Tuesday, May 8, 2018

Waziri Kairuki afungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini


Na Greyson Mwase,

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.

Katika mkutano huo Waziri Kairuki amewataka watumishi kuelekeza nguvu kwenye kutoa kipaumbele kwenye masuala muhimu kama vile kuendelea kutengeneza sera bora zinazosimamia rasilimali za madini na kuweka mfumo mzuri na ulio bora wa ukusanyaji wa mapato ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

Pia, amewapongeza watumishi kwa ukusanyaji wa maduhuli  hadi kuvuka lengo kwa asilimia 130 ya makusanyo ya lengo  lililokuwa limewekwa kwenye Sekta ya Madini.

Aidha, amewataka watumishi kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2017/2018 ili kufanya vizuri kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019.

Aidha amewaasa watumishi wote kuwa waadilifu katika utendaji kazi wa kila siku na kuagiza watumishi wote waelimishwe kuhusu maadili katika utumishi wa umma na wale ambao hawajajaza fomu za maadili kujaza mara moja.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Wizara imebeba matarajio makubwa ya wananchi na kuwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya.

Aidha,  amesema Wizara ya Madini ni miongoni mwa Wizara zinazowajibika kuchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa.

Waziri Biteko amesisitiza mahusiano mazuri baina ya vyama vya wafanyakazi na waajiri  ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na  umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa umma. Masuala mengine  yaliyojadiliwa ni pamoja na  mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017.

Mkutano huo umefanyika leo tarehe 07 Mei, 2018 katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki  (kushoto) akipokelewa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa RasilimaliWatu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi (kulia) mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA)mjini Morogoro, kwa ajili ya kuzindua mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini tarehe 07 Mei, 2018.


Kutoka kushoto Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William (hayupo pichani) katika mkutano huo.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William akielezea majukumu ya chama hicho kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini (hawapo pichani) katika mkutano huo.


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko katika mkutano huo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko  akifafanua jambo katika mkutano huo.


Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini wakiimba wimbo maarufu wa mshikamano (solidarity forever) kwenye mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo.


Sekretarieti ya maandalizi katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akimkabidhi Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila nakala ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William nakala ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Madini na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) katika mkutano huo.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa nne kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la  Wizara ya Madini mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.

Leseni za madini kuanza kutolewa muda wowote


Na Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa zoezi la utoaji wa leseni kwa ajili ya utafiti, uchimbaji na biashara ya madini linatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa mara baada ya uanzishwaji wa Tume ya Madini.

Profesa Msanjila ameyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari  kwenye mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro  tarehe 07 Mei, 2018 wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.

Akielezea hatua iliyofikiwa ya zoezi hilo, Profesa Msanjila amesema kinachofanyika kwa sasa ni uchambuzi wa maombi ya leseni zote zilizokwishawasilishwa na kampuni mbalimbali zenye lengo la kujihusisha na shughuli za madini nchini.

Katika  hatua nyingine, akielezea mkutano huo, Profesa Msanjila amesema mkutano huo wa kwanza unaambatana na uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi ambalo lipo kisheria.

Ameendelea kueleza kuwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa umma.

Ametaja masuala mengine kuwa ni pamoja na mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amesema kuwa tayari tume imekaa na kuweka mkakati  kuhusu masuala ya leseni ili kuhakikisha kuwa leseni zinatolewa kwa wakati baada ya  zoezi la utoaji wa leseni kusitishwa tangu Julai mwaka 2017.

Akielezea hatua iliyofikiwa ya zoezi la uchambuzi wa leseni, Profesa Kikula amesema zaidi ya leseni 8,000 zimeshachambuliwa na kusisitiza kuwa zoezi litakapokamilika  waombaji waliokidhi vigezo watataarifiwa ili  kuanza kufanya taratibu za malipo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William amesema kuwa baraza la wafanyakazi ni chombo  muhimu kinachowaunganisha wafanyakazi wa Wizara katika uongozi kwa pamoja mahali pa kazi ili kuleta tija katika utekelezaji wa shughuli za Wizara.

