Na Veronica Simba, Dodoma
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki amewataka watendaji wote wa Wizara hiyo kuhakikisha wanatafuta
ufumbuzi na kutatua migogoro yote iliyopo katika sekta husika ndani ya kipindi
cha mwaka mmoja.
“Lengo la Wizara ni
kuhakikisha migogoro katika sekta ya madini inakwisha kabisa. Nawapongeza Naibu
Mawaziri kwa kusimamia zoezi la utatuzi wa migogoro mbalimbali ambapo, mingi
imekwishatatuliwa.”
Aidha, Waziri Kairuki
amewaagiza watendaji na wataalam hao wa sekta ya madini, kuandaa taarifa fupi
za migogoro iliyopo katika maeneo yao zikiainisha aina ya mgogoro, hatua zipi
za utatuzi zimechukuliwa hadi sasa pamoja na ushauri wao kuhusu nini kifanyike
ili kuhakikisha mgogoro husika unatatuliwa.
Katika hatua
nyingine, pamoja na kupongeza ufanisi ulioonekana katika ukusanyaji wa
maduhuli, Waziri amewataka watendaji hao kuongeza bidii na ubunifu zaidi ili
kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi katika eneo hilo.
Amewataka kutekeleza
ipasavyo majukumu yao ya kazi, pamoja na kuzingatia umuhimu wa dhana ya
ushirikishaji majukumu mahala pa kazi, ili kupata matokeo bora zaidi.
“Kila mmoja aangalie
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano unataka nini na aone jinsi gani
anautekeleza katika nafasi yake,” alisisitiza.
Vilevile, amewataka
kuhakikisha wanakuwa na uelewa mzuri wa sheria na kanuni mpya za madini ili
waweze kuzitekeleza kikamilifu.
Kuhusu suala la
usalama migodini, Waziri kairuki amewataka watendaji kuendelea kutoa elimu kwa
wachimbaji wadogo wa madini, wananchi wanaozunguka migodi na wadau wengine kwa
ujumla kuhusu namna ya kuepusha ajali katika maeneo yao.
Ameshauri na
kusisitiza kuwa mafunzo hayo yatolewe kwa kutumia lugha rahisi ili hata wale
wenye elimu ndogo waweze kuelewa.
Ufunguzi wa kikao
kazi hicho cha siku tatu, umehudhuriwa pia na Naibu Mawaziri wa Madini, Dotto
Biteko na Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara husika Prof. Simon Msanjila,
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Kamishna wa Madini na Kaimu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Prof Shukran Manya pamoja na viongozi na
wataalam mbalimbali wa Wizara hiyo.
Viongozi na Wajumbe
mbalimbali wakiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda,
Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Mei 3, 2018
Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
|
Viongozi na Wajumbe
mbalimbali wakiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda,
Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Mei 3, 2018
Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
|
Viongozi na Wajumbe
mbalimbali wakiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Madini wa Kanda,
Mikoa na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini kilichofanyika Mei 3, 2018
Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.
|
No comments:
Post a Comment