Na
Greyson Mwase, Tanga
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko amepiga marufuku tabia ya wachimbaji wa madini ya
ujenzi ya kushusha bei ya madini hayo kwa ajili ya kuuza kwa wingi, badala ya
kufuata bei elekezi iliyowekwa na Serikali huku wakiwalipa vibarua kiasi kidogo cha fedha kisichoendana
na kazi ngumu wanazofanya.
Naibu
Waziri Biteko ameyasema hayo mapema leo
alipofanya ziara katika machimbo ya madini ya ujenzi aina ya kokoto katika eneo
la Amboni mkoani Tanga lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji wa madini
pamoja na kuzungumza na wananchi.
Biteko
alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wamiliki wa leseni kuuza madini aina
ya kokoto kwa bei ya chini na kupata
faida huku wakiwalipa kiasi kidogo vibarua wanaofanya kazi ngumu ya kuponda
kokoto kwa kutumia vifaa duni.
Akijibu
kero mbalimbali zilizowasilishwa na wachimbaji madini ya kokoto Biteko alisema
kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni hukakikisha
kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha watanzania na kuwataka kuunda vikundi
ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa na ruzuku kutoka Serikalini.
Alisema
Wizara ya Madini kupitia Mradi wa Usimamizi
Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) imepanga mikakati ya kuwawezesha
wachimbaji wadogo kupitia ruzuku na ununuzi wa vifaa vya uchimbaji ili waweze
kufanya kazi katika mzaingira rafiki na kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji
wa Sekta ya Madini.
Akielezea
hatua zilizofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya madini nchini alisema
imeanza na kufanya marekebisho katika Sheria ya Madini na kanuni zake, kuondoa
urasimu ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa.
Alisema
pia Serikali imeanzisha Tume ya Madini itakayokuwa na jukumu la kusimamia
shughuli zote za madini ikiwa ni pamoja
na kusogeza huduma za utoaji wa leseni
za madini.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wa madini ya ujenzi
kulinda rasilimali za madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Kumekuwepo
na tabia ya baadhi wa wachimbaji madini kutorosha madini nje ya nchi na
kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama, na kama Serikali tumejipanga
kuhakikisha tunalinda rasilimali za madini kwa nguvu zote,” alisisitiza Biteko.
Aidha
katika hatua nyingine Biteko aliwataka wachimbaji wa madini kufuata sheria za
madini pamoja na kanuni zake.
Mchimbaji mdogo wa madini ya kokoto Swalehe Khama akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye ziara hiyo. |
Mponda kokoto, Husna Bakari akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) katika ziara hiyo. |
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo kwa wachimbaji madini ya ujenzi aina ya kokoto kwenye ziara hiyo. |
No comments:
Post a Comment