Amesema baraza huishauri Wizara juu ya kuongeza ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na Wizara ni za kuridhisha kulingana na malengo ya Taifa ya kuleta maendeleo na kupunguza umaskini kwa kuanzisha viwanda vingi vitakavyoongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

Ameendelea kusema kuwa baraza hilo hujadili na kushauri mipango na bajeti ya wizara na kupima mafanikio na kuridhia utekelezaji wake pamoja na upandishwaji wa vyeo wafanyakazi kutokana na miundo ya utumishi.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa nne kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akisoma hotuba ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akitoa ufafanuzi katika mkutano huo

Monday, May 7, 2018

Naibu Waziri Biteko akutana na wachimbaji madini Lugoba


Na Greyson Mwase,

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko leo tarehe 06 Mei, 2018 amekutana na wachimbaji wa madini ya ujenzi aina ya kokoto katika eneo la Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. Mkutano huo uliohusisha Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wananchi, ulilenga kujadili changamoto katika uchimbaji madini ya ujenzi aina ya kokoto.

 Katika mkutano huo, Naibu Waziri Biteko alitoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wawekezaji  kuendeleza maeneo yao,  wawekezaji kutouza leseni kwa mtu mwingine pasipo kushirikisha serikali,    wawekezaji kuandaa mpango wa utoaji huduma kwa jamii pamoja na kuutekeleza na  Ofisi ya Madini ya Kanda ya Mashariki kufuatilia ahadi za wawekezaji katika huduma za jamii na kuwasilisha  ripoti mara moja.

Maelekezo mengine ni pamoja na Ofisi ya Madini Kanda ya Mashariki kuwasilisha  ripoti ya athari za mazingira kabla ya Mei 20, 2018, wawekezaji kushirikiana na wananchi wanaowazunguka, kampuni zenye mgogoro na wananchi kuhakikisha zinamaliza tofauti zao na fedha za halmashauri  kutumika kwenye uwekezaji mwingine kwa ajili ya maendeleo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akitoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wananchi mbalimbali walioshiriki katika mkutano huo.


Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) akielezea shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko na wananchi wa wilaya ya Bagamoyo (hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika katika eneo la Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.


Sehemu ya wakazi wa eneo la Lugoba lililopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakifuatilia ufafanuzi  uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).

Mchimbaji kutoka kampuni ya Gulf Concrete and Cement Products, Augustine Modest akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) katika mkutano huo.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akinukuu maswali mbalimbali yaliyokuwa yanaulizwa na wachimbaji madini ya kokoto (hawapo pichani) katika mkutano huo.

Biteko apiga marufuku bei holela madini ya ujenzi


Na Greyson Mwase, Tanga

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amepiga marufuku tabia ya wachimbaji wa madini ya ujenzi ya kushusha bei ya madini hayo kwa ajili ya kuuza kwa wingi, badala ya kufuata bei elekezi iliyowekwa na Serikali  huku wakiwalipa  vibarua kiasi kidogo cha fedha kisichoendana na kazi ngumu wanazofanya.

Naibu Waziri Biteko ameyasema hayo  mapema leo alipofanya ziara katika machimbo ya madini ya ujenzi aina ya kokoto katika eneo la Amboni mkoani Tanga lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kuzungumza na wananchi.

Biteko alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wamiliki wa leseni kuuza madini aina ya kokoto kwa bei  ya chini na kupata faida huku wakiwalipa kiasi kidogo vibarua wanaofanya kazi ngumu ya kuponda kokoto kwa kutumia vifaa duni.

Akijibu kero mbalimbali zilizowasilishwa na wachimbaji madini ya kokoto Biteko alisema kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na  Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni hukakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha watanzania na kuwataka kuunda vikundi ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa na ruzuku kutoka Serikalini.

