Ø YATAJA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA
Ø TUME YA MADINI YAPONGEZWA
Wizara ya Madini na
Taasisi zake leo Machi 25, imewasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/19,
kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2018 hadi Februari, 2019.
Akiwasilisha kwa
Kamati hiyo taarifa ya utekelezaji wa Wizara, Katibu Mkuu wa Madini
Prof. Simon Msanjila pamoja na mambo mengine, ameelezea Mafanikio ya
utekelezaji wa bajeti kuwa ni pamoja na wizara kuvuka lengo la makusanyo
ya maduhuli kwa asilimia 5.6 kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Februari 2019.
Lengo la makusanyo kwa kipindi kinachorejewa lilikuwa shilingi 207,065,336,001
ambapo makusanyo halisi yamekuwa shilingi 218,650,392,234.
Pia, amesema
Serikali imeondoa kodi kwenye uchimbaji mdogo kwa kuwafutia kodi ya ongezeko la
thamani (VAT 18), na kodi ya zuio
(Withholding tax
asilimia 5).
Pia, amesema
kuzinduliwa kwa Soko la Madini katika mkoa wa Geita ni juhudi za
kuhakikisha uwepo wa masoko ya madini na bei inayoridhisha kwa wachimbaji wa
madini hususan wachimbaji wadogo ili kudhibiti uuzaji holela na utoroshaji
madini hayo.
"Mhe. Kassim
Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi soko
hilo tarehe 17 Machi, 2019," amesema Prof. Msanjila.
Vilevile, ameeleza
kwamba, kufuatia Kongamano lililofanyika nchini China lililojulikana kama China Tanzania Mining Forum, kampuni tatu
zimewasilisha maombi ya miradi ya ubia (JV) kati ya watanzania na wageni Ofisi
ya TIC Kanda ya Kati kwa ajili ya kupatiwa Cheti cha Vivutio vya Uwekezaji
kwenye ujenzi wa viwanda vya kuchataka madini ya Graphite. Miradi hiyo
inatarajiwa kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 30 na kuzalisha ajira
mpya 600 itakapokamilika.
Naye, Waziri wa
Madini Waziri wa Madini Doto Biteko, akizungumza katika kikao hicho,
ameishukuru Kamati hiyo kwa kuendelea kuisimamia na kuishauri vizuri na kueleza
kwamba, Dira Kuu ya wizara ni kuongeza mchango kwenye uchumi wa nchi
unaotokana na rasilimali madini.
Pia, Waziri Biteko
ameiomba Kamati hiyo kuendelea kuishauri wizara ikiwemo kuikosoa kwa lengo la
kuwezesha kuongeza tija zaidi kwenye sekta ya madini.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula,
amepongeza jitihada zilizofanywa na wizara hususan kwa kuwezesha mkutano
wa Kisekta baina ya serikali na wadau wa madini uliofanyika Januari 22 mwaka
huu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt.
John Magufuli na kueleza kwamba, mkutano huo ulifungua ukurasa mpya wa
ushirikiano kati ya Serikali na wadau na hivyo kuutaka ushirikiano huo
kuendelezwa ili uwezeshe kuendeleza sekta ya madini nchini.
Amesema matarajio
ya Rais Magufuli kwenye sekta ya madini ni makubwa na hivyo kutaka jitihada
zaidi kufanyika ili kukidhi maratajio hayo.
Aidha, wakichangia
hoja kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Tume ya Madini
kwa ukusanyaji maduhuli na kwa utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo ukaguzi
migodini.
No comments:
Post a Comment