Na Issa Mtuwa, Dodoma
Uongozi wa Kampuni ya
Acacia kupitia Mgodi wa North Mara umezungumza na Serikali kuelezea hatua zilizochukuliwa
hadi sasa kudhibiti maji yenye sumu ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Waziri wa
Madini Doto Biteko, atangaze kufunga shuguli za mgodi huo endapo utashindwa
kudhibiti maji ya sumu yanayotiririka kwenye makazi ya watu, ifike Machi 30
mwaka huu.
Tamko hilo la
serikali limeifanya kampuni ya Acacia kuchukua hatua za haraka za kudhibiti
maji hayo ili kukwepa rungu la serikali la kuufunga mgodi huo. Machi 12, uongozi wa Acacia North Mara ulikutana
na Waziri Biteko ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kueleza hatua
iliyofikiwa ya kutekeleza agizo la serikali.
Uongozi wa kampuni
hiyo ukizungumza katika kikao hicho, ulieleza kuwa, tayari mgodi huo umechukua
hatua za haraka tangu kutolewa kwa agizo na kwamba hadi sasa suala la kudhibiti
maji yenye sumu limeshetekelezwa na hakuna maji yanayotiririka kuelekea kwenye
makazi ya watu.
Aidha, ulimweleza
kuwa, pamoja na kudhibiti maji hayo kupitia bwawa la kuhifadhia maji yenye sumu
yajulikanayo kitaalam kama “topesumu” (Tailings Storage Facility- TSF) mgodi
umeanza kuchukuwa hatua za kujenga TSF
mpya.
“Mhe. Waziri tumekuja
kutoa mrejesho wa utekelezaji wa agizo lako, tunafurahi kukuambia kuwa
tumetekeleza agizo hilo na kwa sasa hakuna maji yanayotiririka. Pamoja na hatua
hiyo mgodi umeanza mchakato wa ujenzi wa bwawa jipya (TSF) la kuhifadhia topesumu,” walieleza.
Aidha, ulimweleza Waziri
Biteko kuhusu hujuma za uharibifu wa miundombinu ya bomba la maji yenye sumu
unaofanywa kwa maksudi na wakazi wanaozunguka mgodi ili kufifisha juhudi zao za
kudhibiti maji hayo wakiwa na lengo la kuufanya mgodi uonekane haujachukuwa
hatua kudhibiti jambo hilo, ambapo walionesha picha mbalimbali ya namna bomba
lilivyo pasuliwa ili maji yatiririke kuelekeka kwa wananchi.
Akizungumza katika
kikao hicho, Waziri Biteko alieleza kuwa, amepokea taarifa ya kampuni husika na
kuwapongeza kwa hatua zilizochukuliwa na kusema kuwa, ukweli wa jambo hilo atauthibitisha
mara baada ya kupata ripoti ya wataalam watakaokwenda kuhakikisha kuhusu
utekelezaji wa agizo hilo na kuongeza,“katika hili sitanii juu ya kuufunga
mgodi ikiwa utashindwa kudhibiti tope sumu,”.
“Naomba nirudie tena katika hili sitanii, sitabadilisha
msimamo wangu kama serikali na utaendelea kubaki pale pale dawa pekee ni
kutekelezwa kwa agizo hilo. Lakini niseme ukweli, nasikitishwa sana na kitendo
hiki cha wananchi kupasua bomba, kwa hili sikubaliani nao na siwaungi mkono.
Pia, aliongeza kuwa, atawasiliana na Mkuu wa
Mkoa na Mkuu wa Wilaya kuona namna ya kudhibiti hali hiyo ili wale watakao
bainika wachukuliwe hatua.
Waziri Biteko alilitoa
agizo hilo Machi 6, alipoutembelea mgodi huo hapo kwa
ziara ya kikazi pamoja na kuzungumza na wananchi
kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime.
Waziri wa Madini Doto
Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini
kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness
Marwa.
Waziri wa Madini Doto
Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini
kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness
Marwa.
Waziri wa Madini Doto
Biteko akiwa na Viongozi wa Kampuni ya Acacia wa mgodi North Mara, ofisini
kwake jijini Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Agness
Marwa.
No comments:
Post a Comment