Alisema Wizara ya Madini kupitia Mradi wa Usimamizi  Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) imepanga mikakati ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia ruzuku na ununuzi wa vifaa vya uchimbaji ili waweze kufanya kazi katika mzaingira rafiki na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa  Sekta ya Madini.

Akielezea hatua zilizofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya madini nchini alisema imeanza na kufanya marekebisho katika Sheria ya Madini na kanuni zake, kuondoa urasimu ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa.

Alisema pia Serikali imeanzisha Tume ya Madini itakayokuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za madini  ikiwa ni pamoja na  kusogeza huduma za utoaji wa leseni za madini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wa madini ya ujenzi kulinda rasilimali za madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Kumekuwepo na tabia ya baadhi wa wachimbaji madini kutorosha madini nje ya nchi na kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama, na kama Serikali tumejipanga kuhakikisha tunalinda rasilimali za madini kwa nguvu zote,” alisisitiza Biteko.

Aidha katika hatua nyingine Biteko aliwataka wachimbaji wa madini kufuata sheria za madini pamoja na kanuni zake.


Mkuu wa Wilaya ya  Tanga (kulia) Thobias Mwilapwa akielezea Sekta ya Madini katika Wilaya yake kwa watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Vyombo vya Habari (hawapo pichani) kwenye ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara katika eneo linalotumika kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya ujenzi aina ya kokoto  lililopo katika eneo la Amboni Wilayani Tanga mkoani Tanga.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akizungumza na mponda kokoto, Helena  Joackim (aliyekaa chini) kwenye machimbo ya kokoto yanayomilikiwa na Swalehe  Khama yaliyopo katika eneo la Amboni Wilayani  Tanga mkoani Tanga.


Mchimbaji mdogo wa madini ya kokoto Swalehe Khama akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye ziara hiyo.


Mponda kokoto, Husna Bakari akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) katika ziara hiyo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo kwa wachimbaji madini ya ujenzi aina ya kokoto kwenye ziara hiyo.

CANACO yapewa siku saba kuwasilisha mkataba serikalini


Na Greyson Mwase, Tanga

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipa siku saba kampuni  inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited, kuwasilisha mikataba na nyaraka zote kati yake na kampuni ya Tanzania Gold Field Limited ili kubaini namna makubaliano  ya mkataba yalivyofanyika ikiwa ni pamoja na ulipaji kodi serikalini.

Biteko aliyasema hayo  alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo  wilayani Handeni mkoani Tanga mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania  Limited na kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo.

Waziri  Biteko  yupo katika ziara ya siku mbili mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua shughuli za madini pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika shughuli za madini.

Alisema mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania Limited, amebaini kuwa kampuni hiyo mara baada ya kukamilisha shughuli zake za utafiti wa madini ya dhahabu, kampuni hiyo iliikaribisha kampuni nyingine ijulikanayo kama Tanzania Gold Field Limited ya Canada kwa ajili ya kufanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Magambasi wilayani Handeni mkoani Tanga pasipo kufuata taratibu za kisheria.

Aliendelea kusema kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field Limited iliwataka wachimbaji wadogo waliokuwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo kuondoka ili waanze uchimbaji madini jambo ambalo lilitekelezwa.

Alieleza kuwa, kampuni ya Tanzania  Gold Field Limited ilianza shughuli zake bila kuwasilisha makubaliano ya kimaandishi kati yake na kampuni ya CANACO Tanzania Limited  Serikalini pamoja na kodi jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

Biteko aliendelea kusema kuwa kampuni inayotambulika mpaka sasa kisheria ni ya  CANACO Tanzania Limited ambapo shughuli za madini katika eneo la Magambasi zimekuwa zikifanyika bila kufuata sheria na kanuni za mazingira.

