Na
Greyson Mwase, Tanga
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipa siku saba kampuni inayojishughulisha na utafiti wa madini ya
dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited,
kuwasilisha mikataba na nyaraka zote kati yake na kampuni ya Tanzania Gold
Field Limited ili kubaini namna makubaliano
ya mkataba yalivyofanyika ikiwa ni pamoja na ulipaji kodi serikalini.
Biteko
aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo
wilayani Handeni mkoani Tanga mara baada ya kufanya ziara katika kampuni
ya CANACO Tanzania Limited na
kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo.
Waziri Biteko
yupo katika ziara ya siku mbili mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua
shughuli za madini pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto
mbalimbali wanazokabiliana nazo katika shughuli za madini.
Alisema
mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania Limited, amebaini
kuwa kampuni hiyo mara baada ya kukamilisha shughuli zake za utafiti wa madini
ya dhahabu, kampuni hiyo iliikaribisha kampuni nyingine ijulikanayo kama
Tanzania Gold Field Limited ya Canada kwa ajili ya kufanya shughuli za
uchimbaji wa madini katika eneo la Magambasi wilayani Handeni mkoani Tanga
pasipo kufuata taratibu za kisheria.
Aliendelea
kusema kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field Limited iliwataka wachimbaji wadogo
waliokuwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo kuondoka
ili waanze uchimbaji madini jambo ambalo lilitekelezwa.
Alieleza
kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field
Limited ilianza shughuli zake bila kuwasilisha makubaliano ya kimaandishi kati
yake na kampuni ya CANACO Tanzania Limited Serikalini pamoja na kodi jambo ambalo ni
kinyume na sheria za nchi.
Biteko
aliendelea kusema kuwa kampuni inayotambulika mpaka sasa kisheria ni ya CANACO Tanzania Limited ambapo shughuli za
madini katika eneo la Magambasi zimekuwa zikifanyika bila kufuata sheria na
kanuni za mazingira.
“Haiwezekani
wachimbaji wadogo ambao ndio wamiliki wa madini ya dhahabu katika eneo la
Magambasi wakaondolewa halafu akapewa mwekezaji mkubwa ambaye mpaka sasa hakuna
kilichofanyika zaidi ya kuchejua mabaki wa udongo wenye dhahabu na kuuza na
kuharibu mazingira huku wachimbaji wadogo
wenye uwezo wa kuchimba dhahabu wakihangaika na kuishi katika lindi la
umaskini,” alisema Biteko.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Kaimu Afisa Madini Mkazi wa
Handeni, Idrissa Yahya kuanza kazi mara moja ya uchambuzi wa vipengele vyote
vya sheria na kanuni za madini ili
kuangalia namna vilivyokiukwa na kuwasilisha ripoti ofisini kwake.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa
kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na
mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi
na kuahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Madini ili kuimarisha
sekta ya madini katika wilaya yake.
No comments:
Post a Comment