatia pato kubwa linalotokana na shughuli za madini nchini.

Akielezea umuhimu wa masoko ya madini, Majaliwa alieleza kuwa mbali na kupunguza utoroshwaji wa madini, hakutakuwepo na dhuluma kwa wachimbaji wadogo wa madini kwani watakuwa na sehemu yenye uhakika ya kuuzia madini hayo kulingana na bei elekezi iliyotolewa na Serikali.

Aliendelea kueleza kuwa, soko la madini  litarahisisha huduma za uuzaji na ununuzi wa madini ambapo huduma zote zitatolewa ndani ya jengo moja hivyo kuokoa muda wa wauzaji na wanunuzi wa madini.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alitoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa, atakayekamatwa anatorosha madini atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.

Pia aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali  kuhusu sekta ya madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje ya nchi.

Aidha, aliitaka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara na Taasisi nyingine za Serikali  zinazohusika na maendeleo ya sekta ya madini kuheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

“Wizara ya Madini, ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hilo ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini,” alisisitiza Majaliwa.

Aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na maendeleo ya  sekta ya madini ambapo utekelezaji  wa dhamira hiyo unakwenda sambamba na kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha kuimarika kwa sekta ya madini nchini.


Jiwe la Msingi kwenye viwanja vya Soko la Madini Geita mara baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto) akielezea namna Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita ilivyojipanga kwenye usimamizi wa  Soko la Madini Geita kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kabla ya kuanza kwa shughuli za uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kabla ya kuzindua Soko la Madini  Geita tarehe 17 Machi, 2019. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) akizugumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Soko la Madini la Geita kufanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Soko la Madini Geita kabla ya uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa hotuba ya uzinduzi wa Soko la Madini Geita kwa wananchi na watendaji waandamizi wa Serikali (hawapo pichani) tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo kwenye uzinduzi huo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Simon Msanjila akitoa taarifa ya uzalishaji wa madini nchini kwenye uzinduzi huo.

Tutaendelea kuiunga mkono Wizara ya Madini-Mwenyekiti wa Kamati


Na Issa Mtuwa, Songea

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mariam Ditopile Mzuzuri amesema kamati yake inaipongeza na itaendelea kuiunga mkono Wizara ya Madini kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Akiongea na waandishi wa habari mbele ya kamati yake Machi 13, 2019 mjini songea baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha umahiri (Centre of excellence) kwa mkoa wa ruvuma, Mzuzuri amesema kamati yake inaridhishwa na kazi za Wizara ya Madini na wataendelea kuiunga mkono (support) hasa swala la wachimbaji wadogo.

“Tunawapongeza sana Wizara ya Madini, mnafanya kazi nzuri na sisi kama kamati niseme tutaendelea kuwaunga mkono (support) hasa hili la wachimbaji wadogo” alisema Mzuzuri.

Naibu Wziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo ameiambia kamati kuwa wizara yake imejipanga katika kukamilisha ujenzi wa vituo vyote vya umairi kikiwemo cha Songea kwa kuzingatia ubora. Amesema ujenzi wa vituo vyote unakwenda vizuri, hata hivyo kituo cha songea kilichelewa ujenzi wake tofauti na vituo vingine kwa sababu mbalimbali ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa kokoto tatizo ambalo lilisha tatuliwa na kwa sasa ujenzi unaendelea kwa kasi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekusudia kukamilisha ujenzi wa kituo hiki na vingine kwa wakati na kama nilivyo tangulia kusema zile changamoto zimesha tatuliwa na tuaendelea vizuri. Naishukuru kamati yako kwa kutuunga mkono na ushauri wote uliotolewa tutauzingatia.” Alisema Nyongo.

Nae Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Prof. Riziki Shemdoe akiongea kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo amewambia wajumbe wa kamati kuwa ni kweli kuna kipindi mkoa wa Ruvuma ulikumbwa na changamoto za upatikanaji wa kokoto na miradi mingi ya serikali ilisimama kutokana na kuwa na kampuni moja tu ya uzalishaji wa kokoto mkoa nzima, mara baada ya mitambo yake kuharibika na uzalishaji kusimama upatikanaji wa kokoto ulikuwa ni tatiizo.

Kituo cha Umahiri Songea ni miongoni mwa vituo mbalimbali vinavyo jengwa hapa nchini katika maeneo mbalimbali kama vile, kituo cha Bukoba, Simiyu, Tanga, Chuya kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo kujifunza na kupata uelewa wa masuala mbalimbali madini.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alie mbele akikagua na kutoa maelekezo kwa Meja Atupele Mwamfupe Meneja wa Ujenzi SUMA JKT Kanda ya Kusini kulia kwa Meja ni Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali watu  wa Wizara ya Madini Issa Nchasi kabla ya kuwasili kwa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini 

Meneja wa Kanda ya Ujenzi SUMA JKT, Meja Atupele Mwamfup akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa kituo na kutafsiri michoro mbalimbali ya jengo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Wizara ya Madini Issa Nchasi, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Makamu Mwenyekiti Mhe. Mriam Mzuzuri na wajumbe wengine.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akitoa maelezo ya ujenzi wa kituo cha umahiri songea kwa Makamu Mwenyekiti wa kamati Mhe. Mariam Mzuzuri kushoto kwake. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Raslimali Watu Wizara ya Madini Issa Nchasi na Meja Atupele Mwamfupe Meneja wa Ujenzi SUMA JKT Kanda ya Kusini.  

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Mariam Mzuzuri akimueleza jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wa kulia kwake mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha umairi. 