“Haiwezekani wachimbaji wadogo ambao ndio wamiliki wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wakaondolewa halafu akapewa mwekezaji mkubwa ambaye mpaka sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya kuchejua mabaki wa udongo wenye dhahabu na kuuza na kuharibu mazingira huku wachimbaji wadogo  wenye uwezo wa kuchimba dhahabu wakihangaika na kuishi katika lindi la umaskini,” alisema Biteko.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Handeni, Idrissa Yahya kuanza kazi mara moja ya uchambuzi wa vipengele vyote vya sheria na kanuni za madini  ili kuangalia namna vilivyokiukwa na kuwasilisha ripoti ofisini kwake.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi  na kuahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Madini ili kuimarisha sekta ya madini katika wilaya yake.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni kwa ajili ya ziara ya siku mbili ya mkoa wa Tanga yenye lengo la kukagua shughuli za madini pamoja na kuzungumza na wananchi tarehe 05 Mei, 2018. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara katika  eneo la kampuni  inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited.


Mmoja wa watendaji wa kampuni ya Tanzania Gold Field Limited, Robert Slavik (kulia) akielezea namna kampuni yake ilivyoingia makubaliano na kampuni ya CANACO Tanzania Limited kwenye shughuli za uchimbaji madini kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa pili kutoka kulia)


Sehemu wa wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.


Sehemu wa wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.


Sehemu wa wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.


Sehemu wa wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.

Waziri Kairuki akabidhi vifaa vya dola 350,000 kwa Ofisi za Madini za Kanda


Na Veronica Simba, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amekabidhi vitendea kazi mbalimbali vyenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 350,000 kwa Ofisi za Madini za Kanda mbalimbali nchini.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda hizo, jana Mei 4 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma; Waziri Kairuki aliwataka wahusika kuvitunza kutokana na gharama kubwa iliyotumika kuvinunua.

“Serikali imekopa kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelezwa ili iweze kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi. Tunaamini vitawasaidia sana katika utendaji wa majukumu yenu. Mvitunze.”

Akifafanua kuhusu vifaa vilivyotolewa, Waziri alisema kuwa ni pamoja na kifaa maalum kinachotumia teknolojia ya kisasa kung’amua uwepo wa aina ya gesi hatarishi kwa afya, chini ya Migodi ya Madini.

Alisema kuwa kifaa hicho kinamsaidia muhusika kutambua sehemu yenye hewa hiyo hatarishi na hivyo kuchukua hatua stahiki za kujiepusha na ajali inayotokana na kuvuta hewa ya aina hiyo.

Aidha, alitaja vifaa vingine kuwa ni kifaa maalum cha kukuza taswira za madini kinachojulikana kitaalam kama ‘Hand Lens’. “Kifaa hiki hutumika katika shughuli za uthaminishaji madini ya vito ambapo husaidia kuyakuza madini husika katika ukubwa unaotakiwa ili kukokotoa thamani yake halisi tofauti na unapotumia macho ya kawaida,” alifafanua.

Vingine ni pamoja na GPS zinazotumika kupima mipaka ya maeneo, ‘Printer’, viatu na sare maalum vinavyotumika migodini, Kompyuta, na vifaa vingine vya kijiolojia.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya alisema kuwa vifaa hivyo vimetolewa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP).

Alisema kuwa, zoezi la kugawa vifaa hivyo limefanyika katika awamu kadhaa, ambapo kwa awamu ya kwanza, Kanda za Madini zilizogawiwa ni Kanda ya Kusini (Mtwara na Nachingwea), Kanda ya Ziwa Nyasa (Songea, Njombe na Tunduru), Kanda ya Kusini Magharibi (Chunya) na Makao Makuu ya Wizara (Ofisi ya Ukaguzi wa Migodi, wachimbaji wadogo na utoaji leseni).

Nyingine ni Ofisi za Madini za Singida, Dodoma, Morogoro, Tanga, Handeni, Musoma, Bariadi, Mpanda, Kigoma, Mwanza, Geita, Bukoba, Arusha, Moshi, Mirerani na Tabora.

“Vifaa vilivyobaki ni kwa ajili ya Ofisi za Shinyanga, Kahama, Kituo cha Uongezaji Thamani Madini (TGC), Ofisi ya Biashara ya Madini na Ofisi ya Kamishna wa Madini, ambao ndiyo wanaopatiwa leo hii,” alifafanua Prof. Manya.

