Na
Asteria Muhozya,
Waziri wa
Madini Doto Biteko amezitaka taasisi zilicho chini ya Wizara kufikiri
kibiashara ikiwemo kutafuta njia zitakazowezesha sekta ya madini kuchangia
zaidi katika pato la taifa.
Waziri Biteko
ameyasema hayo Machi 23, jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kupitia
na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia
Tanzania (TGC) iliyoandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Aidha,
amezitaka taasisi hizo kuhama katika mtindo wa kutegemea ruzuku ya serikali
badala yake zijiendeshe kibiashara na kuwataka watendaji wa wizara na taasisi
kuhakikisha wanafanya mageuzi yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia zaidi
sambamba na kasi yake ya ukuaji kiuchumi.
“Serikali kwa upande wake imeshafanya mageuzi
makubwa. Tunataka Idara, kitengo na taasisi zifanye mageuzi. Tuwe na taasisi
ambayo mfanyakazi anaweza kueleza amefanya nini kipya,” amesisitiza Waziri
Biteko.
Pia, ameongeza
kuwa, ukataji madini ni suala ambalo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa
kipekee kutokana na umuhimu wake katika biashara ya madini na hususan kipindi
hiki ambacho serikali inasisitiza shughuli za uongezaji thamani madini
kufanyika nchini ikiwemo kuhamasisha ujenzi wa viwanda hivyo.
Vilevile, amewataka
washiriki wa kikao hicho kuwasilisha mawazo chanya yatakayosaidia kuboresha
mkakati huo utakopelekea uboreshaji wa kituo cha TGC.
Aidha,
amewataka watendaji wa Kituo cha TGC kuhakikisha wanakitangaza kituo hicho
ikiwemo kuwafanya wachimbaji wadogo wa madini kuwa marafiki wa kituo hicho.
Kwa upande
wake, Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, amesema serikali iliona umuhimu
wa Kituo cha TGC hali ambayo imepelekea kuandaliwa kwa mikakati hiyo na kueleza
kuwa uwepo wake unapaswa kutoa mabadiliko katika kituo hicho na hususan katika
eneo la uongezaji thamani madini.
Ameongeza kuwa, uongezaji thamani madini ni
jambo ambalo serikali inaliangalia kwa umuhimu wake na kueleza kuwa ni miongoni
mwa mambo yaliyopelekea kufanyika kwa
mabadiliko katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na 2017 ili taifa liweze
kunufaika zaidi.
Ameeleza
masuala mengine yaliyopelekea serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya madini ni
pamoja na kutaka kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na madini, serikali
kushiriki katika uchumi wa madini na kumiliki hisa, kushirikisha jamii katika
miradi ya madini na kampuni za madini kushirikiana na jamii.
Aidha,
amewashukuru wataalam washauri Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga
kutokana na ushauri wao walioutoa kwa wizara wakati wa kupitia Mikakati hiyo.
Kwa upande
wake, Katibu Mkuu wa Wizara yaMadini, Prof. Simon Msanjila amewataka watendaji
wa Wizara kuhakikisha kila mmoja anaangalia eneo linalomhusu katika kituo hicho
na kulifanyia kazi kikamilifu ili kufikia lengo linalotarajiwa.
Wizara ya
Madini iliona umuhimu wa kukiimarisha Kituo cha TGC ili kijiendeshe kibiashara
kutokana na fursa zilizopo katika sekta ya madini hususan kwenye ukataji wa
madini. Pia, kutokana na fursa zilizopo katika ukataji wa madini ya vito na
jimolojia kwa ujumla, wizara iliona TGC inaweza kujiendesha kibiashara na hivyo
kuongeza mapato kwa serikali.
Kazi ya
kuandaa Mikakati hiyo imetekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali
Madini (SMMRP) na kuandaliwa na Wataalam
Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na kupitiwa kikamilifu na Prof. Beatus
Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Kikao hicho
kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizarani na taasisi zake.
Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati
akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa
Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Wengine ni watendaji wa
Wizara na Taasisi.
Waziri wa Madini Doto Biteko katikati kipitia
jambo wakati wa kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa
Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Kulia ni Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo na kushoto ni Katibu Mkuu, Prof. Simon Msanjila.
Viongozi Waandamizi wa Wizara wakiwa katika picha
ya pamoja na watendaji wa wizara na taasisi, Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu
Cha Mzumbe na Wataalam Washauri kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Mtaalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Dkt. George Mofulu akieleza jambo wakati
akiwapitisha wajumbe wa kikao hicho katika mikakati hiyo.
No comments:
Post a Comment