Friday, March 15, 2019

Waziri Kairuki amkabidhi rasmi Wizara Biteko


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki amemkabidhi rasmi Majukumu ya Uwaziri wa Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko katika kikao kilichohudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Waziri Kairuki amemshukuru Waziri Biteko kwa ushirikiano aliompatia kwa kipindi chote alichokuwa Waziri wa wizara hiyo na kueleza kwamba, kabla ya makabidhiano hayo, wamepata wasaa wa kupitia kwa pamoja majukumu na vipaumbele vya wizara ikiwemo maeneo muhimu yanayotakiwa kupewa msukumo.

Naye, Waziri Biteko, akizungumza mara baada ya kukabidhiwa majukumu hayo, amemshukuru Waziri Kairuki na kumwelezea kuwa ni Waziri aliyekuwa mwalimu mzuri kwake kwa kipindi chote alichokuwa Naibu Waziri.

Ameongeza, Waziri Kairuki hakuwahi kumnyima nafasi ya kujifunza ikiwemo kumtuma kutekeleza majukumu mbalimbali nafasi ambayo ilimkomaza.

“ Waziri hakuwahi kuninyima fursa, alinituma popote na nitaendelea kuhitaji ushauri wake katika kutekeleza majukumu yangu,” amesisitiza Biteko.

Makabidhiano hayo yamefanyika Machi 12, ofisini kwa Waziri Biteko Jijini Dodoma.

Waziri Biteko aliteuliwa Januari 8, 2019 kushika wadhifa huo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali. Waziri Biteko alichukua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.


Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, akimkabidhi Nyaraka za majukumu ya Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko.Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, akimkabidhi Nyaraka za majukumu ya Wizara ya Madini, Waziri Doto Biteko.Anayeshuhudia katikati ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Madini Doto Biteko na Waziri Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, wakifurahia jambo mara baada ya makabidhiano. Katikati anayeshuhudia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Thursday, March 14, 2019

Acacia yazungumza na Serikali kunusuru Mgodi usifungwe


Na Issa Mtuwa, Dodoma

Uongozi wa Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa North Mara umezungumza na Serikali kuelezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa kudhibiti maji yenye sumu ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Waziri wa Madini Doto Biteko, atangaze kufunga shuguli za mgodi huo endapo utashindwa kudhibiti maji ya sumu yanayotiririka kwenye makazi ya watu, ifike Machi 30 mwaka huu.

Tamko hilo la serikali limeifanya kampuni ya Acacia kuchukua hatua za haraka za kudhibiti maji hayo ili kukwepa rungu la serikali la kuufunga mgodi huo.  Machi 12, uongozi wa Acacia North Mara ulikutana na Waziri Biteko ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kueleza hatua iliyofikiwa ya kutekeleza agizo la serikali.

Uongozi wa kampuni hiyo ukizungumza katika kikao hicho, ulieleza kuwa, tayari mgodi huo umechukua hatua za haraka tangu kutolewa kwa agizo na kwamba hadi sasa suala la kudhibiti maji yenye sumu limeshetekelezwa na hakuna maji yanayotiririka kuelekea kwenye makazi ya watu.

Aidha, ulimweleza kuwa, pamoja na kudhibiti maji hayo kupitia bwawa la kuhifadhia maji yenye sumu yajulikanayo kitaalam kama “topesumu” (Tailings Storage Facility- TSF) mgodi umeanza kuchukuwa hatua za kujenga TSF mpya.

“Mhe. Waziri tumekuja kutoa mrejesho wa utekelezaji wa agizo lako, tunafurahi kukuambia kuwa tumetekeleza agizo hilo na kwa sasa hakuna maji yanayotiririka. Pamoja na hatua hiyo mgodi umeanza mchakato wa ujenzi wa bwawa jipya (TSF) la kuhifadhia topesumu,” walieleza.

Aidha, ulimweleza Waziri Biteko kuhusu hujuma za uharibifu wa miundombinu ya bomba la maji yenye sumu unaofanywa kwa maksudi na wakazi wanaozunguka mgodi ili kufifisha juhudi zao za kudhibiti maji hayo wakiwa na lengo la kuufanya mgodi uonekane haujachukuwa hatua kudhibiti jambo hilo, ambapo walionesha picha mbalimbali ya namna bomba lilivyo pasuliwa ili maji yatiririke kuelekeka kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko alieleza kuwa, amepokea taarifa ya kampuni husika na kuwapongeza kwa hatua zilizochukuliwa na kusema kuwa, ukweli wa jambo hilo atauthibitisha mara baada ya kupata ripoti ya wataalam watakaokwenda kuhakikisha kuhusu utekelezaji wa agizo hilo na kuongeza,“katika hili sitanii juu ya kuufunga mgodi ikiwa utashindwa kudhibiti tope sumu,”.

 “Naomba nirudie tena katika hili sitanii, sitabadilisha msimamo wangu kama serikali na utaendelea kubaki pale pale dawa pekee ni kutekelezwa kwa agizo hilo. Lakini niseme ukweli, nasikitishwa sana na kitendo hiki cha wananchi kupasua bomba, kwa hili sikubaliani nao na siwaungi mkono.

 Pia, aliongeza kuwa, atawasiliana na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuona namna ya kudhibiti hali hiyo ili wale watakao bainika wachukuliwe hatua.

Waziri Biteko alilitoa agizo hilo   Machi 6, alipoutembelea mgodi huo hapo kwa ziara ya kikazi  pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime.


Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa.

Waziri wa Madini Doto Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness Marwa.