Akizungumza baada ya zoezi hilo la kukabidhi vifaa; Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula alisema kuwa, ni jambo la kutia faraja kwa kupata vitendea kazi kwa Ofisi hizo za Madini, ambazo kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017, sasa ziko chini ya Tume.

Alisema kuwa, upatikanaji wa vifaa hivyo vya kisasa utasaidia Tume kutimiza jukumu lake kubwa la kusimamia mapato stahiki ya Taifa yanayotokana na shughuli za madini.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu.


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (mwenye mtandio-mbele), akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda na watendaji wengine wa Wizara, baada ya zoezi la kukabidhi vitendea kazi lililofanyika Mei 4 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akifuatiwa na Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya. Kulia kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula.


Kutoka kulia ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Meneja Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP) Andrew Eriyo, wakiangalia baadhi ya vitendea kazi kwa ajili ya Ofisi za Madini nchini, muda mfupi kabla ya Waziri kuvikabidhi kwa wahusika, Mei 4 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara Dodoma.

Friday, May 4, 2018

Waziri Kairuki ataka migogoro yote ya madini isuluhishwe ndani ya mwaka mmoja


Na Veronica Simba, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amewataka watendaji wote wa Wizara hiyo kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi na kutatua migogoro yote iliyopo katika sekta husika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Ametoa maagizo hayo mapema leo, Mei 3, 2018 wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

“Lengo la Wizara ni kuhakikisha migogoro katika sekta ya madini inakwisha kabisa. Nawapongeza Naibu Mawaziri kwa kusimamia zoezi la utatuzi wa migogoro mbalimbali ambapo, mingi imekwishatatuliwa.”

Aidha, Waziri Kairuki amewaagiza watendaji na wataalam hao wa sekta ya madini, kuandaa taarifa fupi za migogoro iliyopo katika maeneo yao zikiainisha aina ya mgogoro, hatua zipi za utatuzi zimechukuliwa hadi sasa pamoja na ushauri wao kuhusu nini kifanyike ili kuhakikisha mgogoro husika unatatuliwa.

Katika hatua nyingine, pamoja na kupongeza ufanisi ulioonekana katika ukusanyaji wa maduhuli, Waziri amewataka watendaji hao kuongeza bidii na ubunifu zaidi ili kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika eneo hilo.

Amewataka kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kazi, pamoja na kuzingatia umuhimu wa dhana ya ushirikishaji majukumu mahala pa kazi, ili kupata matokeo bora zaidi.

“Kila mmoja aangalie Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano unataka nini na aone jinsi gani anautekeleza katika nafasi yake,” alisisitiza.

Vilevile, amewataka kuhakikisha wanakuwa na uelewa mzuri wa sheria na kanuni mpya za madini ili waweze kuzitekeleza kikamilifu.

Kuhusu suala la usalama migodini, Waziri kairuki amewataka watendaji kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini, wananchi wanaozunguka migodi na wadau wengine kwa ujumla kuhusu namna ya kuepusha ajali katika maeneo yao.

Ameshauri na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yatolewe kwa kutumia lugha rahisi ili hata wale wenye elimu ndogo waweze kuelewa.

Ufunguzi wa kikao kazi hicho cha siku tatu, umehudhuriwa pia na Naibu Mawaziri wa Madini, Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara husika Prof. Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Kamishna wa Madini na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof Shukran Manya pamoja na viongozi na wataalam mbalimbali wa Wizara hiyo.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki, akifungua kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini (hawapo pichani), kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akizungumza wakati wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini (hawapo pichani), kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akizungumza wakati wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini (hawapo pichani), kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza wakati wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini (hawapo pichani), kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. 
Viongozi na Wajumbe mbalimbali wakiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Viongozi na Wajumbe mbalimbali wakiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
Viongozi na Wajumbe mbalimbali wakiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda, Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Mei 3, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.