Monday, March 18, 2019

Majaliwa atoa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa kukamilisha masoko ya madini


Nuru Mwasampeta na Greyson Mwase, Geita

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi mitatu kwa wakuu wa mikoa hususan mikoa yenye utajiri mwingi wa madini ya metali na vito nchini kuhakikisha wanakamilisha na kufungua masoko ya madini ili kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuwa na soko la uhakika la madini hayo.

Majaliwa alitoa  agizo hilo kwenye uzinduzi wa Soko la Madini la Geita tarehe 17 Machi, 2019 uliofanyika katika viwanja vya Soko Kuu mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa kiserikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya.

Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, watendaji kutoka Tume ya Madini, Wakuu wa Mikoa, wabunge, madiwani, viongozi wa dini, waandishi wa habari pamoja na wananchi kutoka katika mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya  jirani.

Alisema kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini ni  sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa tarehe 22 Januari, 2019 kwenye mkutano wake na wachimbaji wa madini nchini uliofanyika jijini Dar Es Salaam. 

“Ninawataka wakuu wa mikoa kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kabla ya mwaka wa fedha kumalizika Juni 30, 2019,” alisema Majaliwa.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwanufaisha watanzania wote, Serikali kupitia Wizara ya Madini ilianza kwa kuboresha Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo.

Aliongeza kuwa, serikali imeamua kuondoa tozo mbalimbali zilizokuwa mzigo kwa wachimbaji wa madini uli uchimbaji wao uwe na faida kubwa na kuwawezesha kulipa kodi mbalimbali za Serikali.

Alisema kuwa, kufutwa kwa kodi na tozo mbalimbali kutapunguza kwa kiwango kikubwa utoroshwaji wa madini nje ya nchi na Serikali kujipatia pato kubwa linalotokana na shughuli za madini nchini.

Akielezea umuhimu wa masoko ya madini, Majaliwa alieleza kuwa mbali na kupunguza utoroshwaji wa madini, hakutakuwepo na dhuluma kwa wachimbaji wadogo wa madini kwani watakuwa na sehemu yenye uhakika ya kuuzia madini hayo kulingana na bei elekezi iliyotolewa na Serikali.

Aliendelea kueleza kuwa, soko la madini  litarahisisha huduma za uuzaji na ununuzi wa madini ambapo huduma zote zitatolewa ndani ya jengo moja hivyo kuokoa muda wa wauzaji na wanunuzi wa madini.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alitoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa, atakayekamatwa anatorosha madini atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.

Pia aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali  kuhusu sekta ya madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje ya nchi.

Aidha, aliitaka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara na Taasisi nyingine za Serikali  zinazohusika na maendeleo ya sekta ya madini kuheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

“Wizara ya Madini, ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hilo ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini,” alisisitiza Majaliwa.

Aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali imeamua kutoa mwelekeo mpya katika usimamizi na maendeleo ya  sekta ya madini ambapo utekelezaji  wa dhamira hiyo unakwenda sambamba na kuweka mazingira mazuri na miundombinu itakayowezesha kuimarika kwa sekta ya madini nchini.


Jiwe la Msingi kwenye viwanja vya Soko la Madini Geita mara baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto) akielezea namna Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita ilivyojipanga kwenye usimamizi wa  Soko la Madini Geita kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kabla ya kuanza kwa shughuli za uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kabla ya kuzindua Soko la Madini  Geita tarehe 17 Machi, 2019. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati) akizugumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Soko la Madini la Geita kufanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 17 Machi, 2019. 

Soko la Madini Geita kabla ya uzinduzi wake tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa hotuba ya uzinduzi wa Soko la Madini Geita kwa wananchi na watendaji waandamizi wa Serikali (hawapo pichani) tarehe 17 Machi, 2019. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo kwenye uzinduzi huo. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Simon Msanjila akitoa taarifa ya uzalishaji wa madini nchini kwenye uzinduzi huo.

No comments:

Post a Comment